Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kifo cha mvulana wa Kifaransa-Algeria 'wakati wa kukabiliana na ubaguzi wa rangi' - UN
Ufaransa inapinga madai ya ubaguzi wa rangi miongoni mwa polisi wake, wizara ya mambo ya nje imesema katika taarifa yake.
Moja kwa moja
Habari za hivi punde, Brazil: Bolsonaro apigwa marufuku ya kuwania urais kwa miaka minane
Mahakama ya Juu Zaidi ya Uchaguzi nchini Brazil imepiga kura kumzuia aliyekuwa rais wa nchi hiyo Jair Bolsonaro kuwania kiti hicho kwa miaka minane.
Bw Bolsonaro alipatikana na hatia ya kutumia mamlaka yake vibaya kabla ya uchaguzi wa urais wa mwaka jana.
Alikuwa ameshutumiwa kwa kuhujumu demokrasia ya Brazil kwa kudai kwamba mfumo wa kielektroniki uliyotumiwa ungeweza kudukuliwa na ulaghai.
Mawakili wa Bw Bolsonaro wanatarajiwa kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Wamesema kuwa kauli zake hazikuwa na uhusiano wowote na matokeo ya uchaguzi.
Macron awashutumu waandamanaji kutumia vibaya kifo cha kijana aliyeuawa na polisi
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amewashutumu waandamanaji kwa kutumia vibaya kifo cha kijana aliyeuawa risasi na polisi.
Katika mkutano wa dharura wa kushughulikia ghasia hizo, Bw. Macron alisema maafisa zaidi watatolewa ili kudhibiti hali, lakini hakutangaza hali ya dharura.
Aliwataka wazazi kuwasihi watoto kusalia majumbani na kutoka kwenye mitandao ya kijamii ili kuondoa baadhi ya maudhui.
Ufaransa imekumbwa na machafuko ya siku tatu baada ya Nahel M, 17, kuuawa alipokuwa akiendesha gari kutoka kituo cha ukaguzi wa barabarani.
Wakati huo huo Serikali ya Ufaransa imepinga kauli ya awali ya Umoja wa Mataifa kuhusu ubaguzi wa rangi miongoni mwa polisi wake, wizara ya mambo ya nje imesema katika taarifa yake.
"Mashtaka yoyote ya ubaguzi wa rangi au ubaguzi wa kimfumo katika jeshi la polisi nchini Ufaransa hayana msingi kabisa," ilisema katika taarifa hiyo.
"Utekelezaji wa sheria nchini Ufaransa uko chini ya kiwango cha udhibiti wa ndani, nje na mahakama sawa na nchi zingine chache zinavyofanya.
Ufaransa, na vikosi vyake vya polisi, vinapambana kwa nia moja dhidi ya ubaguzi wa rangi na aina zingine zote za ubaguzi," iliongeza taarifa hiyo.
Tunakufa kwa njaa gizani - afisa wa Tigray
Katika muda wa miezi miwili tangu Marekani na Umoja wa Mataifa kusimamisha msaada wa chakula kwa eneo la Tigray lililoathiriwa na vita nchini Ethiopia, takriban watu 728 wamefariki dunia, kulingana na mamlaka ya eneo hilo.
Wengi wa waliokufa walikuwa watoto, akina mama wajawazito, na watu waliokuwa na hali za kiafya, anasema Gebrehiwot Gebregziaher wa Tume ya Kudhibiti Hatari ya Majanga katika jimbo la Tigray.
Anasema kwamba ingawa USAid na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) walisimamisha rasmi msaada mwezi Aprili - baada ya kugundua shehena zilikuwa zikiibiwa na kuuzwa - kwa kweli watu wengi wa Tigray walikuwa hawana msaada kwa muda mrefu zaidi.
Watu wanahisi "wanakufa kwa njaa gizani ingawa inatangazwa kwa ulimwengu [kwamba] amani inastawi," alisema Dk Gebrehiwot, akimaanisha makubaliano ya amani yaliyofanywa mjini Pretoria Novemba mwaka jana kati ya serikali ya Ethiopia na waasi wa TPLF baada ya miaka miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Kifo cha mvulana wa Kifaransa-Algeria 'wakati wa kukabiliana na ubaguzi wa rangi' - UN
Umoja wa Mataifa umeitaka Ufaransa "kushughulikia masuala mazito ya ubaguzi wa rangi" katika utekelezaji wa sheria, baada ya polisi kumpiga risasi mvulana wa miaka 17 kutoka familia ya Algeria.
Nahel M, kijana aliuawa katika kituo cha trafiki katika kitongoji cha Paris siku tatu zilizopita.
