Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania yaua ndege wavamizi milioni tano aina ya kwelea
Ndege aina ya Kwelea kwelea mara nyingi huharibu nafaka kama mchele na ngano.
Moja kwa moja
Viktor Sokolov: Urusi yatoa video 'kuonesha kwamba kamanda wa meli za Bahari Nyeusi bado yuko hai'
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imetoa video inayomuonyesha kamanda wa Meli ya Bahari Nyeusi kwenye mkutano, licha ya Ukraine kudai kumuua.
Haijulikani ni lini kanda hiyo, ambapo Viktor Sokolov alionekana kwenye kiunga cha video na waziri wa ulinzi, ilirekodiwa.
Wizara ilisema mkutano na maafisa wakuu ulifanyika Jumanne.
Vikosi maalum vya Ukraine vilisema Jumatatu Adm Sokolov na maafisa wengine 33 walikufa katika shambulio la kombora kwenye makao makuu ya meli huko Sevastopol, katika eneo la Crimea linalokaliwa kimabavu na Urusi
Hawakumtaja amiri huyo moja kwa moja, wala hawakutoa uthibitisho wowote kwamba alikuwa amekufa.Sasa wanasema "wanafafanua" ripoti hizo.
"Kama inavyojulikana, maafisa 34 waliuawa kutokana na shambulio la kombora kwenye makao makuu ya Meli za Bahari Nyeusi za Shirikisho la Urusi," walisema katika taarifa.
"Vyanzo vilivyopo vinadai kuwa miongoni mwa waliofariki ni kamanda wa msafara Meli za Bahari Nyeusi za Urusi. [Miili] mingi bado haijatambuliwa kutokana na hali ya sehemu za mwili."
Mshukiwa wa mauaji Rwanda apewa kifungo cha siku 30 huku uchunguzi ukiendelea
Mshukiwa wa mauaji Rwanda apewa kifungo cha siku 30 huku uchunguzi ukiendelea
Mshukiwa wa mauaji Denis Kazungu amepewa kifungo cha siku 30 jela na mahakama huko Rwanda wakati uchunguzi dhidi yake ukiendelea huku jaji akisema ni kutokana na uzito wa mashtaka dhidi yake.
Mshukiwa huyo alishtakiwa kwa makosa 10 yakiwemo mauaji, ubakaji na utekaji nyara kwa kuwauwa watu 14 wengi wao wakiwa wasichana.
Yeye mwenyewe alikiri kufanya mauaji hayo.
Mahakamani kulijaa umati wa watu, waandishi wa habari wa ndani na wa kimataifa na raia wa kawaida waliozunguka eneo zima.
Kazungu alifikishwa mahakamani akiwa mikononi mwa polisi huku akizomewa na umati wa watu.
Ombi hilo limezingatiwa na mahakama ambayo imesema kuwa katika kikao kilichotangulia, mshukiwa alikiri kuhusika na mauaji huku akisema mahakama iamue itakavyo.
Hoja ya mshukiwa pia ilikuwa kwamba kesi iendeshwe kwa faragha kwa kile alichosema hataki vyombo vya habari kuhudhuria kesi yake.
Kulingana na mwendesha mashtaka, mshukiwa aliua watu 14 kwa nyakati tofauti na kuwazika shimoni upande wa jikoni kwenye nyumba aliokuwa akiishi katika kitongoji cha Kicukiro-mjini Kigali.
Miongoni mwao ni wavulana 2 na wasichana 12 wengi wao walidaiwa kuwa wafanyabiashara wa ngono na alisisitiza alifanya hivyo kutokana na kwamba walimuambukiza ukimwi.
Ingawa hali ya afya ya Bwana Kazungu haijulikani, mahakamani alionekana mwenye afya njema.
Jaji hakusema mengi lakini kwa hali ilivyo, kawaida katika kesi kama hii nchini Rwanda, ni kwamba kipindi hicho kinaweza kuongezwa hadi mwendesha mashtaka anapokamilisha upelelezi wake kwa kipindi kisichozidi miezi 12.
Jaji amesemapande husika zina siku 5 za kukata rufaa.
