Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Helikopta iliyombeba rais wa Iran 'yatua kwa shida' - Runinga ya serikali

Helikopta iliyombeba rais wa Iran imehusika katika ajali, vyombo vya habari vya serikali vinaripoti.

Muhtasari

  • Waziri wa baraza la vita la Israel kujiuzulu ikiwa hakuna mpango wa baada ya vita kwa Gaza
  • Jeshi la DRC latangaza kuzuia jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais Felix Tshisekedi
  • Jeshi la Uganda lamkamata kamanda wa kundi la waasi wa ADF
  • Chama cha wanasheria Kernya chapinga mpango wa maafisa wa polisi kupelekwa Haiti
  • Zuma apima umaarufu wake wa kisiasa katika kitongoji cha Soweto
  • Helikopta iliomo katika msafara wa rais wa Iran 'yahusika katika ajali - Runinga ya serikali
  • .Ajali ya ndege iliombeba rais wa Iran: Tunachojua kufikia sasa
  • Waokoaji bado hawajawasiliana na msafara wa helikopta
  • Raisi alihudhuria ufunguzi wa mabwawa kabla ya ajali ya helikopta
  • Ajali ya ndege Iran: Tazama video ya waokoaji wakielekea katika eneo la ajali
  • .Itachukua muda kupata eneo la helikopta - waziri wa mambo ya ndani nchini Iran
  • Rais wa Azerbaijan atatizwa na ajali ya ndege iliyombeba rais wa Iran
  • Diddy aomba msamaha kwa tabia yake 'isiyo na sababu'
  • Man City washinda taji la nne la ligi ya England huku Foden akifunga mara mbili

Moja kwa moja

  1. Habari za hivi punde, Raisi wa Iran alionekana karibu na helikopta hii kabla ya ripoti ya ajali

    Rais wa Irani Ebrahim Raisi alikuwa Azerbaijan mapema leo, kabla ya kuripotiwa ajali ya helikopta.

    Shirika la habari la MEHR linasema picha hiyo inamuonyesha Raisi kabla ya kupanda helikopta, lakini haijulikani ikiwa ni kabla au baada ya kutembelea mabwawa mawili kwenye mpaka wa Iran na Azerbaijan.

  2. Man City washinda taji la nne la ligi ya England huku Foden akifunga mara mbili

    Manchester City iliifunga West Ham mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Etihad na kuwa timu ya kwanza kushinda taji la ligi ya Uingereza misimu minne mfululizo.

    Huku City wakihitaji ushindi ili kuwa na uhakika wa kuwazuia Arsenal, ambao walianza siku ya mwisho wakiwa nyuma kwa pointi mbili lakini wakiwa na tofauti nzuri ya mabao, Phil Foden aliweka kikosi cha Pep Guardiola mbele baada ya dakika mbili pekee.

    Nyota huyo wa Uingereza aliongeza jingine kabla ya mapumziko na ingawa Mohammed Kudus alirudisha goli moja, kiungo Rodri alirejesha tofautiya mabao mawili kwa wenyeji kupitia shuti kali kutoka kwenye eneo la hatari baada ya dakika 59.

    City walinusurika hofu ya dakika za lala salama wakati West Ham ilipopata bao la pili lililokataliwa na VAR baada ya mchezaji kuunawa mpira.

    Hatahivyo, ushindi wao haukuwa na shaka kamwe

    Kwani ulikamilisha mwendo wa kushangaza wa ushindi 19 na sare nne tangu kushindwa kwao kwa mara ya mwisho kwenye ligi, huko Aston Villa mnamo 6 Desemba.

    City sasa wameshinda mataji sita kati ya saba iliyopita ya Premier League. Muhula uliopita, waliungana na Huddersfield, Arsenal, Liverpool na Manchester United, mara mbili, kushinda ligi kuu miaka mitatu mfululizo.

    Sasa timu ya Guardiola imepata kitu ambacho hakuna upande mwingine imefanikiwa tangu ligi ya Uingereza ilipoanzishwa mwaka 1888, miaka 136 iliyopita.

  3. Diddy aomba msamaha kwa tabia yake 'isiyo na sababu'

    Sean "Diddy" Combs ameomba msamaha kwa tabia yake "isiyo na udhuru" baada ya CCTV kuonekana kumuonyesha akimshambulia mwimbaji Casandra "Cassie" Ventura.

    Akiongea kwenye video iliyotumwa kwenye ukurasa wake wa Instagram, nyota huyo wa rap alisema aliwajibika kikamilifu kwa matendo yake kwenye klipu hiyo.

    Kanda hiyo, iliyorushwa hewani na CNN mapema wiki hii, ilionekana kumuonyesha Bw Combs akimpiga teke na kumsukuma mpenzi wake wa zamani kwenye njia ya ukumbi wa hoteli.

    "Nilichukizwa nilipofanya hivyo. Nimejichukia sasa," alisema katika taarifa yake. "Nilienda na nikatafuta usaidizi wa kitaalamu.

