Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Onyo la uhaba wa chakula kutokana na shambulizi la mji wa Odesa Ukraine

Katika picha zilizochapishwa mtandaoni na jeshi la Ukraine, wazima moto wanaonekana wakikanyaga vifusi vya kile kilichokuwa kituo cha biashara na ghala la chakula

Moja kwa moja

  1. Nakufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Putin yuko tayari kwa vita virefu nchini Ukraine- Mkuu wa kijasusi wa Marekani

    Vladimir Putin anajiandaa kwa vita vya muda mrefu nchini Ukraine, Marekani inaonya, na ushindi wa Urusi katika eneo la mashariki la Donbas huenda usimalize mashambulizi yake.

    Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa Avril Haines aliambia Baraza la Seneti kwamba miezi michache ijayo inaweza kuona hatua za Urusi zikiongezeka na kuwa zisizotabirika zaidi.

    "Mtindo wa sasa unaongeza uwezekano kwamba Rais Putin atageukia njia kali zaidi," Haines anasema.

    Anaonya kwamba Urusi inaweza kutafuta daraja la ardhi kuelekea eneo lililojitenga la Moldova la Transnistria na anasema kuna uwezekano Rais Putin atataka kuweka sheria ya kijeshi nchini Urusi.

    Haines anasema Putin anategemea azimio la Marekani na washirika wa Ulaya wa Ukraine kudhoofika kwa muda.

    Lakini anafikiri Kremlin itaidhinisha tu matumizi ya silaha za nyuklia ikiwa Putin ataona "tishio lililopo" kwa Urusi.

  3. Tembo wa Zimbabwe waua watu 60 mwaka huu- maafisa

    Tembo wa Zimbabwe wameua watu 60 kufikia sasa mwaka huu, kulingana na msemaji wa serikali. Akiandika kwenye Twitter, Nick Mangwana, alisema ni mada ya kusikitisha.

    "Suala la Migogoro ya Binadamu/Wanyamapori limekuwa la kusisimua sana. Mwaka huu pekee Wazimbabwe 60 wamepoteza maisha kutokana na tembo na 50 kujeruhiwa. Mwaka 2021, 72 walipoteza maisha.

    Zimbabwe itafanya Mkutano wa Tembo mwezi huu." Katika wilaya moja, Bubi, tembo "wamekula kila kitu mashambani na sasa wanahamia makazi," aliandika.

    Pia aliongeza kuwa wanaingia kwenye migogoro na binadamu, na kusababisha tembo waliojeruhiwa ambao wanakuwa "wakali na wasioweza kudhibitiwa".

    Inakadiriwa kuwa kuna tembo 100,000 nchini Zimbabwe, na idadi hiyo inaongezeka. Mtaalamu mmoja wa wanyamapori, T

    inashe Farawo, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba huenda hali ikawa mbaya zaidi.

    "Tishio huenda likaongezeka tunapoelekea msimu wa kiangazi wakati mifugo itakuwa ikienda kutafuta maji na chakula," AFP inamnukuu akisema.

  4. Watu 14 wafariki,wakiwemo watoto, katika shambulio la DR Congo

    Watu 14 wamefariki, wakiwemo watoto, katika shambulio lililotokea katika jimbo la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

    Tukio hilo lililotokea Jumatatu karibu na mji wa Fataki lilikuwa kwenye kambi ya watu waliopoteza makazi yao.

    Washukiwa wa wanamgambo kutoka kundi la Codeco wamelaumiwa na vyanzo vya ndani. Pia walilaumiwa kwa shambulio kwenye mgodi wa dhahabu huko Djugu katika jimbo hilo hilo siku ya Jumapili, ambalo lilisababisha vifo vya makumi ya watu.

  5. Mfanyikazi wa zamani wa Meta nchini Kenya awasilisha kesi mahakamani

    Nchini Kenya mfanyakazi wa zamani wa kampuni mama ya Facebook, Meta, amewasilisha kesi mahakamani akidai kuwa mazingira duni ya kazi yanakiuka katiba ya nchi.

