Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Zelensky awatembelea wanajeshi katika mkoa wa Kharkiv

Rais wa Ukraine amefanya safari isiyo ya kawaida nje ya mji mkuu, Kyiv, ofisi ya rais inasema.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja.

  2. Afisa wa polisi aliyeweka orodha ya maafisa wenzake wa kike wa kuvutia afutwa kazi

    Afisa wa polisi amefukuzwa kazi kwa makosa ya utovu wa nidhamu ikiwa ni pamoja na kuweka orodha ya wanawake wenzake aliowaona wakivutia.

    Inspekta mkuu Paul Crouch, kutoka kitengo cha Polisi wa Usafiri wa Uingereza (BTP), pia alisema kuwa alisisimka alipokuwa akisoma kuhusu unyanyasaji wa kingono wa msichana wa miaka 17, mahakama ilifahamishwa.

    Afisa huyo mwenye makao yake mjini London amekuwa mraibu wa ngono kwa muda wa miaka 10.

    Aliachishwa kazi bila taarifa siku ya Ijumaa kufuatia kusikilizwa kwa kesi hiyo huko Camden.

    Jopo hilo liligundua kuwa Inspekta Crouch alitoa kauli za kibaguzi kuhusu mfanyakazi mwenzake wa kike, akidai alipandishwa cheo kutokana na jinsia yake.

    Katika matukio mawili tofauti, pia alitoa maoni ya kingono na ya kuudhi kuhusu mfanyakazi mwenza mkuu wa kike, mahakama ilisikia.

    Inspekta mkuu Crouch pia alimnyanyasa kingono mfanyakazi mwenzake wa kike katika kipindi kama hicho cha miaka 10.

  3. Katika picha: Ziara ya Zelensky mjini Kharkiv

    Kama tulivyokufahamisha hapo awali Rais Zelensky amefanya ziara nadra nje ya mji mkuu wa Kyiv.

    Alitembelea mkoa wa Kharkiv ambapo alizungumza na wanajeshi na kutoa zawadi.

    Ziara hii inakuja wakati mapigano makali yanaendelea katika eneo hilo huku wanajeshi wakijaribu kurejesha udhibiti wa eneo hilo kutoka kwa Warusi.

    Hizi hapa ni baadhi ya picha za ziara hiyo.

  4. Zelensky afanya ziara adimu nje ya Kyiv

    Rais wa Ukraine amefanya safari adimu nje ya mji mkuu, Kyiv, ofisi ya rais inasema.

    Bw Zelensky alitembelea nafasi za mstari wa mbele katika mkoa wa Kharkiv, ilisema.

    "Nataka kuwashukuru kila mmoja wenu kwa huduma yenu. Mnahatarisha maisha yenu kwa ajili yetu sote na nchi letu," rais aliwaambia wanajeshi.

    Mji huo wa kaskazini-mashariki umeshuhudia mapigano mabaya zaidi tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake nchini Ukraine tarehe 24 Februari.

    Huku hayo yakijiri wachambuzi wanasema Rais Zelensky amebadili mtazamo uliotabiriwa na wengi kuhusu uongozi wake.

    Mchekeshaji huyo wa zamani, sauti ya Kiukraine ya Paddington Bear, aliwahi kudhihakiwa kama mtu dhaifu.

    Sasa, analinganishwa na Winston Churchill.

    Ukakamavu wake katika kukabiliana na Urusi unasifiwa na wengi kuwa jambo muhimu katika utendaji wa ajabu wa nchi yake mwanzoni mwa vita hivi.

    Video zake za dharau kutoka mitaa ya mji mkuu, Kyiv, zilikuwa ishara ya kutotetereshwa na Urusi na rais wake.

  5. Port Harcourt: Mkanyagano katika kanisa la Nigeria wasababisha vifo vya watu 31

    Polisi wa Nigeria wamesema kuwa wameanzisha uchunguzi baada ya watu 31 kufariki katika ajali iliyotokea kusini mwa mji wa Port Harcourt. I

    Mkanyagano huo ulitokea katika uwanja wa michezo Jumamosi asubuhi ambapo kanisa lilikuwa likiwagawia maskini chakula, ambao baadhi yao walikuwa wamekesha hapo usiku kucha.

