Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo ajiuzulu

Sylvestre Ilunga Ilunkamba amejiuzulu rasmi kama waziri mkuu wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na kuwasilisha barua yake kwa Rais Félix Tshisekedi.

Moja kwa moja

Lizzy Masinga, Abdalla Seif Dzungu and Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo, tukutane tena Jumatatu.

  2. Waziri mkuu wa DRC ajiuzulu

    Sylvestre Ilunga Ilunkamba amejiuzulu rasmi kama waziri mkuu wa Jamuhuri ya kisemokrasi ya Congo, na kuwasilisha barua yake kwa Rais Félix Tshisekedi.

    Bw Ilunga, ambaye ni mshirika mkuu wa mtangulizi wa Rais Tshisekedi, Joseph Kabila, ameongoza baraza la mawaziri la serikali ya Muungano kwa miezi 15.

    Hatahivyo wabunge walipitisha kura ya kutokuwa na Imani na serikali yakeJumatano wiki hii na akapewa saa 24 awe amejiuzulu.

    Kujiuzulu kwake kunatoa fursa kwa Rais Tshisekedi ya kuwateua washirika wake kama mawaziri.

    Hadi sasa, utendaji wa Bw Tshisekedi umekuwa ukidhibitiwa na, muungano alionao na Bw Kabila ambao uliafikiwa wakati alipoingia madarakani miaka miwili iliyopita.

    Ushindi wake katika uchaguzi mwezi Disemba 2018 ulisifiwa kama wa kihistoria-ambapo kulikuwa na makabidhiano ya kwanza ya utawala kwa njia ya amani ambayo hayakuwahi kushuhudiwa katika historia ya miongo sita nchini humo.

    Bw Tshisekedi bado hajamchagua waziri mkuu mpya,ambaye ataunda serikali ijayo.

  3. Biden aidhinisha mfumo mpya wa bima ya afya nchini Marekani

    Rais Biden amesaini sheria ya rais inayowawezesha tena Wamarekani kupata bima ya matibabu hususan Wamarekani ambao hawana uwezo wa kupata fursa hii kupitia sehemu zao za kazi.

    Biden amesema ni muhimu kwa kila Mmarekani kupata huduma ya afya wakati huu wanapokabiliana na virusi vya corona.

    Sheria hiyo pia imeondoa marufuku dhidi ya ufadhili wa mashirika yanayotoa msaada wa utoaji mimba au kutoa ushauri kwa wale wanaotaka kutoa mimba.

    Rais Biden ameahidi kutekeleza mpango wa afya wa Obama ili kuboresha bima ya matibabu.

  4. Wasichana wengine wa Chibok wafanikiwa kutoroka mikononi mwa Boko Haram

    Taarifa kutoka Nigeria zinasema kwamba wasichana zaidi waliokuwa wametekwa nyara kutoka shule ya wasichana Chibok mwaka 2014 wametoroka kutoka kwa wanamgambo wa Boko Haram.

    Baba wa mmoja wa wanafunzi wa zamani wa Chibok ameiambia BBC kuwa alizungumza na binti yake ambaye amenusurika.

    Amesema walizungumza nae kwa njia ya simu baada ya kufanikiwa kutoroka na alikuwa analia.

    Yeye na wasichana wengine waliotekwa nyara katika shule ya wasichana ya Chibok na maeneo mengine wameripotiwa kutoroka kutokana na operesheni za kijeshi dhidi za jeshi la Nigeria dhidi ya Boko Haram.

  5. Wanandoa wakamatwa Zimbabwe kwa kutuma 'ujumbe wa WhatsApp'

    Mwanaume mmoja na mke wake nchini Zimbabwe wamekamatwa kwa madai ya kutuma ujumbe wa WhatsApp ambao ulidai kwamba Rais Emmerson Mnangagwa amefariki kutokana na Covid-19, kwa mujibu wa gazeti la serikali la Herald.

    Wawili hao wote wakiwa na umri wa miaka 20 kila mmoja, walikamatwa katika mji wa mpaka wa kusini mwa Zimbabwe, Beitbridge lilisema.

    Wameripotiwa kufika mbele ya hakimu mkazi ambako walishitakiwa kwa kuchapisha au kuwasilisha taarifa ya uongo kuhusu taifa.

    Haijajulikana iwapo walikiri mashitaka au la.

    Serikali inasema Rais Mnangagwa yuko katika likizo yake ya mwaka ya wiki tatu, atarejea kazini mwisho wa mwezi.

