Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Dhehebu la kufunga hadi kufa Kenya: Watoto ndio waliolengwa kufa kwanza - mhubiri msaidizi wa zamani

Watoto walikuwa wakilengwa kuwa wa kwanza kufa kwa njaa katika siku za mwisho za ibada ya siku ya maangamizi iliyoendeshwa na kanisa moja dhehebu la kikiristo linaloamini kufunga hadi kufariki dunia huko nchini Kenya, kulingana na ushahidi mpya unaoibuka.

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri

  2. Ni nani atakayekuwa rais nchini Uturuki?

    Shughuli ya upigaji kura ilikamilika na vituo vya kupiga kura kufungwa huku uhesabu wa kura ukiendelea katika uchaguzi wa rais na wabunge nchini Uturuki.

    Nani amesalia katika kinyang'anyiro cha kuwa rais wa Uturuki?

    Recep Tayyip Erdogan: Rais wa sasa wa Uturuki aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka wa 2003 kama waziri mkuu kufuatia ushindi mkubwa wa chama cha Haki na Maendeleo (AKP) chenye mizizi ya Kiislamu. Alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 11 kabla ya kuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo kuchaguliwa moja kwa moja mwaka wa 2014.

    Kemal Kilicdaroglu: Mgombea wa umoja wa upinzani anawakilisha vyama sita vya upinzani ambavyo vimeungana kwa ajili ya uchaguzi wa rais na wabunge. Kilicdaroglu amekuwa mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Uturuki, Republican People's Party (CHP), tangu 2010.

    Sinan Ogan: Mzalendo wa hali ya juu ana nafasi ndogo ya kupata mafanikio makubwa. Ogan, na pia vile vile, ana nafasi ya kuweka historia.

    Masuala muhimu katika uchaguzi

    Gharama ya maisha inaonekana kama suala kuu la uchaguzi huu.

    Kodi katika miji mikubwa iliongezeka mara tatu kwa mwaka na mfumuko wa bei umefikia kiwango cha juu zaidi tangu 1998, huku gharama ya nishati, vyakula vya msingi na usafiri ikiongezeka zaidi.

    Mamilioni ya Waturuki bado wanalazimika kukabiliana na athari za matetemeko makubwa ya ardhi ya tarehe 6 Februari, ambayo yaliathiri miji 11 na kusababisha makumi ya maelfu ya watu kufariki dunia.

    Serikali imekosolewa kwa kucheleweshwa operesheni ya uokoaji kufuatia tetemeko hilo - ambalo Rais Erdogan aliomba radhi baadaye.

    Serikali imeongeza matumizi ya fedha za umma, ikiahidi malipo ya juu ya uzeeni, ufadhili mkubwa wa masomo kwa wanafunzi, baadhi ya usaidizi wa bili za nishati na upatikanaji mkubwa wa rehani za riba nafuu.

    Lakini Waturuki wengi wanavutiwa na ahadi za upinzani za kupunguza mamlaka ya rais Erdogan, aliyepigiwa kura kidogo mwaka 2017, na kurejea kwa mfumo wa bunge.

    Suala jingine kwa wapiga kura ni jinsi serikali inavyoshughulikia ukosoaji kwenye mitandao ya kijamii. Kulingana na data ya wizara ya sheria, takriban watu 50,000 wameshtakiwa kwa "kumchafulia jina rais" tangu Erdogan aanze kazi mnamo 2014.

    soma zaidi:

  3. Bobi, mbwa mzee zaidi duniani, asherehekea miaka 31 ya kuzaliwa

    Bobi, mbwa wa Kireno ambaye alitangazwa kuwa mbwa mzee zaidi duniani na Guinness World Records mwezi Februari, amesherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 31 siku ya Alhamisi, kulingana na taarifa ya habari kutoka Guinness.

    Familia ya Bobi ilipanga sherehe ya siku ya kuzaliwa Jumamosi nyumbani kwake huko Conqueiros, kijiji cha mashambani kusini mwa Ureno.

    Mmiliki wake, Leonel Costa, aliiambia Guinness kwamba itakuwa sherehe "ya kitamaduni" ya Ureno.

    Zaidi ya watu 100 walihudhuria sherehe hiyo na kikundi cha densi kikatumbuiza, kulingana na taarifa ya habari.

    Costa aliiambia Guinness kwamba Bobi amekuwa akifurahia uangalizi kutoka kila pembe tangu kutawazwa kuwa mbwa mzee zaidi duniani.