    Umati wa watu "wakawa wenye ghasia na wasioweza kudhibitiwa" na waandaaji walishindwa kutuliza hali, polisi wanasema.

    Wengi wa waliokufa katika mkanyagano huo walikuwa wanawake na watoto.

    Walioshuhudia wameliambia shirika la habari la AFP kwamba kulikuwa na msukumano mkali na baadhi walikanyagwa kwa miguu wakati watu waliokuwa wakijaribu kufika langoni walilazimishwa kurudi.

    "Walikuwa wakiwaambia watu 'Rudini, rudini nyuma," Chisom Nwachukwu alisema. "Baadhi ya watu waliokuwa wakisukumwa nyuma walikuwa wakiwaandama watu hao."

    Huduma za usalama na zile za dharura ziliitwa kwenye eneo la tukio ili kujaribu kudhibiti hali hiyo.

    Baadhi ya waliojeruhiwa wanatibiwa katika hospitali ya kijeshi ya Port Harcourt.

    Kanisa la King's Assembly lilisema "limehuzunishwa sana" na tukio hilo, na lilikuwa likikagua taratibu zake za usalama na usimamizi wa umati mkubwa wa watu.

    Kamishena wa polisi wa jimbo la Rivers, Eboka Friday, ametoa wito kwa makundi ya kidini na ya misaada "kuhakikisha yanafanya kazi na polisi kwa ajili ya usalama na udhibiti wa mkusanyiko wa watu wengi "wakati wa kuandaa programu hizo katika siku zijazo.

  6. Urusi yadai kuwaua wanajeshi 300 wa Ukraine katika muda wa saa 24 zilizopita

    Wizara ya Ulinzi ya Urusi inasema makombora yake yameharibu ghala kubwa la silaha za jeshi la Ukraine huko Kryvyi Rih - mji alikozaliwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

    Msemaji wa wizara hiyo Igor Konashenkov anadai katika muda wa saa 24 zilizopita zaidi ya wanajeshi 300 wa Ukraine wameuawa.

    Pia anadai kuwa ngome kadhaa za kijeshi yameshambuliwa, ikiwa ni pamoja na mfumo wa ulizi wa Urusi kudungua ndege ya kivita ya Ukraine chapa SU-25 mjini Dnipro.

    Anasema: "Kwa jumla, kutokana na mashambulio ya angani, zaidi ya wanajeshi 300 na hadi vitengo 50 vya kijeshi na silaha za wanajeshi wa Ukraine ziliharibiwa."

  7. Uuzaji wa Chelsea kukamilika Jumatatu

    Uuzaji wa Klabu ya Soka ya Chelsea unatarajiwa kukamilika Jumatatu baada ya "makubaliano ya mwisho na ya uhakika" kufikiwa na muungano unaoongozwa na mfanyabiashara wa Marekani Todd Boehly.

    Chelsea iliuzwa mwezi Machi kabla ya mmiliki Roman Abramovich kuwekewa vikwazo kutokana na uhusiano wake na Rais wa Urusi Vladimir Putin, ambaye alikuwa ameamuru uvamizi wa Ukraine hivi majuzi.

    Ligi ya Premia na serikali ya Uingereza zimeidhinisha uuzaji huo wa £4.25bn.

    Klabu hiyo imekuwa ikifanya kazi chini ya leseni maalum ya serikali ambayo inaisha tarehe 31 Mei.

    Abramovich, ambaye alinunua Chelsea mwaka wa 2003, alisema "amefurahishwa na kukamilika kwa mchakato huo".

    Aliongeza: "Ninapoikabidhi Chelsea kwa wamiliki wake wapya, ningependa kuwatakia mafanikio mema, ndani na nje ya uwanja.

    "Imekuwa heshima ya maisha kuwa sehemu ya klabu hii - ningependa kuwashukuru wachezaji wote wa zamani na wa sasa wa klabu, wafanyakazi, na bila shaka mashabiki kwa miaka miaka tuliyokuwa pamoja"

  8. Urusi yaondoa kikomo cha umri wa miaka 40 kwa wanajeshi wapya nchini Ukraine

    Urusi imetupilia mbali ukomo wa umri wake kwa wanajeshi wenye taaluma, na hivyo kutoa fursa kwa wataalamu zaidi wa kiraia kuajiriwa kwa ajili ya mzozo wa Ukraine.

