Urusi yashambulia hospitali ya kujifungua Ukraine

Takriban watu 17 wamejeruhiwa na shambulizi la angani la Urusi kwenye hospitali ya Mariupol, kulingana na utawala wa kijeshi wa Ukraine katika eneo la mashariki la Donetsk.

Moja kwa moja

  1. Kwanini Ukraine inaondoa wanajeshi wake wanaolinda amani DRC?

    Kikosi cha wanajeshi 250 wa kulinda amani wa Ukraine wanatarajiwa kuondoka mashariki mwa DRC na kurejea Ukraine.

    Tangazo hilo lilitolewa Jumanne na Umoja wa Mataifa.

    Tarehe ya kuondoka bado haijatangazwa. Uondoaji huo pia utajumuisha vifaa na helikopta.

    Hatua hiyo huenda ikawa na athari kwa kikosi cha kulinda amani nchini DRC .Hata hivyo wadadisi wanasema Ukraine haikuwa na budi ila kufanya uamuzi huo kwa ajili ya vita vinavyoendelea nchini humo baada ya uvamizi wa Urusi .

    Mwandishi wa BBC Mbelechi Msoshi alituma taarifa iliyisheheni maoni ya wenyeji kuhusu uamuzi huo

    Maelezo ya sauti, Ukraine yawaita nyumbani wanajeshi wake 250 walioko DRC chini ya Umoja wa Mataifa
  2. Habari za hivi punde, 17 wajeruhiwa katika shambulizi la hospitali ya kujifungua Ukraine - maafisa

    Takriban watu 17 wamejeruhiwa na shambulizi la angani la Urusi kwenye hospitali ya Mariupol, kulingana na utawala wa kijeshi wa Ukraine katika eneo la mashariki la Donetsk.

    Wafanyikazi na wanawake walio katika harakati za kijifungua walikuwa miongoni mwa waliojeruhiwa, maafisa walisema.

    Pavlo Kyrylenko, mkuu wa utawala wa kijeshi wa Ukraine katika eneo la Donetsk, alisema idadi ya watoto waliojeruhiwa "ni sifuri, namshukuru Mungu, na ninatumai itasalia kuwa hivyo".

  3. Ujerumani yagoma kutuma ndege za kivita Ukraine

    Plane

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ujerumani imesema haitatuma ndege za kivita nchini Ukraine, baada ya Marekani kukataa pendekezo la Poland la kuhamisha ndege zake za kivita aina ya MiG-29 nchini Ukraine kupitia kambi ya Marekani nchini Ujerumani.

    Kansela Olaf Scholz anasema Ujerumani "imetoa kila aina ya vifaa vya ulinzi" ikiwa ni pamoja na silaha, lakini anasema "bila shaka ndege za kivita sio sehemu ya hilo".

    Wakati huo huo nchini Uingereza, Serikali inasema "haiwezekani" kwa marubani wa Nato na ndege zake kuzishambulia ndege za Urusi.

    Msemaji wa Waziri Mkuu anasema Boris Johnson "amesema mara kwa mara" kuwa amejitolea "kutoa silaha ambazo Ukraine inahitaji".

    Mapema, Uingereza ilisema inaongeza usambazaji wake wa silaha kwa Ukraine, ikituma makombora 1,615 zaidi ya kupambana na vifaru na makombora ya Masafa marefu ya Javelin.

  4. Viongozi wa Afrika wazungumza na Putin kuhusu vita vya Ukraine

    Rais Vladmir Putin

    Chanzo cha picha, getty Images

    Maelezo ya picha, Vladmir Putin

    Rais wa Senegal, Macky Sall, ambaye ni mkuu wa sasa wa Umoja wa Afrika (AU), amezungumza na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kuhimiza usitishaji vita "wa kudumu" nchini Ukraine.

    Yeye ni kiongozi wa pili wa Afrika kufichua kwamba amewasiliana na Bw Putin - mwingine ni Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi.