Kazungu ambaye bado hakuwa na wakili mahakamani hakutangaza lolote kuhusu ikiwa atakata rufaa kupinga uamuzi huo.
Mwanafunzi akamatwa nchini Uganda kwa tuhuma za ulanguzi wa binadamu
Polisi nchini Uganda wanasema wamemkamata mwanafunzi mwenye umri wa miaka 17 kwa tuhuma za kusafirisha vijana 170.
Polisi walisema walimkamata mwanafunzi huyo wa shule ya upili tarehe 18 Septemba katikati mwa Uganda.
Polisi wanasema kuwa mwanafunzi huyo aliwaweka vijana 170 katika nyumba ya mwanamke mwenye umri wa miaka 28 wakati wakisubiri usafiri hadi mji mkuu wa Kenya, Nairobi, ambako mwanafunzi huyo alikuwa amewaahidi kazi.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi la Uganda lilisema siku ya Jumanne kwamba mpango huo wa usafirishaji haramu wa binadamu ni ulaghai.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi la Uganda lilisema siku ya Jumanne kwamba mpango huo wa usafirishaji haramu wa binadamu ni ulaghai.
"Alipohojiwa [mwanafunzi] alikiri kwamba alitaka kuwanyang'anya waathiriwa pesa kwa kutumia jina la Kampuni ya Humble nchini Kenya kama siri.
Hakukuwa na uhusiano na kampuni hiyo na tangazo la kazi kwa wahudumu, watengenezaji kahawa na wahudumu wa maduka makubwa nchini Kenya lilikuwa bandia,” Jeshi la Polisi la Uganda lilisema katika taarifa.
Gazeti la kibinafsi la Daily Monitor la Uganda limeripoti kuwa 98 kati ya waathiriwa walimlipa mwanafunzi huyo shilingi 100,000 za Uganda ($26; £21) kila mmoja huku wengine wakilipa shilingi 50,000 kila mmoja.
Mwanafunzi huyo bado hajaombwa kujibu anachodaiwa kufanya.
Watu wanane wauawa kwa kupigwa na umeme Afrika Kusini
Watu wanane wamepigwa na umeme baada ya upepo mkali na mvua kubwa kunyesha katika jimbo la Western Cape nchini Afrika Kusini.
Mamia ya watu wamehamishwa kutoka kwa makazi yao.
Maporomoko ya ardhi na miamba yalilazimu kufungwa kwa barabara kuu kadhaa zinazoingia Cape Town.
Mvua kubwa iliyonyesha hadi usiku wa kuamkia jana ilisababisha mito kadhaa kufurika na kupelekea uharibifu wa miundombinu na kukatika kwa umeme.
Mamlaka imesema kuwa zaidi ya nyumba 1,000 zimefurika na shule 150 kuharibiwa.
Hali ya hewa imeboreshwa kidogo na shughuli za kuondoa uchafu zinaendelea.
Watu watano wanaodaiwa kuwa majasusi wa Urusi wafikishwa mahakamani London
Watu watano wanaotuhumiwa kuwa sehemu ya kikosi cha kijasusi cha Urusi kinachofanya kazi nchini Uingereza wamefikishwa mahakamani.
Raia wa Bulgaria Orlin Roussev, Bizer Dzhambazov, Katrin Ivanova, Ivan Stoyanov, na Vanya Gaberova wanadaiwa kula njama ya kukusanya taarifa ambazo zingekuwa muhimu sana kwa adui.
Inadaiwa walifanya ufuatiliaji kwa watu na maeneo yaliyolengwa na Urusi kati ya Agosti 2020 na Februari 2023.
Washukiwa hao wamepelekwa rumande.
Shughuli zao za uchunguzaji zinadaiwa kuwa zilikuwa kwa madhumuni ya kuisaidia Urusi kuchukua hatua za chuki dhidi ya walengwa, ikiwa ni pamoja na utekaji nyara.
Hawakuwasilisha maombi yao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Westminster, ambapo walionekana kupitia kiunganishi cha video kutoka kwa magereza manne tofauti.
