Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

'Membe alishiriki vikao vya ndani kumuunga mkono Lissu'

Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo anayewania tiketi ya urais Zanzibar Seif Sharif Hamad asikitishwa na majibu ya Bernad Membe kuwa ataendelea na kampeni za kuwania nafasi ya urais.

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Na huo ndio mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa hii leo. Shukran kwa kuwa nasi.

  2. Aliyekuwa rais wa Burundi amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani

    Mahakama ya juu zaidi ya Burundi imemhukumu kifungo cha maisha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Pierre Buyoya kwa jukumu lake alilotekeleza kwenye mauaji ya mrithi wake Melchior Ndadaye.

    Pierre Buyoya, 70, mjumbe wa Umoja wa Afrika eneo la Sahel, hajakuwa akihudhudria vikao vya kesi yake ambayo mwaka jana aliielezea kama yenye kuchochewa kisiasa.

    Nakala ya hukumu iliyotolewa na kuonekana na BBC, imeonesha kuwa watu wengine 15 pia wamehukumiwa kifungo cha maisha – wengi wao wakiwa maafisa waandamizi wa jeshi – huku Bernard Busokoza – aliyekuwa makamu rais wa Burundi akihukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani.

    Mwaka 2018, serikali ya Burundi ilitoa kibali cha kukamatwa kimataifa dhidi ya Bwana Buyoya aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo kati ya mwaka (1987 – 1993 na 1996 - 2003), kwa mauaji ya Bwana Ndadaye yaliyotokea mwaka 1993.

    Kila mwaka Oktoba 21, Burundi huadhimisha mauaji ya Bwana Ndadaye, rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, ambaye ni shujaa wa taifa hilo.

  3. 50 Cent: 'Mpigieni kura Trump' badala ya Biden

    Mwamuziki 50 Cent amewasihi wafuasi wake milioni 26 kwenye mtandao wa Instagram wampigie kura Trump badala ya Biden.

    50 Cent ameandika ujumbe huu "(Mpigieni kura Trump)," ambao umesomwa zaidi ya mara 300,000.

    Malalamishi yake ni kwamba kuongezwa kwa kiwango cha kodi chini ya mpango wa kodi wa Joe Biden matokeo yake atakatwa zaidi akilinganisha na mpango wa Trump.

    Joe Biden ameahidi kuweka kodi ya juu kwa wenye mapato zaidi ya dola 400,000 (£308,000) kwa mwaka – kunakoathiri takriban asilimia 98.5 ya idadi ya watu Marekani.

    Chukulia kwamba mapato ya 50 ni kati ya wenye malipo ya juu zaidi, bila shaka ataingia kwenye kundi la wenye kulipa kodi ya juu chini ya utawala wa Biden.

    Wakfu wa kodi ulitoa ripoti yenye kuonesha athari ya mpango wa Biden kwa wanaopata mapato ya juu na kunakiliwa na shirika la habari la CNBC.

  4. Maalim Seif: Membe alishiriki vikao vya ndani kumuunga mkono Lissu

    Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo anayewania tiketi ya urais Zanzibar Seif Sharif Hamad amesema amesikitishwa sana na majibu ya Bernad Membe kuwa ataendelea na kampeni za kuwania nafasi ya urais.

    Maalim Seif amesema hilo limemshangaza sana kwani wakati tangu anajiunga cha ACT Wazalenzo walimwambia nia yao ya kushirikiana na vyama vingine.

    Maalim amesema kampeni zao zilikuwa zinasuasua hata kupata wadhamini hivyo wakakaa kikao wakati Membe akiwepo na kushauriana kuwa mgombea wetu haonekani, hivyo tumuunge mkono Lissu.

    ‘’Kamati ya uongozi pamoja na Membe mwenyewe tulikubaliana kuwa tunamuunga mkono Lissu. Hivyo ni jambo la kushangaza kumuona tena Membe akikanusha makubaliano hayo. ’’

    “Msimamo wa ACT wazalendo ni kumuunga mkono Tundu Lissu.’’ Alisema Maalim Seif

    ‘’Mimi kama mwenyekiti wa Chama ninafahamu hivyo na kiukweli upande wa upinzani mgombea anayeonekana anaweza kumshinda Magufuli ni Lissu”.

    Maalim aliongeza kusema kuwa uamuzi huo si wake binafsi au msimamo wa Zitto bali ni wa chama.