    Katika ujumbe wake wa Twitter, Bw Sall alisema: "Kama rais wa Umoja wa Afrika, nimefurahishwa na mazungumzo yangu asubuhi ya leo na Rais Putin kushinikiza kusitishwa kwa mapigano kwa kudumu.

    "Ninampongeza kwa kusikiliza na kwa nia yake ya kudumisha mazungumzo kwa ajili ya matokeo ya mazungumzo ya mzozo."

    Ofisi ya Bw Sisi ilisema mazungumzo yake na Bw Putin yalilenga mzozo wa Ukraine, na kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

    Baada ya wanajeshi wa Urusi kuingia Ukraine tarehe 24 Februari, AU ilitoa taarifa ikitaka Ukraine kuheshimiwa na sheria ya kimataifa kuzingatiwa.

    Jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi Ecowas ilisema inalaani uvamizi huo.

  5. Serikali ya Tanzania yatahadharisha uwepo wa homa ya manjano nchini Kenya

    Mbu aenezaye homa ya manjano

    Chanzo cha picha, SPL

    Serikali ya Tanzania imetoa tahadhari ya Mlipuko wa Ugonjwa wa Homa ya Manjano.

    Hatua hiyo imekuja baada ya taarifa za kuwepo kwa mlipuko wa ugojwa huo nchi jirani ya Kenya.

    Wizara ya Afya ina utaratibu wa kufuatilia taarifa za magonjwa ya milipuko yakiwemo yale yanayozuilika kwa chanjo kama Surua, Rubella, Polio na Homa ya Manjano ili kudhibiti magonjwa nchini Tanzania.

    Wizara ya Afya imesema pia hufuatilia uwepo wa milipuko ya magonjwa mbalimbali katika nchi jirani ilizopzakana nazo ili kuchukua tahadhari za haraka na kuzuia magonjwa hayo yasiingie Tanzania kutokana na mwingiliano wa watu katika shughuli za kibiashara au kijamii.

    Taarifa ya wizara imesema mnamo tarehe 03 Machi, 2022 ilipokea taarifa kutoka Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyopo Tanzania, ikielezea kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Manjano nchini Kenya katika Kaunti ya Isiolo umbali wa takribani Kilomita 285 (Kaskazini mwa Nairobi) .

    Taarifa hiyo ilieleza kuwa, mgonjwa wa kwanza mwenye dalili za ugonjwa huo alipatikana mnamo tarehe 12 Januari 2022 na hadi kufikia tarehe 03 Machi 2022, kulikuwa na jumla ya wagonjwa 15 na vifo vitatu (3) vilivyotokana na ugonjwa huo.

    Aidha, kati ya sampuli sita (6) zilizopimwa katika maabara ya Kenya (KEMRI), sampuli tatu (3) zilithibitika kuwa va virusi vya homa ya Manjano kwa kutumia vipimo vya serology na PCR.

    Katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania haijawahi kuwa na taarifa ya mgonjwa yeyote aliyethibitika kuwa na ugonjwa wa Homa ya Manjano tangu mwaka 1950.

  6. McDonald's, Coca-Cola zasitisha biashara Urusi

    McDonald's ilisema ilikuwa inafunga kwa muda migahawa yake takriban 850

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kampuni kubwa zikiwemo McDonald's, Coca-Cola na Starbucks wamejiunga na orodha ya makampuni yanayositisha biashara nchini Urusi kutokana na uvamizi nchini Ukraine.

    McDonald's ilisema ilikuwa inafunga kwa muda migahawa yake takriban 850 nchini Urusi, wakati Starbucks pia ilisema maduka yake 100 ya kahawa yatafungwa.

    Siku ya Jumatano, Heineken ilisimamisha uzalishaji na uuzaji wa bia nchini Urusi.

