Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Zaidi ya watu 150,000 wako hatarini wakati kimbunga Freddy kikikaribia Msumbiji
Mamlaka ya Msumbiji inasema watu 158,000 wanaweza kuathiriwa na Kimbunga Freddy katika kitovu chake katika jimbo la kati la Zambezia.
Moja kwa moja
Mapigano nchini DR Congo siku chache baada ya kusitishwa kwa mapigano,
Ndege ya huduma ya kwanza imewasili katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kama sehemu ya operesheni mpya ya Umoja wa Ulaya kusaidia mamia kwa maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na migogoro.
Hatua hii Inakuja baada ya mapigano katika eneo hilo kati ya jeshi na waasi wa M23 siku tatu baada ya kuanza kwa usitishaji mapigano.
Mapigano hayo yanazunguka kijiji cha Murambi ambacho kiko chini ya kilomita 30 kutoka Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.
Waasi wa M23 wanaripotiwa kuungwa mkono na Rwanda ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikishutumu mamlaka ya Congo kwa kushindwa kuwashinda waasi wa Kihutu ambao baadhi yao wanahusishwa na mauaji ya kimbari ya Rwanda.
Rwanda inakanusha kuunga mkono kundi hilo.
Umoja wa Mataifa walaani shambulizi linaloshukiwa kuwa la wanamgambo wa Kiislamu Nigeria
Umoja wa Mataifa umelaani mauaji ya kikatili yanayoripotiwa ya takriban raia 37 katika kijiji cha Mukdolo katika eneo la serikali ya mtaa ya Ngala katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Makumi ya wanakijiji walipigwa risasi na kufa katika shambulio la watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Jimbo la Kiislamu la Jimbo la Afrika Magharibi (Iswap), ripoti zinasema.
Shambulio hilo lilifanyika karibu na ngome ya waasi wa Boko Haram. Kando na vifo hivyo, wengine kadhaa pia walijeruhiwa, huku wengi wao wakiwa bado hawajulikani walipo kufuatia shambulio hilo baya.
Duru za usalama zinasema kuwa makumi ya wapiganaji wa Iswap waliokuwa wakiendesha pikipiki walivamia uwanja na kuanza kufyatua risasi mara kwa mara.
Tisa kati ya waathiriwa walifanikiwa kukimbia. Katika taarifa yake, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Misaada ya Kibinadamu nchini Nigeria, Matthias Schmale, alituma salamu za rambirambi kwa familia zilizofiwa. Alibainisha kuwa waathiriwa wa shambulio hilo baya ni wavuvi na wakulima wanaotafuta riziki katika mazingira yasiyo salama sana.
"Shambulio hili la kushangaza ni ukumbusho mwingine wa kutisha wa vitisho vya kweli vya ghasia na ukosefu wa usalama ambavyo IDPs na watu wengine walioathiriwa na zaidi ya miaka 13 ya mzozo wa kijeshi usio wa kimataifa katika eneo hilo wanaendelea kukabili kila siku katika mapambano yao ya kuishi," taarifa ilisema.
Bw Schmale alitoa wito kwa mamlaka ya serikali kuchunguza kwa haraka tukio hilo na kuwafikisha wahusika haraka mahakamani. Pia alizikumbusha pande zinazohusika katika mzozo huo kuzingatia wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu ili kuwalinda raia dhidi ya madhara.
Kimbunga Freddy ni 'hatari' - WMO
Msumbiji "inajiandaa kupambana na athari" za Kimbunga Freddy, ambacho kinatarajiwa kutua huko katika saa 24 zijazo, baada ya kukumba Madagascar mapema wiki hii, Anne-Claire Fontan, kutoka Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), alikiambia kipindi cha BBC Newsday.
Alielezea kimbunga Freddy kama "hatari sana" na anasema Msumbiji inaweza kutarajia kuona "upepo mkali" pamoja na tishio la mafuriko.
Mara tu Freddy kitakapopiga, itakuwa ni mara ya pili kugonga Msumbiji, hapo awali ilipiga nchi hiyo mnamo Februari.
Takribani watu 21 wamepoteza maisha kutokana na kimbunga Freddy, na kinatarajiwa kusababisha uharibifu zaidi kitakapoikumba Msumbiji.
Inaweza kuishia katika vitabu vya historia kama dhoruba ya kitropiki iliyodumu kwa muda mrefu zaidi katika rekodi ingawa hii bado haijathibitishwa.
Zaidi ya watu 150,000 wako hatarini wakati kimbunga Freddy kikikaribia Msumbiji
Mamlaka ya Msumbiji inasema watu 158,000 wanaweza kuathiriwa na Kimbunga Freddy katika kitovu chake katika jimbo la kati la Zambezia.