    Rais Vladimir Putin ametia saini sheria inayowawezesha watu walio na zaidi ya umri wa miaka 40 kujiunga na jeshi.

    Hapo awali jeshi lilikuwa na ukomo wa miaka 18-40 kwa Warusi na 18-30 kwa wageni.

    Urusi inawasilisha sheria hiyo kama hatua ya kuajiri wataalamu zaidi wa kiufundi.

    Sheria hiyo mpya inasema wataalamu wanatakiwa kutumia silaha zenye ubora wa hali ya juu na "uzoefu unaonyesha kuwa wanakuwa hivyo wakiwa na umri wa miaka 40-45".

    Madaktari zaidi, wahandisi na wataalam wa mawasiliano wanaweza pia kuajiriwa.

    Wataalamu wa kijeshi wa Ukraine na nchi za Magharibi wanasema Urusi imepata hasara kubwa katika vita hivyo: takriban 30,000 waliuawa, kulingana na Ukraine, wakati serikali ya Uingereza inakadiria idadi ya watu 15,000.

    Urusi ilitoa jumla ya wanajeshi wake 1,351 waliouawa nchini Ukraine tarehe 25 Machi, jambo ambalo haijasasisha.

    Rais Putin ameepuka kuangazia kwa kiasi kikubwa kwa kile Urusi inachokiita "operesheni yake maalum ya kijeshi" nchini Ukraine.

    Lakini mwezi Machi wizara ya ulinzi ya Urusi ilikiri kwamba baadhi ya watu walioandikishwa kujiunga na jeshi walihusika katika mzozo huo na baadhi walichukuliwa mateka na vikosi vya Ukraine.

    Wizara ya ulinzi ilisisitiza kuwa haikuwa sera rasmi kutuma wanajeshi vitani.

    Unaweza pia kusoma:

  9. Burkina Faso : Miili miwili zaidi ya wachimba migodi yapatikana

    Maiti mbili zaidi zimepatikana kutoka kwa mgodi wa zinki uliofurika nchini Burkina Faso.

    Mamilioni ya lita za maji yametolewa nje ya sehemu inayomilikiwa na kampuni ya Trevali ya Canada huku juhudi za uokoaji zikiendelea.

    Kesi hiyo imezua taharuki nchini humo .

    Jumla ya wachimba migodi wanane walikuwa wamenaswa huko na mvua isiyotarajiwa wiki sita zilizopita.

    Katika hatua hii wawili wa kundi hilo bado hawajapatikana.

    Trevali na serikali ya Burkinabè wameanzisha uchunguzi kuhusu sababu za tukio katika mgodi wa zinki wa Perkoa, ambao uko takriban kilomita 100 (maili 60) magharibi mwa mji mkuu, Ouagadougou.

    "Tumeleta wataalam kutoka duniani kote. Tumepata watu kutoka Australia, kutoka Afrika Kusini, kutoka Kanada," Ricus Grimbeek, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Migodi la Trevali, alisema kuhusu majaribio yanayoendelea ya uokoaji.

    Kufikia sasa hakuna mwili wowote ambao umetambuliwa rasmi.

    Wachimba migodi hao wanane - Mtanzania mmoja, Mzambia mmoja na Wabukinabe sita - walikuwa wakifanya kazi katika kina cha zaidi ya 500m.

  10. Ukraine yaanza kupokea makombora hatari ya Harpoon kukabiliana na Urusi

    Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Oleksii Reznikov amesema Ukraine imeanza kupokea makombora ya kivita aina ya Harpoon kutoka Denmark na ndege za zisizo na rubani kutoka Marekani.

    "Ulinzi wa pwani wa nchi yetu hautaimarishwa tu na makombora ya Harpoon - yatatumiwa na timu zilizofunzwa za Ukraine," Reznikov aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

    Reznikov alisema usambazaji wa makombora ya Harpoon ni matokeo ya ushirikiano kati ya nchi kadhaa.

    Ukraine imekuwa ikiomba silaha za kisasa zaidi lakini hadi sasa misaada mingi imekuwa katika mifumo ya masafa mafupi kama vile silaha za kukinga vifaru.

