Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rais William Ruto awaapisha majaji sita 'waliopuuzwa' na rais Uhuru Kenyatta
Majaji sita walioteuliwa na Idara ya mahakama kabla ya kukataliwa na rais Uhuru Kenyatta hatimaye wameapishwa.
Moja kwa moja
Amani yawarejesha walimu zaidi ya 2500 waliokimbia mapigano kaskazini mwa Msumbiji
Zaidi ya wafanyakazi 2,500 katika sekta ya elimu wakiwemo walimu waliokuwa wamekimbia makazi yao katika jimbo la kaskazini la Msumbiji lililokumbwa na mashambulizi ya wanajihadi la Cabo Delgado wamerejea makwao baada ya kurejeshwa kwa amani katika eneo hilo.
Afisa elimu wa mkoa huo, Manuel Bacar, alisema baadhi ya shule zimefunguliwa katika wilaya za Mocimboa da Praia, Palma, Macomia na Quissanga kwa sababu ya kurejea kwa walimu hao.
"Katika wilaya hizi, tuna jumla ya wanafunzi 102,808 ambao tayari wameanza tena masomo." Eneo hilo limekuwa likikumbwa na ghasia za wanamgambo tangu mwaka 2017.
Bunge la Uganda lamuenzi Malkia Elizabeth II
Bunge la Uganda limefanya kikao maalum cha kumuenzi Malkia Elizabeth II, aliyefariki nchini Scotland siku ya Alhamisi.
Hoja ya kikao hicho ilitolewa na waziri mkuu na iliendelea kwa saa mbili. Malkia alitembelea Uganda kwa mara ya kwanza mwaka wa 1954 na kisha akarejea tena mwaka wa 2007 kwa Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola - ziara yake rasmi ya mwisho barani Afrika.
Wabunge hao ambao kila mmoja alipewa dakika mbili za kuzungumza, walisema kuwa Malkia ameiongoza Jumuiya ya Madola vyema na alikuwa na jukumu muhimu na la kuunganisha wanachama.
Kwa upande wa wabunge wa kike walisema kuwa alikuwa mfano mwenye ushawishi kwa wanawake katika uongozi na kiongozi mashuhuri.
Mbuga ya Kitaifa ya Malkia Elizabeth iliyoko magharibi mwa Uganda ilipewa jina lake ili kuadhimisha ziara yake ya mwaka 1954.
Barabara kadhaa na njia za kuzunguka katika mji mkuu Kampala pia zimepewa majina ya watu wa familia ya kifalme ya Uingereza. Ingawa upinzani uliunga mkono hoja hiyo na kuthamini uongozi wa muda mrefu wa Mfalme, walizungumza vikali dhidi ya viongozi wa jamhuri kukaa muda mrefu madarakani. Rais wa Uganda Yoweri Museveni amekuwa madarakani tangu 1986.
Zelensky: Crimea na maeneo mengine yaliyotekwa na Urusi yatarejeshwa
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameonesha imani yak kwamba eneo la Crimea na maeneo mengine yanayokaliwa na Urusi yatarejea Ukraine.
"Lazima tutume ujumbe kwa watu wetu katika maeneo yanayokaliwa, huko Crimea. Hawa ni watu wetu," Interfax-Ukraine ilimnukuu Zelensky. Urusi inashambulia kwa televisheni na vyombo vingine vya habari."
"Ujumbe wangu ni kwamba tutashinda. Haijalishi wamesikia nini katika kipindi cha miaka minane kutoka kwa televisheni ya propaganda," Zelensky aliwaambia waandishi wa habari. "Tunajua kwamba ukweli uko upande wetu."
Kulingana na Zelensky, bado hawezi kusema ni lini hii itatokea, kwa sababu hakuna mtu anayejua. Lakini tushinda kwa sababu hii ni ardhi yetu na watu wetu, alihitimisha.