    Hakuhudhuria mazishi ya mawaziri wake wawili waliokufa baada ya kuugua virusi vya corona.

  6. Walimu Kenya wataka kupatiwa bunduki ili kujilinda dhidi ya wahalifu

    Chama cha walimu nchini Kenya (KUPPET) kinaitaka serikali kutoa mafunzo ya usalama kwa walimu na kuwapa silaha wale wanaopelekwa kufundisha kwenye maeneo yaliyo ya hatari.

    Kaimu Katibu Mkuu wa KUPPET Moses Nthurima amesema kuwapa walimu silaha si kuwa tu kutawaogopesha watu wanaowashambulia lakini pia kutawapa walimu hali ya kujiamini kufanya kazi katika mazingira ya hatari.

    “Tunarudia ombi hilikwamba katika hali ya ukosefu wa usalama, lazima walimu wafundishwe na kupatiwa bunduki.''

    ''Huwezi kumkabili mtu mwenye bunduki kwa kutumia chaki. Tunapompeleka mwalimu katika maeneo ambayo usalama ni mbovu mwalimu ataishi kwa hofu kila wakati. Lakini ikiwa bunduki inaning'inia mgongoni hata majambazi watajua kuwa mwalimu ni eneo lisilofaa na watachukua sekunde kufikiri kabla ya kufanya makosa, "Alisema Bw. Nthurima.

    Ombi hilo limekuja baada ya kutokea matukio ya kuuawa kwa walimu na watu wenye silaha katika maeneo ya Kaskazini-Mashariki na Pwani ya Kenya.

  7. Dkt Abbas:Tanzania inazingatia tahadhari dhidi ya corona,

    Msemaji mkuu wa serikali nchini Tanzania Dkt. Hassan Abbas amesema Tanzania inazingatia miongozo yote ya tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona na hata wakati huu ambao dunia inapambana na wimbi la pili la maambukizi ya virusi hivyo.

    Akihojiwa na kitoa cha redio cha EFM kilichopo jijini Dar es salam, Dkt. Abbas amesema “Sisi Tanzania msimamo wetu ni ule ule,tunafahamu tatizo lipo duniani na dunia inahangaika lakini cha kwanza watanzania waondoe hofu wizara ya afya ilishatoa miongozo, ile miongozo bado ipo haijawahi kufutwa kuna tahadhari za kuchukua hivi wewe kunawa mikono mpaka covid? Alihoji Dkt Abbas.

    ‘’ Tulikuwa tuna nawa sana shule baadaye tukaacha kwahiyo kuna zile tahadhari kama alivyosema juzi Mh Rais tuendelee kuzichukua lakini Tanzania tunaamini tumedhibiti haya maambukizi kwa njia zetu za kisayansi na kumshukuru Mwenyezi Mungu’’.

    ‘’Unajua Tanzania watu wanasahau wanafikiri tulidharau sana huu ugonjwa tulichukua hatua zote dunia ilizokuwa inataka isipokuwa kujifungia ndani maana kuna watu wanatamani sana kufungiwa ndani sijui kuna nini huko ndani” Alisema Bw. Abbas.

    Kauli hii inakuja siku moja baada ya shirika la Afya duniani WHO kupitia ofisi yao ya kanda ya Afrika kutoa taarifa ikizitaka mamlaka nchini kujiandaa kupokea chanjo ya corona kama mataifa mengine yanavyofanya na kuikumbusha Tanzania hayo ni sehemu ya makubaliano ya kanuni za afya za kimataifa ambapo nchi wanachama wamekubali kwa pamoja kuzuia kusambaa kwa magonjwa.

    Rais Magufuli ameweka wazi chanjo hazifai na kuwataka watanzania kusimama imara na kuwa waangalifu na mambo ya kuletewa huku akiendelea kusisitiza msimamo wake wakutojifungia ndani na kutaka watu kuchukua tahadhari ikiwemo kujifukiza na kumuomba Mungu.

    Mapema mwanzoni mwa juma Kanisa Katoliki nchini humo kupitia baraza la maaskofu lilitoa ujumbe wa tahadhari kwa waumini wake na kukusitiza ni muhimu kuendelea kuchukua tahadhari kwani wao kama kanisa wameona iko haja ya kufanya hivyo.

  8. Wasaidizi wa rais wa Tunisia waugua baada ya kufungua ‘kifurushi chenye sumu’

    Wasaidizi wawili wa rais wa Tunisia wanaugua baada ya kufungua kifurushi kilichofikishwa katika ofisi yao kilichoshukiwa kuwa na sumu , taarifa ya ofisi ya rais imeeleza.

