Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Watu waliougua malaria hawawezi kuathirika kwa kiasi kikubwa na Covid-19-Utafiti
Utafiti mpya uliochapishwa na jarida la Lancet Microbe unasema kwamba watu ambao waliwahi kuambukizwa Malaria wana nafasi kubwa ya kutokuwa wagonjwa sana au kulazwa hospitalini kutokana na Covid-19.
Moja kwa moja
Lizzy Masinga
Ufaransa yawashauri raia wake kuondoka Ethiopia - AFP
Ufaransa imekuwa nchi ya hivi punde zaidi kuwashauri raia wake kuondoka Ethiopia huku waasi wa Tigray wakisema wanasonga mbele karibu na mji mkuu Addis Ababa, shirika la habari la AFP linaripoti.
"Raia wote wa Ufaransa wanahimizwa rasmi kuondoka nchini bila kuchelewa," ubalozi wa Ufaransa mjini Addis Ababa ulisema katika barua pepe iliyotumwa kwa raia wa Ufaransa, shirika hilo linaripoti.
Marekani na Uingereza ni kati ya nchi ambazo zimetoa ushauri kama huo katika wiki za hivi karibuni huku pia zikiwaondoa wafanyikazi wasio wa lazima.
Afisa wa ubalozi wa Ufaransa alisema kunaweza kuwa na kuondoka kwa "hiari" kwa wafanyikazi wa ubalozi, haswa wale walio na familia, ripoti ya AFP.
Watu waliougua malaria hawawezi kuathirika kwa kiasi kikubwa na Covid-19-Utafiti,
Utafiti mpya uliochapishwa na jarida la Lancet Microbe unasema kwamba watu ambao waliwahi kuambukizwa Malaria wana nafasi kubwa ya kutokuwa wagonjwa sana au kulazwa hospitalini kutokana na Covid-19.
Watafiti wa Uganda waligundua kuwa kuugua ugonjwa huo unaoenezwa na mbu kunawaepusha wagonjwa dhidi ya kuwa na hali mbaya.
Mwanzoni mwa utafiti, watafiti walitaka kujua juu ya athari zinazowezekana za maambukizo ya pamoja kati ya Malaria na Covid-19.
Lakini, walishangaa kubaini kwamba kuambukizwa Malaria kulipunguza visa vya kulazwa hospitalini miongoni mwa wagonjwa wa Uganda ambao walithibitishwa kuwa na virusi vya Covid-19.
Ugonjwa wa awali wa Malaria ulitoa mfumo wa kinga ya mtu na uwezo wa kudhibiti uvimbe.
Ingawa utafiti haukuangalia uhusiano kati ya malaria na Covid-19, watafiti wanasema matokeo haya yanaweza kuwa na athari katika kutengeneza dawa ya kutibu Covid-19.
Takriban watu 600 walishiriki katika utafiti huo ambao ulifanywa kati ya Aprili na Oktoba 2020.
Rais Kenyatta, Ramaphosa kujadili ushirikiano wa Kenya na Afrika Kusini
Rais Cyril Ramaphosa anamkaribisha mwenzake wa Kenya Uhuru Kenyatta katika ziara rasmi ya siku mbili wiki hii.
Wakuu hao wawili wa nchi walijadili biashara, ushirikiano wa kiuchumi, utengenezaji wa chanjo na usambazaji katika bara la Afrika.
Rais Ramaphosa na Rais Kenyatta walitia saini mikataba kadhaa kuanzia utalii, usafiri na uhamiaji.
Kuhusu suala la visa, ambalo linaonekana kuwa gumu kwa Wakenya, Rais Ramaphosa alisema ataunda timu kazi kuchunguza masuala yaliyoibuliwa na wasafiri wa Afrika Mashariki.
Mwaka jana Afŕika Kusini ilisafirisha bidhaa zenye thamani ya dola milioni 480 kwenda Kenya, huku ikiagiza bidhaa za dola milioni 20.
Marais hao wawili waliazimia kushughulikia usawa huu wa kibiashara na Bw Ramaphosa alisema vizuizi vyovyote vya biashara visivyo vya lazima vitaondolewa na anataka kuona bidhaa nyingi zaidi za Kenya nchini.
