Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Mganga Mkuu asimamishwa kazi kwa kutoa 'taarifa zisizo za kweli'

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Dkt Doroth Gwajima ameamuru kusimamishwa kazi kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Dkt Felista Kisandu kwa kutoa taarifa kuhusu kuwepo kwa ugonjwa usiofahamika

Moja kwa moja

Lizzy Masinga, Dinah Gahamanyi and Asha Juma

  1. Na hadi kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa hii leo. Mola akijalia kesho pia ni siku.

  2. Maisha yarejea kama kawaida nchini Rwanda baada ya kufungiwa

    Jumatatu yenye ukungu katika mji mkuu wa Rwanda, watu wamejaa mitaani wakirejelea kutoka katika shughuli zao za kila siku baada ya kuzuiwa kutotoka nje kwa wiki tatu kama njia moja ya kupunguza makali ya virusi vya corona.

    Maafisa wa afya wanasema wa marufku ya kutoka nje, maambukizi ya virusi vya corona yamepungua kwa kiwango kikubwa katika mji wa Kigali na kote nchini humo.

    "Maisha yamerejea tena, sio kama kawaida, lakini kuwa nyumbani kwa wiki tatu haikuwa jambo rahisi," mwendesha pikipiki amezungumza na idhaa ya BBC Great Lakes.

    Mjini Kigali, maduka mengi yamefunguliwa, mabasi na pikipiki sasa zinafanyakazi na raia wameanza tena kujishughulisha na mambo yao tofauti tofauti, amesema mwandishi wa habari wa BBC Yves Bucyana katika mji huo lakini bado hayajarejea kama ilivyokuwa.

    Shule zote nchini humo zimefungwa ,makanisa,misikiti na maeneo ya burudani na mikusanyiko ya umma bado yamepigwa marufuku.

    Na pia kuanzia Jumatatu, kutakuwa na marufuku ya kutotoka nje usiku.

    "Wakati ambao raia hawakuruhusiwa kutoka nje, maambukizi ya virusi vya corona yalipungua kutoka 365 hadi 150 kwa siku nchini humo … na idadi ya vifo kutoka 10 hadi viwili au vitatu kwa siku," Dkt. Tharcisse Mpunga, afisa wa juu katika wizara ya afya amezungumza na shirika la habari la Rwanda linalomilikiwa na serikali.

    Jumapili, Rais Paul Kagame amesema katika mkutano na timu ya taifa ya Rwanda kuwa nchini hiyo inatarajia chanjo ya virusi vya corona kufikia mwisho wa Februari lakini "bado watu watazingatia hatua za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo".

  3. Bangi yanaswa nchini Msumbiji

    Polisi nchini Msumbiji imesema kuwa imekamata kilo 100 za bangi maarufu kama souruma, katikati mwa mkoa wa Zambezia.

    Wapelelezi wanasema wamemkamata mmiliki wa bangi hiyo pamoja na wanunuzi wawili waliokiri kuwa wao huvuta bangi.

    Inaaminika kuwa bangi hiyo imetoka bandari ya Beira, maafisa wamesema.

    Polisi imeongeza kuwa uchunguzi unaendelea ili kukabiliana na mtandao unaojishughulisha na biashara hiyo haramu.

  4. Kambi ya jeshi ya Uingereza nchini Kenya yatengwa

    Kambi ya kijeshi ya Uingereza nchini Kenya imetengwa baada ya kubainika kwa na watu kadhaa wenye maambukizi ya ugonjwa wa corona miongoni mwa wanajeshi wa Uingereza.

    Wanajeshi waliothibitishwa kuwa na corona wametengwa katika maeneo maalum kwenye kambi hiyo ya jeshi ya Nyati iliyopo mjini Nanyuki, huku wengine wakiwa kwenye mahema na pia hali zao za afya zikiwa zinafuatiliwa kila wakati, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa ubalozi wa Uingereza.

    Msemaji huyo amesema kuwa "wanajeshi wote wanaopelekwa nchini humo kwanza wanajitenga na pia wanapimwa kuhakikisha hawana maambukizi ya virusi vya corona kabla ya kusafiri kwenda nchini Kenya".

    "Maeneo yanayopita watu wengi ikiwemo ya kula chakula yanafanyiwa usafi wa kina na wakati huo huo wanajeshi wanatakiwa kula kwa zamu," taarifa hiyo imesema.

