Wanahabari mjini Banjul wanaripoti kuwa marais wa Mauritania na Guinea watamwambia Yahya Jammeh kwamba lazima aondoke nao kwa ndege watakayokuwa wanatumia, la sivyo aondolewa kwa nguvu.
Mwenyekiti wa tume ya Ecowas Marcel de Souza, amesema majeshi ya muungano huo yataingilia kati “asipokubali kuondoka Gambia”.
Jammeh ameahidiwa hifadhi Nigeria na Morocco.
Mke wa Jammeh, Zineb alizaliwa nchini Morocco – babake ni mzaliwa wa Guinea na mamake raia wa Morocco.
Jammeh anadaiwa kuwa bado ikulu na mkewe na mwana wao wa kiume.
Haijabainika hatima ya Jammeh itakuwa gani iwapo atakamatwa na wanajeshi wan chi jirani.
Wiki iliyopita, Barrow aliambia BBC kwamba hakuna haja ya Jammeh kutafuta hifadhi nje ya nchi.
„Twamtaka Jammeh awe Gambia, sidhani anahitaji kwenda nchi nyingine,” alisema.
Alhamisi, msemaji wa Barrow, Halifa Sallah, alisema Jammeh hafai kushtakiwa kwa makosa aliyotekeleza tangu achukue madaraka kupitia mapinduzi yasiyokuwa na umwagikaji wa damu mwaka 1994.
Bw Sallah alisema pia kuwa Jammeh atajivunia hadhi inayopewa viongozi wa zamani.