Kesho Rais Kenyatta atazuru kituo cha kutengeneza chanjo, alikosoa jinsi nchi za Magharibi zinavyojirundikia chanjo na kutoa wito kwa Afrika kutengeneza chanjo zake.
Ripoti ya mauaji ya Lekki ya Nigeria ni ya kughushi, asema waziri
Waziri wa Habari wa Nigeria Lai Mohammed amepuuzilia mbali ripoti iliyovuja ya uchunguzi uliobaini kuwa wanajeshi walifanya mauaji katika maandamano ya kupinga ukatili wa polisi katika mji mkuu wa Lagos mwaka jana.
Lai Mohammed aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu, Abuja, kwamba madai hayo yalikuwa "hadithi". “Kamwe katika historia ya jopo lolote la mahakama hapa nchini ripoti yake haijajawa na makosa mengi, sintofahamu, hitilafu, minong’ono, minong’ono, kuachwa na hitimisho ambazo haziungwi mkono na ushahidi,” alisema.
Ripoti ya kile kilichotokea kwenye lango la ushuru la Lekki ilivuja wiki iliyopita na bado haijawekwa wazi.
Ripoti iliyovuja ilisema kwamba vikosi vya jeshi viliwapiga risasi kwa makusudi waandamanaji wanaopinga ukatili wa polisi kwenye lango la ushuru la Lekki mnamo Oktoba 2020, na kisha kujaribu kuficha.
Bw Mohammed alikanusha kuwa kulikuwa na mauaji na kusema inashangaza kwamba madai yaliyotolewa na Wanigeria kwa jopo hilo yalikusanywa tu katika ripoti hiyo bila uchunguzi.
"Ripoti hiyo si chochote ila ushindi wa habari za uwongo na vitisho vya watu wengi wasio na sauti na kundi la watu wenye kelele," alisema.
Makumi kwa maelfu ya Wanigeria waliingia mitaani Oktoba mwaka jana wakitaka Kikosi Maalum cha Polisi cha Kupambana na Ujambazi (Sars) kivunjwe.
Maandamano ya #EndSars yalitikisa nchi kwa wiki mbili. Kitengo cha polisi kilikuwa kimeshutumiwa kwa kuiba, kushambulia na hata kuua watu.
Ligi ya Mabingwa Ulaya: Man Utd, Chelsea, Barcelona kufuzu leo?
Ni wiki ya kusisimua ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kukiwa na mapambano ya uzito wa juu kabisa kati ya Manchester City na Paris St-Germain na lile la Chelsea dhidi ya Juventus. Lakini ni nani anahitaji nini na ni nani aliyefuzu?
Kuna nafasi 12 kati ya 16 za hatua ya mtoano huku ikisalia michezo miwili ya hatua hiyo ya makundi.
Timu gani zilizofuzu?
Liverpool, Ajax, Bayern Munich, Juventus zimefuzu. Besiktas, RB Leipzig, Malmo zimeshaaga.
Nani anahitaji nini kufuzu?
Kundi A: Manchester City au Paris St-Germain kuongoza kundi. City itafuzu kama itaichapa PSG wiki hii. Sare yoyote itazifanya timu zote mbili zitafuzu kama Club Bruges itashindwa kushinda dhidi ya RB Leipzig.
Kundi B: Porto itafuzu pamoja na Liverpool kama itawachapa vijogoo hao wa Anfield na AC Milan itaichapa dhidi ya Atlectico Madrid pale Wanda Metropolitano. Kama Liverpool na AC Milan zote zitashinda itailazimisha Porto kusaka ushindi dhidi ya Atletico katika mchezo wa mwisho.
Ajax yenyewe ishafuzu, nafasi iliyosalia itategemea matokeo ya Borussia Dortmund itakayokuwa mgeni wa Sporting Lisbon. Ushindi wa Dortmund itawafanya wafuzu bila kujali matokeo megine ya mchezo wa mwisho. Ushindi kwa Inter Milan na Real Madrid tawafanya wote wafuzu kabla ya kukutana zenyewe kwa zenyewe pale Bernabeu Disemba 7, mechi itakayoamua nani ataongoza kundi D.