Mechi kati ya Arsenal na Manchester City yaahirishwa
Mechi ya ligi ya Uingereza kati ya Arsenal na Manchester City, iliopangwa kuchezwa tarehe 19 Oktoba, imeahirishwa ili kuruhusu upangaji upya wa mechi za Ligi ya Yuropa kati ya The Gunners dhidi ya PSV Eindhoven.
Mchezo wa Arsenal dhidi ya PSV ulipangiwa chezwa Alhamisi, lakini "vikwazo vikali kwa rasilimali za polisi" baada ya kifo cha Malkia Elizabeth II kuliahirisha.
Arsenal sasa itacheza na timu hiyo ya Uholanzi tarehe 20 Oktoba.
Ligi ya Premia ilisema inatafuta tarehe mpya "kwa wakati ufaao".
Raundi nzima ya mechi za Ligi Kuu ya Uingereza iliahirishwa wikendi iliyopita huku mechi zikiahirishwa kama ishara ya heshima kufuatia kifo cha Malkia.
Mechi nyingine tatu za ligi kuu, zilizopaswa kuchezwa wikendi hii, zimeahirishwa katika maandalizi ya mazishi ya Malkia Jumatatu.
Gavi asaini mkataba mpya Barcelona wenye kifungu cha kuuzwa kwa euro 1bn
Kiungo wa kati wa Hispania Gavi amesaini mkataba mpya utakaombakiza Barcelona hadi mwaka 2026. Mkataba huo unakifungu cha kuuzwa kwa euro 1bn sawa £865m kwa timu itakayomtaka.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 ameichezea Barcelona tangu 2015 na alikuwa mkataba ambao ulikuwa unamalizika mwaka 2023.
Alianza kucheza katika kikosi cha kwanza mnamo Agosti 2021, akiwa na umri wa miaka 17 na siku 24, na kuwa mchezaji wa nne mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya klabu hiyo kucheza.
Gavi anayeonekana lulu ya Barca kwa muda mrefu ujao ameanza katika mechi zote za Barcelona za ligi kuu ya La Liga msimu huu. Aliingia kwenye orodha ya mfungaji bora namba tatu kinda wa klabu hiyo alipofunga bao dhidi ya Elche mnamo Desemba 2021.
Habari za hivi punde, Rais William Ruto awaapisha majaji sita
Majaji sita walioteuliwa na Idara ya mahakama katika mahakama ya rufaa hatimaye wameapishwa.
Sita hao waliapishwa na rais William Ruto baada ya kuahidi kufanya hivyo wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.
Rais aliyeondoka madarakani Uhuru Kenyatta alikataa kuwaapisha sita hao kwa madai kwamba walikuwa wameshindwa kuafikia ‘masharti ya kuteuliwa kuhudumu’.
Sita hao ni Joel Ngugi, George Odunga, Aggrey Mchelule, Weldon Korir, Evans Makori na Elizabeth Omange.
Jaji Muchelule alikuwa wa kwanza kula kiapo kama kilivyosimamiwa na Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama Anne Amadi.
Kisha akafuatwa na Majaji Korir, Prof Ngugi na Odunga. Mwisho Bw Makori na Bi Omange walikula kiapo cha kuwa majaji wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi.
"Nawapongeza majaji wapya ambao wameapishwa. Nawatakia kila la kheri mnaposhiriki majukumu yenu mnapohudumia Wakenya," Rais Ruto alisema.
"Majaji wamesubiri kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyopaswa kuwa lakini yote yamefanyika vizuri," aliongeza.
Habari za hivi punde, Watu 10 wauawa katika mashambulizi ya hivi punde ya ndege huko Tigray - Maafisa
Watu kumi wameuawa katika siku ya pili ya mashambulizi ya anga dhidi ya mji mkuu wa eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia, kulingana na maafisa wa hospitali.
Mkuu wa Hospitali ya Ayder huko Mekelle, Kibrom Gebreselassie alielezea shambulio la asubuhi ya leo kama shambulio la ndege zisizo na rubani.