Kimbunga hicho kinatarajiwa kuanguka katika ufuo wa katikati mwa Msumbiji siku ya Ijumaa.
Kimbunga Freddy kinarejea Msumbiji baada ya kusababisha maafa mwishoni mwa mwezi Februari.
Inaweza kuishia kwenye rekodi za dhoruba ya kitropiki iliyodumu kwa muda mrefu zaidi katika rekodi.
Shirika la kitaifa la majanga ya asili linasema 8,000 kati ya walioathiriwa wanaweza kuhitaji msaada wa haraka wa kibinadamu, kulingana na makadirio yao. Serikali ya mkoa imeamuru kufungwa kwa shule zote kuanzia Ijumaa hii.
Takriban watu 25 wameuawa katika shambulizi la wanajihadi Nigeria
Polisi nchini Nigeria wamesema kuwa takribani watu 25 wameuawa katika shambulizi lililofanywa na wanamgambo wa Kiislamu kaskazini mashariki mwa jimbo la Borno.
Shambulio hilo limetokea katika mji wa wavuvi wa Dikwa ulio karibu na ngome ya waasi wa Boko Haram.
Umoja wa Mataifa unasema ghasia za itikadi kali tangu mwaka 2009 zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 350,000 na mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao.
Serikali ya Uganda yaidhinisha mchakato wa muswada dhidi ya mapenzi ya jinsia moja
Serikali imemuidhinisha Mbunge wa Manispaa ya Bugiri Asuman Basalirwa kufanya mchakato unaostahili wa kuunda na kukamilisha Muswada wa Kupinga mapenzi ya jinsia moja wa 2023, unaonuiwa kupiga marufuku mahusiano ya watu wa jinsia moja nchini Uganda.
Hatua hiyo ilimruhusu kuwasilisha muswada huo kwa mara ya kwanza jana.
Alipokuwa akiwasilisha muswada huo, Bw Basalirwa alikariri msimamo wa wiki jana kwamba muswada huo unanuiwa kuihami jamii nchini Uganda dhidi ya utamaduni wa mapenzi ya jinsia moja. "Kutokana na hayo, kuna haja ya kuwa na sheria ya kuimarisha makosa yanayohusiana na hilo na vifungu wazi vya kuchunguza, kushtaki, kuwatia hatiani na kuwahukumu wahalifu," Bw Basalirwa alisema.
Katika kuelekea kusomwa kwa mara ya kwanza kwa muswada huo, Spika Anita Among aliwataka wabunge ‘kutotetereka’ au ‘kutishwa’ kwa kulazimishwa kupiga kura dhidi ya kupita huku kukiwa na taarifa kwamba wangenyimwa viza ya kusafiri katika baadhi ya nchi. "Nataka kuwasihi wabunge [kwamba] wasiogope, tunafanya hivi kwa ajili ya ubinadamu, tuko hapa kuwakilisha watu huko nje. Sisi ni sauti ya wasio na sauti. Spika Among alisema.
Kenya yaanzisha msako dhidi ya LGBTQ shuleni
Wizara ya elimu nchini Kenya imeanzisha msako mkali dhidi ya kile ilichotaja kuwa kupenyezwa kwa ajenda ya LGBTQ shuleni.
Hatua hiyo itapekelekea serikali kuanzisha kitengo cha viongozi wa dini shuleni, waziri Ezekiel Machogu aliwaambia maseneta siku ya Alhamisi.
Kuna hofu kwamba programu inaweza kuwa na Habari za watu wa LGBTQ na uhusiano wa jinsia moja kufundishwa shuleni.
Mapenzi ya jinsia moja bado ni kinyume cha sheria lakini mitazamo dhidi ya LGBTQ imekuwa ikiongezeka kufuatia uamuzi wa mwezi uliopita wa Mahakama ya Juu kwamba jamii hiyo ina haki ya kusajili chama chao.
Kamati tayari imeundwa kushughulikia masuala ya LGBTQ shuleni, waziri alisema, na kupendekeza jukumu lake linaweza kujumuisha kupitia upya mtaala shuleni.
Kamati hiyo itaongozwa na askofu mkuu kutoka kanisa la kianglikana nchini Kenya.
“Haya ni masuala ambayo hatuwezi kuruhusu yaingie katika shule zetu,” Bw Machogu alisema.
Waziri huyo alikuwa akimjibu seneta ambaye alikuwa na wasiwasi juu ya madai ya kuenea kwa ajenda ya LGBTQ katika shule za msingi.