    Ombi la Daniel Motaung linasema wafanyakazi wa ndani, ambao husimamia machapisho ya Facebook, wanapata malipo yasiyo ya kawaida na kupokea usaidizi duni wa afya ya akili baada ya kutazama maudhui yanayoathiri mawazo.

    Bw Motuang anasema kazi hiyo ya kudhibiti imemsababishia msongo wa mawazo unaotokana na kiwewe.

    Alifukuzwa kazi baada ya kujaribu kuwashawishi makumi ya wenzake kuunda muungano wa kutetea maslahi yao.

    Kesi hiyo inataka fidia ya fedha na ukaguzi huru wa haki za binadamu katika ofisi ya Bw Motaung.

    Pia inataka mahakama iamuru kwamba haki za muungano zilindwe.

    Msemaji wa Meta alisema ilihitaji washirika wake kutoa malipo, faida na usaidizi unaoongoza katika tasnia.

    Kampuni Sama,inayotoa huduma za nje, hapo awali ilikanusha madai ya kuwadhulumu wafanyikazi wake.

  6. Chuo kikuu Ethiopia chakanusha kusaidia uharibifu mkubwa Tigray magharibi

    Chuo kikuu cha Gondar nchini Ethiopia kimekanusha ripoti kwamba baadhi ya wataalam wake waliwasaidia wanamgambo wa Amhara kuharibu ushahidi wa makaburi ya halaiki yenye miili ya watu wa Tigray.

    Walioshuhudia waliambia BBC kwamba wameona wataalamu hao wakiwashauri wanamgambo.

    Katika barua kwa BBC, chuo hicho kikuu kilielezea ripoti hiyo ka "shutumiwa zisizo na uthibitisho".

    Pia ilikanusha kuwa kulikuwa na ushahidi wowote kwamba miili ya watu wa Tigray ilipatikana kwenye makaburi ya halaiki.

    Ikiwa kitu kama hicho kingegunduliwa basi "timu ya watafiti... ingekuwa ya kwanza kukiri na kutoa ushahidi", chuo kikuu kilisema.

    "Chuo kikuu ni mojawapo ya taasisi za elimu zinazoheshimika zaidi za utafiti nchini Ethiopia ambayo imejitolea kutatua baadhi ya masuala muhimu zaidi ya jamii," iliongeza.

  7. Goodluck Jonathan: Rais wa zamani wa Nigeria akataa uteuzi wa APC

    Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan amekataa kupokea fomu ya uteuzi wa Urais , akisema kuwa ilinunuliwa bila ridhaa yake.

    Fomu hiyo ilikuwa ya chama tawala cha All Progressives Congress (APC) ambacho kilimshinda Bw. Jonathan 2015 baada ya kuwa madarakani kwa miaka mitano.

    Kundi la wafuasi lilinunua fomu ya uteuzi kwa niaba yake siku ya Jumatatu, mwelekeo wa unaotumiwa na wawaniaji kukununua fomu hiyo kupitia wandani wao.

    Lakini taarifa iliyotolewa na msemaji wa rais huyo wa zamani ilisema Bw. Jonathan "hakuwa na ufahamu wa hatua hii na hakuidhinisha".

    "Tunasema kwamba ikiwa rais wa zamani alitaka kugombea uchaguzi, angeweka wazi nia yake kwa umma na wal asio kutumia mlango wa nyuma," ilisema taarifa hiyo.

    Vyama vikuu vya kisiasa nchini Nigeria vinatarajiwa kufanya uteuzi baadaye mweizi huu ili kufikia makataa ya Tume ya Uchaguzi ya Juni 3 kuwasilisha wagombea wao wa uchaguzi wa Februari 2023.

    Inagharimu karibu dola 240,000 au £195,000 kununua makaratasui ya uteuzi wa APC.

    Yeyote atakayepata uteuzi wa APC wa uchaguzi atakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa chama cha PDP.