Washtakiwa wote watano muda mwingi walikaa kimya zaidi ya kuzungumza kuthibitisha majina yao na tarehe za kuzaliwa.
Maafisa wa Polisi wa kukabiliana na ugaidi waliwakamata mwezi Februari chini ya Sheria ya Siri.
Msako wa bosi wa genge ambaye alidhibiti jela ya kifahari nchini Venezuela
Polisi kote Amerika Kusini wanamsaka kiongozi wa genge la Venezuela ambaye alitoroka kutoka kwa gereza la kifahari alilokuwa akilidhibiti, muda mfupi kabla ya kuvamiwa.
Wakati wanajeshi na polisi 11,000 walipoingia katika jela ya Tocorón inayosimamiwa na Venezuela siku ya Jumatano, Héctor Guerrero Flores hakupatikana popote.
Chini ya utawala wa Guerrero Flores,Tocoron ilikuja kufanana na eneo la mapumziko ya kifahari.
Jela ilijivunia bustani ndogo ya wanyama, klabu ya usiku na bwawa la kuogelea.
Flores mwenye umri wa miaka 39 kutoka jimbo la Aragua nchini Venezuela amekuwa akiingia na kutoka katika gereza la Tocorón kwa zaidi ya muongo mmoja.
Mnamo mwaka wa 2012, kiongozi huyo wa genge la uhalifu wa kimataifa la Tren de Aragua alifanikiwa kutoroka jela kwa kuwahonga walinzi.
Baada ya kukamatwa tena mwaka 2013, alirejeshwa katika gereza hilo hilo, lakini inaonekana uwezo wake ndani ya jela - na juu ya wale waliopewa jukumu la kumlinda - uliongezeka tu.
Sio tu kwamba aligeuza Tocorón kuwa kituo cha biashara ya uhalifu ya Tren de Aragua, lakini chini ya utawala wake, jela ilikuwa na vifaa vyote vya hoteli ya kifahari.
Familia za wafungwa zilihamia kwenye gereza hilo na kuligeuza kuwa makazi yao.Wafungwa walikuwa na uwezo wa kupata huduma za benki , duka la kucheza kamari huku watoto wao wakistaajabia flamingo na mbuni kwenye bustani ya wanyama.
Tanzania: Wanasarakasi wa Ramadhani Brothers kushiriki fainali ya 'America's Got Talent' leo usiku
Kundi la wanasarakasi la Ramadhani Brothers linaloundwa na Fadhili Ramadhani pamoja na Ibrahim Jobu, wote raia wa Tanzania wanatarajiwa kushiriki Fainali za Shindano la Kusaka Vipaji la 'America's Got Talent' linalofanyika leo Septemba 26, 2023 majira ya jioni saa za Las Vegas, Marekani.
Wanasarakasi hao wawili wa Tanzania wamebobea Sanaa ya kutumia kichwa, ikimaanisha kwamba Fadhili anatumia kichwa chake mwenyewe (na sio kitu kingine) kumbeba juu Ibrahim ambaye kichwa chake kinakuwa kinageukia chini.
Mapema leo, Fadhili ameiambia BBC kuwa wamefanya mazoezi vizuri, wamepumzika vyema na wako tayari kushiriki kwenye fainali hizo.
Fadhili anasema, "Tulifanya mazoezi yetu ya mwisho, sasa tunapumzika tunangoja jioni (saa 12 jioni saa za Las Vegas) ili kuonyesha kile tulichonacho.
Kwa mujibu wa orodha ya watakaoshiriki, tutakuwa wa kwanza kuonyesha ulimwengu kile tulichokuja nacho kutoka Tanzania.”
Wakati huo huo, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania imewatakia kheri wanasaraksi hao wawili.
Wanaowania ushindi katika fainali hiyo ni Pamoja na; Putri Ariani (Mwanamuziki), Chibi Unity (Kundi la Densi), Murmuration (Kundi la Densi), Mzansi Youth Choir (Kwaya), Lavender Darcangelo (Mwanamuziki), Avantgardey (Kundi la Densi), Ahren Belisle (Comic), 82nd Airborne Chorus (Chorus), Anna Deguzman (Mwanamazingaumbwe) Pamoja na kundi la Pamoja la Adrian Stoica na Hurricane.
