Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Kagame ataja 'unafiki' katika usambazaji wa chanjo ya corona

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema mkataba kati ya mataifa tajiri na watengenezaji wa chanjo umefanya mpango wake wa Covax kutofanikiwa.

Moja kwa moja

Ambia Hirsi

  1. Watu 10 wafariki katika shambulio linashukiwa kuwa la Boko Haram

    Shambulio la siki ya Jumanne linaloshuiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Boko Haram katika mji wa Maiduguri uliopo jimbo la Borno limesababisha vifo vya watu 10 na wengine 47 kujeruhiwa.

    Gavana wa jimbo hilo Babagana Zulum amesema washambuliaji walitumia guruneti iliyorushwa kwa kutumia roketi katika mji huo unaokaliwa na watu wengi, ikiwemo viwanja vya watoto kucheza. Alisema guruneti hizo zilirushwa kutoka viungani mwa mji huo.

    Picha zilizotolewa na mamlaka za jimbo hilo zinaonesha makumi ya watu waliojeruhiwa miongoni mwao watoto wakiwa hospitali.

  2. Mkutano wa wanahabari kukanusha uvumi wa kifo wakosolewa Tanzania

    Video ya kufadhaisha ya Waziri wa Fedha wa Tanzania akiwahutubia waandishi wa habari ili kukomesha uvumi kwamba amefariki imekosolewa pakubwa, baadhi ya watu wakiitaja kuwa ya kikatili.

    Wiki iliyopita Rais John Magufuli alipuuzilia mbali uvumi huo, akisema Dkt Philip Mpango "yuko hai na anaendelea kupata nafuu".

    Siku ya Jumanne, Dkt Mpango akiwa pamoja na wahudumu wawili wa afya, ambao hawakua wamevalia barakoa, walizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Benjamin Mkapa katika mji mkuu, Dodoma.

    katika video hiyo alionekana akikohoa na kutulia kidogo mara kwa mara ili kuvuta pumzi wakati akisoma taarifa yake.

    Kiongozi wa upinzani Tundi Lissu aliwakosoa maafisa kwa kuruhusu mkutano wake na wanahabari kufanyika.

    "Nani aliyemruhusu mtu mgonjwa kufanya hivi, anakohoa na hajavalia barakoa. Anastahili kupumzika na kupokea matibabu," alisema.

    Haijabainika anaugua nini lakini alisema ana "tatizo la kupumua" na kwamba anahitaji oksijeni yaya ziada. Pia alisema amepona.

  3. Msumbiji inachunguza vifo vya pomboo 111 katika kisiwa kimoja

    Mamlaka nchini Msumbiji zinachunguza chanzo cha vifo vya zaidi ya pombo 100 katika kisiwa kimoja Kusini mwa nchi hiyo.

    Pomboo hao walipatikana wamekufa katika pwani ya kisiwa cha Bazaruto, Mkoani Inhambane.

    Pomboo 25 wa kwanza walipatika Jumapili na wengine 86 siku ya Jumanne.

    Wote ni wa spishi moja inayofahamika kama, Stenella Longirostris.

    Mkuu wa kitengo cha ukaguzi cha mbuga ya kitaifa ya Bazaruto Archipelago, Tomás Manasse, amesema uchunguzi wa awali unaashiria “tatizo katika ngoziproble, ulimi au utumbo” lakini sampuli zimepelekwa katika maabara mji mkuu, Maputo.

  4. Hofu baada ya nzige kuvamia mkoa wa Kilimanjaro,

    Kundi la Nzige waharibifu wa jangwani limeingia wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro Kaskazini mwa Tanzania na kuibua hofu ya uharibifu wa mazao ya chakula.

    Wilaya hiyo inazalisha mazao mbali mbali ya chakula na kibiashara kama mahindi, mboga, maharage na mengineyo.

    Sio mara ya kwanza kwa uvamizi wa kuripotiwa katika wilaya ya Siha, siku za hizi karibuni.

    Taarifa hizi zinakuja wakati ambapo kikosi cha wataalamu kinaendelea na kazi ya kuwanyunyizia dawa wakitumia ndege mkoani Arusha kwenye wilaya za Longido na Simanjiro ambapo waliripotiwa mwishoni mwajuma.

    Tayari Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda na jopo la wataalamu wameshafika mkoani Kilimanjaro kutathimini athari na kuweka mikakati ya kuwaangamiza wadudu hao ambao huzalia kwa wingi na kwa muda mfupi.

    Wilaya zilizoshambuliwa awali hazikuwa na hofu kubwa ya uharibifi wa mazao kwani makundi hayo yalishambulia zaidi maeneo ya malisho ya mifugo.

    Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, amesema kazi ya kuwadhibiti bado inaendelea kwani wadudu hao waharibifu walivamia maeneo ya malisho na tayri asilimia kubwa ya eneo hilo limeshapuliziwa dawa ambayo kwa mujibu wa wataalamu matokeo yake huanza kuonekana ndani ya saaa 24 hadi 72.

    Wananchi wameendelea kuonywa kuwa waangalifu kutokula au kuokota nzige hao au kulisha mifugo kwenye maeneo yaliyopuliziwa dawa, huku shule zikiendelea kufungwa kupisha zoezi hilo.

    Soma zaidi:

    • Namna nzige mmoja anavyosababisha baa
    • Nzige huenda wakasababisha ukosefu wa chakula na utapia mlo
  5. Mwili wa balozi wa Italia umesafirishwa Roma kutoka DR Congo

    Mwili wa balozi wa Italia aliyeuawa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika jaribio la utekaji nyara uliotibuka siku ya Jumatatu, umesafirishwa mjini Rome.

    Luca Attanasio, mlinzi wake Vittorio Lacovacci, na dereva wake raia wa DR Congo Moustapha Milambo, waliuawa katika shambulio lililofanywa dhidi ya msafara wa magari ya chakula ya Umoja wa Mataifa, Mashariki mwa nchi hiyo.

    Ndege ya kijeshi ya Italia iliyokuwa imebeba majeneza mawili yaliyokuwa yamefunikwa bendera ya kitaifa ilitua katika uwanja wa ndege wa Ciampino mjini Rome na kupokelewa na Waziri Mkuu, Mario Draghi.

    Mamlaka nchini DR Congo zimelaumu kundi la waasi wa Rwanda la FDLR kwa mauaji.

    Kundi hilo limekanusha kuhusika na shambulio hilo.

    Maelezo zaidi:

    • Balozi wa Italia auawa DRC
  6. Uganda yapinga madai ya Museveni kupewa kisiri chanjo ya corona

    Waziri wa Afya wa Uganda, Jane Aceng, amekanusha ripoti zinazoashiria kwamba maafisa wa ngazi ya juu serikalini wamepewa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kabla ya nchi kupokea rasmi chanjo hiyo.

    Bi. Aceng alikuwa akijibu taarifa zilizochapishwa katika gazeti la Daily Monitor nchini humo na gazeti la Marekani la Wall Street Journal.

    Katika ujumbe wa Twitter, Wizara ya Afya imesema hakuna aliyepewa chanjo kati ya rais na wandani wake wa karibu kama ilivyodaiwa.

    "Ninataka kusema waziwazi kwamba Rais Museveni na maafisa wake wakuu hawajachanjwa dhidi ya Covid-19," waziri alisema.

    Kufikia sasa Uganda imethibitisha kuwa na wagonjwa 40,221 wa corona.

    Nchi hiyo inatarajia kupokea msaaada wa dozi 100,000 za chanjo aina ya AstraZeneca kutoka India na dozi zingine 300,000 za chanjo ya Sinopharm kutoka China.

    Haijabainika ni lini chanjo hizo zitawasili nchini humo.

    Soma zaidi:

    • Ni mataifa gani yamepata chanjo ya corona Afrika
  7. Taharuki yatanda Niger baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa

    Makabiliano kati ya waandamanaji na yameshuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu wa Niger, Niamey, kabla na baada ya Mohamed Bazoum kutangazwa mshindi katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais

    Wafuasi wa mpinzani wake Mahamane Ousmane waliokuwa na hasira waliandamana katika ngome ya upinzani na maeneo ya karibu na makao makuu ya chama Hama Hamadou,kiongozi wa zamani wa upinzani.

    Magurudumu ya magari yalichomwa na magari ya kampeni ya chama tawala cha Tyres PND kuharibiwa.

  8. Kagame ataja 'unafiki' katika usambazaji wa chanjo ya corona

    Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema kuna "unafiki" katika usambazaji wa chanjo ya Covid-19 duniani.

    Rais Kagame amesema hayo katika ujumbe wa Twitter baada ya Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, kusema kwamba mkataba ulioafikiwa kati ya mataifa tajiri na watengenezaji wa chanjo umefanya kuwa vigumu kwa shirika hilo kupata chanjo kwa ajili ya mpango wake wa Covax.

    Covax ni mpango wa kuhakikisha kuna usambazaji sawa wa chanjo ya Covid-19 katika nchi zote duniani.

    Mataifa tajiri yamekosolewa kwa kuhodhi chanjo na kufanya kuwa vigumu kwa nchi masikini kupata chanjo yoyote.

    Soma zaidi:

    • Ni mataifa gani yamepata chanjo ya corona Afrika
    • Ukipata maambukizi ya corona utakuwa na kinga kwa miezi kadhaa
  9. Karibu katika matangazo mubashara Jumatano 24.02.2021