Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

’’Kasri la angani’’ la Gaddafi latua nyumbani Libya baada ya muongo

Ndege ya kibinafsi ya kiongozi wa zamaniwa Libya Hayati Muammar Gaddafi imetua Libya

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi

  1. Mnyarwanda anayeshukiwa kumtusi Rais Kagame apinga kesi yake kuendeshwa faraghani,

    Kesi ya Myarwanda anayeshukiwa kumtusi Rais Kagame apinga kesi yake kuwa faraghani.

    Kesi ya Bi Idamange Yvonne anayeshtakiwa kukana mauaji ya kimbari na kumtusi rais wa Rwanda Paul Kagame imeendelea leo.

    Mshitakiwa amepinga jopo la majaji wanaoendesha kesi hiyo baada ya jopo hilo kuamuru kuwa kesi itasikilizwa kwa faragha.

    Mwanamke huyo aliyejipatia umaarufu kupitia vipindi vyake vya kuikosoa serikali ya Rwanda anataka kesi yake kusikilizwa hadharani jambo linalopingwa na mwendeshamashitaka akisema huenda likasababisha athari mbaya na mkanganyiko miongoni mwa wananchi.

    Idamange anakanusha mashitaka dhidi yake akisema yeye ni mwanaharakati anayetetea demokrasia nchini.

    Yvonne Idamange amepandishwa kizimbani leo kwa kutumia teknolojia ya video akiwa katika Gereza la Mageragere na jopo la majaji likiwa mjini Nyanza ,

    Amesema mshukiwa aliyemtusi rais hadharani kwa kutumia Channel yake ya Youtube na sio lazima mahakama impe fursa tena kuendelea na kauliza zake na matusi.

    "Rais ni mtu maalum ambaye ametukanwa hadharani na sasa unataka korti iwe njia ya kupitishia matamshi hayo?’’ alihoji mwendesha mashtaka.

    Idamange na mawakili wake wamesema kesi lazima iendeshwe hadharani kwa sababu hata mashtaka dhidi yake yaliwekwa hadharani aliposhitakiwa na kusema katu hawezi kuhudhuria vikao vya kesi itakayoendeshwa kwa faraghani.

    Baada ya kusikiliza pande zote mbili, jopo la majaji limekata kauli kuwa kesi itaendeshwa faraghhani ili kuepuka kuwepo kwa mkanganyiko miongoni mwa wananchi kutokana na kauli za mshukiwa Bi Yvonne Indamange.

    Mara tu baada ya kusikia uamuzi wa korti Yvonne Idamange amesema anaamini hatapewa haki na kutangaza kupinga jopo la majaji.

    Jaji alisema kwamba kutokana na uamuzi wa mshukiwa kupinga jopo , korti itaamua tarehe itakapounda jopo jingine, terahe nyingine ya kesi na namna kesi hiyo itakavysikilizwa.

    Idamange Yvonne mwenye umri wa miaka 42 anayedai kuwa mwanaharakati na mtetezi wa demokrasia alikamatwa Aprili, 2021 kufuatia matamshi na video alizokuwa akiweka kwenye mtandao wake wa Youtube dhidi ya serikali.

  2. Diamond na Zari kushiriki katika kipindi cha maisha halisi cha Netflix

    Netflix imejiandaa kuanzisha kipindi cha maisha halisi kitakacho muhusisha nyota wa muziki nchini Tanzania, Abdul Naseeb al maarufu Diamond Platnumz.

    Msanii huyo ametoa tangazo hilo kwenye mitandao ya kijamii akisema kuwa atashiriki katika kipindi kinachoonyesha maisha halisi ya vijana maarufu wa kiafrika.

    Katika kipindi hicho Diamond atakuwa na mama wa watoto wake Zarina Hassan al maarufu Zari.

    Netflix South Africa ilikuwa imetuma kionjo kwenye ukurasa wake ikiwataka watumiaji wake kubashiri ni nani atakayeshiriki katika kipindi hicho kipya.

    “ Ni vijana, wako fresh, ni hawaombi msamaha kuwa Waafrika na watakuja kwenye skrini zenu ! Unaweza kubashiri baadhi ya nyota na misemo yao maarufu?” Netflix iliuliza.

    Zari Hassan, mama watoto wa Diamond anayeishi nchini Afrika Kusini, pia alituma ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii ili kuwafahamisha mashabiki wake kuwa atashiriki katika kipindi kipya cha maisha halisi:

  3. Wimbi la panya lawalazimisha wafungwa kuhama gereza

    Uharibifu mkubwa wa panya mmoja katika eneo la New South Wales, Australia, umelazimisha gereza moja kuwahamisha mamia ya wafungwa ili kufanya ukarabati na usafi.

    Zaidi ya wafungwa 400 na wafanyakazi 200 wa gereza laWellington watahamishia kwenye magereza mengine katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

    Panya hao wamesababisha uharibifu mkubwa kwa miundo mbinu ya gereza, ikiwa ni pamoja na nyaya za ndani ya gereza pamoja na paa.