Mashambulizi hayo yanajiri siku chache baada ya mamlaka katika eneo hilo lenye vita kueleza kuwa iko tayari kusitisha mapigano.
Watakaouona mwili Malkia Elizabeth II kupanga foleni kwa saa 30
Waziri wa utamaduni wa Uingereza Michelle Donelan ameonya kuwa huenda kukawa na misururu mirefu kuliko inavyotarajiwa kuufikia mwili wa Malkia Elizabeth II katika ukumbi wa Great Hall wa Westminster.
Alisema kuwa huenda kukawa na mistari mirefu ya maelfu ya wafariji, na unaweza kusubiri kwa saa 30 mstarini kabla ya kufika Great Hall.
Kwa misingi hii, aliionya jamii kujianda kusimama saa nyingi kila siku, na kujiandaa kuihimili hali ya hewa.
Lakini alisema, "Serikali itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha watu waliosafiri kuja London hawana matatizo yoyote."
Bi Donelan alisema kwamba zaidi ya watu 1,000 watakuwa wakisubiri kwenye mstari kila siku kuwasaidia.
Aliongeza kuwa Tate Modern na Shakespeare Globe watawasha mataa kwenye ofisi zao mjini London pamoja na kuweka picha ya Malkia Elizabeth, na maduka yatasambaza viburudisho kwa umma.
Vyumba 500 zaidi vimehifadhiwa kwenye barabara inayoelekea katika ukumbi wa Westminster kukidhi mahitaji ya umma.
Unaweza pia kusoma:
- Malkia Elizabeth II: Maisha yake kabla ya kuwa Malkia
- 'Kuwaambia nyuki kifo cha Malkia' na mila nyingine zisizo za kawaida katika Familia ya Kifalme
- Malkia Elizabeth II: Maisha katika picha
- Haya ni matukio 6 ya ucheshi wa Malkia Elizabeth II
"Sisi ni binadamu katika kutekeleza kuna maeneo tunakosea" - Mwigulu Nchemba
Waziri wa Fedha nchini Tanzania, Dkt Mwigulu Nchemba amesema kuwa wamepokea maelekezo ya Chama cha mapinduzi CCM ya kuangalia upya utaratibu wa utozaji na wanayafanyia kazi mapendekezo na watatoa majibu hivi karibuni.
Akiongea na wananchi wilayani Tarime mkoani Mara alipofanya ziara ya kikazi, Waziri huyo wa fedha amekiri kuwa inawezekana walikosea kama binadamu yeyote anavyoweza kukosea hivyo walishapokea maelekezo kutoka kwa Rais wa nchi hiyo na Chama cha Mapinduzi.
"Katika kugusana gusana kuna maeneo ambayo tunakosea, sisi ni binadamu tutashindwa kwani kukosea?... Sisi ni wanadamu katika kutekeleza kuna maeneo tunakosea" anasema Mwigulu Nchemba waziri wa Fedha.
Anaongeza kuwa "tumepokea maelekezo ya kuangalia upya utaratibu wa utozaji inawezekana tunakosea namna tunavyokusanya lakini isiondoe mantiki ya watu wetu ya kufanya kazi ya ukusanyaji, nchi haiwezi kwenda bila makusanyo.”
Amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu kwani wanafanyia kazi kitaalamuna watatoa majibu ya utekelezaji na kutoa suluhu itakayolinda kazi za wananchi.
Mnamo Septemba 8 Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka alitoa maelekezo kwa serikali kusikiliza maoni na ushauri wa wananchi kuhusuutekezaji wa bajeti ya 2022/23 hususani eneo la tozo za miamala ya kielektroniki.
Hatua hii ilikuja baada ya serikali kuanza kutekeleza ukusanyaji wa tozo ya miamala ya kibenki na kuibua mijadala mipya kuhusu utitiri wa tozo ikiwemo yamiamala ya simu iliyoanza kupigiwa kelele tangu ilipoanza kutumika mwaka jana.