    Coca-Cola Co (KO.N) na PepsiCo Inc (PEP.O) walisema Jumanne wanasitisha uuzaji wa soda zao nchini Urusi, na kufanya kuwa bidhaa za hivi karibuni za watumiaji wa Magharibi kupunguza shughuli katika eneo hilo kufuatia uvamizi wa Moscow nchini Ukraine.

    Coca-Cola ilisema biashara yake nchini Urusi na Ukraine ilichangia takriban 1% hadi 2% ya mapato halisi ya uendeshaji wa kampuni hiyo mnamo 2021.

    PepsiCo, ambayo cola zake zilikuwa moja ya bidhaa chache za Magharibi zilizoruhusiwa katika Umoja wa Kisovieti kabla ya kusambaratika, ilisema itaendelea kuuza bidhaa muhimu za kila siku, kama vile maziwa na matoleo mengine ya maziwa, maziwa ya watoto na chakula cha watoto, nchini Urusi.

    McDonald's Corp (MCD.N) ilisema Jumanne kwamba itafunga kwa muda mikahawa yake yote nchini Urusi ikijumuisha eneo lake maarufu la Pushkin Square, na kuongeza shinikizo kwa chapa zingine za kimataifa kusitisha shughuli nchini humo kufuatia uvamizi wa Moscow nchini Ukraine.

  7. Joel Jaffer A’ita: Bilionea wa Uganda aweka nia ya kuinunua klabu ya Chelsea

    Joel Jaffer A’ita

    Chanzo cha picha, Joel Jaffer A’ita

    Joel Jaffer A’ita amekuwa gumzo baada ya kuwasilisha ombi la kuinunua Klabu ya Soka ya Chelsea inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza.

    Mhandisi huyo wa Ujenzi ambaye ana Shahada ya Kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, pia anamiliki Klabu ya Michezo ya Arua Hill ya Ligi Kuu ya Uganda.

    Aliwasilisha rasmi ombi lake la kuinoa The Blues, na kuwa raia wa pili wa Uganda kutoa zabuni kwa klabu ya soka ya Uingereza baada ya jaribio la Michael Ezra Mulyoowa kwa Leeds United mwaka 2004 (Pauni Milioni 60).

    "Niko tayari kutwaa Klabu ya Soka ya Chelsea " A’ita aliiambia Kawowo Sports Media Alhamisi, Machi 3, 2022. A’ita anatoa ofa ya dola bilioni 3.3 kwa Bilionea wa Urusi Roman Abramovich, mmiliki wa Klabu ya Soka ya Chelsea na anakusudia kuuita klabu hiyo Klabu ya Soka ya Kongolo (Kongolo FC)

    “Kufuatia taarifa kwa umma kuhusu nia ya kuuza Chelsea FC, ningependa kueleza nia yetu ya kununua klabu. Kwa thamani ya sasa ya $ 3.2 bilioni, tunatoa $ 3.3 bilioni. Tunakusudia kubadili jina la klabu kama Kongolo FC” Aita aliandika barua kwa Abramovich.

    Aita aliingia katika ulingo wa soka nchini Uganda mwaka wa 2019 alipotwaa Klabu ya Soka ya Doves All Stars.

  8. Ndege za Urusi zinaweza kuzuiliwa nchini Uingereza

    Ndege hiyo inachunguzwa na mamlaka kwa sababu inaaminika kutumiwa na oligarch wa Urusi

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mawaziri wanafanya kuwa kosa la jinai kwa ndege zinazomilikiwa au kukodishwa na Warusi kuingia kwenye anga ya Uingereza.

    Meli zinazomilikiwa na Urusi tayari zimepigwa marufuku kukanyaga maji ya Uingereza, lakini hatua hiyo mpya inalenga ndege za binafsi zilizosajiliwa katika nchi ya tatu iliyokodiwa na matajiri wa Urusi.

    Serikali ilisema kuwa vikwazo hivyo vitalenga watu walio karibu na Kremlin. Ndege moja katika uwanja wa ndege wa Farnborough huko Hampshire tayari inachunguzwa.