    Gereza la New South Wales limekuwa likihangaishwa vibaya na panya kwa miongo kadhaa.

    Msimu wa mavumo mazuri umeongeza idadi ya panya katika jimbo hilo lililopo kusini-mashariki mwa Australia, ambako wanyama hao wamekuwa wakifanya uharibifu mkubwa wa mazao kwa miezi mashambani.

    Maafisa wa magereza ya taifa wanasema wafungwa katika gereza hilo watapunguzwa kwa miezi minne huku likisafishwa, kukarabariwa na kulindwa dhidi ya uharibifu siku za usoni.

  4. Rais mteule wa Iran ajitolea kuzungumza na Saudi Arabia

    Rais mteule wa Iran Ebrahim Raisi amesema kuwa "hakuna kikwazo" katika juhudi za kurejesha uhusiano na Saudi Arabia, ambaye ni mshirika wake mkuu ni Marekani katika Mashariki ya Kati.

    "Hakuna vikwazo kwa upande wa Iran kufungua tena ubalozi wake nchini Saudi Arabia," alisema.

    Kauli hizi za rais mteule zimekuja huku nchi mbili zikijadili jinsi ya kurejesha tena uhusiano wake ulioingia dosari tangu mwaka 2016.

    Bw Raisi ametoa wito kwa Saudi Arabia na washirika wake kusitisha mara moja mashambulio yote nchini Yemen.

    Amesema kuwa lengo kuu ni kuboresha uhusiano na majirani katika Mashariki ya kati.

  5. Rais wa zamani wa Ivory Coast amtaliki mke wake

    Vyombo vya habari vya Ivory Coast vinaripoti kwamba rais wa zamani wa nchi hiyo Laurent Gbagbo amempa talaka mke wake na mshirika wake Simone Gbagbo, siku kadhaa baada ya kurejea katika taifa hilo la Afrika magharibi akitokea Ubelgiji.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wa kibinafsi , wakili wa Laurent Gbagbo Claude Mentenon alisema kuwa Gbagbo alikuwa anataka kumtaliki Simone baada ya "kukataa mara kwa mara miaka mingi" kwa mama huyo "kukubali kuachana naye ".

    Simone kwa sasa ni Naibu mwenyekiti wa chama cha Laurent Gbagbo cha Ivorian Popular Front (FPI).

    Wote wawili walishitakiwa na Mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC) kwa uhalifu unaohusiana na mzozo uliotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 na 2011, lakini walipatikana bila hatia na kuachiliwa huru.

    Wakati mumewe alipokuwa hayupo nchini, mara kwa mara Simoni aliunga mkono na kutoa wito wa kurejea kwake nchini.

    Laurent Gbagbo, mweye umri wa miaka 76, amekuwa akiishi Nady Bamba, mwandishi wa zamani wa habari mwenye umri wa miaka 47-kwa miaka mingi. Alirejea naye nchini Ivory Coast tarehe 17 Juni.

  6. Muungano wa Ulaya kuiondolea vikwazo Burundi

    Muungano wa Ulaya uko katika mchakato wa kuiondolea vikwazo vya kifedha nchi ya Burundi, imesema ofisi ya rais nchini Burundi.

    Uamuzi wa kuondoa vikwazo hivyo ulitolewa na rais wa Burundi Emariste Ndayizeye wakati alipokutana na ujumbe wa Muungano wa Ulaya (EU) Jumatatu katika mji mkuu wa kisiasa wa Gitega na ofisi ya rais ilitangaza hayo kupitia mtandao wa Twitter.

    Mwakili wa EU nchini Burundi, Claude Bochu, alisema kuwahuu ni "mwanzo wa mchakato wa kuondoa vikwazo juu ya Burundi".

    Mwaka 2016, EU iliondoa usaidizi wa moja kwa moja wa kifedha kwa serikali ya Burundi kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu baada ya ghasia zilizofuatia jaribio la mapinduzi dhidi ya utawala wa aliyekuwa rais wan chi hiyo hayati Nkurunziza mwaka 2015.

    Tangu mwaka 2020, chini ya utawala wa Rais Evariste Ndayishimiye, Burundi imefanya juhuzi za kurejesha haki za binadamu na uhusiano na mataifa ya kigeni, na ilikuwa imeiomba EU kuiondolea vikwazo.

    Lakini makundi tofauti ya haki za binadamu Jumatatu wiki hii yauandikia Muungano wa Ulayakukemea “ ukosefu mkubwa wa kuwaadhidbu wenye makosa yaliyofanyika miaka ya nyuma na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea ” nchini humo.

  7. Wataalam wa Umoja wa Mataifa waitaka Vatican kukomesha unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto

    Wataalam huru wanaofanya kazi na Umoja wa Mataifa wameyataka makao makuu ya Kanisa Katoliki Vatican kufanya juhudi zaidi kuzuia ghasia na unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto.

    Wataalamu hao wametoa wito huo wakielezea ‘’kuendelea kwa madai ya kuwepo kwa vizingiti na ukosefu wa ushirikiano ''kutoka kwa Kanisa Katoliki'', imesema ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

    Katika barua yao ya tarehe 7 Aprili ambayo ilitangazwa kwa umma Jumatatu wiki hii, wataalamu hao walielezea hitilafu katika juhudi za kanisa ikiwa ni pamoja na ''kuwalinda wakiukaji, kuficha uhalifu, kuzuia uwajibishwaji wa wanaodaiwa kutekeleza unyanyasaji, na kukwepa kulipa fidia wanazopaswa kupewa waathiriwa''.

    Kwa ujumla, wataalam wanadai baadhi wajumbe wa kanisa hilo wamekuwa wakizuia kwa makusudi juhudi katika sheria za nchi za kuwashitaki wahusika wa makosa ya unyanyasajii wa kingono wa watoto.

    Wataalam hao wameelezea kuwepo kwa harakati za kuweka ukomo wa muda ambao waathiriwa wanaweza kuripoti uhalifu waliotendewa baada ya kuwa watu wazima

    Wanasema unyanyasaji huo unadaiwa kutekelezwa zaidi ya miongo kadhaa katika nchi nyingi huku kukiwa na maelfu ya waathiriwa.

    Makao makuu ya Vatican hayajatoa tamko kwa umma kujibu barua hiyo.

    Mamlaka hiyo imekuwa ikikosolewa vikali kwa kushindwa kushighulikia unyanyasaji wa mkubwa wa waathiriwa unaofanyika katika nchi nyingi na kushindwa kuwaadhibu au kuwaondoa maaskofu, mapadre na viongozi wao wengine kuficha unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto.

  8. ’’Kasri la angani’’ la Gaddafi latua nyumbani Libya baada ya muongo

    Ndege ya kibinafsi ya kiongozi wa zamani wa Libya Hayati Muammar Gaddafi imetua katika mji mkuu wa Libya Tripoli baada ya karibu muongo mmoja ikiwa nchini Ufaransa, vimeripoti vyombo vya habari vya Libya na vya Kiarabu.

    Ndege hiyo kubwa, aina ya Airbus A340, ilipaa juu ya anga la Tripoli kabla ya kutua katika uwanja wa kimataifa wa Mitiga karibu na mji mkuu, iliripoti televisheni ya Arab Al Arabiya TV.

    Vyombo mbali mbali vya habari vilinukuu kauli za Waziri Mkuu Abdul Hamid Dbeibah, ambaye alikuwa katika uwanja wa ndege kushuhudia ndege hiyo ikiwasili jana usiku.

    Amesema kuwa ukarabati wa ndege hiyo na taratibu nyingine vimekamilika, na serikali ya mpito imelipia gharama zilizohitajika kuirejesha Libya, ilitangaza ofisi ya Waziri mkuu kwenye ukurasa wake wa Facebook.

    Bw. Dbeibah alisema kwamba ndege nyingine 14 aina ya jet zilizosalia, 12 kati yake zimepangiwa kurejea Libya, huku serikali ikishughulikia kurejea kwa ndege mbili bora zaidi.

    Kulingana na televisheni ya Al Arabiya, jet ya Gaddafi, ambayo inafahamika pia kama "Kasri inayopaa", ilipaa kimo cha chini juu ya mji wa Tripoli na kuyazunguka maeneo kabla ya kutua ardhini.

    Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ndege hiyo, Bw Dbeibah alisema "watu wa Libya ndio watakaoamua hatma yake" na kama itatumiwa na maafisa au wengine, manufaa ya umma, kulingana na Al Arabiya.

    Alisema kuwa kurejea kwa ndege hiyo maarufu nchini ni "hatua nzuri kwa Libya, usalama wake na utajiri", ilisema televisheni hiyo.

    Ndege hiyo ya kifahari, ilielezewa na baadhi kama "ndege ya Airbus yenye muonekano wa nyumba ya [James] Bond ndani ", ilivivutia vyombo vya habari vya kimataifa kwa miaka iliyopita.

    Gaddafi – ambaye aliiongoza Libya kwa miongo sita-na ambaye anafahamika kama kiongozi aliyekuwa na nguvu za mamlaka kibinafsi ambaye alionekana katika jukwaa la dunia kama mwenye mtindo wake wa uongozi, aliuawa katika mji wa nyumbani kwa wa Sirte mwezi Oktoba 2011 wakati wa mzozo ulioibuka kufuatia uasi mwezi Aprili mwaka huo.

    Mamlaka ya serikali mpya ya Libya, Serikali ya Umoja wa kitaifa(GNU) inayoongozwa na Bw Dbeibah, iliinga mamlakani baada ya kuchukua mamlaka kutoka kwa serikali iliyokuwa na makao yake mjini Tripoli na iliapishwa mwezi Machi kufuatia uchaguzi uliofanyika mapema mwaka huu katika mchakato uliodhaminiwa na Umaoja wa Mataifa.

  9. Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu mubasha leo Jumanne tarehe 22.06.2021