    Aidha ACT Wazalendo haimkatazi Membe kufanya kampeni kama alivyosema.

    ‘’Msimamo wetu kama chama ni kumuunga mkono mgombea mwenye nguvu ambaye ni Lissu huyu Membe hatujui ana nia gani?”

    Hata hivyo Maalim alisema uamuzi wao hauna tofauti na wanasiasa wengine wa upinzani ambao walisema wanamuunga mkono Magufuli, ila ameshangaa kipindi wanasiasa hao walipotangaza Tume ilikaa kimya.

    Hata hivyo mgombea urais wa chama cha upinzani nchini Tanzania cha ACT- Wazalendo Bernard Membe hapo jana alijitokeza na kusisitiza kuwa yeye yungali kwenye mbio za kuwania urais wa nchi hiyo.

    Membe alijitokeza baada ya ukimya wa takribani majuma mawili ambapo viongozi wakuu wa chama chake Zitto Kabwe na Maalim Seif Sharif Hamad wamekuwa wakimnadi mgombea wa Chadema, Tundu Lissu katika tiketi ya urais dhidi ya mgombea wa chama tawala CCM rais John Magufuli.

    Sikiliza alichosema Bernard Membe:

  5. Wapiganaji wa Jihad wanadhani uchaguzi wa Marekani utaongeza machafuko

    Utawala wa Trump ulisaidia kuondoa kundi la Islamic State katika ngome yao ya mwisho walikokuwa wanadhibiti huko Syria na kusababisha mauaji ya msemaji na kiongozi wa kundi hilo mwaka 2019 pamoja na mauajiya kiongozi wa al-Qaeda nchini Yemen mwaka huu.

    Hata hivyo mpango wa Marekani wa kupunguza kuhijuhusisha na migogoro ya nje ya nchi huenda pia kulifaidi makundi ya jihadi. Kundi la Taliban lilipata hakikisho la Marekani kuondoa vikosi vyake ilipokubali kutia saini makubaliano ya amani.

    Hatua hii imetia moyo makundi mingine ya Jihadi nchini Syria na Afrika kutafuta kufikia makubaliano sawa na hayo.

    Lakini hadi kufikia sasa makundi ya Jihadi yamesema machache mno kuhusu uchaguzi ujao wa Marekani.

    Wanaimani kwamba uchaguzi huo utaendelea kutenganisha siasa za Marekani na jamii zingine. Itakuwa fursa muhimu kwao kujinufaisha na kukengeusha fikira kwa vita dhidi yao.

  6. 'Wapinzani tuliporwa haki yetu bungeni',

    Bunge lililovunjwa hivi karibuni Tanzania *Bunge la 11* licha ya kuwa limejipambanua kama chombo chenye mafanikio makubwa kwa kutunga sheria nyingi na muhimu lakini wabunge wa upinzani wanahisi sheria nyingi zinapitishwa kutokana na wingi wa wabunge wa chama tawala licha ya kuwa wapinzani wanaziona hazifai.

    Bunge ni muhimili wa pili wa serikali, wenye majukumu muhimu kwa nchi kupitisha bajeti, kurekebisha na kutunga sheria zitakazotumika Tanzania.

    Bunge hilo lilikuwa na wabunge 393, wabunge wa CCM wakiwa 288 na wale wa upinzani 105..

    Kwa mujibu wa marekebisho hayo ya sheria mbali na Rais, sasa hata Makamu wa Rais, Jaji Mkuu, Spika na Naibu hawatashtakiwa kwa kuvunja sheria wakiwa madarakani kwa makosa walioyafanya wakiwa kwenye majukumu yao.

    Sasa atakayeshtakiwa kwa niaba ya viongozi wote hao ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

    Kupitishwa kwa sheria hiyo , kulizua mvutano huku kambi rasmi ya upinzani na wana harakati wakipendekeza mabadiliko hayo yafutwe.

    Miongoni mwa wabunge wa upinzani waliopaza sauti katika bunge hilo la kumi na moja ni Zitto Kabwe na Halima Mdee.

    ‘’Kwangu mimi niliona kwamba lile bunge kama sio chombo ambacho kinaangalia mahitaji ya wawakilishi ila limekuwa ni bunge ambalo limekuwa likibariki kile kinacholetwa na serikali na hilo limekuwa changamoto,’’ Halima Mdee aeleza.