Pia unaweza kusoma:
- Ghetto Kids: Nini kilicho nyuma ya harakati zao kinazowafanya watambe dunia nzima?
Wanasarakasi wa Ramadhani Brothers wa Tanzania wanatarajiwa kushiriki fainali ya 'America's Got Talent' leo usiku
Kenya kuanzisha kinu cha nishati ya nyuklia mnamo 2027
Kenya itaanza kujenga kinu cha nyuklia mnamo mwaka wa 2027.
Kinu cha nyuklia cha Megawati 1,000 ni sehemu ya mpango wa nchi kuhamia kwa nishati safi na kuongeza uzalishaji wa kawi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Nishati ya Nyuklia Justus Wabuyabo aliliambia gazeti la Business Daily la Kenya kwamba shirika hilo kwa sasa linafanya tathmini ya eneo na kukamilisha maandalizi ya kufungua zabuni za ujenzi wa kiwanda hicho.
Bw Wabuyabo alisema kuwa kiwanda hicho kitajengwa katika eneo la pwani ya Kenya kwa muda wa miaka sita hadi kumi, huku mtambo wa kwanza ukianza kufanya kazi mwaka wa 2034 .
Baadhi ya Wakenya wamekosoa mpango huo wakidai kuwa kiwanda cha nyuklia si cha lazima na Kenya haina uwezo wa kushughulikia taka za nyuklia.
"Tuna rasilimali za kutosha za umeme wa maji, jotoardhi, jua na upepo.Mbaya zaidi, sidhani kama tuna uwezo wa kuhakikisha usalama wa kinu cha nyuklia au kusafisha janga linapotokea," mtumiaji wa Twitter alisema.
Kwa sasa, Afrika Kusini ndiyo nchi pekee ya Afrika inayozalisha nishati ya nyuklia kibiashara.
Baadhi ya mataifa mengine ya Afrika yameanza mipango ya kupitisha nishati ya nyuklia, ikiwa ni pamoja na Rwanda na Misri, ambayo kwa sasa inajenga kinu cha nyuklia cha $30bn (£24bn).
Ubaguzi wa kuwa mpenzi wa jinsia moja hautoshi kupewa hifadhi ya makazi Uingereza
Kuogopa kuwa utabaguliwa kwasababu ya kushiriki mapenzi ya jinsia moja au kwa kuwa ni mwanamke haipaswi kuwa sababu ya kutosha kuwezesha kupata hifadhi kimataifa kama mkimbizi, Waziri wa mambo ya ndani amesema.
Akihutubia baraza la wasomi la Marekani, Suella Braverman atahoji kama utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi wa 1951 "unafaa kwa zama zetu za kisasa".
Anatarajiwa kusema kuwa sheria zimebadilika kutoka kusaidia wale wanaotoroka mateso hadi wale wanaoogopa kuwa watachukuliwa vibaya.
Chama cha Labour kimemshutumu kwa "kukata tamaa ya kufanyia marekebisho" mfumo wa kutoa hifadhi kwa wakimbizi.
"Sasa ameamua kufurahisha umma kwa manufaa yake mwenyewe na kutafuta mtu mwingine yeyote wa kumlaumu," amesema waziri kivuli Yvette Cooper.
Mkataba wa Wakimbizi uliundwa kufuatia Vita vya Pili vya Dunia, na una msingi wake kwamba wakimbizi hawapaswi kurejeshwa katika nchi ambako wanakabiliwa na vitisho kwa maisha au uhuru wao.
Waziri wa mambo ya ndani atawaambia hadhira katika Taasisi ya Biashara ya Marekani ya mrengo wa kulia huko Washington DC kwamba "sasa tunaishi katika wakati tofauti kabisa" na wakati mkataba huo ulipotiwa saini.
Anatarajiwa kusema: "Kama sheria ya kesi inavyoendelea, kile tumeona katika utendaji ni mabadiliko ya kitafsiri kutoka kwa 'mateso', kwa mapendelea ya kitu sawa na ufafanuzi wa 'ubaguzi'.