    "Tumekuwa na waandishi wa habari wengi na watu wanakuja kutoka duniani kote kupiga picha na Bobi," alisema katika toleo hilo.

  4. Dhehebu la kufunga hadi kufa Kenya: Watoto ndio waliolengwa kufa kwanza - mhubiri msaidizi wa zamani

    Watoto walikuwa wakilengwa kuwa wa kwanza kufa kwa njaa katika siku za mwisho za ibada ya siku ya maangamizi iliyoendeshwa na kanisa moja dhehebu la kikiristo linaloamini kufunga hadi kufariki dunia huko nchini Kenya, kulingana na ushahidi mpya unaoibuka.

    Polisi wanaochunguza kesi inayoonekana kuwa kujitoa mhanga hadi sasa wamefukua miili 201 katika msitu ulioko kusini mashariki mwa taifa hilo.

    Mhubiri msaidizi wa zamani wa ibada hiyo aliliambia gazeti la New York Times kwamba watoto waliuawa kwanza, na kuamriwa "kufunga kwenye jua ili wafe haraka."

    Wanawake na wanaume walikuwa wakifuatia kwa utaratibu huo katika mpango wa kujiua, Titus Katana alisema.

    Bw Katana - ambaye anawasaidia polisi katika uchunguzi - pia alielezea kwa Sunday Times madai ya kutendewa ukatili watoto hao, akisema walifungiwa kwenye vibanda kwa siku tano bila chakula wala maji.

    “Kisha wakawafunga blanketi na kuwazika, hata wale ambao bado wanapumua,” alinukuliwa akisema.

    Inadaiwa kuwa wafuasi wa dhehebu hilo waliambiwa wangefika mbinguni haraka ikiwa wangekufa kwa njaa.

    Uchunguzi rasmi wa baadhi ya miili katika shamba kubwa la Shakahola, karibu na mji wa pwani wa Malindi, ulibaini dalili za njaa, kukosa hewa na kupigwa.

    Zaidi ya watu 600 wanaoripotiwa kuwa washiriki wa ibada ya siku ya maangamizi inayodaiwa kuongozwa na Mchungaji Paul Mackenzie bado hawajulikani walipo.

    Mchungaji Mackenzie, ambaye kwa sasa yuko chini ya ulinzi wa polisi, alisema alifunga Kanisa lake la Good News International miaka minne iliyopita baada ya takriban miongo miwili ya operesheni.

    Lakini BBC ilikuwa imefichua mamia ya mahubiri yake ambayo bado yanapatikana mtandaoni, ambayo baadhi yake yalionekana yalirekodiwa baada ya tarehe hii.

    Katika mahojiano na gazeti la Daily Nation la Kenya wiki chache zilizopita, Mchungaji Mackenzie pia alikanusha kuwa aliwalazimisha wafuasi wake kujilaza kwa njaa.

    Lakini Mchungaji Mackenzie alihubiri dhidi ya elimu, akisema kwamba ilikuwa ya kishetani, baada ya kupokea "ufunuo kutoka kwa Mungu", Bw Katana aliambia New York Times.

    Akieleza sababu zake za kuacha dhehebu hilo, Bw Katana, ambaye pia anasaidia katika uchunguzi wa polisi dhidi ya mchungaji huyo, alisema mafundisho yake yamekuwa ya "ajabu sana".

    Mchungaji Mackenzie pia aliwahimiza akina mama kuepuka kutafuta matibabu wakati wa kujifungua na kutowachanja watoto wao.

    Mengi ya mahubiri ya Mchungaji Mackenzie yanahusiana na utimizo wa unabii wa Biblia kuhusu Siku ya Hukumu.

    Soma zaidi:

  5. Kenya: Wafugaji waua simba 6 waliopotea katika Hifadhi baada ya 'usiku wa hofu'

    Wafugaji wenye hasira wamewaua simba sita katika Kaunti ya Kajiado Kusini Jumamosi asubuhi, kufuatia shambulio la simba katika kijiji jirani cha Nashipa.

    Ripoti zilionyesha kuwa simba 11 - watu wazima 10 na mtoto - walitangatanga katika kijiji hicho Ijumaa usiku kutoka Hifadhi ya Kitaifa ya Amboseli, kutafuta chakula.

    Walishambulia nyumba moja na kuua kondoo 11 na mbwa katika kile ambacho wakazi walielezea kuwa usiku wa hofu.

    "Juhudi za mwenye nyumba kuwatisha hazikufua dafu. Wanyama hao [ambao waliuawa] ndio waliokuwa wenye bahati kwani walinusurika ukame wa hivi majuzi," alisema mwanakijiji ambaye hakutaka jina lake litajwe.