  8. Wafananisha bomu la ardhini na Magimbi Kenya

    Bomu la ardhini la enzi za ukoloni ambalo halijalipuka lilmegunduliwa katika kijiji kimoja katikati mwa Kenya ambapo baadhi ya wakazi walidhania kuwa ni mzizi wa mboga za kienyeji.

    Polisi wa Kenya walisema wanakijiji wanaohusika walikusanyika karibu na kitu hicho, wengine wakihoji "kuwa ni kombora huku wengine wakidai kuwa ilikuwa mizizi ya mboga iliyokua sana".

    Maafisa wa Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), walienda mara moja mara baada ya kupewa taarifa na kubaini kitu hicho kuwa ni bomu. "Kuna uwezekano mkubwa liliachwa na vikosi vya Uingereza wakati wa ghasia za Mau Mau Mwaka 1953, ambapo sehemu za misitu ya Mlima Kenya na Aberdare zilikumbwa na mashambulio ya angani, ili kuwaondoa wapiganaji wa Mau Mau," ofisi ya DCI ilisema

    Bomu hilo lilipaswa kulipuliwa kwa usalama siku ya Jumatatu, DCI ilisema.

    Wakenya wamekuwa wakilinganisha kisa hicho na kile kilichotokea wiki kadhaa dhidi ya simba aliyedhaniwa kupotea katikati mwa Kenya.

    Maafisa wa wanyama pori wa Kenya waliitwa kwenye eneo hilo baada ya mfanyakazi wa shamba kuona kile alichofikiri ni simba aliyejificha chini ya kichaka kwenye ukingo wa boma hilo.

    Lakini ikawa ni mfuko tu na picha kubwa ya kichwa cha simba juu yake.

    Hata hivyo, Katika tukio la hivi punde zaidi, kile kilichofikiriwa kuwa mboga ya mizizi maarufu kiligeuka kuwa "sheria hatari ya kijeshi", kulingana na polisi.

    • Simba wa karatasi awahangaisha wakazi Kenya
    • Vita vya Ukraine: Je! bomu la kutawanya lilitumika katika shambulio kwenye kituo cha Ukraine?
  9. Serikali ya Tanzania imetoa ruzuku ya bilioni 100 kwenye mafuta ili kupunguza bei ya bidhaa hiyo

    Serikali ya Tanzania imetoa ruzuku ya bilioni 100 kwenye mafuta ili kupunguza bei ya bidhaa hiyo kuanzia June 1, 2022.

    Akiongea Bungeni wakati wa kutoa mkakati wa kukabiliana na kupanda kwa bei ya mafuta, Waziri wa Nishati January Makamba anasema "Ruzuku hii (Shilingi Bilioni 100) inatolewa kwa kupunguza matumizi ya Serikali katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2021/22.

    Anaongeza kuwa Kutolewa kwa ruzuku hii hakutagusa miradi ya maendeleo ambayo inaendelea. Hatua hii imekuja baada ya Bunge la Tanzania wiki iliyopita kumpa Waziri huyo muda wa siku tano kuhakikisha anakuja na mkakati wa kupunguza bei ya mafuta ili kupunguza mzigo kwa wananchi.

    Mbali na hatua hiyo Waziri huyo pia ameelezea mipango mingine ya kukabiliana na kupanda kwa bei ya mafuta ikiwemo kuruhusu watu wenye uwezo wa kuleta mafuta kufanya hivyo na kuwa na hifadhi ya mafuta ya kimakakati ambayo itawezesha kupata unafuu wa mafuta na mpango wa Ushirikiano wa kujenga maghala makubwa ya mafuta kwa ajili ya kuuza nje ya nchi.

    Bei za mafuta zinaweza kupungua zaidi kuanzia Agasti 2022.