Afrika Kusini yaondoa idhini ya makazi ya kudumu nchini humo kwa wafanyakazi wa kidini wa kigeni
Wafanyakazi wa kidini wa kigeni hawataweza tena kupata viubali vya kazi au ukaaji wa kudumu nchini Afrika Kusini, mtandao wa habari wa EWN umeripoti ukinumnukuu waziri wa mambo ya ndani.
Waziri Aaron Motsoaledi alikuwa mbele ya kamati ya bunge inachunguza ni kwa jinsi gani Muinjilisti maarufu wa Malawi Shepherd Bushiri na mmke wake, Mary, walitoroka nchi mwaka 2020 wakati walipokuwa wakikabiliwa na mashitaka ya utakatishaji wa pesa.
Afisa wa ngazi ya juu na maafisa wengine wa ngazi ya chiniambao ni maafisa wa wizara ya mamboya ndani ya Afrika Kusini wamefutwa kazi kwa madai ya kutoa kibali cha kuishi nchini humo kwa Bw Bushiri.
Afrika Kusini ilituma ombo rasmi kwa kwa Malawi kwa ajili ya kumrejesha Afrika Kusini bw Bushiri.
“Ninataka kuthibitisha kwamba kwenye mifumo yetu ya udhibiti, hatuoni rekodi yoyote ya akina Bushiri wakiondoka, jambo ambalo linamaanisha kuwa waliondoka nchini kinyume cha sheria,” Bw Motsoaledi salisema jumanne, EWN imeripoti.
Waziri pia alisema kwamba uchunguzi umeanzishwa kubaini ni jinsi gani muinjilisti mwingine, Mnigeria Timothy Omotoso,ambaye anakabiliwa na ubakaji na mashitaka ya biashara haramu ya usafirishaji wa watu, alikuwa amepata kibali cha kuishi Afrika Kusini.
“Tunasema wanapaswa kuja tu kama wageni, lakini kama wageni wanaoweza kufanya kazi. Mabadiliko haya yanamaanisha kuwa hakuna njia iliyopo kwa wafanyakazi wa kidini kuhamia kwa hadhi ya makazi ya kudumu ,” Bw Motsoaledi alisema.
Unaweza pia kusoma:
- Mchungaji Bushiri: 'Mhubiri anayeweza kutembea angani
- Mchungaji Bushiri atoroka kesi Afrika Kusini
- Shepherd Bushiri:Mchungaji milionea aiomba dunia iingilie kati kesi dhidi yake.
- Shepherd Bushiri:Mchungaji milionea aiomba dunia iingilie kati kesi dhidi yake.
Ruto abatilisha maagizo ya Kenyatta katika siku yake ya kwanza mamlakani
Katika siku yake ya kwanza mamlakani, Rais wa Kenya William Ruto alitoa maagizo ya kutekelezwa kinyume na sera za mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta.
Rais Ruto aliwateua majaji sita walioteuliwa na Tume ya huduma za mahakama miaka mitatu iliyopita, ambao Bw Kenyatta alikuwa amekataa kuwaidhinisha kwa madai kuwa kuwa walikuwa na "madoa".
Majaji hao wataapishwa Jumatano.
Rais mpya pia alitangaza mwisho wa ruzuku za mafuta ya petroli na chakula. Pia alisema zilikuwa za gharama na hazikuwa na maana.
Bw Ruto pia aliagiza kwamba shuguli zote za huduma za utoaji wa vibali vya mizigo zirejeshwe katika bandari ya mombasa - kinyume na agizo la Bw Kenyatta ambapo shughuli zote za huduma za bandari zilihamishiwa Naivasha ili kuhakikisha malipo ya mkopo uliochukuliwa kutoka kwa Uchina kwa ajili ya ujenzi wa leri kati ya Mombasa na mji mkuu Nairobi.
Maagizo hayo yalikuwa ni sehemu ya ahadi alizotoa Bw Ruto wakati wa kampeni.
Unaweza pia kusoma:
- William Ruto:Je rais mpya wa Kenya anakabiliwa na changamoto zipi?