Habari za hivi punde, Urusi inaweza kupigana nchini Ukraine kwa miaka miwili zaidi - Lithuania
Mkuu wa upelelezi wa jeshi la Lithuania amesema Urusi ina rasilimali za kutosha kuendeleza vita nchini Ukraine kwa miaka miwili zaidi na kwa kasi ya sasa.
Moscow inasema ilizindua "operesheni yake maalum ya kijeshi" nchini Ukraine mwaka mmoja uliopita ili kukabiliana na tishio la usalama wake. Kyiv na nchi za Magharibi zinavitaja vita hivyo kama visivyochochewa kulitiisha taifa huru.
"Rasilimali ambazo Urusi inazo kwa sasa zingetosha kuendeleza vita kwa kasi ya sasa kwa miaka miwili," mkuu wa upelelezi wa Lithuania Elegijus Paulavicius aliwaambia waandishi wa habari.
"Kwa muda gani Urusi itaendeleza vita hivyo pia itategemea uungwaji mkono wa jeshi la Urusi kutoka mataifa kama vile Iran na Korea Kaskazini", aliongeza.
Paulavicius alikuwa akiwasilisha muhtasari wa tishio la kitaifa na mashirika ya kijasusi ya Lithuania, ambayo pia yalidai wadukuzi wanaohusishwa na serikali ya Urusi na China walijaribu mara kwa mara kuingia katika kompyuta za serikali ya Lithuania mwaka 2022.
"Kipaumbele chao kinabaki kuwa ukusanyaji endelevu wa muda mrefu wa habari zinazohusiana na mambo ya ndani na nje ya Lithuania," mashirika hayo yalisema.
Ramaphosa awaonya wafanyikazi wanaogoma baada ya maandamano mabaya
Rais Cyril Ramaphosa anasema ana wasiwasi kuhusu mgomo unaoendelea wa mishahara wa wafanyikazi wa umma ambao unaathiri huduma muhimu nchini.
Mgomo wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyakazi wa Elimu, Afya na Washirika (Nehawu) ulianza Jumatatu, huku wafanyikazi wakidai nyongeza ya 10% ya mishahara baada ya kukataa nyongeza ya 3% ya serikali.
Takriban watu wanne wamefariki huku wafanyakazi hao wakiripotiwa kuwazuia wagonjwa kuingia katika hospitali na kliniki nyingi nchini, Waziri wa Afya Joe Phaahla alisema.
Rais alisema siku ya Alhamisi kwamba ingawa wafanyikazi wana haki ya kugoma, vitendo vya ghasia havitavumiliwa.
“Sote tuna wasiwasi kuhusu hali ya vurugu ya mgomo unaoendelea. Wafanyakazi katika nchi yetu wana haki ya uhuru wa kujumuika na kugoma. Lakini haki hiyo si kamilifu," Rais Ramaphosa alisema.
Alisema kuwa kanuni ya "hakuna kazi, hakuna malipo" inapaswa kutumika kwa wafanyikazi wa huduma muhimu wanaogoma.
Ten Hug amsifu nahodha Bruno Fernandes katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Real Betis
Meneja wa Manchester United Erik ten Hag alimsifu nahodha aliyefunga goli Bruno Fernandes kama nyota katika ushindi wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 bora wa Ligi ya Europa dhidi ya Real Betis.
Fernandes alilaumiwa sana United kufuatia rekodi ya kufedheheshwa ya magoli 7-0 Jumapili na Liverpool kwenye Ligi ya Premia.
Lakini Ten Hag alithibitisha katika maandalizi hayo Mreno huyo angesalia kuwa nahodha ikiwa Harry Maguire hangekuwa uwanjani - na Fernandes alilipa imani hiyo kwa mchango mkubwa katika ushindi uliohitajika sana.
Ulijumuisha bao lake la nane msimu huu alipofunga kwa kichwa kona ya Luke Shaw dakika ya 58.
"Alikuwa mchezaji bora zaidi uwanjani," alisema Ten Hag. "Alicheza nyuma kidogo na alikuwa mzuri, akionyesha ushawishi wake katika mchezo kutoka eneo la nyuma, na pasi nyingi nzuri katikati ya uwanja. Kutoka hapo tulitengeneza nafasi nyingi."
Mpenzi wa zamani wa Tiger Woods asema alidanganywa ili atoke kwa nyumba walioishi
Kesi iliyowasilishwa na mpenzi wa zamani wa Tiger Woods inadai kwamba alimdanganya kubeba begi na kuondoka katika nyumba yao ya pamoja kabla ya kumfungia nje.
Mawakili wa Erica Herman, ambaye alianza kuchumbiana na mchezaji huyo wa gofu mwaka wa 2017, wanahoji anahitaji kulipwa $30m (£25m) kutokana na jinsi alivyofukuzwa ghafla kutoka kwa nyumba hiyo.