    • Mzozo Ukraine: Je dunia inategemea vipi mafuta na gesi ya Urusi?
    • Mzozo wa Ukraine: Kwa kiasi gani dunia inategemea mafuta na gesi ya Urusi?
  10. Makombora yashambulia kituo cha biashara Odesa

    Makombora yaliyotumiwa yanaweza kuwa ya enzi za Usoviet lakini uharibifu uliofanyika bado ni mkubwa.

    Katika picha zilizochapishwa mtandaoni na jeshi la Ukraine, wazima moto wanaonekana wakikanyaga vifusi vya kile kilichokuwa kituo cha biashara na ghala.

    Moshi mnene na mweusi ulisambaa katika mji huo wa bandari lakini kwasababu ya amri ya kutotoka nje mitaa ilikuwa tupu wakati makombora yalipopigwa usiku.

    Mamlaka inasema mtu mmoja alifariki na wengine watano kupelekwa hospitalini.

    Mashambulizi hayo yalitokea Jumatatu jioni, siku hiyo hiyo ambayo rais wa Baraza la Ulaya alikuwa katika mji huo.

    Charles Michel alisema ameona maghala yaliyojaa nafaka, ngano na mahindi huko Odesa ambayo yalikuwa tayari kusafirishwa nje ya nchi lakini yamezuiwa.

    Tishio la usalama wa chakula duniani ni jambo lililosisitizwa na Rais Zelensky wa Ukraine katika hotuba yake ya usiku.

    Alisema kuwa bila Ukraine kusafirisha nje, nchi kadhaa ...walikuwa "tayari wana uhaba wa chakula" na kwamba hali inaweza "kuwa, kusema ukweli, ya kutisha".

    Unaweza pia kusoma

  11. Shindano la Miss Rwanda lasitishwa kutokana na madai ya ubakaji

    Serikali ya Rwanda imesitisha shindano la urembo la Miss Rwanda kufuatia kukamatwa kwa mwandalizi wake mwezi uliopita.

    Hatua hiyo imekuja baada ya uchunguzi wa unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya Dieudonné Ishimwe, mtendaji mkuu wa Rwanda Inspiration Backup, ambayo huandaa shindano hilo.

    Bw Ishimwe alikamatwa mwezi uliopita kwa madai ya unyanyasaji wa kingono kwa washindani. Hajajibu tuhuma hizo.

    "Wizara ya Vijana na Utamaduni inafahamisha umma kwa ujumla kwamba shindano la urembo la Miss Rwanda limesimamishwa hadi uchunguzi ukamilike," wizara ya utamaduni ya Rwanda ilisema katika taarifa yake siku ya Jumatatu.

  12. Mtoto wa Rais Museven afikishwa mahakamani kwa kuutaka Urais wa Uganda

    Mahakama ya kikatiba ya Uganda imemtaka mtoto wa Rais Yoweri Museveni, Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kujibu shtaka analotuhumiwa la kueleza nia yake ya kuwania urais akiwa bado anahudumu katika jeshi la nchi hiyo, tovuti ya Daily Monitor imeripoti.

    Wakili wa haki za binadamu Gawaya Tegulle aliiomba mahakama katika mji mkuu, Kampala, kumzuia Jenerali Kainerugaba kufanya shughuli za kisiasa akiwa bado anatumikia jeshi.

    Gawaya pia anataka jenerali huyo afunguliwe mashtaka ya uhaini kufuatia madai yake ya njama ya kumrithi babake kwa kutumia mbinu "haramu".

    Jenerali Kainerugaba, kamanda wa jeshi la nchi kavu la Uganda, ana siku 10 kuwasilisha majibu yake. Mnamo tarehe 2 Mei, alitangaza mipango ya kuzindua mpango wa kisiasa, na kuchochea uvumi kwamba alinuia kumrithi babake wa muda mrefu.

    Mnamo Machi 8, alitangaza kustaafu kutoka kwa jeshi kwenye Twitter lakini Rais Museveni alikataa. Rais Museveni amekanusha kumuandaa mwanawe kuchukua wadhifa wake.

