Ujumbe wa Kenya wakutana na polisi wa Haiti kutathmini usalama
Ujumbe wa Kenya umefanya mikutano na maafisa wa polisi wa Haiti, wiki kadhaa baada ya serikali ya Kenya kujitolea kuongoza timu ya kimataifa katika kukabiliana na ghasia kali za magenge nchini humo.
Haiti imekumbwa na ghasia mbaya tangu kuuawa kwa Rais wa nchi hiyo Jovenel Moïse miaka miwili iliyopita.
Ghasia hizo zimeongezeka tangu Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry alipoomba msaada kwa mara ya kwanza Oktoba mwaka jana, na kusababisha Marekani kuwahamisha wafanyakazi wake wa kidiplomasia.
Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulisema kuwa zaidi ya watu 2,439 waliuawa, 902 walijeruhiwa na 951 kutekwa nyara katika nusu ya kwanza ya Januari.
Ujumbe wa Kenya uliwasili katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, Jumapili na unatarajiwa kuondoka Jumatano, baada ya majadiliano zaidi na waziri mkuu.
Umepewa jukumu la kutathmini hali nchini, ambayo itaarifu juhudi za kuingilia kati zinazoungwa mkono na UN na Marekani. Kenya pia inatarajiwa kuongoza juhudi za kukabiliana na hali hiyo kwa kutuma maafisa 1,000 wa polisi nchini Haiti.
Nchi za Caribbean kama Jamaica, Bahamas, Antigua na Barbuda na Trinidad na Tobago pia zimeahidi kutuma vikosi vyake kusaidia polisi wa Haiti.