    Wafanyakazi wengi nchini Kenya katika kambi hiyo wametakiwa kufanyakazi wakiwa nyumbani.

    Kambi ya jeshi ya Nyati ilifunguliwa tena mwezi jana na Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace.

  5. Raia Afrika Kusini wakatishwa tamaa na kusitishwa kwa chanjo ya corona

    Raia wengi nchini Afrika Kusini wamepokea kwa mshutuko na kuonekana kukatishwa tamaa na taarifa za kuwa chanjo ya Oxford ya AstraZeneca haitakuwa na ufanisi mkubwa kama vile wataalamu walivyokuwa na matumaini nayo katika kukabiliana na virusi vipya vya corona nchini humo.

    Nchi hiyo imesitisha mpango wake wa kuwachanja watu chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa corona wakati ambao tayari taifa hilo lilikuwa imepokea mamilioni ya chanjo hiyo.

    Chanjo hiyo ilikuwa imepangiwa kuanza kutolewa wiki ijayo.

    Wakati huu ambapo maswali ni mengi kuliko majibu, ujumbe kutoka kwa maafisa wa afya ni kwamba bado kuna matumaini.

    Wanaamini kuwa chanjo hiyo bado itakuwa na ufanisi katika kuzuia mtu kuwa mgonjwa sana na kupunguza idadi ya watu ambao huenda wangelazwa hospitalini kupata matibabu.

    Suala hili ni muhimu katika nchi ambayo asilimia 80 ya idadi ya watu hawana uwezo wa kupata huduma za afya kutoka taasisi za kibinafsi na hivyo basi hutegemea sana hospitali za umma, ambazo sasa hivi zimejaa.

    Sasa je kuna mipango gani?

    Waziri wa afya nchini Afrika Kusini amesema watachukua jukumu la kiuongozi kwa wanasayansi wa eneo hilo juu ya namna ya kuboresha chanjo hiyo ili iweze kuwa na ufanisi zaidi.

    Kuna baadhi wanasema kuwa chanjo hiyo huenda ikawa na umuhimu mkubwa kwa wazee na kwa watu wenye magonjwa mengine makali yaliyoambatana.

    Kwa kuangazia wasiwasi wa wananchi, serikali na wanasayansi huenda wakalazimika kuchukua hatua zaidi na kuwahakikishia wananchi kwamba bado serikali ina mpango madhubuti – na maisha yatanusurika.

    Soma zaidi taarifa hii:

  6. Upinzani wakataa kumtambua Farmajo kama Rais wa Somalia

    Viongozi wa upinzani nchini Somalia wamesema kuwa hawamtambui tena Rais wa nchi hiyo baada ya siku ya ukomo ya uchaguzi kupita na muda wa kuwa madarakani wa Mohamed Abdullahi Farmajo kumalizika.

    Mazungumzo kati yao na serikali kuu ya jinsi ya kusonga mbele na uchaguzi huo yaligonga mwamba Ijumaa iliyopita.

    Wanasiasa wa upinzani wametoa wito wa kuundwa kwa jopo litakalosimamia mamlaka ya mpito.

    Kuna hofu kuwa mgogoro huo huenda ukasababisha kundi la wanamgambo la Al Shabab kuhangaisha raia.

    Mgogoro wa kisiasa na ukosefu wa utawala ni hatari zaidi kwa taifa la Somalia ambalo tayari lipo katika hali tete.

    Huku muda wa utawala wa Rais Framajo ukiwa umemaliza rasmi, viongozi wa upinzani wametoa wito kwa jeshi la taifa kuacha kuchukua maagizo kutoka kwake.

    Ikiwa mambo yangeenda kama ilivyokuwa imepangwa, wabunge wapya sasa hivi wangekuwa wanamchagua Rais mpya.

    Lakini kufanyika kwa zoezi hilo hadi siku ya mwisho iliyokuwa imewekwa haikuweza kufikiwa kwasababu wanasiasa walikuwa wanalUmbana.

    Jaribio lolote la kueongeza muda wa utawala wa Farmajo litapingwa vikali – kwasababu wakosoaji wake wanasema amekuwa akijaribu kuchelewesha mchakato wa uchaguzi akitaka kujihakikishia muda zaidi wa kuhudumu.

    Sasa hivi jumuiya ya kimataifa ndio itakayokuwa inasubiriwa - nchi za Marekani na Ulaya ambazo zilikuwa zikisaidia nchi hiyo katika masuala ya kiusalama na kifedha.