  13. Kim Jong Un ampongeza rais Putin kwa Siku ya Ushindi

    Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un ametuma salamu za pongezi kwa Rais Vladimir Putin baada ya kusherehekea Siku Ushindi ya Urusi, akielezea "mshikamano thabiti" wa nchi yake na Moscow, shirika la habari la Korea Kaskazini KCNA limeripoti.

    Katika barua yake iliyotumwa tarehe 9 Mei, Kim anasema "Mshikamano madhubuti wa muda mrefu kwa sababu ya watu wa Urusi kung'oa vitisho vya kisiasa na kijeshi na usaliti wa vikosi vya adui".

    Kiongozi wa Korea Kaskazini pia ameelezea imani yake kwamba uhusiano wa kimkakati na wa jadi wa urafiki kati ya nchi hizo mbili utakuwa kwa kasi".

    Hivi karibuni Korea Kaskazini imeangazia uhusiano wake wa karibu na Urusi, na kuunga mkono hadharani Moscow juu ya uvamizi wake nchini Ukraine.

    Mwezi Februari, ililaumu mzozo wa Ukraine juu ya "sera ya kivita" ya Marekani na Magharibi.

  14. Mpango wa wanaotafuta hifadhi Rwanda kuchukua muda kutekelezwa- Patel

    Mpango wa kupeleka baadhi ya watu wanaotafuta hifadhi nchini Rwanda "utachukua muda" kuanza kutekelezwa, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Priti Patel anasema.

    Mpango huo unahusisha watu wanaotafuta hifadhi baada ya kuonekana kuwa wameingia nchini Uingereza kinyume cha sheria ambapo watasafirishwa hadi nchini Rwanda ambapo maombi yao yatashughulikiwa.

    Alisema mpango wa kupeleka baadhi ya watu kuomba hifadhi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki utatoa "ishara ya wazi" kwamba hakutakuwa na haki ya kusalia Uingereza.

    Wizara ya Mambo ya Ndani imesema itaanza kuwafahamisha watu kwamba watahamishwa hadi Rwanda hivi karibuni, lakini ilikiri kwamba ucheleweshaji ulitarajiwa kutokana na changamoto za kisheria.

    Aliongeza kuwa serikali imejitolea kutekeleza mpango huo na itatumia "kila chombo na kila sheria tuliyo nayo" kumuondoa yeyote anayefika "kinyume cha sheria".

    Alipoulizwa kama ana uhakika mpango huo utafanya kazi na utachukua muda gani kuanza, Bi Patel alisema: "Nimesema tangu siku ya kwanza, hata niliposaini mkataba na kutangaza ushirikiano, kwamba hii itachukua muda na itachukua muda kwa sababu mbalimbali.

    Idara ya mambo ya ndani ilisema serikali "ina uwezo wa kuwaweka kizuizini watu wanaosubiri kuondolewa kwao kutoka Uingereza", na kuongeza kwamba safari za kwanza za ndege zilitarajiwa kufanyika katika miezi ijayo.

    Hata hivyo, mawakili wa baadhi ya wale watakaosafirishwa hadi Rwanda wanatarajiwa kuwasilisha madai ya kusitisha kuondolewa kwao.

    Uamuzi huo ulikuja baada ya kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya vivuko vidogo vya boti katika milango ya bahari Uingereza, huku zaidi ya watu 6,000 wakivuka mpaka sasa kwa mwaka huu. Takwimu za Ofisi ya Mambo ya Ndani zinaonyesha watu 28,526 walivuka mwaka 2021, kutoka 8,466 mwaka uliopita.

  15. Mbwa atunukiwa tuzo ya heshima ya rais kwa kugundua mabomu Ukraine

    Rais wa Ukraine Vladimir Zelensky amemtunukia tuzo ya heshima ya Rais mbwa aliyepewa jina Pattern kwa huduma zake tangu uvamivi wa Urusi.