    Mamlaka ya Uingereza imeshikilia ndege ya kibinafsi iliyosajiliwa Luxembourg kuchunguza kama inamilikiwa na Urusi na kuleta abiria wa Urusi nchini Uingereza kinyume na vikwazo.

    Serikali pia imetangaza vikwazo vipya vya kibiashara ambavyo vitazuia mauzo yote ya Uingereza ya anga au teknolojia inayohusiana na anga kwenda Urusi, ikijumuisha huduma zinazohusiana nazo kama vile bima.

    Akitangaza hatua hizo mpya, Waziri wa Mambo ya Nje Liz Truss alisema mabadiliko hayo yatasababisha "maumivu zaidi ya kiuchumi kwa Urusi na wale walio karibu na Kremlin".

    Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono Ukraine na "kufanya kazi kuitenga Urusi katika jukwaa la kimataifa".

    Katibu wa Uchukuzi Grant Shapps alisema Uingereza ilikuwa "moja ya nchi za kwanza kupiga marufuku ndege za Urusi na leo tunaenda mbali zaidi kwa kuifanya kuwa kosa la jinai kwa ndege za Urusi kufanya kazi katika anga ya Uingereza".

    "Siku zote tutafanya kazi kumnyima [Rais wa Urusi Vladimir] Putin na wasaidizi wake haki ya kuendelea kama kawaida huku raia wa Ukraine wasio na hatia wakiteseka."

    Nick Watt, mhariri wa kisiasa wa BBC Two's Newsnight, alisema hatua hizo zitashughulikia "eneo la kijivu" la ndege binafsi ambazo zimesajiliwa katika nchi ya tatu iliyokodiwa na Warusi matajiri.

    Alisema ndege hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Farnborough, ambao ni uwanja wa ndege wa binafsi, inachunguzwa na mamlaka kwa sababu inaaminika kutumiwa na oligarch wa Urusi.

    Vyanzo vya habari viliiambia Newsnight kwamba kutambua ndege kama ya Kirusi sio tu suala la kuifuata kwenye rada, lakini ni "kazi ya upelelezi" ili kubaini asili yake halisi.

    Vikwazo hivyo vipya vimekuja muda mfupi baada ya serikali ya Uingereza kuthibitisha kuwa itapiga marufuku mafuta yote ya Urusi ifikapo mwisho wa mwaka huu, huku hatua sawa na hiyo ikitangazwa na Marekani.

    Urusi yaishambulia Ukraine:Mengi zaidi

  9. Marekani yamrejesha nyumbani 'mteka nyara wa 20' wa shambulio 9/11 kutoka Guantanamo

    Mohammed al-Qahtani alikuwa amezuiliwa Guantanamo Bay kwa zaidi ya miaka 20

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanaume mmoja wa Saudia anayeshutumiwa kuwa "mteka nyara wa 20" katika shambulio la Septemba 11 ameachiliwa kutoka kizuizini katika gereza la Guantanamo, Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema.

    Mohammed al-Qahtani, 46, alirejeshwa Saudi Arabia baada ya bodi ya ukaguzi kubaini kwamba hakuwa tena "tishio kubwa". Bodi ilibaini "hali yake ya afya ya akili iliyoathiriwa sana".

    Qahtani aliteswa vibaya sana na wapelelezi wa Marekani baada ya kuzuiliwa mwaka 2001 kiasi kwamba hakuweza kufikishwa mahakamani.

    Bodi ya mapitio ilisema mwezi uliopita kwamba sharti la uhamisho wake linapaswa kuwa ushiriki wake katika kituo cha kurekebisha tabia cha wanajihadi cha Saudi Arabia, kinachojulikana kama Kituo cha Ushauri na Matunzo cha Prince Mohammed Bin Nayef, ambapo anaweza kupata huduma kamili ya afya ya akili

    Mamlaka za Marekani zimedai kuwa Qahtani alikusudiwa kuwa kwenye ndege ya United Airlines ndege namba 93, iliyoanguka Pennsylvania baada ya kutekwa nyara na wanamgambo wanne wa al-Qaeda mnamo 9/11.