    Na kwa upande wake Zitto anasema;

    ‘’..Katika demokrasia inatakiwa wengi wape wachache wasikilizwe. Bahati mbaya hata haki yetu ya kusikilizwa sisi wapinzani tuliporwa kwa maana kwamba tukizungumza tunasimamishwa, tunacheleweshwa au tunaambiwa tufute kauli’’.

    Lakini kwa upande wake Ali Kessy mbunge kutoka chama tawala CCM, anakanusha madai hayo.

    Miongoni mwa masuala ambayo yalizua mjadala ndani ya bunge hilo ni pamoja na kuzuia kurushwa kwa matangazo ya moja kwa moja na kukataa kufanya kazi na aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

    Kwa upande wake Spika anayemaliza muda wake Job Ndugai anatetea kuwa wamefanya kazi nzuri na bunge hilo limetekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, na ana hoja tofauti juu ya suala la kupora wapinzani haki yao ya kusikilizwa.

    Iwapo imani ya bunge hilo itaongezeka au la, hilo litategemea aina ya wabunge watakaopata ridhaa ya wananchi katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea huku wapiga kura wakiwa na matumaini ya maslahi yao kupiganiwa.

  7. Raia wa kigeni wakamatwa wakiingiza dawa za kulevya Ethiopia

    Polisi nchini Ethiopia wamewakamata washukiwa 14 kwa kujaribu kuingiza dawa za kulenya aina ya kokeini kupitia uwanja mkubwa wa ndege mjini Addis Ababa.

    Polisi nchini humo wamesema washukiwa 13 raia wa Nigeria na mmoja wa Brazil wamepatikana na kilo 14 za dawa za kulevya aina ya kokeini katika mabegi yao, nguo za ndani na baadhi zilikuwa wamezimeza.

    Washukiwa hao walikuwa wamewasili Sao Paulo, Brazil, Jumatatu.

    Walikamatwa na kuzuiliwa uwanja wa ndege, kwa mujibu wa kamanda anayeshughulikia oparesheni ya dawa za kulevya Mengisteab Beyene.

    Polisi waliongeza kusema kuwa Ethiopia imenasa kilo 39 za dawa za kulevya aina ya kokeini na kilo 36 za bangi kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

  8. Sasa unaweza kupiga kura Tanzania kwa kutumia vitambulisho hivi

    Tume ya uchaguzi nchini Tanzania imeruhusu vitambulisho mbadala kutumika kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28.

    Vitambulisho mbadala ambavyo mpiga kura ataruhusiwa kutumia ni kitambulisho cha taifa kinachotolewa na NIDA, hati ya kusafiria na leseni ya udereva.

    Hata hivyo tume hiyo imesema ni lazima majina ya mpiga kura kwenye vitambulisho hivyo yafanane na majina yaliomo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura katika kituo cha husika cha kupiga kura.

  9. Kiongozi wa upinzani Guinea ajitangaza mshindi kabla ya matokeo

    Kiongozi wa upinzani nchini Guinea, Cellou Dalein Diallo, amejitangaza mshindi katika uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili kabla ya kutangazwa kwa matokeo rasmi.

    Bwana Diallo aliwaambia wanahabari na wafuasi wake kwamba ameshinda duru ya kwanza ya uchaguzi.

    Hakutoa takwimu zozote lakini amesema kuwa hitimisho lake ni kutokana na hesabu ya chama chake wala sio tume rasmi ya uchaguzi.

    Tume ya uchaguzi imejibu kwa kusema shughuli ya kuhesabu kura bado inaendelea na hiyo ndio pekee yenye mamlaka ya kumtangaza mshindi.

    Wafuasi wa Bwana Diallo ambao walikuwa wamekusanyika kusherehekea walitawanywa na maafisa wa polisi. Baadae aliandika ujumbe kwenye Twitter kwamba watu watatu wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa na polisi.

    Raia wa Guinea wamekuwa wakiandamana kwa miezi kadhaa sasa tangu Rais Alpha Condé alipotangaza kuwania muhula wa tatu.

    Matokeo ya uchaguzi huo uliotanda wasiwasi yanatarajiwa kutolewa Jumatano na baada ya hapo wagombea watakuwa na siku nane za kukata rufaa ikiwa wana malalamiko yoyote.

    Mgombea wa urais anahitaji zaidi ya asilimia 50 ya kura kupata ushindi wa moja kwa moja au kutakuwa na duru ya pili ya uchaguzi Novemba 24.

  10. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja leo ikiwa ni tarehe 20.10.2020.