    Marekani inazingatia ombi kutoka Ukraine kuipatia Kyiv silaha nzito za masafa marefu lakini bado haijafikia uamuzi wa mwisho.

    Unaweza pia kusoma:

  11. Wanajeshi wawili wa Rwanda waliokamatwa DRC watambulishwa kwa vyombo vya habari

    Wanajeshi wawili wanaodaiwa kuwa wa Rwanda waliokamatwa katika mpaka wa DRC na nchi hiyo wametambulishwa kwa wanahabari .

    Koplo Élysée Nkundabangezi na Pte Ntwari Gad walikamatwa na wakazi wa Bwisha, kilomita 20 kutoka mpaka wa Rwanda alisema JeneralI Sylvain Ekenge, msemaji wa jeshi wa mkoa wa Kivu-Kaskazini.

    Msemaji huyo wa jeshi aliongeza kuwa wanajeshi hao wawili wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) waliingia DRC, Jumatano iliyopita ili kushambulia kambi ya kijeshi ya Runangabo, kabla ya kukamatwa na watu.

    Taarifa iliyotolewa na Jeshi la ulinzi la Rwanda (RDF) hapo jana iliomba kuachiliwa kwa wanajeshi hao waliotekwa nyara wakiwa kwenye doria na Vikosi vya Wanajeshi wa DRC na FDLR [kundi la waasi lenye asili ya Rwanda], baada ya uvamizi katika ardhi ya Rwanda Mei 23, 2022.

    Hivi majuzi serikali ya Congo iliishutumu Rwanda kwa kusaidia kundi la wanamgambo wa M23, tuhuma ambazo Rwanda inakanusha, lakini badala yake, kama ilivyokaririwa katika barua hiyo, inaishutumu DRC kwa kushirikiana na FDLR, ambayo inatuhumiwa kufanya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

    Mapigano mapya yalizuka kati ya FARDC na M23[Kundi linaloongozwa na Watutsi wa Kongo] yameleta biashara ya shutuma za mashambulizi kati ya Rwanda na DRC, huku nchi zote mbili zikilaumiana kuunga mkono makundi yao yenye silaha yaliyoasi.

    Karibu watu 37,000 wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano ya hivi karibuni, kulingana na Baraza la Wakimbizi la Norway.

    Soma:

  12. Hali ya taharuki yatanda Jerusalem kabla ya maandamano ya vijana wa Israel

    Maelfu ya Wayahudi wa Israel wanatarajiwa kufanya maandamano katika maeneo ya Waislamu katika Mji Mkongwe wa Jerusalem huku kukiwa na onyo kwamba Wapalestina huenda wakazusha vurugu.

    Tukio hilo la kila mwaka linakuja wakati wamvutano mkubwa kufuatia miezi kadhaa ya matukio mabaya.

    Maandamano ya Bendera hufanyika siku ya Israeli ya Jerusalemu, kusherehekea kutekwa kwake kwa Jerusalemu Mashariki katika vita vya 1967.

    Israel inauchukulia Jerusalem nzima kama mji mkuu wake, jambo ambalo lilikataliwa na nchi nyingi na Wapalestina.

    Hali ya mji huo inaendelea kuwa chanzo cha mzozo wa Israel na Palestina.

    Wapalestina wanadai Jerusalem Mashariki inayokaliwa na Israel kama mji mkuu wa taifa lao linalotarajiwa siku za usoni, ingawa Israel inasema mji huo hautawahi kugawanywa tena.

  13. Liverpool v Real Madrid: Fainali ya Ligi ya Mabingwa ilicheleweshwa kwa 'sababu za kiusalama'

    Liverpool wanataka uchunguzi ufanyike kuhusu "maswala yasiyokubalika" yanayowakabili mashabiki ambayo yalisababisha fainali yao ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Real Madrid kucheleweshwa.

    Uefa ilichelewa kuanza kwa zaidi ya dakika 30, ikitaja "sababu za kiusalama".

    Mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Stade de France jijini Paris haikuanza hadi 20:36 BST, huku Real ikiichapa Liverpool 1-0.