"Na mabadiliko sawa kutoka kwa 'hofu yenye msingi' hadi 'hofu ya kuaminika' au 'hofu inayowezekana kutokea'.
"Matokeo ya kiutendaji ambayo yamekuwa yakilenga kuongeza idadi ya wale ambao wanaweza kupita vigezo vilivyowekwa vya kupata hifadhi, na kupunguza kizingiti cha kufikia hilo."
Ufafanuzi huu unatoa haki kwa takriban watu milioni 780 duniani kote kuhamia nchi nyingine, kulingana na taasisi iliyoanzishwa na Margaret Thatcher, Kituo cha Mafunzo ya Sera.
Pia unaweza kusoma:
- Mzozo mpya wazuka kuhusu tamasha la Nyege Nyege la Uganda
Mzozo mpya wazuka kuhusu tamasha la Nyege Nyege la Uganda
Viongozi wa Uganda wametofautiana kuhusu kuandaliwa kwa tamasha maarufu la Nyege Nyege katika jiji la Jinja mashariki mwa nchi hiyo, ambalo wakosoaji wake wameeleza kuwa wanaendeleza ukosefu wa maadili.
Nyege Nyege, tamasha la kila mwaka la muziki na sanaa ambalo limekuwa likifanyika nchini Uganda tangu 2015, ni moja ya tamasha maarufu lakini lenye utata katika Afrika Mashariki.
Baadhi ya Viongozi wa Kiislamu wa Jinja wakiongozwa na Kadhi wa Wilaya ya Jinja Sheikh Ismail Basoga Adi wamepinga kufanyika kwa hafla hiyo mjini humo.
“Shughuli zinazofanyika Nyege Nyege si za kupongezwa, hasa kuhusiana na athari zake kwa kizazi kipya.Ingawa wanazalisha mapato makubwa, pia wanakuza ukosefu wa maadili katika jamii,” Bw Adi alisema hivi majuzi, kulingana na gazeti la kibinafsi la Daily Monitor Newspaper la Uganda.
Hata hivyo, Waziri wa Uganda wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Rebecca Alitwala Kadaga amekosoa msukumo wa viongozi wa Kiislamu kupiga marufuku tamasha hilo, akiwataja "watafutaji binafsi wanaojificha nyuma ya dini".
Alisema siku ya Jumatatu kuwa tamasha hilo halipaswi kufutwa kwa sababu za ukosefu wa maadili kwa kuwa halihudhuriwi na watoto na viongozi wa Kiislamu wa Jinja hawajapinga kuandaliwa kwa hafla kama hizo jijini hapo awali.
Katika miaka ya nyuma, baadhi ya viongozi wa Uganda walipigania kupigwa marufuku kwa tamasha hilo, ambalo wamelitaja kuwa "kitovu cha uasherati" na "mapenzi ya jinsia moja".
Tanzania yaua ndege wavamizi milioni tano aina ya kwelea
Zaidi ya ndege wavamizi milioni tano aina ya kwelea wameuawa katika msako mkali nchini Tanzania, mamlaka imesema katika taarifa iliyoripotiwa kwenye vyombo vya habari vya ndani.
Ndege hao walikuwa wamevamia zaidi ya ekari 1,000 za mashamba ya mpunga katika mkoa wa Manyara kaskazini mwa nchi na kusababisha hasara kubwa.
Kwa zaidi ya siku nne maafisa walitumia ndege zisizo na rubani kunyunyizia makundi ya ndege kwa viua ndege, gazeti la Tanzania Times limeripoti.
Ndege hao wavamizi walikuwa na uwezo wa kuharibu zaidi ya tani 50 za mazao ya chakula kila siku, kulingana na Gadman Mbuko kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania.
Ndege aina ya kwelea mara nyingi huharibu nafaka kama mchele na ngano.
Mnamo mwaka wa 2021, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) lilikadiria kuwa mazao yenye thamani ya $50m (£41m) yanapotea kutokana na ndege kila mwaka, wengi wao katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Soma zaidi:
- Nzige Afrika: Je, mataifa yanahitaji nini kukabiliana na tishio la wadudu hawa?