Rais Macron sasa anaongoza mkutano wa dharura kuhusu ghasia zilizoikumba Ufaransa tangu wakati huo, na kuacha msururu wa majengo yanayoteketea, magari yanayofuka moshi na kuporwa kwa majengo ya umma.
Serikali ya Ufaransa inasema inafanya kila iwezalo kurejesha utulivu.
Miji mitatu mikubwa nchini humo - Paris, Marseille na Lyon - inasimamisha au kuzuia usafiri wa umma kuanzia Ijumaa jioni.
Takriban watu 900 wamekamatwa huku maafisa 250 wa polisi wakijeruhiwa.
Machafuko pia yameshuhudiwa katika eneo la Bahari ya Hindi la Ufaransa la Réunion.
Naomi Campbell apata mtoto wa pili, akiwa miaka 53
Mwanamitindo maarufu duniani Naomi Campbell amekuwa mama kwa mara ya pili, akiwa na umri wa miaka 53.
Nyota huyo ambaye alimkaribisha mtoto wake wa kwanza miaka miwili iliyopita, alitangaza kuwasili kwa mtoto wake mtandaoni siku ya Alhamisi, na kuwaambia wafuasi wake "hatujachelewa".
Hakuwa ameweka wazi kama anatarajia kupata mtoto wa pili na hakutoa maelezo zaidi kuhusu kuzaliwa kwake.
Mwanamitindo huyo wa Uingereza alisema kupita Instagram kuwa hii ni "zawadi ya kweli kutoka kwa Mungu".
"Zawadi ya Kweli kutoka kwa Mungu, barikiwa! Karibu Babyboy. #mumoftwo."
Campbell aliwahi kupamba vichwa vya habari kama hivyo mwaka 2021 alipotangaza kuwasili kwa mtoto wake wa kwanza wa kike kupitia Instagram.
Mcheza tenisi wa Afrika Kusini ataka Wimbledon iombe radhi baada ya miaka 52
Mchezaji nyota wa tenisi wa Afrika Kusini ambaye alizuiwa kushiriki mashindano ya Wimbledon katika miaka ya 1970 ameomba msamaha wa umma kutoka kwa waandaaji wake na bodi inayosimamia mchezo wa kimataifa.
Hoosen Bobat alikuwa amefurahishwa na kufuzu kwa mashindano ya vijana mwaka 1971 wakati ambapo ubaguzi wa rangi ulikuwa katika kilele chake - lakini baadaye mwaliko huo ukabatilishwa wiki moja tu kabla ya tukio hilo.
"Baada ya miaka yote hiyo ya mazoezi na kujiandaa, nilipata fursa ya kucheza katika hatua kubwa zaidi duniani.
Kushiriki kwangu kulipokubaliwa - kulikuwa na mhemko kubwa barani Afrika miongoni mwa wachezaji weusi... Ingekuwa hatua kubwa ya maisha yangu ya baadaye ya mchezo wa tenisi," aliambia BBC Newsday.
Anaamini kuwa sababu halisi ya yeye kuzuiwa ni ya ubaguzi wa rangi.
Serikali ya Uingereza wakati huo iliunga mkono utawala wa ubaguzi wa rangi ingawa upinzani wa kimataifa dhidi yake ulikuwa ukiongezeka.
Kwa wakati huo nchini Afrika Kusini wachezaji waafrika hawakuruhusiwa kucheza na wenzao wa kizungu, na anasema mechi katika vituo vya tenisi vya wazungu peke yao zilitazamwa kutoka kwa sehemu zilizofungwa.
Wiki hii wabunge wawili wa Uingereza na maveterani waliopinga ubaguzi wa rangi - Peter Hain na Jeremy Corbyn - waliibua suala hilo bungeni na kuunga mkono matakwa ya Bw Bobat ya kuombwa msamaha.
Waandalizi wa Wimbledon AELTC, na bodi ya kimataifa ya tenisi inayoongoza ITF, wanasema wanapitia taarifa hizo
Bw Bobat anasema mchezo huo bado una safari ndefu nchini Afrika Kusini, akiambia The Guardian: "Hata sasa, hakuna kilichobadilika. Kuna Waafrika wachache - ambao tunawafafanua kama Wahindi- wachezaji wa tenisi wa sasa kuliko wakati huo.
Mkuu wa kutetea haki wa UN aitaka Uingereza kuachana na mpango wa uhamiaji wa Rwanda
Kamishna wa kutetea haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ameitaka serikali ya Uingereza kufikiria upya sera yake iliyopendekezwa ya kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda.
Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa Mahakama ya Rufaa huko London suku ya Alhamisi kwamba sera hiyo ni kinyume cha sheria.
Türk alisema mipango ya Uingereza imeibua wasiwasi mkubwa sana katika suala la sheria za kimataifa za haki za binadamu na wakimbizi.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi la (UNHCR)pia limekaribisha uamuzi wa mahakama, likisema Uingereza inapaswa kufuata hatua nyingine, ikiwa ni pamoja na ushirikiano na majirani zake wa Ulaya.
Serikali ya Uingereza inapanga kukata rufaa zaidi, ikisema kuwa imedhamiria kusitisha kuwasili kwa wahamiaji kwenye boti ndogo.
Maelezo zaidi:
Je, hali ya dharura itatangazwa nchini Ufaransa?
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatarajiwa kukutana na baraza lake la mawaziri kwa mara ya pili kufuatia ghasia na maandamano yanayoendelea kote nchini.
Haya yanajiri huku wanasiasa wa mrengo wa kulia na wale wa siasa kali za mrengo wa kulia wakitaka hali ya dharura itangazwe.
Hatua hiyo inatoa mamlaka maalum kwa serikali wakati taasisi za nchi zinachukuliwa kuwa "tishio".
Inaruhusu serikali kutekeleza amri ya kutotoka nje na kupiga marufuku mikusanyiko na hafla za umma.
Uharibifu mkubwa ulionekana kote nchini Ufaransa asubuhi ya leo huenda ukaongeza wito wa utekelezaji wake.
Makamu wa Rais wa Seneti Roger Karoutchi tayari ametuma ujumbe kwenye Twitter na kusema kwamba kutotangaza hali ya dharura itakuwa "kosa".
Lakini serikali ya Ufaransa inaweza kusita kuchukua hatua hiyo ambayo ni nadra sana.
Hali ya ya dharura ilitangazwa na rais wa wakati huo Jacques Chirac wakati wa ghasia za banlieue za 2005.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza hatua hiyo kuchukuliwa katika miaka 50.
Miaka kumi baadaye, serikali ya Ufaransa ilitangaza hali ya hatari kufuatia mashambulizi ya kigaidi ya 2015 Paris.
Hatua hiyo ilidumu miaka miwili. Jana, mawaziri mbalimbali wa serikali walisema hali ya hatari haizingatiwi.
Rais Ruto, naibu wake na wabunge kuongezwa mishahara - SRC
Maafisa wa serikali, akiwemo Rais, Naibu Rais, Makatibu wa Baraza la Mawaziri na Wabunge, wamepangiwa nyongeza ya mishahara ya asilimia 14 kwa wastani katika kipindi cha miaka miwili ijayo kuanzia mwezi ujao katika ukaguzi uliopendekezwa na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) ili kuwanusuru dhidi ya kupanda kwa gharama za maisha.
Ikiidhinishwa, maafisa watafurahia ahueni kubwa kutokana na athari za mfumuko wa bei unaoendelea ambao umeathiri mapato ya kibinafsi huku gharama ya bidhaa za muhimu zikipanda.
Kulingana na gazeti la Busines Daily, badala yake, wafanyikazi wanaolipwa mishahara, wafanyikazi wa muda na wafanyikazi katika sekta isiyo rasmi wataendelea kujikuta katika hali mbaya zaidi katika mazingira ya mfumuko wa bei.
Malipo ya jumla ya kila mwezi ya Rais William Ruto yatapanda kwa asilimia 7.1 kuanzia Julai 2023 hadi Sh1,546,875 kutoka Sh1,443,750 kwa sasa kabla ya kupanda kwa asilimia 6.7 hadi Sh1,650,000 kuanzia Julai 2024.
Malipo ya Makatibu wa Baraza la Mawaziri yanapanda kwa kiasi sawa na hicho, hadi Sh1,056,000 kwa mwezi kuanzia Julai 1, 2024 kutoka Sh924,000 kwa sasa.
Wabunge, wakiwemo maseneta, watapata Sh741,003 na Sh769,201 katika miaka miwili ijayo ya kifedha mtawalia kutoka Sh710,000 kwa sasa, ikiwa ni nyongeza ya asilimia 8.3 ya nyongeza ya mishahara katika kipindi hicho.
Kifurushi kilichorekebishwa cha mishahara kwa wabunge na maseneta hata hivyo hakijumuishi marupurupu ya vikao vya kamati ambayo ni kikomo cha Sh120,000 kwa mwezi.
Katika kaunti, magavana watapokea nyongeza ya Sh1,056,000 kufikia Julai 2024 kutoka kwa malipo ya sasa ya kila mwezi ya Sh924,000.
