Polisi ya Uganda yawakamata makumi ya watu katika uteuzi wa urais
Karibu watu 50 wamekamatwa nchini Uganda kufuatia sarakasi zilizoshuhudiwa katika mji mkuu wa Kampala baada ya mwanasiasa wa Bobi Wine kuidhinishwa kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwezi Januari mwaka 2021.
Baada ya makabiliano ya saa kadhaa, Bobi Wine,ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, alilazimishwa kuingia katika gari la polisi punde baada ya uteuzi wake wa urais kuidhinishwa na kupelekwa nyumbani kwake.
Lakini alipofika nyumbani alikataa kushuka kutoka kwa gari la polisi, akisistiza kuwa anataka kwenda katika makao makuu ya chama kuzidua ilani yake .
Akizungumza na wafuasi wake nyumbani kwake ,Bw. Kyagulanyi alisema polisi waliwapulizia maji ya pili pili machoni yyeye na viongozi wenzake.
Maafisha watatu wa polisi walijeruhiwa katika pata shika hiyo.
Kuanzia mapema asubuhi ya Jumanne, polisi waliojihami walipelekwa katika barabra ambazo Bw. Kyagulanyi alitarajiwa kupitia kuelekea kituo cha uteuzi.
Wagombea uraisi wanatakiwa kuandamana wajumbe wachache, kama sehemu ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.
Lakini baadhi yao walifanya maandamano yaliyovutia mikusanyiko ya watu.
Wafuasi wa Bw. Kyagulanyi walitawanywa kwa kutumia vitoa machozi.
Wagombea 11 wanawania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa Uganda miongoni mwao Yoweri Museveni na majenerali wake wawili wa zamani waliokuwa naye vitani kabla ya aingie madarakani.
Tume ya uchaguzi ya Uganda imepiga marufuku mikutano ya kampeni,na wagombea wanatakiwa kufanya kampeni zao kupitia vyombo vya habaro au mitandao ya kijamii.