- Masaibu ya nzige Kenya
Nagorno-Karabakh: Mlipuko wa bohari ya mafuta wawaua watu 20 huku idadi ya wakimbizi ikiongezeka maradufu
Kazi ya uokoaji na matibabu kufuatia mlipuko katika ghala la gesi karibu na barabara kuu ya Stepanakert-Askera huko Berkadzor mnamo 26 Septemba.
Mlipuko katika ghala la mafuta katika mji wa Nagorno-Karabakh nchini Azerbaijan umeua watu 20 na kujeruhi mamia zaidi, mamlaka ya eneo la Armenia inasema.
Takriban watu 300 walilazwa hospitalini, huku kadhaa kati yao wakiwa "bado wako katika hali mbaya".
Mlipuko huu unatokea wakati serikali ya Armenia imekwishasema wakimbizi 13,350 walivuka na kuingia nchini kutoka kwa enclave.
Eneo linalozozaniwa la Nagorno-Karabakh ni nyumbani kwa wengi wa Waarmenia wa makabila 120,000.
Bado haijabainika ni nini kilisababisha mlipuko huo siku ya Jumatatu jioni katika mji mkuu wa Stepanakert.
Afisa wa Haki za Kibinadamu Gegham Stepanyan aliandika kwenye mtandao wa kijamii: "Kutokana na mlipuko katika ghala la mafuta, idadi ya waliojeruhiwa inazidi watu 200.
"Hali ya afya ya walio wengi ni mbaya au mbaya sana. Uwezo wa matibabu wa Nagorno-Karabakh hautoshi."
Katika taarifa siku ya Jumanne maafisa wa eneo hilo walisema miili 13 ambayo haikutambuliwa ilipatikana katika eneo la tukio na wengine saba walikufa hospitalini.
Tangu Azerbaijan ilipoiteka Nagorno-Karabakh wiki iliyopita, maelfu ya watu wameondoka eneo hilo baada ya serikali ya Armenia huko Yerevan kutangaza mipango ya kuwahamisha wale walioachwa bila makazi na mapigano.
Azerbaijan imesema inataka kuwajumuisha tena Waarmenia wa kabila kama "raia sawa"
Nagorno-Karabakh - eneo lenye milima katika Caucasus Kusini - linatambuliwa kimataifa kama sehemu ya Azerbaijan, lakini limedhibitiwa na Waarmenia wa kabila kwa miongo mitatu.
Nagorno-Karabakh: Maelfu ya watu wakimbia huku Armenia ikisema mauaji ya kikabila yanaendelea
Mtiririko unaoongezeka wa wakimbizi wa kabila la Armenia wanakimbia Nagorno-Karabakh kufuatia Azerbaijan kuliteka eneo hilo linalozozaniwa wiki iliyopita.
Zaidi ya watu 6,500 hadi sasa wamevuka hadi Armenia kutoka eneo hilo, ambalo ni nyumbani kwa wengi wa Waarmenia wapatao 120,000.
Waliondoka baada ya serikali ya Yerevan kutangaza mipango ya kuwahamisha wale walioachwa bila makao kufuatia mapigano.
Waziri Mkuu wa Armenia ameonya kwamba mauaji ya kikabila "yanaendelea" katika eneo hilo.
"Hiyo inafanyika hivi sasa, na huo ni ukweli wa kusikitisha sana kwa sababu tulikuwa tunajaribu kuhimiza jamii ya kimataifa kuhusu hilo," Nikol Pashinyan aliwaambia waandishi wa habari.
Azerbaijan imesema inataka kuwajumuisha tena wat wa kabila la Waarmenia kama "raia sawa".
Maandamano yalizuka kwa mara ya kwanza wiki iliyopita kupinga jinsi serikali inavyoshughulikia mzozo wa Nagorno-Karabakh.
Adam Britton: Mtaalamu wa mamba wa Uingereza akiri kuwanyanyasa kingono mbwa
Mtaalamu mashuhuri wa mamba wa Uingereza amekiri mashtaka 60 yanayohusiana na ngono na wanyama na nyenzo za unyanyasaji wa watoto.