    Niliingia kwenye matibabu, kwenda kituo cha kupata usaidizi. Ilibidi nimuombe Mungu rehema na neema zake. Samahani sana." BBC haijaithibitisha kwa uhuru video hiyo, ambayo inaonekana kuwa ni mkusanyiko wa video za uchunguzi wa tarehe 5 Machi 2016.

    Kulingana na CNN, ilirekodiwa katika Hoteli ya InterContinental ambayo sasa imefungwa huko Century City, Los Angeles

  4. Rais wa Azerbaijan atatizwa na ajali ya ndege iliyombeba rais wa Iran

    Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev anasema "alifadhaika sana" baada ya kusikia ripoti kuhusu ajali ya helikopta iliyomhusisha Ebrahim Raisi.

    Aliyev alikuwa na rais wa Iran mapema leo kufungua mabwawa mawili karibu na mpaka wa Iran na Azerbaijan.

    "Leo, baada ya kumuaga kwa urafiki Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ebrahim Raisi, tulifadhaishwa sana na habari za helikopta iliyobeba wajumbe wakuu wa Iran," aliandika kwenye X."

    Dua zetu kwa Mwenyezi Mungu ziko pamoja na Rais Ebrahim Raisi na ujumbe aliofuatana nao".

    Anaongeza kuwa Azerbaijan iko tayari kutoa msaada wowote unaohitajika.

  5. Habari za hivi punde, Itachukua muda kupata eneo la helikopta - waziri wa mambo ya ndani nchini Iran

    Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Ahmad Vahidi, anasema "timu mbalimbali za uokoaji" bado zinaitafuta helikopta hiyo.

    Akizungumza na televisheni ya taifa ya Iran, Vahidi anasema kwamba itachukua "muda kufika eneo" la eneo la ajali kwa sababu ya "hali mbaya ya hewa na ukungu katika eneo hilo".

    "Mambo yamedhibitiwa na timu za uokoaji zinafanya kazi yao. Tunatumai itafanyika haraka iwezekanavyo," anaongeza.

  6. Ajali ya ndege Iran: Tazama video ya waokoaji wakielekea katika eneo la ajali

  7. Raisi alihudhuria ufunguzi wa mabwawa kabla ya ajali ya helikopta

    Rais wa Iran Ebrahim Raisi alikuwa akielekea katika mji wa kaskazini-mashariki wa Tabriz baada ya kurejea kutoka eneo la mpaka wa Iran na Azerbaijan wakati tukio hilo lilipotokea.

    Raisi alikuwa akitembelea mpaka wa Iran na Azerbaijan, ambapo alifungua mabwawa ya Qiz Qalasi na Khodaafarin pamoja na mwenzake wa Azeri Ilham Aliyev.

    Hizi ni baadhi ya picha za hivi punde ambazo tumepokea za ziara yake mapema leo.

  8. Waokoaji bado hawajawasiliana na msafara wa helikopta

    Hali mbaya ya hewa - yenye ukungu mkubwa na mvua - inatatiza juhudi za timu za uokoaji kufika eneo la ajali katika milima kaskazini magharibi mwa Iran.

    Hali ya waliokuwemo ndani ya helikopta hiyo bado haijajulikana kwa sasa, huku ripoti kuwa bado hakuna mawasiliano yaliyofanywa.

    Rais Raisi alikuwa akisafiri na waziri wa mambo ya nje wa Iran katika msafara wa helikopta tatu katika eneo hilo - helikopta mbili kati ya hizo zimeripotiwa kutua salama.

    Raisi alichaguliwa kuwa rais katika jaribio lake la pili mnamo 2021.

    Anaonekana kama mtu mwenye msimamo mkali na anachukuliwa kuwa mrithi anayetarajiwa siku moja wa Ayatollah Khamenei kama Kiongozi Mkuu.

  9. Ajali ya ndege iliyombeba rais wa Iran: Tunachojua kufikia sasa

    Ebrahim Raisi alikuwa amesafiri hadi Mkoa wa Azarbaijan Mashariki kuzindua bwawa la Qizqalaasi kwenye mto wa mpaka wa Aras, na vyombo vya habari vya Iran viliripoti ajali iliyohusisha msafara wa helikopta yake.

    Ebrahim Raisi, Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje, Malik Rahmati, Gavana wa Azarbaijan Mashariki, Muhammad Ali Al Hashem, Imamu wa Juma Tabriz, walikuwa miongoni mwa waliokuwemo kwenye msafara huu.

    Kulingana na IRNA, "Hali mbaya ya hali ya hewa na ukungu mkubwa umefanya juhudi za vikundi vya uokoaji kuwa ngumu

  10. Helikopta iliyombeba rais wa Iran 'yatua kwa shida' - Runinga ya serikali

    Helikopta iliyombeba rais wa Iran imehusika katika ajali, vyombo vya habari vya serikali vinaripoti.

    Vyombo vya habari vya serikali vinasema Rais Ebrahim Raisi alikuwa kwenye helikopta ambayo ilitua kwa shida siku ya Jumapili.