    Mbwa huyo mwenye umri wa miaka miwili na nusu amekuwa shujaa wa kitaifa nchini Ukraine, ishara ya upinzani wa Ukraine dhidi ya Urusi. Mbali na kubaini marundo zaidi ya 200 ya nyaya zinazohusishwa na vipulizi, mwezi April alitajwa kugundua mabomu zaidi ya 90.

    Rais Zelensky alisema: "Ninataka kuwatunuku mashujaa hawa wa Kiukreni ambao tayari wanasafisha ardhi yetu."Rais Zelensky alisema katika hafla ya Jumapili huko Kyiv kwamba mbwa huyo sio tu anasaidia kubaini vilipuzi, lakini pia hufundisha watoto wetu kanuni muhimu za usalama katika maeneo ambayo kuna hatari.Sherehe ya tuzo hiyo pia ilihudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, ambaye aliwasili Ukraine siku ya Jumapili. Justin Trudeau alitangaza kwamba Canada itatoa silaha zaidi na vifaa kwa Ukraine.Rais Zelensky alikabidhi medali kwa mbwa huyo na mmiliki wake My Hello Ilyo. Mbwa huyo mdogo kiumbo amekuwa maarfu nchini chini ya kitengo cha usalama tangu uvamizi wa Urusi,

  16. Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan kuwania tena urais

    Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan amejitosa tena kuwania kurejea madarakani katika uchaguzi wa mwaka ujao baada ya kuhama chama cha siasa, BBC inaelewa. Bw Jonathan amejiunga na chama tawala cha All Progressives Congress (APC) ambacho kilimshinda mwaka 2015 baada ya kukaa madarakani kwa miaka mitano.

    Kundi la wafuasi lilinunua fomu ya uteuzi kwa niaba yake siku ya Jumatatu, na kuendeleza mtindo wa wanaotaka kutumia washirika kununua fomu hiyo. Uamuzi wake wa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho cha kuwania urais akiwa na chama cha APC umewashangaza sana Wanigeria wengi, hasa wale wa chama chake cha zamani, People’s Democratic Party (PDP).

    Kwa muda wa miezi kadhaa, uvumi ulikuwa umezagaa kuhusu kujithusisha kwake kwa siri katika chama tawala lakini si Bw Jonathan wala washirika wake walikuwa wametoa maoni yao.

    Haijabainika kwa nini Bw Jonathan aliamua kubadili vyama, lakini kumekuwa na fununu kwamba amekuwa hana furaha kufuatia kushindwa kwake kwenye uchaguzi wa 2015, ambapo inasemekana alihisi kusalitiwa na washirika wakuu ndani ya chama.

    Anastahiki muhula mmoja zaidi iwapo atashinda katika uchaguzi wa mwaka ujao jambo ambalo linaweza kumaanisha mamlaka kurejea katika eneo la kaskazini mwa Nigeria katika mpangilio ambao haujaandikwa, wenye utata ambao unabadilisha mamlaka kati ya kaskazini na kusini.

    Bw Jonathan anatoka kusini mwa Nigeria. Yeyote atakayepata uteuzi wa APC kwa uchaguzi atatarajia ushindani mkali kutoka kwa PDP. Wagombea wake kama vile Peter Obi, Makamu wa Rais wa zamani Atiku Abubakar na gavana wa jimbo la Rivers Nyesom Wike ni maarufu sana, haswa kusini mwa Nigeria.

  17. Askari Magereza aliyemsaidia 'mpenzi' wake mtuhumiwa kutoroka jela ajiua

    Askari magereza wa kike ambaye alitoroka na mshukiwa wa mauaji kutoka jela ya Alabama, Marekani amefariki dunia baada ya kujipiga risasi wawili hao wakikamatwa, polisi wanasema.

    Vicky White, 58, alifariki hospitalini baada ya yeye na Casey White (hawana uhusiano wa kindugu), 38, kukamatwa huko Indiana kufuatia msako wa polisi.