Mahakama ya Australia ilisikimsikiliza Adam Britton alijirekodi binafsi akiwatesa makumi ya mbwa hadi karibu wote wakafa.
Kisha alichapisha video za matukio hayo mtandaoni, ambapo pia alipata nyenzo za unyanyasaji wa watoto.
Bw Britton ambaye ni mtaalamu wa masuala ya wanyama ambaye amefanya kazi katika BBC na filamu za National Geographic, atahukumiwa baadaye.
Wakati iliposikilizwa kesi yake Mahakama Kuu ya Eneo la Kaskazini (NT) siku ya Jumatatu, waendeshamashtaka waliwasilisha mashitaka dhidi yake.
Mengi ya maelezo ya uhalifu ya Bw Britton ni ya kuogofya na hayawezi kuchapishwa "ni ya kustaajabisha" hakimu alionya watu kuondoka kwenye chumba cha mahakama.
Jaji Mkuu Michael Grant alisema alikuwa na wasiwasi kusikia ukweli wa kesi hiyo kunaweza kusababisha "mshtuko wa neva", kabla ya kuchukua hatua adimu ya kuwaruhusu maafisa wa usalama na maafisa wadogo wa mahakama kuondoka mahakamani, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
Bw Britton alikuwa na "hasira mbaya ya kingono" kwa wanyama tangu mwaka 2014, waendesha mashtaka waliambia mahakama.
Licha ya kuwatumia vibaya mbwa wake kipenzi, aliwalaghai wamiliki wengine wa mbwa kumpa mbwa wao na kuwanyanyasa kingono.
Kati ya mbwa 42 aliowadhulumu katika muda wa miezi 18 kabla ya kukamatwa kwake, 39 walikufa.
Bw Britton amewekwa rumande tangu kukamatwa kwake na atarejea mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa kwa hukumu dhidi yake mwezi Desemba.
Mjukuu wa Nelson Mandela Zoleka afariki akiwa na umri wa miaka 43
Zoleka Mandela, mjukuu wa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Afrika Kusini Nelson Mandela, amefariki dunia kwa saratani akiwa na umri wa miaka 43, familia yake imetangaza.
Katika taarifa kwenye Instagram, msemaji alisema kuwa Zoleka aliaga dunia Jumatatu jioni akiwa amezungukwa na marafiki na familia.
Katika miaka ya hivi majuzi alijulikana sana kwa kuelezea matibabu yake ya saratani na pia kuwa wazi juu ya historia yake ya uraibu wa dawa za kulevya na mfadhaiko, na ukweli kwamba alidhulumiwa kingono akiwa mtoto.Aliandika hadithi yake katika tawasifu When Hope Whispers.
Zaidi ya muongo mmoja uliopita Zoleka alikuwa amegundulika kuwa na saratani ya matiti, alipata matibabu na alikuwa katika hali ya utulivu lakini baadaye ikarejea.
Mwaka jana, alithibitisha kuwa alikuwa na saratani kwenye ini na mapafu, kisha ikasambaa kwa viungo vingine.
Alikuwa akipokea matibabu na kulazwa hospitalini tarehe 18 Septemba."Nilifanyiwa uchunguzi wa CT scan wiki chache zilizopita, ambayo imeonyesha kuwa nina damu iliyoganda pamoja na uvimbe wa Fibrosis kwenye pafu langu. Hii inaelezea maumivu ya kifua niliyokuwa nikiyasikia.
Daktari wangu wa saratani amependekeza dawa za kupunguza damu na tiba ya mionzi ya saratani (chemotherapy) ya mdomo. upande wa juu, ninashukuru sana kwamba bado ninatibika," aliandika kwenye Instagram mnamo 17 Septemba.
Nissan kutumia umeme kufikia 2030 licha ya kucheleweshwa kwa marufuku ya petroli
Nissan itaharakisha mipango ya kusambaza umeme ikiahidi kwamba magari yote yanayouzwa barani Ulaya yatakuwa ya umeme ifikapo 2030.
Tangazo hilo linakuja licha ya Uingereza kuahirisha marufuku yake ya 2030 ya uuzaji wa magari mapya ya petroli na dizeli hadi 2035.