Katika kesi nyingine, anataka makubaliano ya kutofichua (NDA) aliyotia saini na Bw Woods kufutiliwa mbali
Mwakilishi wa Bw Woods, 47, hakutoa maoni yake mara moja.
Kutengana kwa wanandoa hao hakujatangazwa rasmi. Hawajaonekana pamoja hadharani tangu kuhudhuria mashindano ya tenisi ya US Open huko New York Agosti mwaka jana.
Bi Herman, 38, aliwahi kufanya kazi katika mgahawa wa bingwa huyo mara 15 wa Florida, The Woods Jupiter.
Kesi aliyofungua Oktoba dhidi ya wakfu wa nyumba inayoshikiliwa na Bw Woods ndiyo imeibuka sasa. Inadai kuwa alifungiwa nje ya nyumba yao ya pamoja huko Hobe Sound, Florida.
"Hasa, kwa hila, maajenti wa mshtakiwa walimshawishi mshtakiwa kubeba koti kwa ajili ya likizo fupi na, alipofika uwanja wa ndege, walimwambia kuwa alikuwa amefungiwa nje ya makazi yake," kulingana na hati za mahakama zilizoonekana na BBC.
Gavana wa Taliban auawa katika ofisi yake
Gavana wa Taliban wa jimbo la Balkh kaskazini mwa Afghanistan ameuawa katika shambulio la kujitoa mhanga linalodaiwa na kundi la Islamic State (IS).
Mohammad Dawood Muzammil aliuawa katika ofisi yake katika mji mkuu wa mkoa, wa Mazar-e Sharif, siku ya Alhamisi.
Ndiye afisa mkuu wa Taliban kuuawa tangu wanamgambo hao warejee mamlakani mwaka 2021.
Ghasia zimepungua sana tangu wakati huo, lakini maafisa wakuu wanaounga mkono kundi la taliban wamekuwa wakilengwa na IS.
Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid alisema kwenye Twitter kwamba gavana huyo "aliuawa kama shahidi katika mlipuko wa maadui wa Uislamu".
Muzammil alikuwa ameongoza vita dhidi ya IS katika wadhifa wake wa awali kama gavana wa jimbo la mashariki la Nangarhar. Alihamishiwa Balkh Oktoba iliyopita.
Msemaji wa polisi wa Balkh Mohammed Asif Waziri alisema mlipuko huo ulitokea Alhamisi asubuhi kwenye ghorofa ya pili ya ofisi ya gavana.
"Kulikuwa na kishindo. Nilianguka chini," Khairuddin, ambaye alijeruhiwa katika mlipuko huo, aliliambia shirika la habari la AFP. Alisema ameona rafiki yake akipoteza mkono katika mlipuko huo.
Shambulio baya la risasi lafanyika katika Jumba la Jehovah Witness Hamburg Ujerumani
Watu kadhaa wameuawa kwa kupigwa risasi kwenye jumba la mikutano la Jehovah Witness katika jiji la Hamburg kaskazini mwa Ujerumani.
Polisi wanasema kuwa mtu aliyepiga risasi alikuwa pekee na anadhaniwa amekufa. Haijabainika iwapo mshambuliaji huyo ni miongoni mwa vifo sita au saba vilivyoripotiwa na vyombo vya habari vya Ujerumani.
Bado, "hakuna taarifa za kuaminika juu ya nia yake," polisi wanasema.
Watu kadhaa pia walijeruhiwa katika ufyatulianaji wa risasi kwenye mtaa wa Deelböge katika wilaya ya Gross Borstel ya jiji hilo.
Polisi wanasema walimpata mtu aliyekufa katika eneo la tukio ambaye wanaamini kuwa huenda alikuwa mhusika na uchunguzi unaendelea.
Polisi waliitwa mwendo wa 21:15 (20:15 GMT) kufuatia ripoti kwamba kuripoti kwamba risasi zilifyatuliwa kwenye jengo hilo, msemaji wa polisi Holger Vehren alisema.
Maafisa walioingia ndani walipata watu ambao "huenda wamejeruhiwa vibaya na risasi, baadhi yao wakiwa wamepoteza maisha", alisema.
"Maafisa hao pia walisikia mlio wa risasi kutoka sehemu ya juu ya jengo hilo na wakapanda juu, ambapo pia walimkuta mtu. Hadi sasa hatuna dalili zozote kwamba wahalifu wowote walitoroka."
Alisema polisi bado hawajawatambua wahasiriwa na uchunguzi katika eneo la uhalifu inaendelea.
Natumai hujambo