Bei mpya ya mafuta Kenya kutangazwa leo - EPRA
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA) nchini Kenya itatangaza hii leo bei mpya za mafuta.
Bei hizo mpya zinatokana na Kodi mpya ya Ongezeko la Thamani kwenye bidhaa za petroli, ambayo sasa itakuwa asilimia 16, kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Fedha, 2023.
"Mnamo tarehe 26 Juni 2023, Rais Dkt William Ruto alitia saini kuwa sheria Mswada wa Fedha wa 2023 wa kuwasilisha VAT ya asilimia 16 kwa bidhaa za petroli. Kwa hivyo, @EPRA_ leo tarehe 30 Juni 2023 itatoa bei iliyopitiwa ya mafuta ya petroli kulingana na mswada wa fedha wa 2023. ," EPRA ilisema katika notisi.
Hapo awali, bidhaa za Petroli zilitozwa asilimia 8 ya VAT.
Haya yanajiri takriban wiki mbili baada ya EPRA kutangaza bei mpya za mafuta kwa mwezi wa Juni-Julai. Mabadiliko ya bei yangeanza Juni 15 hadi Julai 14, 2023.
Mnamo Juni 14, Mamlaka ilitangaza kuwa bei ya petroli ilipungua kwa Sh0.66 hadi rejareja kwa Sh182.04, huku dizeli ikipunguzwa kwa Sh1.12 hadi 167.28 jijini Nairobi.
Hata hivyo, bei ya mafuta ya taa iliongezwa kwa Sh0.35 hadi rejareja kwa Sh161.48.
Huku kiwango kipya cha VAT kikianza kutekelezwa, bei ya petroli huenda ikauzwa kwa Sh196.60 jijini Nairobi, dizeli Sh180.66, na Mafuta ya taa kwa Sh174.39.
Tanzania yaondoa marufuku ya kusafiri kwa mabasi ya usiku baada ya miongo kadhaa
Tanzania imeondoa marufuku ya usafiri wa mabasi yaendayo usiku ambayo iliwekwa miongo kadhaa iliyopita.
Serikali inasema mabadiliko hayo yamekuja baada ya kuzingatia maoni ya wadau wa sekta ya usafiri, pamoja na uboreshaji wa miundombinu na usalama.
Wakati akitangaza hatua hiyo bungeni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema zuio hilo liliwekwa miaka ya 1990 kufuatia kuongezeka kwa ajali za barabarani na utekaji wa mabasi.
Sasa ameziagiza mamlaka husika kufanya kazi ya “kuweka utaratibu utakaofuatwa na wamiliki na madereva wa mabasi ya abiria wanaokusudia kusafirisha abiria usiku”.
Kuondolewa kwa marufuku hiyo inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta ya usafiri, kumepokelewa kwa shangwe na chama cha wamiliki wa mabasi Tanzania.
Trump asema jaribio la uasi wa Wagner 'limemdhoofisha' Putin
Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, ambaye kwa muda mrefu amekua akivutiwa na rais wa Urusi Vladimir Putin, alisema Alhamisi kwamba Putin "amedhoofishwa kwa kiasi fulani" na uasi uliokomeshwa na kwamba sasa ni wakati wa Marekani kujaribu kufanya makubaliano ya amani kati ya Urusi na Ukraine.
"Nataka watu waache kufa kutokana na vita hivi vya kipuuzi," Trump aliambia Reuters katika mahojiano ya simu.
Kuhusu Ukraine, Trump hakuondoa kwamba serikali ya Kyiv inaweza kulazimika kutoa eneo fulani kwa Urusi ili kusitisha vita, vilivyoanza na vikosi vya Urusi kuivamia Ukraine miezi 16 iliyopita.
Alisema kila kitu kitakuwa "chini ya mazungumzo", ikiwa angekuwa rais, lakini kwamba Waukraine ambao wamepigana vikali kutetea ardhi yao "wamepata sifa nyingi." "Nadhani watakuwa na haki ya kuhifadhi mengi ya waliyochuma na nadhani Urusi vile vile ingekubali hilo. Unahitaji mpatanishi sahihi, na hatuna hiyo hivi sasa," alisema.
Akiwa rais, Trump aliendeleza uhusiano wa kirafiki na Putin, ambaye Biden alisema Jumatano "amekuwa mtu wa kutengwa duniani kote" kwa kuivamia Ukraine.
Trump alisema Putin aliharibiwa na uasi wa jeshi la mamluki la Urusi, Kundi la Wagner na kiongozi wake Yevgeny Prigozhin, wikendi iliyopita.