  7. Waliohusika na zabuni zinazohusu covid-19 Afrika Kusini kukiona

    Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema atachukua hatua ''kali'' na ''stahiki'' dhidi ya wazabuni wanaohusiana na virusi vya corona.

    Bw. Ramaphosa amesema mashirika ya serikali yameelekezwa kutolipa watoa huduma kusubiri matokeo ya uchunguzi au hatua ya mahakama.

    "Hawatafurahia faida yao iliyopatikana kwa namna ovu, kwani hatua zimechukuliwa kupata pesa zilizoibiwa, pamoja na kufungia akaunti za benki," alisema.

    Ripoti ilitolewa mwaka jana kuhusu matumizi ya fedha za kupambana na Covid-19, ilibaini gharama kubwa na udanganyifu.

    Vifaa vya kujikinga (PPE) zilinunuliwa kwa bei mara tano zaidi ya gharama ambayo hazina ya nchi hiyo imeelekeza

    Rais Ramaphosa amesema '' wamepata funzo kubwa'' kutoka kwa watu ambao ''wametumia mwanya wa uharaka iliyopo''.

    "Uzoefu wa taifa letu katika ununuzi wa vifaa na huduma muhimu wakati wa janga la kitaifa ni suala la aibu ambalo linapswa likomeshwe kwa nguvu,'' Alisema.

    • Morocco yatetea taji la CHAN baada ya kuichapa Mali 2-0

      Morocco inakuwa timu ya kwanza kufanikiwa kulitetea kombe la matifa ya Afrika kwa wachezaji ndani(CHAN) baada ya kuifunga Mali 2-0nchiniCameroon.

      Wamorocco walilazimika kuutafuta ushindi kwa nguvu katika mechi ya fainali iliyopigwa Jumapili nchini Cameroon.

      Magoli yote mawili yalifungwa katika kipindi cha pili kwa mikwaju ya kona mbele ya mashabiki takriban 6,700 waliokua wamefurika ndani ya uwanja wa Ahmadou Ahidjo mjini Yaounde.

      Bao la kwanza liliingizwa wavuni na Soufiane Bouftini na la pili lilifungwa na Ayoub El Kaabi, ambaye alifunga magoli tisa mwaka 2018 na kuisaidia Morocco kushinda taji katika ardhi ya nyumbani.

      Mali walikamilisha mchezo wakiwa na wachezaji 10 uwanjani baada ya kutolewa uwanjani kwa Issaka Samake baada ya kupata kadi ya pili ya manjano, wakati wa kipindi cha majeruhi.

    • Jamii ya Wayazid wa Iraq yawazika wenzao 104 waliouliwa na IS

      Jamii ya Wayazid kutoka Kaskazini mwa Iraq wameileta miili ya watu wao 104 waliouliwa na kikundi cha Islac State wakati wa utawala wa kigaidi mwaka 2014.

      Mabaki ya miili yao yametambuliwa na kufufuliwa kutoka kwenye makaburi ya pamoja na kuzikwa katika kijiji cha Kocho kilichopo karibu na Mlima Sinjar katika jimbo la Ninevah.

      Maelfu ya wanaume waliuawa na wanawake na watoto kutumikishwa kama watumwa na kubakwa wakati IS walipochukua eneo la Wayazid.

      Umoja wa Mataifa unasema kuwa IS walitekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Yazid.

      Wayazid ni wafuasi wa wa dini yenye mchanganyiko wa imani ya kale ya dini ya Wairan, dini ya Kibudha, Ukristo, na Uislamu.

      Wanachukuliwa na IS- ambalo ni kundi la jihadi la Sunni kama wafuasi wa dini ya uzushi.

      Iliaminiwa kuwa walikuwepo Wayazidi wapatao 550,000 waliokua wakiishi Iraq kabla ya kuvamiwa na IS tarehe 3 Agosti, 2014. Wayazidi wapatao360,000 Yazidis walitoroka na kupata hifadhi katika maeneo mengine.

    • Rwandair yasitisha safari zake za Afrika Kusini

      Kampuni ya ndege ya Rwanda, Rwandair imesitisha kwa muda safari zake katika mataifa ya Afrika Kusini, Zimbabwe na Zambia.

      Kampuni hiyo imesema imechukua uamuzi huo kutokana na aina mpya ya Covid-19 inayoripotiwa katika mataifa ya kusini mwa Afrika.