Ushindi wa Barcelona dhidi ya Benfica watafuzu pamoja na Bayern Munich. Ushindi wa Benfica utawafanya wawe katika nafasi nzuri ya kufuzu wakiwa na mchezo wa mwisho nyumbani dhidi ya Dynamo Kyiv. Manchester United inasafiri kwenda kucheza na Villarreal ikijua ushindi utawafanya wafuzu kutoka kundi F.
Kundi G kila timu inaweza kufuzu, ingawa ushindi wa RB Salzburg dhidi ya Lille utawafanya wafuzu, bila kujali matokeo mengine. Mabingwa watetezi Chelsea watafuzu 16 bora ikitoka sare tu bila kujali matokeo ya Zenit St Petersburg itakayosafiri kwenda Sweden.
Mechi za leo Jumanne
GROUP E
Dynamo Kyiv v Bayern Munich
Barcelona v Benfica
GROUP F
Villarreal v Manchester United
Young Boys v Atalanta
GROUP G
Lille v FC Red Bull Salzburg
Sevilla v VfL Wolfsburg
GROUP H
Chelsea v Juventus
Malmö FF v Zenit St Petersburg
Mechi za kesho Jumatano
GROUP A
Club Bruges v RB Leipzig
Manchester City v Paris Saint Germain
GROUP B
Atlético Madrid v AC Milan
Liverpool v FC Porto
GROUP C
Besiktas v Ajax
Sporting Lisbon v Borussia Dortmund
GROUP D
Inter Milan v Shakhtar Donetsk
Sheriff Tiraspol v Real Madrid
Nusu ya idadi ya watu duniani hawapati lishe bora-utafiti,
Utafiti uliofanywa na wataalam wa kimataifa wa afya unaonesha kuwa karibu nusu ya idadi ya watu ulimwenguni hawapati lishe bora kutokana na aidha wanakula chakula kidogo mno au wanakula kupitiliza.
Ripoti inayotolewa kila mwaka kuhusu lishe bora imegundua kuwa utapia mlo unasababisha matatizo ya kiafya kwa asilimia 48 ya idadi jumla ya watu duniani.
Hawa ni pamoja na watu walio na uzito wa mwili mkubwa mno, walio na uzito uliopindukia au walio na uzito wa chini mno.
Utafiti huo pia umegundua kuwa vifo vitokanavyo na tatizo hilo la lishe vimeongezeka kwa asilimia kumi na tano tangu mwaka 2012 na utapia mlo unachangia robo ya vifo vya watu wazima ulimwenguni.
Ripoti hiyo inakadiria kuwa takriban watoto milioni 150 walio chini ya umri wa miaka mitano ni wafupi mno kuliko umri wao, zaidi ya milioni arobaini na tano wameonda mno na watoto wasiopungua milioni arobaini ni wanene kupindukia.
Hisia zinazohusha raia wa kigeni na vifo vya watoto baada ya kula tambi Afrika Kusini zaibua wasiwasi
Tume ya haki za binadamu nchini Afrika Kusini imeibua wasiwasi kuhusu ujumbe wa mitandao ya kijamii zinazohusisha raia wa kigeni na vifo vya watoto watano baada ya kudaiwa kula tambi.
Tume ya Haki za Kibinadamu ya Afrika Kusini (SAHRC) ilibainisha kuwa baadhi ya ujumbe ulikuwa ukidai kwamba huenda raia wa kigeni waliharibu bidhaa maarufu ya chakula cha watoto - na kuwataka umma kutoeneza habari ghushi kuhusiana na matukio hayo.
Ilisema kuwa mamlaka za afya na polisi bado zinachunguza suala hilo na "hakuna ushahidi wa kupendekeza uwezekano wa kuchezewa au uhusiano wowote na biashara zinazomilikiwa na wageni".
Ilisema maoni kwamba "vifo vya kutisha ..kuwa ni matokeo ya kulipiza kisasi kwa raia wa kigeni hayana msingi wowote".