    Katika taarifa Mkurugenzi wa ofisi ya rais alikifungua na hakukuta barua yoyote iliyoandikwa ndani ya kifurushi hicho. Hatahivyo baada ya kukifungua ‘’afya yake ilianza kuwa mbaya, na alijihisi kama alikuwa anazimia, alikuwa pia na maumivu makali ya kichwa.

    Mfanyakazi mwingine alikuwepo wakati wa tukio, taarifa imeeleza, akapata dalili kama hizo ‘’lakini hali haikuwa mbaya zaidi’’.

    Bahasha ilichanwa kablaya kufikishwa kwenye Wizara ya mambo ya ndani, taarifa iliongeza.

    Haijulikani ndani ya bahasha hiyo ilikuwa na nini kilichosababisha athari kwa maafisa hao.

    Taarifa hiyo imesema vipimo vimechukuliwa na kupelekwa kwenye hospitali ya kijeshi ili kubaini sababu za maafisa kuonesha dalili hizo.

  9. Uganda yaongoza kwa rushwa, Tanzania, Kenya ,Rwanda zang’ara

    Nchi ya Uganda imetajwa kuongoza Afrika Mashariki kwa vitendo vya rushwa, kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la kimataifa la Transparency.

    Ripoti hiyo ya mwaka 2020 inayotolewa kila mwaka iliyohusisha mataifa 180 na iliyolenga zaidi ufisadi kwenye janga la Covid 19, inaonesha nchi za Tanzania, Kenya na Rwanda kufanya vizuri kwenye kudhibiti rushwa na ufisadi katika sekta hiyo ya afya.

    Mwaka 2020 ilishika nafasi ya 142 kati ya mataifa 180, tofauti na mwaka 2019 ambapo ilishika nafasi ya 137 kati ya mataifa 180.

    Mkurugenzi wa shirika la Transaprency International nchiniUganda, Peter Wandera amesema

    ‘’Ripoti hii ni ya kimataifa ya masuala ya ufisadi inayotolewa na mataifa mbalimbali duniani kwa wakati mmoja kulingana na viwango vya ufisadi kila taifa na ripoti hii imezinduliwa jana, imezinduliwa kwa wakati mmoja katika mataifa husika’’.

    Mwaka 2020 shirika hilo kote duniani liliangazia janga la Covid-19, kutokana na ripoti hiyo mataifa 180 yalifanyiwa utafiti,na mengi yameshindwa kuonesha matumizi ya fedha walizopewa kwa ajili ya vita dhidi ya virusi vya corona.

    ‘’Mwaka 2020 janga la corona limesababisha ufisadi Zaidi, katika ripoti hiyo inaonesha kwamba, mataifa mengi yaliyotajwa kupanda kwa vitendo vya ufisadi imetokana na kushindwa kusimamia rasilimali za kupambana na Covid-19.’’

    ‘’Sasa licha ya Uganda kuonesha jitihada katika mapambano ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona, kuna tuhuma za ufisadi zinazotokana na kushindwa kuonesha matumizi halisi ya rasilimali.’’Aliongeza Bw.Wandera.

    Ripoti hiyo inaoneshamwaka 2020 robo tatu ya mataifa yaliyoshiriki yalipata alama chini ya 50

    Hii inamaanisha kuwa ufisadi si katika sekta ya afya pekee, bali hata katika demokrasia ikiwa mataifa jirani na Uganda kama vile Rwanda, Tanzania na Kenya yamefanya vyema ikilinganishwa na Uganda, Rwanda ikishika nafasi ya 49, Tanzania 94, Kenya nafasi ya 124

    Mamlaka nchini Uganda hazijatoa tamko lolote mpaka sasa kuhusu ripoti hiyo.

  10. Zuma aamriwa kufika mbele ya jopo la wachunguzi

    Mahakama ya kikatiba ya Afrika Kusini imesema kuwa rais wa zamani Jacob Zuma ni lazima afike mbele ya jopo linalochunguza madai ya vitendo vya rushwa vilivyotokea wakati wa utawala wake.

    Mahakama iliamua kuwa kuwa hakuwa na haki kukaa kimya mbele ya tume.

    Bwana Zuma anashutumiwa kupora mali za taifa hilo wakati alipokuwa rais.

    Zuma amekana madai hayo dhidi yake.

    Matokeo ya jopo hilo hayatawaongoza moja kwa moja kwenye mashtaka lakini yanaweza kupelekwa kwa waendesha mashtaka.

  11. Habari! karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya taarifa zetu