Mkuu wa kampuni ya Nissan Makoto Uchida alisema hatua ya kampuni hiyo "ni jambo sahihi kufanya".
Shirika la biashara ya magari SMMT limeelezea wasiwasi kuwa kuahirishwa kwa marufuku hiyo kutasababisha watumiaji kuchelewesha kubadili magari ya umeme.
Nissan pia itaanzisha teknolojia mpya ya betri mwishoni mwa muongo huo ambayo ilisema itapunguza muda wa malipo na gharama ya magari ya umeme (EVs).
Katika mahojiano na BBC, mkuu mtendaji wa Nissan Bw Uchida alisema kampuni hiyo inalenga kupunguza gharama ya magari yanayotumia umeme kwa wateja, ili yasiwe ghali zaidi kuliko magari ya petroli na dizeli.
Raia wa Marekani apigwa faini ya sh 500,000 za Tanzania kwa kupata kitambulisho cha Tanzania kinyume cha sheria
Raia mmoja wa Marekani ameagizwa – kulipa shilingi 500,000 au afungwe miezi sita baada ya kukiri kupata kitambulisho cha Tanzania (ID) kinyume cha sheria, limeripoti gazeti la The Citizen nchini humo.
Bw Yaki Lee, al maarufu Khalid Juma, alikiri makosa mengi katika mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, jijini Dar es salaam, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa zisizo sahihi na ukiukaji wa sheria ili kupata kitambulisho cha taifa cha Tanzania.
Baada ya kukiri mashtaka , Bw Lee alichagua kulipa faini ili kuepuka kifungo cha jela, na mahakama aliamuru arejeshwe nchini Marekani.
Unaweza pia kutazama:
Tazama Video: Ufilipino yaondoa kizuizi cha China katika eneo linalogombaniwa
Ufilipino inasema imeondoa kizuizi cha kuelea kilichowekwa na China ili kuzuia boti za uvuvi za Ufilipino kuingia katika eneo linalozozaniwa katika Bahari ya Kusini ya China.
Walinzi wa pwani ya Ufilipino walisema kuwa wameagizwa kufanya hivyo na Rais Ferdinand Marcos Junior.
Manila inasema China ilikiuka haki zake za uvuvi kwa kutumia kizuizi cha mita 300 (1,000ft) katika Scarborough Shoal.
Uchina inadai kumiliki zaidi ya 90% ya Bahari ya Uchina Kusini ambayo iliinyakuwa mwaka 2012.
Mtu wa tatu akamatwa New York kufutia kifo cha mtoto wa chekechea kilichohusishwa na mihadarati
Polisi wamemkamata mwanamume anayedaiwa kusaidia kusambaza dawa za kulevya zilizopatikana katika kitalu cha New York ambapo mtoto wa mwaka mmoja alikufa baada ya kuathiriwa na mihadarati aina ya fentanyl.
Renny Antonio Parra Paredes, mwenye umri wa miaka 38, ni mtu wa tatu kukamatwa kufuatia kifo cha Nicholas Dominici mwezi huu.
Kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kilipatikana katika msako uliofanyika kwenye kituo cha chekechea cha Bronx.
Mnamo Jumatatu maafisa walisema walipata mihuri wakati wa upekuzi katika nyumba ya mshukiwa ambayo ilitumiwa kuweka alama za vifurushi vya dawa za kulevya.
Bw Paredes anashtakiwa kwa kula njama ya kusambaza mihadarati na kusababisha kifo.
Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DEA) inasema kuwa Bw Paredes alitekeleza jukumu muhimu katika oparesheni inayodaiwa kuwa ya ulanguzi wa dawa za kulevya uliofanyika katika kituo cha kulelea watoto cha Divino Niño.
Polisi waliitwa katika kituo hicho mnamo tarehe 15 Septemba kwa tuhuma za matumizi ya dawa za kulevya.
Watoto wanne waligundulika kuumwa kutokana na dawa hizo, ambazo zilikuwa zimehifadhiwa karibu na mahali walipolala.
Mtoto Nicholas Dominici alikufariki baadaye.