Serikali
ya Rwanda kupitia msemaji wake, Yolande Makolo, imetangaza kwamba uamuzi
wa Mahakama ya Rufaa ya mahakama ya kimataifa kusitisha kesi ya Kabuga
Félicien, ni wa kusikitisha kwa waathiriwa wa mauaji ya kimbari dhidi ya
Watutsi, lakini kwamba Rwanda inaheshimu uamuzi huo.
Wakati
huo huo mwendeshamashtaka wa mahakama hiyo Serge Brammertz naye amesema
kwamba uamuzi wa mahakama ya rufaa lazima uheshimiwe, hata ikiwa
matokeo hayaridhishi.
Msemaji
wa serikali ya Rwanda,Yolande Makolo ameviambia vyombo vya habari mjini Kigali
kwamba Rwanda inaheshimu uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Rufaa wa kusimamisha
kwa muda usiojulikana kesi ya mshukiwa mkuu wa mauaji ya kimbari Felicien
Kabuga akisisitiza kwamba, sio jambo la kufurahisha kwa manusura wa
mauaji hayo na kusema kwamba ‘’kwa vyovyote vile Kabuga bado
ni mshukiwa wa uhalifu mkubwa."
Awali
jumuiya ya manusura wa mauaji ya kimbari IBUKA ilitangaza kusikitishwa na
uamuzi huo wa mahakama ya rufaa kuamuru Kabuga aachiliwe huru.
Jumuiya
hiyo imelaani ilichokitaja kuwa ‘’aibu kwa sheria ‘’ya kimataifa na
kutowatendea haki manusura wa mauaji ya kimbari na kuiomba serikali ya Rwanda
kusitisha ushirikiano na mahakama hiyo.
Mwezi
Juni, majaji katika mahakama ya uhalifu wa kivita ya Umoja wa Mataifa waliamua
kuwa Bw Kabuga hafai kufikishwa mahakamani kutokana na ugonjwa wa akili lakini
walipendekeza taratibu mbadala zifanyike. Kwa sasa majaji wa rufaa wamekataa
pendekezo hilo.
Kwa
upande mwingine ,mwendeshamashtaka wa mahakama hiyo ya kimataifa Bwana Serge
Brammertz kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema matokeo hayo yanatokana
kwanza kabisa na Kabuga kukwepa mkono wa sheria kwa miaka
mingi.
Alisema
Kabuga akiwa na ufahamu kamili wa hatua zake kabla na wakati wa Mauaji ya
Kimbari ya 1994, alikataa kushitakiwa mbele ya mahakama ya kimataifa iliyo huru na isiyopendelea upande kujibu mashtaka dhidi yake.
Ameongeza
kwamba baada ya kupitia kwa makini uamuzi wa chumba cha rufaa
,’’ni lazima uamuzi huo uheshimiwe, hata ikiwa matokeo
hayaridhishi’’.
‘’Uamuzi
huu unaweza kuwa wa kukatisha tamaa, lakini ninaweza kuwahakikishia waathiriwa
kwamba sio mwisho wa mchakato wa haki’’. Brammertz alisema.
- Mauaji ya Rwanda: Jinsi Felicien Kabuga alivyojificha kwa miaka 26
- Félicien Kabuga: 'Huo wote ni uongo, sikumuua Mtutsi yeyote'
- Félicien Kabuga: Mshukiwa mkuu wa mauaji ya kimbari Rwanda akamatwa