    Hata hivyo, alikuwa amezuiwa kuingia Marekani mwezi uliopita. Qahtani alikamatwa miezi minne baadaye kwenye mpaka wa Afghanistan na Pakistan na kupelekwa katika kambi ya jeshi la wanamaji la Marekani huko Guantanamo Bay nchini Cuba Februari 2002.

    Wachunguzi huko walipokea kibali cha kutumia "mbinu kali zaidi za kuhoji" kwa Qahtani baada ya kukataa mbinu za kawaida.

    Kati ya Novemba 2002 na Januari 2003, alitengwa kwa muda mrefu, kunyimwa usingizi, udhalilishaji wa kijinsia na kupigwa na baridi.

  10. Mpango wa Poland kutuma ndege za kivita nchini Ukraine 'unashangaza' - mtaalam wa kijeshi wa Marekani

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Marekani imekataa pendekezo la Poland la kutuma ndege zake zote za kivita aina ya Mig-29 zilizoundwa na Usovieti nchini Ukraine kupitia kambi ya anga ya Marekani nchini Ujerumani.

    Msemaji wa Pentagon John Kirby alisema, "matarajio ya ndege za kivita kwa serikali ya Amerika kuondoka kutoka kambi ya Amerika / Nato huko Ujerumani na kuruka kwenye anga ambayo inashindaniwa na Urusi juu ya Ukraine inaleta wasiwasi mkubwa kwa nchi nzima. Na Muungano wa Nato".

    Marekani ina tahadhari na ofa ya Poland, ambayo ilikuja ili kuitikia wito unaokua wa Ukraine kwa washirika wa Magharibi kuipatia ndege za kijeshi kusaidia kupambana na uvamizi wa Urusi.

    Mchambuzi wa masuala ya kijeshi Kanali Brendan Kearney aliambia BBC kuwa "amechanganyikiwa na mbinu ambayo Wapoland wanachukua".

    Alisema "marubani wa Kiukreni wanaweza kuvuka mpaka na kuingia Poland na kuzirejesha Ukraine", ambayo "inaonekana kama hatua rahisi zaidi na nadhifu zaidi.

    "Lengo la mwisho la muda mrefu la kupata MIG-29 za ziada mikononi mwa Ukraine ni zuri, ni zuri, lakini lazima tuwe na watu wanaokaa chini ambao wanajua wanazungumza nini na waje na mpango. hiyo inaweza kutekelezwa," Kanali Kearney aliongeza.

  11. Mfanyabiashara wa Kisomali: Niliacha kila kitu nchini Ukraine

    Mohamud Arab

    Chanzo cha picha, Mohamud Arab

    Mfanyabiashara wa Kisomali aliyekimbia mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, amewasili Ujerumani ambako anatafuta hifadhi "kuanza maisha mapya".

    Mohamud Arab alikuwa akiendesha biashara ya faida huko Kyiv, akisafirisha nguo za mitumba na vifaa vya elektroniki kwa nchi kadhaa za Kiafrika.

    Lakini mara tu baada ya majeshi ya Urusi kuivamia nchi hiyo, alikodi gari na kuelekea mpaka wa Ukraine na Poland.

    Aliwasili katika jiji la Kassel katikati mwa Ujerumani siku ya Jumapili baada ya siku nyingi zaidi kwenye barabara kutoka mji mkuu wa Poland, Warsaw.

    Sasa anatatizika kupata riziki na anategemea usaidizi kutoka kwa familia yake. "Siwezi kufikia akaunti yangu ya benki huko Kyiv. Nimesaidiwa kifedha na marafiki wa karibu na familia,” alisema.