- Rais William Ruto aweka mikakati ya kupunguza gharama ya maisha Kenya
Xi na Putin kujadili kuhusu vita vya Ukraine katika mkutano - Kremlin
Kiongozi wa China Xi Jinping na Vladimir Putin wa Urusi watajadili kuhusu vita vya Ukraine na "mada nyingine za kimataifa na kikanda" katika mkutano wao utakaofanyika baadaye wiki hii, Kremlin inasema.
Wawili hao watakutana Uzbekistan katika mkutano wa kilele ambao utaonyesha "mbadala" kwa ulimwengu wa Magharibi, Kremlin ilisema.
Xi anafanya safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu kuanza kwa janga la corona.
Anawania muhula wa tatu wa kihistoria huku uhusiano wa Bw Putin na nchi za Magharibi ukizidi kudorora kutokana na uvamizi kwa Ukraine.
Bw Xi anaanza safari yake ya siku tatu nchini Kazakhstan siku ya Jumatano. Kisha atakutana na Putin siku ya Alhamisi katika Mkutano wa Wakuu wa Shirika la Shanghai Cooperation Organisation (SCO) huko Samarkand, ambao utaanza Septemba 15-16.
Bw Putin pia atakutana na viongozi wengine ikiwa ni pamoja na wale wa India, Pakistan, Uturuki na Iran lakini mkutano wake na kiongozi wa China "ni muhimu sana," alisema msemaji wa sera za kigeni wa Kremlin Yuri Ushakov.
China na Urusi kwa muda mrefu zimekuwa zikijaribu kuweka SCO, iliyoanzishwa mnamo 2001 na mataifa manne ya zamani ya Asia ya Kati, kama mbadala wa vikundi vya kimataifa vya Magharibi.
Huu ni mkutano wa pili wa viongozi hao wawili mwaka huu walikutana mara ya mwisho kwenye Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi mjini Beijing mwezi Februari.
Kufuatia mkutano wa Februari, viongozi hao wawili walitoa taarifa ya pamoja wakisema urafiki kati ya nchi zao "hauna kikomo".
Urusi iliivamia Ukraine siku chache baadaye hatua ambayo China haijashutumu wala kutoa sauti ya kuunga mkono.
Beijing, kwa kweli, imesema pande zote mbili ni za kulaumiwa.
China sio sehemu ya vikwazo vya kimataifa dhidi ya Urusi na biashara kati ya nchi hizo mbili imeendelea kukua.
William na Harry kutembea nyuma ya jeneza la Malkia hadi Westminster Hall
Wanawafalme William na Harry watatembea pamoja nyuma ya jeneza la Malkia katika maandamano huko London Jumatano.
Ndugu, pamoja na Mfalme, watafuata jeneza kwa miguu kutoka Buckingham Palace hadi Westminster Hall, ambapo mwili wa Malkia utalazwa .
Msafara huo utaondoka ikulu saa 14:22 BST na unatarajiwa kufika katika Ukumbi wa Westminster saa 15:00 BST.
Ibada itakayochukua takriban dakika 20 itaongozwa na Askofu Mkuu wa Canterbury.
Ndugu watatu wa Mfalme - Princess Anne, Prince Andrew, na Prince Edward - pia watatembea kwenye maandamano.
Camilla, mke wa mfalme , na Catherine, Princess wa Wales, watasafiri kwa gari, pamoja na Sophie, Countess wa Wessex, na Meghan, Duchess wa Sussex.
Inakuja baada ya Prince William na Prince Harry, wakiandamana na wake zao, kuonekana mbele ya umati uliokusanyika nje ya Windsor Castle siku ya Jumamosi.
Kikundi hicho kilifika kwa gari moja na kutumia takriban dakika 40 kusalimia waombolezaji na kutazama maua yaliyoachwa kwa bibi yao.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa ndugu hao kuonekana pamoja hadharani tangu mazishi ya babu yao, Duke wa Edinburgh, Aprili mwaka jana.