    Jumamosi asubuhi, makumi ya wenyeji waliokuwa wamejihami kwa mikuki waliwasaka simba hao na kuwaua sita kati yao.

    Mizoga mingi ilikuwa na mishale na mikuki ndani yake.

    Simba hao waliuawa katika makao makuu ya Big Life Foundation ndani ya hifadhi ya kibinafsi inayopakana na mbuga ya Amboseli.

    Walirudi kwenye eneo hilo baada ya kutangatanga kijijini.

    Kwa muda wote wa Jumamosi mchana, maafisa kutoka Huduma ya Wanyamapori ya Kenya, utawala wa ndani na Big Life, pamoja na washikadau wengine walikuwa kwenye mkutano wa dharura katika makao makuu ya taasisi hiyo.

    Kulingana na gazeti la Daily Nation, Jitihada za kumpata msemaji wa KWS Teresia Igiria hazikufua dafu kwani hakuwa amejibu simu wala kujibu ujumbe mfupi wa simu kwa wakati.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Rais Zelensky wa Ukraine atembelea Ujerumani siku moja baada ya ahadi ya silaha

    Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine yuko Berlin kwa mazungumzo na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Rais Frank-Walter Steinmeier, ikiwa ni ziara yake ya kwanza nchini Ujerumani tangu uvamizi wa Urusi.

    Safari hiyo inawadia siku moja baada ya Ujerumani kutangaza kuwa itasambaza silaha zenye thamani ya karibu dola bilioni tatu kwa Kyiv.

    Baadaye siku ya Jumapili, Rais Zelensky atapewa kwa heshima na fahari, Tuzo ya Charlemagne.

    Tuzo hiyo inawatambua wale wanaofanya zaidi kukuza umoja wa Ulaya.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Vita vya Ukraine: Mji wa washiriki wa mashindano ya Ulaya washambuliwa na Urusi kabla hawajapanda jukwaani

    Mji wa nyumbani nchini Ukraine wa kundi linaloshiriki mashindano ya kuimba ya nchi za Ulaya (Tvorchi) umeshambuliwa kwa makombora na Urusi muda mfupi kabla ya kundi hilo kupanda jukwaani huko Liverpool, maafisa wanasema.

    Mkuu wa utawala wa jimbo la Ternopil, Volodymyr Trush, amethibitisha kuwa watu wawili wamejeruhiwa.

    Meya wa Ternopil Serhiy Nadal alisema maghala yameharibiwa.

    Wizara ya mambo ya nje ya Ukraine iliishutumu Urusi kwa kushambulia mikoa ya Kyiv na Ternopil kabla na wakati kundi la nchi hiyo linashiriki mashindano hayo.

    Dakika kumi kabla ya kupanda jukwaani katika uwanja wa Liverpool, kundi la Tvorchi liliweka ujumbe kwenye Instagram likitaja ripoti za kushambuliwa kwa mji wa Ternopil magharibi mwa Ukraine.

    Baada ya kushiriki maonyesho, waliongeza: "Ternopil ni jina la mji wetu, ambao meshambuliwa na Urusi wakati tunaimba kwenye jukwaa la Eurovision kuhusu mioyo yetu ya chuma, isiyoweza kushindwa na yenye mapenzi tele.

    "Huu ni ujumbe kwa miji yote ya Ukraine ambayo inashambuliwa kwa makombora kila siku.

    Kharkiv, Dnipro, Khmelnytsky, Kyiv, Zaporizhzhia, Uman, Sumy, Poltava, Vinnytsia, Odesa, Mykolaiv, Chernihiv, Kherson na mengine yote.

    "Ulaya, inaungana dhidi ya uovu kwa ajili ya amani!"

    Pia unaweza kusoma:

  8. Kimbunga Mocha: Dhoruba kali yakumba Bangladesh na pwani ya Myanmar

    Kimbunga kikali kimekumba ufuo wa Bangladesh na Myanmar baada ya kuzidi na kuwa sawa na dhoruba ya aina ya tano.

    Kimbunga Mocha kinasababisha mvua kubwa na upepo wa hadi 195kph (120mph), ambao unaweza kusababisha mafuriko hatari kwenye ardhi karibu na Ghuba ya Bengal.

    Mawimbi ya dhoruba ya hadi mita nne yanaweza kusomba vijiji katika maeneo ya tambarare

    Kuna hofu kuwa huenda kikagonga kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani, Cox's Bazar, ambapo karibu watu milioni moja wanaishi.