Ndugu wawili wanaripotiwa kufariki hivi majuzi katika jimbo la Limpopo baada ya kula tambi, huku watoto wengine watatu wakifariki huko Eastern Cape.
SAHRC inasema mamlaka za afya zimezingatia kurejesha "bidhaa zinazohusika iwapo ushahidi unaonesha kuwa hili linahitajika". Zana za kushiriki makala.
Kenya, Rwanda zaanza kutoa chanjo kwa watoto
Watoto nchini Kenya na Rwanda sasa wanastahili kupokea chanjo ya Pfizer huku nchi zote mbili zikianzisha kampeni za chanjo kwa rika hilo.
Rwanda itakuwa ikiwachanja watoto wenye umri wa kuanzia miaka 12 na kuendelea kuanzia Jumanne huku Kenya ikiwaruhusu wale wenye umri wa kuanzia miaka 15.
Rwanda ina idadi kubwa zaidi ya watu waliopata chanjo kamili katika Afrika Mashariki ikiwa na zaidi ya 20% ya jumla ya watu wote.
Nchi zilizosalia za ukanda huo ikijumuisha Kenya,Tanzania na Uganda wamechanja chini ya asilimia 10 ya watu wote.
Mpango wa chanjo ya vijana wa Rwanda utashughulikia nchi nzima na wazazi au walezi wanapaswa kutia saini fomu za idhini kabla ya watoto wao kupewa chanjo.
Rwanda itafanya kazi na shule kwa usambazaji na ukusanyaji wa fomu za idhini.
Nchini Kenya, Wizara ya Afya inatarajia kupokea dozi milioni nne za chanjo ya Pfizer kwenye kampeni yake ya kuwachanja vijana.
Mourinho amtunuku Felix Afena-Gyan jozi ya viatu baada ya kuifungia Roma
Kocha wa Roma Jose Mourinho amemnunulia Felix Afena-Gyan jozi mpya ya viatu baada ya kijana huyo kufunga bao lake la kwanza la Serie A Jumapili usiku.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 aliingia akitokea benchi dakika ya 75 ya mchezo wa Roma huko Genoa, na kufunga mabao mawili dakika za mwisho na kuwapa Giallorossi ushindi wa 2-0.
Mghana Afena-Gyan alikimbilia kwenye benchi kushangilia na meneja wake baada ya kufunga bao la kufutia machozi alipounganisha pasi ya Henrikh Mkhitaryan dakika ya 82.
"Nilimuahidi jozi ya viatu vya bei ghali sana, kwa euro 800, na alikuja kwangu kuhakikisha kuwa sisahau," Mourinho alimweleza mtangazaji wa DAZN. "Ninapenda sana utulivu wake, umbile lake lakini juu ya unyenyekevu wake wote."
Afena-Gyan kisha akaongeza bao la kustaajabisha la mkwaju mrefu katika dakika za majeruhi na kumalizia pointi kwenye Uwanja wa Luigi Ferraris na kuwapandisha Roma hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi.
Mourinho alitimiza ahadi yake na kumpa kijana huyo viatu Jumatatu. Baada ya mechi huko Genoa Afena-Gyan alizungumza juu ya "hisia zake kubwa" huku akishukuru familia yake kwa msaada wao. "Lazima niseme shukrani nyingi kwa Mwenyezi Mungu kwa kile alichonifanyia usiku wa leo," aliiambia tovuti ya Roma. "Ninajitolea kwa klabu, kwa wafuasi, kwa kila mtu, kwa familia yangu na kwa mama yangu. Mama... asante sana kwa jinsi ulivyonifikisha hapa. Ninashukuru sana."
Watu 12 wapoteza maisha baada ya kuvamiwa na wanamgambo DRC
Watu 12 wamepoteza maisha baada ya wanamgambo kuvamia kwenye kambi ya watu waliokimbia makazi yao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Baadhi ya mashirika ya kiraia yamesema idadi ya waathirika ni kubwa zaidi.
Kundi la waangalizi limesema shambulio hilo katika jimbo la kaskazini-mashariki la jimbo la Ituri limetekelezwa na wanamgambo wanaodai kutetea jamii ya Lendu.
Watu wengi katika kambi hiyo walikuwa washirika wa jamii pinzani ya Hema.
Kundi lenye silaha, Cooperative for the Development of Congo (Codeco) - ambalo wanachama wake wengi ni Lendu - limelaumiwa kwa kuua mamia ya raia huko Ituri katika miaka miwili iliyopita.
Waziri Mkuu wa Ethiopia aapa kuongoza wanajeshi kwenye uwanja wa vita
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed anasema sasa atawaongoza wanajeshi wake "kwenye uwanja wa vita" huku mzozo wa mwaka mzima ukiukaribia mji mkuu, Addis Ababa.
"Kuanzia kesho, tutakwenda mbele ili kuongoza vikosi vya ulinzi," Bw Abiy alisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye Twitter Jumatatu jioni.
"Wale wanaotaka kuwa miongoni mwa wazawa wa Ethiopia, ambao watasifiwa na historia, inukeni kwaajili ya nchi yenu leo. Tukutane mbele," aliongeza.
Hatua hii ilikuja baada ya kamati kuu ya chama tawala cha Prosperity kukutana siku ya Jumatatu kujadili vita hivyo.
Waziri wa ulinzi aliviambia vyombo vya habari vya ndani baada ya mkutano huo kwamba vikosi vya usalama vitaanza "hatua tofauti" kuhusu mzozo huo.
Tangu Novemba mwaka jana, serikali na vikosi vya waasi vya Tigray People’s Liberation Front (TPLF) vimekuwa vikishiriki katika vita vilivyoanzia Tigray na kuenea katika mikoa jirani ya Amhara na Afar.
TPLF limeunda muungano na vikundi vingine vya waasi likiwemo Jeshi la Ukombozi la Oromo (OLA) huku mzozo huo ukikaribia mji mkuu.
Wajumbe maalumu kutoka Umoja wa Afrika na Marekani wamekuwa wakijaribu kusuluhisha mzozo katika siku za hivi karibuni lakini kumekuwa na mafaniko madogo hadi sasa.
Mzozo huo umesababisha vifo vya maelfu ya watu, mamilioni ya watu wamelazimika kuondoka makwao na mamia ya maelfu wengine wanakabiliwa na njaa.
Afrika Kusini yatoa 'Suluhu' ya klabu ya Manchester United
Mashabiki wa soka nchini Afrika kusini wamempendekeza Pitso Mosimane – mmoja ya wakufunzi bora nchini humo kuchukua kazi ya ukufunzi katika klabu ya Manchester United .
Baada ya msusuru wa matokeo mabaya , klabu hiyo ya ligi ya premia ilimfuta kazi Ole Gunnar Solskjaer wikendi na kuanza kumtafuta mrithi wake ili kubadilisha matokeo hayo.
Wakufunzi kadhaa wamehusishwa na kazi hiyo lakini kulingana na Afrika Kusini ni mtu mmoja tu anayeweza kuifanya vyema kazi hiyo.
Picha bandia ya Mosimane akivalia jaketi lenye nembo ya Manchester United imesambazwa na wamiliki wengi wa mtandao wa twitter nchini humo.
Mmoja wao alifanya kazi ya ziada ya kumtagi kocha huyo na akaunti ya klabu hiyo.
Mosimane kwasasa anaifunza klabu kuu ya Misri Al Ahly.
Mwaka uliopita, aliiongoza timu hiyo kushinda taji la pili la klabu bingwa Afrika na baadaye timu hiyo ilifanya vyema katika michuano ya klabu bingwa duniani ambapo ilifikia nusu fainali.
Raia huyo mwenye umri wa miaka 57 awali alipata ufanisi mkubwa katika ligi ya Afrika kusiniakiifunza klabu ya Mamelodi Sundowns, akiongoza hadi kushinda taji la klabu bingwa Afrika mwaka 2016 pamoja na mataji matano ya ligi.
Inashangaza kuona ni nini Manchester United wanasubiri….
Hujambo . Ni siku nyengine ambapo tunakupasha kuhusu habari kutoka maeneo tofauti duniani