    Kadi zake za benki zinaweza kutumika tu nchini Ukraine, na kama mgeni anayeishi Kyiv, hakuweza kutumia akaunti yake kwa kuwa sheria inakataza wageni kutumia mtandao au benki ya simu - hatua inayolenga kukomesha utoroshaji wa pesa.

    Katika kutafuta hifadhi nchini Ujerumani, Bw Arab anatarajia kujiandikisha kupitia Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na kuzifikia akaunti zake za benki huko Ukraine.

    "Siwezi kufikiria kuwa nilikuwa na biashara ya kuuza nje yenye faida pamoja na washirika wangu, lakini sasa yote yamepita. Tuliacha kila kitu pale, niliondoka na koti tu."

    Biashara na Ukraine tangu wakati huo ilikoma kwani meli zimeacha kupiga simu bandarini hapo. “Nimekuwa Ukraine kwa takriban miaka sita, nikishughulika na biashara ya kuagiza na kuuza nje ya mitumba; labda sasa kila kitu kitaharibiwa. Ni hali ngumu," Bw Arab alisema.

    "Nina wafanyakazi 150 nchini Ukraine, na shughuli zangu zimekuwa za takriban dola za Marekani 300,000 kwa mwezi," aliongeza.

    Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu milioni mbili wameikimbia Ukraine tangu kuanza kwa mashambulizi ya Urusi.

    Urusi yaishambulia Ukraine:Mengi zaidi

  12. Aliyelipwa fidia ya mamilioni ya fedha kimakosa akataa kurejesha fedha

    Mlipuko wa bomu huko Nairobi ulisababisha vifo na majeruhi

    Mfuko wa Marekani ambao ulijitwikwa jukumu la kuwalipa fidia waathiriwa wa shambulizi la kigaidi la 1998 jijini Nairobi umemshtaki mwanamke ambaye alipokea kimakosa mamilioni ya pesa ambayo inadaiwa alikataa kurejesha.

    Mfuko huo umeomba Mahakama Kuu itoe amri ya kurejeshewa fedha alizopokea Mary Ngunyi Muiruri, kiasi cha dola za Marekani 65,683.50 (Sh milioni 7.4 za Kenya) mnamo Novemba mwaka 2020, Gazeti la Nation la Kenya limeripoti.

    Hazina hiyo ilinuia kumlipa Mary Njoki Muiruri pesa hizo, lakini mkanganyiko wa majina ya kati ulisababisha mtu ambaye hakukusudiwa akipokea pesa hizo.

    Bi Ngunyi hajajibu madai hayo.

    Mfuko huo wa fidia ulikuwa umeomba benki ya eneo hilo kurejesha pesa hizo. Benki ya Nairobi, hata hivyo, ilisema Bi Ngunyi alikataa kuridhia ombi hilo, hivyo kuwasilisha shauri la kisheria.

    Benki hiyo inaongeza kuwa mawasiliano kati ya Mfuko wa Udhibiti wa Mabomu wa Ubalozi wa Marekani wa 1998 na Ngunyi yalionesha kuwa kulikuwa na mzozo kuhusu ni nani mpokeaji halisi wa mamilioni hayo.

    Bi. Ngunyi alisisitiza kuwa fedha hizo ni zake

    Benki imeongeza kuwa Bi. Ngunyi ameshatumia kiasi kikubwa cha fedha.

    Kufikia mwaka 1998, Mfuko wa Ubalozi wa Marekani ulipopata maagizo ya mahakama ya kufungia akaunti ya Ngunyi mnamo Februari 2021, Bi Ngunyi alikuwa ametoa pesa nyingi na alikuwa na $5,553 pekee (Sh633,319) kama salio la akaunti .

    Benki hiyo inahoji kwenye karatasi za mahakama kwamba haikuwa mhusika katika kesi za mahakama nchini Marekani kuhusu fidia ya waathiriwa wa mashambulizi ya kigaidi na kwa hivyo haikuweza kuthibitisha kwa mamlaka ni nani alikuwa mpokeaji halisi wa pesa hizo.

    Wakenya kadhaa waliwasilisha kesi katika mahakama za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Sudan na Iran kati ya 2008 na 2012 wakitaka walipwe fidia kwa majeraha na kupoteza jamaa zao katika shambulio la bomu la Agosti, 1998 katika Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi.

  13. Nini kinachofanyika Ukraine? Huu hapa muhtasari wa matukio yote

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ni Siku ya 14 ya uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine. Kwa hivyo, ikiwa unajiunga nasi, hapa kuna muhtasari wa haraka kuhusu matukio makuu katika saa 12 zilizopita:

    • Kulikuwa na taarifa za ving'ora vya anga Jumatano asubuhi katika miji kadhaa ya Ukraine, ukiwemo mji mkuu wa Kyiv

    • Hatua zote mbili za uhamishaji wa watu kutoka mji wa kaskazini-mashariki wa Sumy - ambao kwa siku kadhaa umekuwa chini ya mashambulizi makali ya Urusi - zilikamilika kwa mafanikio, Ukraine ilisema.

    • Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alitoa hotuba ambayo haijapata kifani kutoka ofisi yake mjini Kyiv kwa wabunge wa Uingereza katika Baraza la Commons.

    • Alimnukuu Winston Churchill, akiionya Urusi kwamba "tutapigana msituni, mashambani, ufukweni, mitaani"

    • Rais wa Marekani Joe Biden alitangaza kupiga marufuku kabisa Marekani kuagiza mafuta, gesi na makaa ya mawe nchini Urusi

    • Umoja wa Mataifa ulisema wakimbizi milioni mbili sasa wameikimbia Ukraine - katika hali ambayo sasa ni mzozo wa wakimbizi unaokua kwa kasi zaidi barani Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia.

    • McDonald's, Starbucks na Coca-Cola ni kampuni za hivi punde zaidi za Magharibi kusitisha kazi zao nchini Urusi

    Urusi yatangaza usitishaji mwingine wa mapigano kwa raia kuondoka mijini

    Moscow imetangaza usitishaji vita kwa muda ili kuruhusu raia katika miji inayoshambuliwa kukimbia, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.

    Barabara zitawekwa tena kwa Kyiv, Chernihev, Sumy, Kharkiv na Mariupol saa 10:00 kwa saa za huko. Ni mara ya tatu ya usitishaji vita kutangazwa na Moscow.

    Jana, maafisa wa Ukraine walisema walifanikiwa kuwahamisha watu 5,000 kutoka Sumy - uokoaji wa kwanza wa watu wengi uliofaulu.

    Walakini, jaribio kama hilo kwa wale wa Chernihiv lilishindwa kwa sababu Urusi iliendelea kushambulia njia ya kutokea, Ukraine ilidai.

    Ukraine: Mke wa Rais Olena Zelenska alaani mauaji ya watu

    Mke wa Rais wa Ukraine Olena Zelenska ametoa taarifa ya kusikitishwa na uvamizi wa Urusi, akilaani "mauaji ya watu wengi" nchini humo.

    Aliangazia zaidi vifo vya watoto, akitaja majina ya watoto watatu waliokufa katika mashambulizi ya mabomu.

    Amesema Ukraine inataka amani lakini italinda mipaka yake na utambulisho wake.

    Bibi Zelenska, 44, hajulikani aliko, na mumewe Rais Volodymyr Zelensky anasema familia yake inalengwa na vikosi vya Urusi.

    Urusi yaishambulia Ukraine:Mengi zaidi

  14. Mbowe asema Chadema haitakuwa na kisasi dhidi ya viongozi wa nchi

    Maelezo ya video, Freeman Mbowe: Chadema haitakuwa na kisasi dhidi ya viongozi wa nchi

    Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania Freeman Mbowe amesema chini ya uongozi wake, chama chake hakitakuwa na kisasi dhidi ya viongozi wa nchi hiyo.

    Mwenyekiti huyo wa Chadema amesema hayo, siku nne baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kufuta mashtaka ya ugaidi dhidi yake na wengine watatu.

    Akihutubia Baraza la Wanawake la Chama cha Wananchi (BAWACHA) mjini Iringa, Mbowe alisema: "Mahakama ilipotuweka huru, nilipokea mwaliko kutoka kwa Rais Samia Suluhu. Nilikubali mwaliko wake, na ilikuwa heshima kubwa kukutana naye.

    Aliongeza kuwa Rais Samia amekuwa Rais wa kwanza kutangaza hadharani nia yake ya dhati ya kurejesha haki ya kweli nchini.

    "Nawaomba Watanzania wenzangu wote kukumbatia msingi huu wa Rais," Mbowe alisema zaidi

    Rais Samia na Mbowe walionekana kwenye picha zilizotolewa Ijumaa jioni na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais na inasemekana walijadili masuala yenye maslahi kwa taifa.

  15. Kyiv yajitayarisha kwa mashambulizi zaidi ya Urusi

    th

    Wakaazi katika mji mkuu wa Ukraine wamekuwa wakijitayarisha kwa uwezekano wa mashambulizi Zaidi kutoka kwa vikosi vua Urusi .

    Kamanda anayejiita Johnny Dragan, na anayevuta sigara kila wakati kana kwamba ndio ungekuwa mwisho wake anaonyesha hatua wanazochukua kukabiliana na vikosi vya Urusi .

    Dragan alikuwa akiimarisha nafasi ya kuzuia katika njia panda ya kimkakati kaskazini-magharibi mwa Kyiv. Ikiwa Warusi wataivunja, Dragan na watu wake watalazimika kuwazuia. Nyuma yake kulikuwa na njia mbili za magari zinazoelekea moja kwa moja hadi Kyiv.

    Askari wasiokuwa kazini walikuwa wakila na kupumzika kwenye mgahawa uliokuwa kwenye njia panda ambayo Dragan alikuwa ameichukua kuwa makao yake makuu. Chakula kilikuwa cha moyo, na waliweka bunduki zao kwenye marundo nadhifu karibu na meza zao.

    Nje, zamu ya kazi ilikuwa ikifanya kazi wakati wa siku nyingine ya baridi kali, na theluji ikitua kwenye mabega yao. Tangi lilikuwa kwenye nafasi. Kipande cha silaha chenye sura mbaya kiliwekwa kurusha moja kwa moja, juu ya maeneo ya wazi, kwa kitu chochote kinachokuja kwenye barabara ambacho Dragan aliamua kuwa tishio.

    "Tuko hapa kuharibu vikosi vya adui," alisema. "Wavamizi ambao wamekuja katika nchi yetu - na wanaelekea kwetu."

    Putin alipanga kuiteka Kyiv katika siku mbili - mkuu wa CIA

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Urusi Vladimir Putin alikuwa amepanga kuuteka mji mkuu wa Ukraine wa Kyiv ndani ya siku mbili, mkuu wa CIA William Burns amesema.

    Akizungumza katika kikao cha bunge siku ya Jumanne, Burns aliwaonya wabunge wa Marekani: "Nadhani Putin amekasirika na amechanganyikiwa hivi sasa. Kuna uwezekano anaweza kujaribu kuwakandamiza wanajeshi wa Ukraine bila kujali majeruhi wa raia."

    Burns alisema Putin amekuwa "akisisitiza katika mchanganyiko wa malalamiko na matamanio kwa miaka mingi".

    Alielezea uvamizi wa Februari 24 wa Ukraine kama suala la "uaminifu wa kina wa kibinafsi" kwa kiongozi wa Kremlin.

    Urusi yaishambulia Ukraine:Mengi zaidi

  16. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja hii leo.