    Watabiri walionya Kimbunga Mocha kinaweza kuwa kimbunga chenye nguvu zaidi kuwahi kutokea nchini Bangladesh katika takriban miongo miwili.

    Takriban watu 500,000 wamehamishwa hadi maeneo salama.

    Tazama hali ilivyokuwa:

    Pia unweza kusoma:

  9. Mwanamke, 99, atimiza ndoto yake ya kushiriki onyesho la kurushiwa visu

    Mwanamke mwenye umri wa miaka 99 ametimiza ndoto yake maishani ya kutupiwa visu wakati wa maonyesho ya moja kwa moja ya sarakasi.

    Annie Duplock, kutoka Sharnford, Leicestershire, aliingia ulingoni kustahimili makali ya visu anavyotupiwa mbele ya umati wa watu waliokuwa wakimshangilia huko Coventry siku ya Ijumaa.

    Mfanyikazi huyo wa zamani wa sarakasi, ambaye anasherehekea miaka mia moja katika kipindi cha miezi mitatu ijayo, alikuwa kwenye fainali kuu ya onyesho la Zippo Circus.

    Baadaye alisema "amefurahiya sana" uzoefu huo.

    Akisaidiwa na mkongojo, Bi Duplock alichukua nafasi yake mbele ya jopo huku akiwa anarushiwa visu na mtaalamu wa hilo.

    Alikuwa amemshawishi binti yake kumwomba mkuu wake wa zamani, mwanzilishi wa maonyesho Martin Burton, amruhusu kushiriki.

    Bw Burton alisema: "Annie alinifanyia kazi miaka 30 iliyopita. "Alikuwa na umri wa miaka 70 wakati huo na atakuwa na umri wa miaka 100 mwezi huu wa Agosti."

    Aliiambia hadhira mfanyakazi wake wa zamani alikuwa ameona onyesho usiku uliopita na akaomba kuwa sehemu ya tamasha hilo la kusisimua kama ishara ya kusherehekea miaka 100 ya kuzaliwa kwake.

    Baada ya onyesho hilo, alisema: "Sikuzote nilitaka mtu anirushie visu! "Niko tayari kwa onyesho lijalo."

    Pia unaweza musoma

  10. Milio ya risasi yasikika Sudan kabla ya mazungumzo ya kusitisha mapigano

    Mapigano makali kati ya pande zinazozozana yameendelea katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum na miji mingine kabla ya mazungumzo ya kusitisha mapigano siku ya Jumapili.

    Wakaazi wanasema jeshi la Sudan limeshambulia maeneo ya raia, huku Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) kikichukua mali za raia.

    Mapigano yaliripotiwa mjini Khartoum, nchi jirani za Omdurman na Geneina katika eneo la Darfur.

    Vita kati ya jeshi la nchi hiyo na RSF vilianza karibu mwezi mmoja uliopita.

    Mkazi mmoja Hani Ahmed, 28, alisema hali ilikuwa mbaya zaidi asubuhi ikilinganishwa na siku mbili zilizopita.

    "Ungeweza kusikia vizuri mizinga na RSF walikuwa wakishika doria mitaani kuliko kawaida," aliongeza.

    "Tunaona tu jeshi angani, lakini katika suala la mawasiliano ya ana kwa ana, tunaona tu kikosi cha RSF. Ndio walio chini," Bw Ahmed alisema.

    Mamia wameuawa na karibu 200,000 wametoroka makazi yao na kuelekea majimbo jirani huku watu 700,000 wameondoka makazi yao ndani ya nchi.

    Uporaji ulioenea, pamoja na kuondoka kwa mashirika ya misaada ya kimataifa, umesababisha uhaba mkubwa wa chakula na dawa.

    Watu waliotoroka makazi yao wanaoishi katika kambi kubwa kaskazini mwa Darfur wamepunguza mlo mmoja kwa siku.

    Shirika la misaada la kimatibabu la Medecins Sans Frontieres (MSF) lilionya kuwa hali za watoto zinaweza kuzorota.

    Pande zinazozozana zilitia saini "tamko la kujitolea" siku ya Alhamisi, baada ya wiki moja ya mazungumzo yaliyopatanishwa na wenyeji Saudi Arabia na Marekani.

    Mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya wawakilishi wa pande zinazozozana yataanza tena mjini Jeddah siku ya Jumapili.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Hujambo na karibu katika matangaozo yetu ya moja kwa moja