    Polisi waliokuwa nje ya uwanja walirusha gesi ya kutoa machozi huku idadi ndogo ya wafuasi wakijaribu kuvuka vizuizi vya usalama.

    Mlinzi wa Liverpool Andy Robertson alisema mpangilio wa mechi hiyo ulikuwa "shida".

    Maafisa wa siku ya mechi wa Polisi wa Merseyside walituma ujumbe kwenye Twitter kwamba ilikuwa "mechi mbaya zaidi ya Ulaya kuwahi kufanya kazi au uzoefu".

    Picha ziliibuka katika mkusanyiko wa umati mkubwa wa mashabiki waliokuwa wakipanga foleni kuingia.

    Wengi walidai walikuwa wamefika uwanjani saa kadhaa kabla ya kuanza lakini walizuiwa kuingia ndani.

  14. Putin ahimizwa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Zelensky

    Viongozi wa Ufaransa na Ujerumani wamemhimiza Vladimir Putin wa Urusi kufanya "mazungumzo ya moja kwa moja [na] mazito" na rais wa Ukraine, ofisi ya kansela wa Ujerumani ilisema.Emmanuel Macron na Olaf Scholz walizungumza na Bw Putin kwa simu kwa dakika 80.

    Wawili hao "walisisitiza kusitishwa kwa mapigano mara moja na kuondolewa kwa wanajeshi wa Urusi", ofisi ya kansela ilisema.Kiongozi wa Urusi alisema Moscow iko tayari kuanza tena mazungumzo na Kyiv, kulingana na Kremlin.

    Haikutaja uwezekano wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Bw Putin na mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.

    Rais wa Ukraine hapo awali alisema "hakuwa na shauku" ya mazungumzo, lakini akaongeza kuwa kuna uwezekano wa kuhitajika kumaliza mzozo huo.Wajumbe wa Urusi na Ukraine wamefanya duru nyingi za mazungumzo kwa mbali na ana kwa ana tangu Urusi ilipovamia tarehe 24 Februari, lakini juhudi zimekwama hivi karibuni.

    Ufaransa na Ujerumani pia zilimtaka Bw Putin kuwaachilia huru wapiganaji 2,500 wa Ukraine waliochukuliwa kama wafungwa wa vita katika kiwanda cha kutengeneza chuma cha Azovstal huko Mariupol.Kiwanda hicho kilichokuwa kinasambaa kilikuwa cha mwisho katika mji wa bandari wa kusini, ambao ulistahimili mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa vikosi vya Urusi na sasa ni magofu.

    Unaweza pia kusoma:

  15. Urusi haitatumia silaha za kinyuklia nchini Ukraine, asema balozi wake nchini Uingereza

    Balozi wa Urusi nchini Uingereza ameiambia BBC haamini kuwa nchi yake itatumia mbinu za kinyuklia katika vita dhidi ya Ukraine.

    Andrei Kelin alisema kuwa kulingana na sheria za kijeshi za Urusi, silaha kama hizo hazitumiwi katika migogoro kama hii.

    Urusi ina masharti magumu sana ya matumizi ya silaha hizo , alisema, haswa wakati uwepo wa serikali unatishiwa.

    "Haina uhusiano wowote na operesheni ya sasa," aliambia Sunday Morning.

    Wakati Vladimir Putin aliweka vikosi vyake vya nyuklia katika hali ya tahadhari mwishoni mwa Februari, mara tu baada ya uvamizi, ilionekana kuwa onyo.

    Bw Putin alilaumuru hatua hiyo kutokana na uchokozi wa nchi za Magharibi na Nato. Lakini Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace alilitaja kuwa ni jaribio la kuwavuruga watu kutoka "nini kinaendelea vibaya nchini Ukraine", akisema Urusi ilikuwa nyuma ya ratiba ya uvamizi wake baada ya siku chache tu, na kujaribu "kukumbusha ulimwengu" ilikuwa na kizuizi.

    Silaha za nyuklia za mbinu ni zile zinazoweza kutumika kwa umbali mfupi, kinyume na silaha za nyuklia za "kimkakati" ambazo zinaweza kurushwa kwa umbali mrefu zaidi na kuibua hofu ya vita vya nyuklia.

    Unaweza pia kusoma:

  16. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja leo leo Jumapili Mei tarehe 29 2022