      Safari zote za kutoka na kuelekea katika miji ya Johannesburg, Cape Town, Lusaka na Harare zimesitishwa mara moja kuanzia Jumatatu.

      Kampuni hiyo ya ndege imewatolea wito wateja wake waombe kurudishiwa fedha na kupanga upya safari zao.

      Taarifa kamili ya kuahirishwa kwa safari za Rwandair ilitumwa kwenye mtandao wa kijamii wa twitter:

    • Mganga Mkuu asimamishwa kazi kwa kutoa 'taarifa zisizo za kweli'

      Waziri wa Afya nchini Tanzania, Dkt Doroth Gwajima ameamuru kusimamishwa kazi kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Dkt Felista Kisandu kwa kutoa taarifa kuhusu kuwepo kwa ugonjwa wa ajabu katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya na kusababisha ''taharuki isiyo ya lazima''

      Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Dkt Kisandu hakuchukuahatua za kujiridhisha na taarifa hizo kwa utaratibu wa miongozo ya kitaalamu na badala yake aliendelea na ajenda hiyo bila ushahidi wa kitaalamu na kusababisha taharuki bila sababu ndani ya jamii.

      Timu ya uchunguzi imejiridhisha kuwa hata kama kungekuwa na mlipuko wa aina yoyote ile ni dhahiri kuwa Dkt Kisandu alikiuka muongozo wa utoaji taarifa za milipuko kama iliyoelezwa katika sheria ya Afyakuwa mwenye dhamana hiyo ni Waziri wa Afya baada ya kujiridhisha na si vinginevyo.

      ''Kwa upande mwingine, taarifa na takwimu ambazo zilizotolewa na Diwani wa katia ya Ifumbo hazikuwahi kuripotiwa popote kwenye mifumo rasmi ya afya hivyo hoja hiyo bado inahitaji utafiti'' Iliieleza taarifa ya Wizara ya Afya kwa Umma.

      Waziri wa Afya nchini humo, Dkt Dorothy Gwajimaameagiza kusimamishwa kazi kwa Dkt Felista ili kupisha uchunguzi chini ya Baraza la madaktari na kuagiza kupatiwa taarifa ndani ya siku kumi.

      Katika hatua nyingine, Waziri Gwajima amesema kuwa Televisheni ya ITV nayo haikuchukua hatua stahiki ya kujiridhisha kuhusu taarifa hiyo kabla ya kutangaza, hivyo Wizara yake itachukua hatua ya kupeleka malalamiko au mashtaka kwenye Wizara ya Mawasiliano katika vyombo husikavinavyoshughulika na maadili ya upashaji habari.

      Wizara ya Afya ilikana taarifa zilizosambaa za kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa usiofahamika nakuua watu 15 kwa mara moja, Wizara imesema kuwa ni wagonjwa watatu tu waliripoti katika Zahanatiambao uchunguzi wa kitabibu ulibaini kuwa walikuwa na matatizo ya ini na vidonda vya tumbo, ambapo mmoja alifariki akipatiwa matibabu , mwingine alipona na mwingine anaendelea na matibabu.

    • Mtu mmoja agundulika na ugonjwa wa Ebola

      Mtu mmoja amegundulika kuwa na virusi vya Ebola Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Wizara ya Afya nchini humo imeeleza.

      Mwanamke mmoja kutoka mji wa Biena karibu na mji wa Butembo amepoteza maisha kutokana na Ugonjwa huo.

      Mamlaka zimesema zinapeleka timu ya wataalamu katika eneo hilo.

      Huu ni mlipuko wa 12 wa Ebola nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia

      Ya awali ilitokea karibu miezi mitatu iliyopita Magharibi mwa DRC.

      Ebola ni nini?

      ◾Ebola ni ugonjwa unaoambukizwa na virusi ambapo aliyepata maambukizi hupata dalili za homa, uchovu, maumivu ya viungo na koo.

      ◾Kisha mgonjwa hutapika, kuharisha na kutoka damu.

      ◾Watu huambukizwa kwa njia ya kugusana, njia ya mdomo na pua, pia kwa njia ya damu, matapishi, kinyesi,majimaji ya kwenye mwili wa mtu mwenye Ebola

      ◾Wagonjwa hupoteza maisha kutokana na kupungukia maji mwilini na viungo kushindwa kufanya kazi.

    • Tunatumai hujambo... Karibu kwa matangazo yetu mubashara ya leo Jumatatu tarehe 08.02.2020