Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Rais Museveni aishutumu Facebook kuwa na upendeleo dhidi ya chama chake

Kwa mara nyingine tena Rais Yoweri Museveni ameishutumu kampuni kubwa ya teknolojia ya mawasiliano Facebook kwa kuwa na upendeleo dhidi ya chama tawala cha Uganda na wafuasi wake.

Moja kwa moja

Ambia Hirsi

  1. Meli ya kijeshi ya Marekani yawasili Sudan baada ya meli ya Urusi

    Meli ya kivita ya Marekani imetia nanga katika mwambao wa Sudan Port Sudan siku moja baada ya meli ya Urusi kuwasili katika bandari hiyo hiyo iliyopo katika bahari nyekundu.

    Wanadiplomasia wa Marekani wanasema ziara ya pili ya meli ya kikosi cha wanamaji cha Marekani inaonesha utashi wa kuimarisha ushirikiano mpya baina ya nchi mbili.

    Marekani iliiondoa Khartoum katika orodha ya nchi zinazodhamini ugaidi kufuatia kupinduliwa kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Omar al-Bashir mwaka 2019.

    Urusi inajenga ngome ya jeshi la majini karibu na bandari ya Port Sudan, yenye ukubwa wa kutosha kuweza kupokea meli nne za kijeshi na wanajeshi 300.

  2. Rais wa zamani wa Ufaransa ahukumiwa kifungo

    Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani, miwili kati ya hiyo mitatu ni kifungo cha nje, kwa kujihusisha na rushwa.

    Kiongozi huyo wa zamani amekutwa na hatia ya kujaribu kumpa rushhwa jaji kwa kumpa kazi nzuri yakiwa ni malipo ya kupatiwa taarifa kuhusu kesi ya jinai dhidi yake.

    Ni rais wa kwanza wa zamani kupatiwa adhabu ya kifungo .

    Jaji na wakili wa zamani wa Sarkozy walipata adhabu hiyo hiyo. Na wote watatu wanatarajiwa kukata rufaa.

    Katika hukumu, jaji jijini Paris alisema Sarkozy anaweza kutumikia kifungo cha mwaka mmoja nyumbani akiwa na utambulisho wa kielektroniki , kuliko kwenda gerezani.

    Mwanasiasa huyo wa kihafidhina "alijua kuwa alichokuwa anakifanya kilikuwa kibaya", jaji alisema, akiongeza kuwa vitendo vyake na vya wakili wake vilitoa "picha mbaya sana kuhusu haki".

  3. Rais Museveni asema Facebook ina upendeleo

    Kwa mara nyingine tena Rais Yoweri Museveni ameishutumu kampuni kubwa ya teknolojia ya mawasiliano Facebook kwa kuwa na upendeleo dhidi ya chama tawala cha Uganda na wafuasi wake.

    Matandao huo wa kijamii ulifunga akaunti kadhaa zenye uhusiano na chama cha National Resistance Movement (NRM) siku kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi Januari, ikizituhumu kuhusika katika uratibu wa mienendo isiyo ya kuaminika katika jaribio la kushawishi mdahalo wa umma kabla ya uchaguzi huo.

    Wakati huo Bw Museveni aliishutumuFacebook kwa "majivuno " na akatangaza kupigwa marufuku kwa mtandao huo. Hadi sasa mtandao huo haupatikani nchini Uganda isipokuwa kwa kutumia mtandao wa) Virtual Private Network (VPN

    Katika mkutano wa Jumapili na "waathiriwa wa Facebook" – Wajumbe wa NRM ambao akaunti zao zilifungwa-rais aliwaambia wako vyema bila mtandao huo.

    "Tangu Facebook iondoke, mliwahi kusikia kuna uhaba wa sukari mjini? Hamna nguo ? Facebook itaongea lakini tutasonga, wao sio Mungu ,"Bw Museveni alisema.

    Aliongeza kuwa: ‘’Hii ndio sababu katika baahdi ya nchi hawaruhusiwi, je wanafanya kazi Uchina? Tuachane na hayo, kile nilichosikia ni kwamba Mungu yupo kila mahali, kila mahali na anafahamu kila kitu.Sijawahi kusikia kwamba Facebook iko katika kitengo hicho."