"Unaweza kusema kwamba yeye (Putin) bado yuko, bado ana nguvu, lakini hakika amekuwa naweza kusema amedhoofika angalau katika akili za watu wengi," alisema.
Mkoba 'mdogo kuliko chembe ya chumvi' wauzwa kwa $63,750
Mkoba wa hadubini "mdogo kuliko chembe ya chumvi" umeuzwa kwa $63,750 (£50,569) katika mnada.
Hadubini inahitajika ili kuona muundo wa mfuko, na kitu kidogo cha kupima mikromita 657 x 222 x 700.
"Nyembamba na inaweza kutosha kupita kwenye tundu la sindano, huu ni mkoba mdogo sana utahitaji darubini kuuona," kikundi cha sanaa nyuma ya begi kilisema.
Sanaa ya pamoja MSCHF, iliyoko Brooklyn, inajulikana kwa miundo yake yenye utata.
Ni pamoja na viatu vilivyo na damu ya binadamu na buti kubwa nyekundu za mpira.
Wakati huu, iliamua kuchukua mwenendo wa mikoba mdogo zaidi. "Kuna mikoba mikubwa, mikoba ya kawaida na mikoba midogo, lakini hili ndilo neno la mwisho katika uboreshaji wa begi," MSCHF ilisema kwenye chapisho kuhusu begi hilo.
Begi hilo lina chapa ya mbunifu wa mikoba ya kifahari Louis Vuitton, lakini haina uhusiano na chapa hiyo. Imetengenezwa kwa resin ya photopolymer na iliundwa kwa kutumia teknolojia ya uchapishaji ya 3D ambayo mara nyingi hutumiwa kutengeneza mifano na miundo midogo ya mitambo.
Ilipokuwa ikiundwa, baadhi ya sampuli za mifuko midogo zilizotumwa kukaguliwa na chapa hiyo zilikuwa ndogo sana hivi kwamba zilipotea na timu ya MSCHF, gazeti la Smithsonian linaripoti.
Lakini hasara ya kipengee haipaswi kuwa na wasiwasi mdogo kwa mmiliki wa mfuko mpya, kwani darubini yenye onyesho la dijitali ilijumuishwa katika ununuzi.
Hadubini zenye maonyesho ya dijiti zinaweza kununuliwa kutoka kwa wauzaji reja reja mtandaoni na zinaweza kuanzia bei ya $60 hadi maelfu ya dola.
Tovuti ya mnada haikuorodhesha bei ya darubini kando na begi. Zabuni za bidhaa zilianza kwa $15,000. Akizungumzia kuhusu matumizi ya chapa ya Louis Vuitton kwenye begi, afisa mkuu wa ubunifu wa MSCHF, Kevin Wiesner, aliliambia gazeti la New York Times mapema mwezi huu kwamba kundi hilo halijaomba ruhusa kutoka kwa kampuni hiyo kuitumia.
Jihadhari na Sprite 'yenye uchafu', yasema Nigeria
Raia wa Nigeria wanaonywa kuwa baadhi ya chupa za Sprite ni chafu.
"Chembe chembe" zimepatikana katika kreti tano za kinywaji hicho katika maduka na kituo cha uzalishaji, kwa mujibu wa Shirika la Kitaifa la Kudhibiti Chakula na Dawa.
Haijulikani ni chembe gani hizo, lakini mamlaka inasema ni chupa ya Sprite yenye ukubwa wa 50cl haswa ambayo imeathirika.
Wateja wengine mtandaoni wanasema tangazo hilo halieleweki sana na wanadai maelezo zaidi.
Ghasia zazuka nchini Ufaransa huku polisi aliyemuua kijana akiomba msamaha
Polisi aliyempiga risasi Nahel Jumanne asubuhi ameomba msamaha kwa familia yake akiwa kizuizini.
Wakili wake Laurent-Franck Liénard alisema "amefadhaika" na "haamki asubuhi kuua watu".
"Maneno ya kwanza aliyotamka yalikuwa ya kusema pole na maneno ya mwisho aliyosema yalikuwa ya kuomba pole kwa familia."
Pia alisema afisa huyo, ambaye ameshtakiwa kwa mauaji ya hiari, "alishtushwa na vurugu za video hii".
Kanda za video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha watu waliofanya ghasia mapema leo usiku wakiingia kwenye maduka kando ya Rue de Rivoli katikati mwa Paris.
Ofisi ya waziri wa mambo ya ndani inasema takriban watu 421 wamekamatwa kote nchini.
Wengi wa waliokamatwa walikuwa na umri wa kati ya miaka 14 na 18.
Natumai hujambo