    Wawili hao walikuwa walitoroka katika gereza la Kaunti ya Lauderdale tarehe 29 Aprili. Inaaminika kuwa walikuwa wapenzi. Kulingana na maafisa, walionekana mara ya mwisho alipokuwa akimsafirisha kwa kisingizo cha uongo cha matatizo ya afya ya akili.

    Ilikuwa siku ya mwisho ya Bi White kazini kabla ya kustaafu. Alikuwa ameuza nyumba yake hivi majuzi na akawaambia wenzake kwamba alipanga kutumia wakati mwingi ufukweni.

    Ofisi ya Wachunguzi wa Kaunti ya Vanderburgh ilithibitisha kwamba Vicky White alifariki katika hospitali ya eneo hilo baada ya kujipiga risasi wakati wa kukamatwa. Taarifa zaidi kuhusu kifo chake zinatarajiwa kutolewa leo Jumanne kufuatia uchunguzi wa maiti yake.

    Sherifu wa Kaunti ya Lauderdale Rick Singleton alisema hapo awali kwamba gari la wapenzi hao hao lilipinduka wakiwa kwenye harakati za kutoroka baada ya msako wa polisi huko Evansville, Indiana, ambapo Casey White alijisalimisha. "Tumemkamata mtu hatari mtaani leo. Hataona mwanga wa jua tena," alisema.

    Casey White alikuwa anatumikia miaka 75 jela kwa makosa mengine mbalimbali ikiwemo ya wizi aliyoyafanya mwaka 2015.

  18. Biden asaini sheria ya kukopa au Kukodisha vifaa vya ulinzi kwa Ukraine

    Rais wa Marekani Joe Biden alitia saini Sheria ya Kukodisha kwa Mkopo, iliyoundwa ili kurahisisha utaratibu wa kusambaza silaha kwa Ukraine.

    Hati hiyo, kipengele hicho kilichopewa jina la "Sheria ya Kukodisha ya Kulinda Demokrasia nchini Ukraine ya 2022," iliwasilishwa kwa Bunge la Congress hata kabla ya kuanza kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, Januari mwaka huu.

    Mnamo Mei 3, mswada huo uliidhinishwa kwa kura nyingi za Baraza la Wawakilishi la Bunge la Marekani (417 waliunga mkono, 10 walipinga), na kabla ya hapo mswada huo uliidhinishwa na Seneti.

    Kwa mujibu wa muswada huo, Rais wa Marekani "anaweza kuidhinisha serikali kukopesha au kukodisha mali ya ulinzi kwa Ukraine na nchi nyingine za Ulaya Mashariki zilizoathiriwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ili kusaidia kuimarisha ulinzi wa nchi hizi na kulinda raia dhidi ya mashambulizi yanayoweza kutokea au kuendelea. uchokozi kutoka upande wa Urusi.

    Mswada huu utafanya kazi sawa na sheria ya kukodisha ya Vita vya Kidunia vya pili, wakati Marekani iliwapa washirika wake silaha, vifaa vya kijeshi na chakula bila malipo ya mapema na kwa kuchelewa kwa muda mrefu.

    Wakati wa Vita vya Kidunia vya pili, mmoja wa wapokeaji wakuu wa misaada kama hiyo alikuwa Umoja wa Kisovieti.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alishukuru Marekani na Biden kwa kufufua mpango wa msaada. "Asante @POTUS na watu wa Marekani kwa kuunga mkono Ukraine katika kupigania uhuru na mustakabali wetu," akaunti rasmi ya rais wa Ukrain ilituma ujumbe huo kupitia Tiwtter kwa Kiingereza.

    "Leo siku ya kutia saini Sheria ya Kukodisha Mkopo ni hatua ya kihistoria. Nina hakika kwamba tutashinda pamoja. Na tutatetea demokrasia nchini Ukraine. Na Ulaya. Kama miaka 77 iliyopita." Alisema Biden.

    Unaweza pia kusoma

  19. Hujambo, karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja leo 10.05.2022