  4. Chanjo ya Corona ‘haitaangamiza kizazi cha Waafrika’

    Ghana inapojiandaa kutoa chanjo ya corona wiki hii, Rais Nana Akufo-Addo ametoa wito kwa raia wake kupuzilia mbali dhana za uongo zinazotilia shaka mpango huo.

    Bw. Akufo-Addo amesema baadhi ya watu wanahoji uwezo wa chanjo hiyo, na wengine wanaamini chanjo hizo zimebuniwa kuangamiza kizazi cha Waafrika, lakini hiyo si kweli.

    Bw. Akufo na mke wake wanatarajiwa kuchanjwa leo, kabla ya chanjo hiyo kutolewa rasmi kwa wananchi wa Ghana siku ya Jumanne.

    Wimbi la pili la Covid-19 limesababisha vifo vya watu 200 nchini humo katika miezi ya hivi karibuni, idadi ambayo inakaribia thuluthi moja ya jumla ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa huo.

  5. Wazanzibari sasa kupeleka malalamiko kwa Rais ki-elektroniki

    Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imezindua mfumo wa kielekronik ambao utawezesha kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na kueleza changamoto wanazopitia wanapokwenda kuhudumiwa katika taasisi za serikali.

    Mfumo huo uliopewa jina la “Sema na Rais Mwinyi (SNR)” unawezesha wananchi kupiga simu au kutuma ujumbe kwa njia ya tovuti.

    Aidha mlalamikaji anaweza Kuambatanisha hati, sauti na hata picha kama ushahidi wakati wa kuwasilisha malalamiko kisha mlalamikaji atapokea namba ya siri ili kufuatilia kujua lalamiko lililotolewa limefika wapi kupata ufafanuzi na afisa anayeshugulikia.

    Rais Mwinyi anasema mfumo huo ni moja ya utekelezaji wa ahadi zake kipindi cha kampeni “Baada ya kuwasikiliza Wazanzibari nilitoa ahadi ya kuwa karibu yenu kwa kusikiliza na kutatua changamoto zenu, Ahadi yangu leo imepata ufumbuzi wa kudumu baada ya kuwatengenezea wananchi mfumo wa ki-elektoniki wa malalamiko ambao nimeuzindua rasmi” amesema Rais Mwinyi.

    Pia unaweza kusoma:

    • Siku 100 za utawala wa Rais Mwinyi,mafanikio, changamoto
    • Hussein Mwinyi: Mfahamu zaidi rais wa Zanzibar

    Baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wanaona Rais Mwinyi ameanza vizuri katika kupambana na kero za wananchi ambazo zimedumu kwa kipindi kirefu huku wakitaka mfumo huo uwe endelevu.

    “Mfumo huu utakuwa msaada sana maana Rais hawezi kwenda kusikiliza kila mtu lakini sasa anaweza kupata malalamiko yao na hao wananchi wanaweza kutoa madukuduku yao kwa uhuru'',anasema Issa Jumaa -Mchambuzi wa siasa.

    ''Lakini kupokea kero ni jambo moja na kero kushugulikiwa ni jambo lingine''. Issa Jumaa-Mchambuzi wa siasa'', aliongeza kusema .

    Kipindi cha kampeni za uchaguzi Rais Mwinyi, alitangaza baadhi ya vipaumbele vyake ikiwa ni pamoja na kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma kuboresha uwajibikaji kwa kupambana na uzembe wa watumishi wa serikali, ambapo ameahidi kushughulikia tatizo hilo kwa mtindo wa Rais Magufuli.

  6. Okonjo-Iweala aanza rasmi kazi kama mkuu wa WTO

    Mnageria-Mmarekani, Ngozi Okonjo-Iweala, anaanza rasmi kazi kama mkuu mpya wa Shirika la Biahsara Duniani (WTO) Jumatatu ya leo.

    Dkt Okonjo -Iwela ambaye ni waziri wa zamani wa fedha na mambo ya nje wa Nigeria, ni mwanamke wa kwanza wa Afrika kuongoza WTO.

    Ngozi Okonjo-Iweala amesema kipaumbele chake ni kushughulikia masuala ya afya na athari za kiuchumi zinazotokana na majanga.