Wote wawili walikuwa kwenye ibada ya shukrani katika Kanisa Kuu la St Paul's Cathedral wakati wa sherehe za Jubilee ya Platinum mwezi Juni, lakini waliketi pande tofauti za kanisa kuu.
Unaweza pia kusoma
Urusi ilitumia $300m kisiri kushawishi siasa za mataifa mengine-Marekani
Urusi imetumia kwa siri zaidi ya $300m (£260m) tangu 2014 kuwashawishi wanasiasa katika zaidi ya nchi 24, Marekani imedai.
Madai ya Wizara ya Mambo ya Nje yametokana na tathmini ya kijasusi ya Marekani iliyotolewa Jumanne.
Afisa mkuu kutoka kwa utawala wa Rais Joe Biden alisema: "Tunadhani hii ni ncha ya barafu."
Urusi haijatoa maoni hadharani kuhusu suala hilo. Moscow yenyewe imeishutumu Marekani mara kwa mara kwa kuingilia mataifa mengine .
Mashirika ya Ujasusi ya Marekani "yanatathmini kwamba hizi ni takwimu za chini zaidi na kwamba Urusi ina uwezekano wa kuhamisha fedha za ziada kwa siri katika kesi ambazo hazijatambuliwa", afisa wa utawala wa Biden alisema wakati wa mkutano wa simu.
Afisa huyo alikuwa akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.
Tathmini ya kijasusi ya Marekani iliyotolewa kwa njia ya kebo haikutaja nchi maalum au maafisa wanaoaminika kulengwa na Urusi - lakini ilisema walipitia mabara manne.
Afisa huyo wa utawala alisema jumuiya ya kijasusi ya Marekani sasa inazifahamisha kwa faragha nchi zilizoathiriwa juu ya madai ya ufadhili wa siri wa Urusi. Arifa hizo zitabaki kuwa siri, afisa huyo aliongeza.
Chanzo cha utawala kinachofahamu matokeo hayo kinadaiwa kuwa Urusi ilitumia takriban dola 500,000 kuunga mkono chama cha mrengo wa kati cha Democratic Party cha Albania katika uchaguzi wa 2017 na pia ilisajili vyama au wagombeaji katika Bosnia, Montenegro na Madagascar, kulingana na shirika la habari la AFP.
Chanzo hicho pia kilisema Kremlin imetumia Brussels kama kitovu cha misingi na nyanja zingine ambazo zinawaunga mkono wagombea wa siasa kali za mrengo wa kulia.
Kampuni za uwongo zilisemekana kutumiwa kufadhili vyama vya Ulaya na kununua ushawishi mahali pengine.
Mamlaka ya Urusi hadi sasa haijatoa taarifa za umma kuhusu madai ya Marekani.
Hapo awali Moscow ililaumu shirika la kijasusi la Marekani CIA kwa kuingilia masuala ya nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono mapinduzi mbalimbali duniani.
Marekani imeingilia chaguzi za kigeni zaidi ya mara 80 duniani kote kati ya 1946-2000, bila kujumuisha mapinduzi au majaribio ya kubadilisha serikali, kulingana na hifadhidata iliyohifadhiwa na mtafiti wa Chuo Kikuu cha Carnegie Mellon Dov Levin.
Siku ya Jumanne, msemaji wa idara ya serikali Ned Price alitaja madai ya ufadhili wa siri ya Urusi kuwa "mashambulio dhidi ya uhuru".
Mwaka jana, maafisa wa ujasusi wa Marekani walitathmini katika ripoti kwamba Rais wa Urusi Vladimir Putin alikuwa na uwezekano wa kuidhinisha majaribio ya kushawishi uchaguzi wa Amerika wa 2020 ili kumpendelea Rais wa zamani Donald Trump.
Lakini ilisema hakuna serikali ya kigeni iliyoathiri matokeo ya mwisho.
Urusi ilitaja madai ya kuingiliwa kwa uchaguzi kuwa " hayana msingi".
Unaweza pia kusoma
Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja