Wanaharakati wa haki za Rwanda wanataka tamasha la Olomide lifutiliwe mbali

Wanaharakati wa haki za wanawake nchini Rwanda wamesitisha tamasha la nyota wa muziki wa Congo Koffi Olomide kwa tuhuma za ubakaji na unyanyasaji wa kingono anazokabiliwa nazo katika mahakama za Ufaransa.

Moja kwa moja

  1. Mwisho wa habari za moja kwa moja leo, tukutane tena kesho majaliwa

  2. Boti iliyozama Ufaransa yaua 27 wakiwemo watoto

    Boti

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takriban watu 27, akiwemo binti mdogo, wamefariki baada ya boti waliokuwa wakisafiri kuzama maji. Boti hiyo ilikuwa ikielekea Uingereza ilipozama muda mfupi baada ya kuondoka kwenye bandari ya Ufaransa ya Calais.

    Mashua zinazotumiwa kufanya safari kama hizo kupitia Idhaa ya Kiingereza mara nyingi ni ndogo na zinajaza watu kupita kiasi, na hivyo kkuhatarisha maisha ya watu.

    Mwendesha mashtaka wa eneo hilo anasema wanawake saba na watoto watatu ni miongoni mwa waliofariki - huku watu wawili wakiokolewa.

    Hakuna linalofahamika zaidi kuhusu waliokufa, uraia wao au kilichosababisha boti hiyo kuzama. Tayari Polisi wa Ufaransa wamewakamata watu watano kuhusiana na tukio hilo.

    Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wamekubaliana "kufanya kila linalowezekana kukomesha magenge yanayohusika", lakini Johnson anasema Ufaransa inapaswa kufanya zaidi kuwazuia wahamiaji kuvuka, huku Macron akisema Uingereza inapaswa kuacha kuweka siasa katika suala hilo.

    Inaelezwa waliokufa walikuwa wakimbizi wanaotaka kuelekea Uingereza.

    Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Priti Patel amewaambia wabunge wa Uingereza kwamba ametoa ofa mpya kutoka Uingereza kuanza doria ya pamoja na Ufaransa.

  3. Kesi ya Rais wa Shirikisho la soka Kenya (FKF), Mwenda imetupiliwa mbali

    Mwenda

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kesi ya kisheria dhidi ya rais wa Shirikisho la Soka nchini (FKF), Nick Mwendwa, imetupiliwa mbali.

    "Shirikisho la Soka la Kenya linapenda kuwafahamisha wanachama wa FKF na umma kwa ujumla kwamba mahakama leo, 25 Novemba 2021, imeifunga kesi dhidi ya Nick Mwendwa kufuatia serikali kushindwa kupendelea mashtaka dhidi yake," FKF ilisema katika taarifa rahisi.

    "Rais wa FKF anashukuru na ataendelea kufanya kazi ili kuhakikisha kuwa soka la Kenya linarejea katika hali yake ya kawaida."

    Mwendwa alikamatwa tarehe 12 Novemba na kukaa gerezani mwishoni mwa juma, kabla ya kuachiliwa kwa dhamana ya Kshs4 milioni (takriban dola 36,000) huku uchunguzi zaidi ukifanywa. Mwenda alikanusha makosa yote anayotuhumiwa nayo.

    Alipokamatwa kwa mara ya kwanza, msemaji wa FKF alisema: "Hakuelezwa sababu zozote za kukamatwa kwake, kwa hivyo bado tunajaribu kufuatilia."

    Kukamatwa kwake na uchunguzi uliofuata ulikuja baada ya ripoti ya mapema mwaka huu chini ya Wizara ya Michezo ya Kenya, ambayo ilipendekeza kwamba mamlaka inapaswa kulitupia jocho FKF. Ripoti hiyo ililenga kubainisha masuala ya ufujaji wa fedha.

    Maafisa wa Fifa hivi majuzi walikuwa Nairobi kufanya uchunguzi wao katika shirikisho hilo la FKF, ambalo Mwendwa ameliiongoza tangu 2016.

  4. Wanaharakati wa haki za wanawake Rwanda wasitisha tamasha la Koffi Olomide,

    Koffi Olomide

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wanaharakati wa haki za wanawake nchini Rwanda wamesitisha tamasha la nyota wa muziki wa Congo Koffi Olomide kwa tuhuma za ubakaji na unyanyasaji wa kingono anazokabiliwa nazo katika mahakama za Ufaransa.

    Mwezi Desemba, mahakama ya Paris itatoa uamuzi wa rufaa iliyoombwa kwa mashtaka dhidi ya nyota huyo, ambaye alikuwa amepatikana na hatia hapo awali, lakini amekuwa akikanusha madai ya wachezaji wake wanne wa zamani.

    Juliette Karitanyi, mwanaharakati mjini Kigali, anasema kumruhusu Koffi kutumbuiza nchini Rwanda itakuwa "kutoheshimu waathiriwa wa unyanyasaji wa kingono".

    BBC ilizungumza na waandaaji wa tamasha lakini hawakuzungumzia madai ya wanaharakati hao.

    "Inaniuma zaidi kwamba tunamruhusu kutumbuiza hapa ilhali leo (Alhamisi) Rwanda imezindua siku 16 za harakati za kukomesha Unyanyasaji wa kijinsia" - Bi Karitanyi aliambia BBC.

    Wengine kwenye mitandao ya kijamii hata hivyo wanasema kuwa hakuna msingi wa kisheria wa kumzuia nyota huyo wa Rumba kutumbuiza nchini Rwanda.

    Vincent Karega, balozi wa Rwanda nchini DR Congo amesema kwenye Twitter kwamba "mapokezi makubwa yanamngoja" nyota huyo mwenye umri wa miaka 65 nchini Rwanda.

    Wakati Emma Uwingabire, mkazi wa Kigali anaiambia BBC kwamba "ni kinyume cha maadili kwa nchi ambayo inasema inawainua wanawake" kumkaribisha Koffi Olomide.

  5. Serikali ya Tanzania yaagiza kuanzishwa madawati kijinsia katika shule za msingi na Sekondari

    Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema serikali itaendeleza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na haitavumilia aina yoyote ya ukatili wa kijinsia utakaofanywa na yeyote.

    Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

    Majaliwa amesema nguvu kubwa inatakiwa kuongezwa katika kukabiliana na tatizo hilo linaloathiri vijana wengi wa kike.

    “Lazima jamii yetu ijenge msukumo wa kuhakikisha kuwa kila mtu katika nafasi yake anapaza sauti na kuchukua hatua ya kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani ukatili wa kingono kama vile rushwa ya ngono, ukatili baina ya wenza, ubakaji, mimba na ndoa za utotoni”.

    Majaliwa ameiagiza Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuandaa mpango mpya; Kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa za ukatili katika ngazi zote; kusimamia utekelezaji wa sera na sheria hususan Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, pamoja na kusimamia uendeshaji wa usimamizi wa Mahakama ya Familia ili kuimarisha ushughulikiaji wa migogoro ya ndoa na familia.

  6. Kanye West alilia ndoa yake na Kim Kardashian

    Kanye West na Kim Kardashian

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanamuziki wa miondoko ya kufoka foka nchini Marekani Kanye West amekiri kuwa alifanya makosa katika ndoa yake na Kim Kardashian

    Amesema kuwa ni mpango wa Mungu yeye na mke wake Kim Kardashian kurudiana na kutengeneza maisha kwenye nyumba pamoja na watoto wao .

    Akiwa mjini Los Angeles kwenye sherehe za shukrani , Kanye west, 44 alisema anaamini kuwa atarudiana tena na mke wake Kim Kardashian licha ya mwanamitindo huyo na nyota wa kipindi cha 'Keep up with the kardashians' kuwa katika mahusiano na muigizaji Pete Davidson

    “Mungu anataka kuona tunafufua mahusiano yote haya, tunafanya makosa. Nimefanya makosa” Alikiri Kanye Mshindi huyu wa tuzo za Grammy

    Kanye aliongeza kuwa amefanya vitu vingi hadharani ambavyo havikubaliki akiwa kama mume wa mtu,

    “lakini sasa kwa sababu yoyote ile sikujua nitakuwa mbele ya kipaza sauti hiki, lakini nipo sasa kubadilisha kauli zangu” alikiri Kanye.

    Akizungumza kuhusu mpenzi mpya wa Kim na nyota wa kipindi cha SNL, Kanye alisema hatoruhusu televisheni ya E kuandika simulizi juu ya familia yake, “sitaruhusu Hulu iandike simulizi ya familia yangu… mimi ni mchungaji katika nyumba yangu.”

    Aliongeza Kanye Aliendelea kueleza kuwa ana imani na Mungu kuwa ataungana tena na mke wake na watoto nyumbani, na kuanza kusambaratisha matendo ya shetani.

    “Kama kuna adui anaweza kutenganisha KIMYE, basi kutakuwa kuna mamia ya familia ambazo zinahisi kuwa kutengana ni sawa” anasema Kanye.

    Anasema “lakini wakati Mungu analeta KIMYE pamoja, kuna mamia ya familia ambazo zinashawishika kuona tumeweza kushinda utengano huu, vurugu za shetani ambazo zinatumia mtaji kuweka watu katika taabu.

  7. Watoto wachanga walizaliwa na aina ya HIV sugu kwa dawa kabla ya matibabu-WHO,

    Kipimo cha HIV

    Chanzo cha picha, SPL

    Shirika la Afya Ulimwenguni limesema kuwa karibu nusu (asilimia 45) ya watoto wachanga waliozaliwa katika nchi kumi za Afrika walizaliwa na aina ya HIV ambayo ni sugu kwa dawa inayotumika hata kabla ya kuanza matibabu.

    Wataalam wana wasiwasi kuwa takwimu zinaweza kuwa za juu zaidi.

    WHO inasema watu milioni 25.4 wanaishi na virusi vya ukimwi barani Afrika.

    Ni Nigeria, Cameroon, Togo, Afrika Kusini, Uganda, Kenya, Malawi, Msumbiji, Zimbabwe na Eswatini pekee ndizo zimefanya tafiti zinazoangalia ukinzani wa dawa za HIV kabla ya matibabu.

    Hii hugunduliwa kwa watu ambao hawana historia ya kutumia dawa za HIV kabisa.

    Nchi nyingine za Kiafrika hazijaweza kufanya tafiti za kina kuhusu hili.

    WHO inasema watoto wanaozaliwa na virusi vya ukimwi wanaweza kuwa ni matokeo ya wanawake wajawazito kutopimwa mara kwa mara na wengine kutokunywa dawa zao mara kwa mara.

    Dk Fausta Moesha kutoka ofisi ya WHO kanda ya Afrika anasema matokeo haya yanaangazia haja ya nchi kununua na kuwapa watoto dawa inayojulikana kama Dolutegravir.

    Matibabu haya yametajwa kuwa ya mabadiliko kutokana na ufanisi wake na ni rahisi kwa matumizi.

    Ni nchi chache tu barani Afrika ambazo zimesambaza dawa hii hadi sasa.

  8. Mume na mke wake wakamatwa kwa kuwauza watoto wao

    Vanguard

    Chanzo cha picha, Police Nigeria

    Vikosi vya usalama vya vya ulinzi wa raia nchini Nigeria vimemkamata mwanaume mmoja kwa jina , Elisha Effiong, kwa madai ya kupanga njama na mke wake ya kuwauza watoto wao wawili pesa za Nigeria - N700,000 (dola 1707) katika jimbo la kusini mwa nchi hiyo laAkwa Ibom.

    Gazeti la Vanguard limechapisha taarifa ya msemaji wa kamishna wa polisi Umana Ukeme Jumatano, akisema kuwa binti zao waliotaka kuwauza walikuwa na umri wa miaka sita na miaka minne.

    Kulingana naye, Effiong, ambaye anaishi nchini Cameroon na mke wake walikamatwa katika eneo la Uyo tarehe 15, 2021,kufuatia taarifa iliyotolewa kwa siri huku wakijaribu kuwauza watoto wao Abasifreke Edet na Rachael Edet .

    Taarifa hiyo imemnukuu mshukiwa akisema alitaka kuwauza watoto wake kwasababu ya umasikini mkubwa alionao.

  9. Shambulio la kujitoa muhanga dhidi ya msafara wa kampuni ya vikosi vya usalama Somalia laua 8

    Shababu

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Mlipuko ulitokea asubuhi wakati wa shuguli nyingi

    Police nchini Somalia wamethibitisha vifo vya raia wanane katika shambulio la bomu katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu , runinga ya serikali imeripoti imeripoti.

    Watu wengine 17 wamejeruhiwa , ikiwemo Watoto 13 kutoka shule jirani iliopo karibu na eneo la tukio.

    Mlipuaji wa kujitoa muhangaaliyekuwa akiendesha gari lililoja vilipuzi alilenga msafara wa magari ya kampuni binafsi ya vikosi vya usalama ya, Duguf iliopatiwa kandarasi kulinda Umoja wa mataifa UN.

    Polisi haikusema iwapo wafanyakazi wa Umoja wa mataifa waliumia katika shambulio hilo.

    Vyombo vya habari nchini humo vimesema kuwa mlipuko huo ulitokea wakati wa msongamano wa magari karibu na makutano yanayofahamika kama -Kilometre Four junction.

    Kundi lenye uhusiano na al-Qaeda la wanamgambo wa al-Shabab limethibitisha kutekeleza shambulio hilo. Vyanzo vya habari vinavyounga mkono al-Shabab media vimesema wanamgambo hao waliwalenga “maafisa wa kijeshi wazungu”.

    Mara kwa mara Al-Shabab wamekuwa wakiwalenga maafisa wa vikosi vya usalama na serikali mjini Mogadishu.

  10. Picha za baada ya mlipuko wa Somalia

    Mkurugenzi wa huduma za ambyulansi za Aamin Mogadishu, Abdikadir Abdirahman, ametuma picha za baada ya mlipuko uliotokea leo asubuhi.

    Moja ya picha hizionenyeshi basi za shule ya Mocaasir zilizoharibiwa.

    Chanzo cha usalama kilisema kuwa wanafunzi walikuwa miongoni mwa wale waliojeruhiwa.

    Dkt Adbdirahman alituma ujumbe wa Twitter kwamba mlipuko ulikuwa ni "janga":

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

  11. Watu watano wafariki katika mlipuko somalia- taarifa zinasema

    Watu watano wameuawa na wengine makumi kadhaa kujeruhiwa katika mlipuko uliotokea katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu, taarifa ya shirika la habari la AFP imesema, ikimnukuu afisa wa usalama.

    Bomu hilo lililokuwa limebebwa ndani ya gari , lililoripotiwa kuulenga msafara wa magari ya Muungano wa Afrika, pia limeharibu shule moja iliyopo karibu.

    Wale waliojeruhiwa ni pamoja na watoto wa shule, afisa alinukuliwa na AFP akisema.

  12. Saif Gaddafi azuiwa kugombea urais Libya

    Saif al-Islam Gaddafi anatafutwa na Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita na huonekana nadra hadharani(picha ya kumbukumbu)

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Saif al-Islam Gaddafi anatafutwa na Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita na huonekana nadra hadharani (picha kutoka maktaba)

    Mwana wa kiume wa aliyekuwa kiongozi wa Libya hayati Muammar Gaddafi ameenguliwa katika kinyang’anyiro cha kuwania uchaguzi wa tarehe 24 Disemba.

    Tume ya uchaguzi ilikataa maombi kadhaa ya kugombea kiti hicho yakiwemo ya Saif al-Islam Gaddafi, ikitaja "sababu za kisheria", vyombo vya habari viliripoti.

    Bw Gaddafi aliibua utata baada ya kutangaza kwamba atagombea urais.

    Anasakwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa madai ya uhalifu wa kivita na mauaji wakati baba yake alipoongoza taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.

    Maombi ya kuwania urais ya mwanasiasa mwenye ushawishi Khalfa Haftar pia yalisababisha wasiwasi katika nchi hiyo, kwani anakabiliwa na mashitaka katika mahakama za Marekani, lakini haijawa wazi iwapo yuko miongoni mwa wale ambao wamekataliwa.

    Waendesha mashitaka wa kijeshi wa Libya walikuwa wameiomba tume ya uchaguzi kuzuwia mchakato wa makaratasi ya kugombea ya Bw Gaddafi na Bw Haftar hadi watakapojibu maswali juu ya shutuma dhidi yao.

    Watu sitini waliwasilisha maombi ya kugombea urais wa Libya kufikia Jumatatu.

    Mwanaharakati wa haki za wanawake Leila Ben Khalifa, 46, ni mwanamke pekee anayegombe kiti hicho.

    Taarifa zaidi kuhusu Saif-al -Islam:

    • Libya: Mtoto wa Gaddafi Saif al-Islam yuko hai ataka kuongoza Libya
    • Saif al-Islam Gaddafi: Mwana wa kiume wa kiongozi wa zamani wa Libya kugombea urais
    • Mwana wa Gaddafi Saif al-Islam aachiliwa huru Libya
  13. Mkuu wa wafanyakazi wa Peru alificha dola 20,000 katika bafu la kasri

    Pesa hizo zilipatikana katika bafu katika kasri la serikal

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Pesa hizo zilipatikana katika bafu katika kasri la serikali

    Waendesha mashitaka nchini Peru wamepata $20,000 (£15,000) zimefichwa katika bafu ndani ya kasri la rais.

    Waendesha mashitaka walivamia kasri hilo Ijumaa kama sehemu ya uchunguzi kuhusiana na madai ya ushawishi wa kibiashara.

    Bruno Pacheco, ambaye alijiuzulu wadhifa wake wa mkuu wa wafanyakazi wa rais Pedro Castillo Ijumaa, aliwaambia wapelelezi kwamba pesa hizo zilikuwa ni zake , lakini akakana kufanya kosa lolote.

    Alisema kuwa pesa hizo ni mkusanyiko wa fedha za akiba yake na mshahara wake.

    Mshahara wa mwezi wa Pacheco ni jumla ya 25,000 ($6,250; £4,600), waraka rasmi umefichua.

    Kulingana na waraka huo, hakuwaambia wapelelezi ni kwanini alitunza kiasi hicho cha pesa katika bafu la ofisi yake.

  14. Waziri mkuu wa kwanza mwanamke Sweden ajiuzulu saa kadhaa baada ya kuteuliwa

    Sweden

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Wabunge wengi walisimama kumpigia makofi Magdalena Andersson (kulia) bungeni mapema Jumatano

    Waziri mkuu wa kwanza mwanamke kuwahi kushikilia wadhifa huo nchini Sweden amejiuzulu saa kadhaa tu baada ya kuteuliwa.

    Magdalena Andersson, alitangazwa kama kiongozi Jumatano, lakini alijiuzulu baada chama kushiriki katika muungano wake kujiuzulu serikalini na bajeti yake kushindwa kupitishwa.

    Badala yake, bunge lilipigia kura bajeti iliyoandaliwa na upinzani ambayo ilijumuisha mpango wa mrengo wa kulia zaidi wa kupinga uhamiaji.

    "Nimemwambia spika kwamba ningependa kujiuzulu ,"Bi Andersson aliwaambia waandishi wa habari.

    Mshirika wake katika muungano, chamba cha kijani (Greens Party) kilisema kuwa hakikuweza kuikubali bajeti "iliyoandaliwa kwa mara ya kwanza na chama cha upinzani cha mrengo wa kulia zaidi ".

    Bi Andersson alisema kwamba ana matumaini ya kujaribu kuwa waziri mkuu tena kama kiongozi wa serikali wa chama kimoja.

  15. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu mubashara leo Alhamisi tarehe 25.11.2020