    Kuna wasiwasi huko Washington na miji mikuu mingine kuhusu sera za biashara za China na jinsi WTO inavyojiandaa kushughulikia masuala hayo.

    Dkt Okonjo-Iweala anafahamika kwa kuwa mwana -mageuzi, lakini atakabiliwa na mslahi ya nchi wanachama.

    Soma zaidi:

    • Ngozi Okonjo awa Mwafrika na mwanamke wa kwanza kuongoza Shirika la biashara la dunia
  7. Bobi Wine ajipata 'mashakani kwa kuwa na gari la kifahari'

    Kiongozi wa upinzani wa Uganda Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine amejipata mashakani kwa madai ya kuwa na gari ambalo haliingii risasi, kulingana na taarifa katika gazeti la Daily Monitor.

    Gari hilo limevutia mamlaka nchini Uganda, huku mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru ya Uganda (URA) ikisema maelezo yaliyotolewa si sahihi na kwamba thamani yake iko chini kuliko inavyostahili kuwa.

    URA, sasa inataka gari hilo kukaguliwa upya.

    Bobi Wine, hata hivyo amekataa kuwasilisha gari hilo kwa misingi kwamba agizo hilo haliambatani na sheria, kulingana na taarifa yake iliyonukuliwa na gazeti la Daily Monitor.

    “Japo mna uwezo chini ya kifungu cha 236(d) cha usimamizi wa forodhani katika Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, kukagua bidhaa, hamna uwezo wa moja kwa moja kukagua tena bidhaa ambayo ilikuwa katika (bohari lenu), na ambayo ilikuwa imekaguliwa, kutathmini kodi na kodi hiyo kulipwa kabla ya bidhaa kutolewa kwa mmiliki/mlipa kodi," ilisema.

    Gari hilo liliingizwa nchini na kusajiliwa Kenya mwaka jana na kisha kupelekwa Uganda kupitia mpaka wa Busia.

    Katika ujumbe alioweka mtandaoni Februari 21, Bw. Kyagulanyi alidai kuwa gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser lilitolewa kwake kama msaada na marafiki na wafuasi wake nchini Unganda na ughaibuni:

  8. Chadwick Boseman ashinda tuzo ya muigizaji bora Golden Globe

    Chadwick Boseman alishinda tuzo yake ya kwanza ya Golden Globe katika filamu ambayo hakuishi kuiona.

    Mjane wa nyota huyo Taylor Simone Ledward, alikubali tuzo hiyo ya muigizaji bora kwa niaba ya muigizaji huyo , ambaye alifariki mwezi Agosti kutokana na saratani ya utumbo akiwa na umri wa miaka 43 – miezi mitatu kabla ya filamu kwa jina ‘’Ma Rainey’s Black Bottom’’ kuzinduliwa.

    ‘’Angesema kitu kizuri chenye msukumo , kitu ambacho kingepaza ile sauti ndogo ndani yetu sote inayosema unaweza’’, alisema Simone Ledward, huku yeye na waliohudhuria wakijifuta machozi.

    ‘’Hilo linakwambia endelea, hilo linakuita na kukurudisha katika kile ambacho unapaswa kufanya wakati huu katika historia’’.

    Boseman ni mtu mweusi wa kwanza katika orodha hiyo katika kipindi cha miaka 15.

    Forest Whitaker alishinda katika sherehe ya 2007 kwa kuigiza kama Idi Amin ‘’the Last king of Scotland’’.

    Tuzo hiyo pia inamfanya Boseman kuwa mtu mweusi wa kwanza aliyefariki kushinda tuzo hiyo katika orodha ya uigizaji.

    Boseman alikuwa maarufu katika filamu ya michezo ya '42' ya mwaka 2013 kuhusu ubaguzi aliofanyiwa mchezaji wa kulipwa wa besiboli Jackie Robinson na ile ya 'Get on Up' mwaka 2014 kuhusu maisha ya mwimbaji wa nyimbo aina ya soul James Brown.

    Nyota huyo, Boseman, aliigiza kama mtawala wa Wakanda, filamu iliyoangazia Afrika ya kufikirika yenye teknolojia zilizoendelea sana za kisasa.

  9. Natumai Hujambo.Karibu tena katika habari zetu mubashara