    Pia ilisemekana kumbeba Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amirabdollahian.Waziri wa Mambo ya Ndani alisema waokoaji bado wanajaribu kufika eneo hilo kutokana na hali ngumu ya hewa.Hali ya waliokuwemo ndani ya helikopta hiyo bado haijajulikana kwa sasa, huku ripoti kuwa bado hakuna mawasiliano yaliyofanywa.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, Rais Raisi alikuwa akielekea katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran, baada ya kurejea mpakani na Azerbaijan, ambako alifungua mabwawa ya Qiz Qalasi na Khodaafarin.

    Ukungu mkubwa unafanya msako kuwa mgumu katika eneo ambalo inadhaniwa kuwa huenda helikopta hiyo ilitua, kulingana na ripota wa shirika la habari la Fars.

    Alisema mwonekano katika eneo la milima na misitu ulikuwa chini hadi takriban mita tano tu.Eneo hilo ni kama kilomita 50 kaskazini mwa Tabriz.

    Ahmad Alirezabeigi, Mbunge wa Iran katika mji wa Tabriz amewaambia waandishi wa habari mjini Tehran kwamba waokoaji bado hawajapata eneo la helikopta iliyombeba rais na waziri wa mambo ya nje.

    Aliongeza kuwa helikopta nyingine mbili katika msafara huo zilitua salama.Kanda za video zimeibuka kwenye televisheni ya taifa zikionyesha waumini wakimuombea afya rais katika mji mtakatifu wa Mashhad.

    Rais wa Iran Ebrahim Raisi ni nani?

    Bw Raisi, 63, alichaguliwa kuwa rais katika jaribio lake la pili mwaka wa 2021.

    Anaonekana kama mhubiri mwenye msimamo mkali na anachukuliwa kuwa mrithi wa Ayatollah Khamenei siku moja, kiongozi mkuu wa nchi hiyo tangu 1989.

    Mnamo mwaka wa 2019, Kiongozi Mkuu alimteua kwenye nafasi yenye nguvu ya mkuu wa mahakama.

    Bw Raisi pia alichaguliwa kuwa naibu mwenyekiti wa Bunge la Wataalamu, baraza la makasisi lenye wanachama 88 walio na jukumu la kumchagua Kiongozi Mkuu ajaye.

  11. Zuma apima umaarufu wake wa kisiasa katika kitongoji cha Soweto

    Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma alionyesha nguvu zake katika kitongoji cha kihistoria cha Soweto alipokuwa akifanya kampeni za kutafuta kura katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Mei 29.

    Wapiganaji wa Kizulu waliandamana kuzunguka Uwanja wa Orlando wakiwa na mikuki na ngao zao, wanaume waliojificha waliimba na kucheza nyimbo za mapinduzi, huku baadhi ya waimbaji maarufu wa Afrika Kusini - akiwemo rapa Big Zulu - wakitoa burudani kwa umati wa watu waliohudhuria mkutano huo wa Jumamosi.

    Kwa wafuasi wa Bw Zuma mapinduzi makubwa yalikuwa ni kuwepo kwa mwanamume anayejulikana kama mfalme wa disko, Papa Penny.

    Baada ya kutangaza kujiuzulu kutoka chama tawala cha African National Congress (ANC) wiki iliyopita, sasa amejiunga na chama kipya cha rais wa zamani, uMkhonto weSizwe, ambacho kinatafsiriwa kama Spear of the Nation. "Unganisha Afrika.

    Unganisha Afrika Kusini," alisema katika hotuba fupi kwa umati wa watu, na kuongeza: "Phansi [Chini na] ukabila."

  12. Chama cha wanasheria Kenya chapinga mpango wa maafisa wa polisi kupelekwa Haiti

    Chama cha Wanasheria nchini Kenya kimepinga mpango wa kutumwa kwa maafisa 1,000 wa polisi katika kisiwa cha Caribbean cha Haiti.

    Katika taarifa ya Rais wa LSK Faith Odhiambo, LSK inamtaka Rais William Ruto, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki na Inspekta Jenerali wa Polisi Japheth Koome kutii agizo la mahakama lililokataza kutumwa kwa maafisa hao wa polisi.

    "Imetufikia kwamba licha ya maagizo ya mahakama, serikali imeidhinisha kutumwa kwa jeshi hilo.

    Huku ikiripotiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Waziri Mkuu wa zamani wa Haiti walitekeleza mkataba wa nchi mbili unaodaiwa kuidhinisha kutumwa kwa maafisa wa polisi wa Kenya, Sheria.

    ''Jamii ya Kenya inalazimishwa, katika kutetea Utawala wa Sheria, kueleza kwamba mahitaji ya kisheria, kama yalivyofasiriwa na Jaji C Mwita hayajatimizwa Kwa hiyo, hatua yoyote ya kupeleka maafisa wa polisi nchini Haiti ni kinyume cha sheria'' , Odhiambo alisema.

  13. Jeshi la Uganda lamkamata kamanda wa kundi la waasi wa ADF

    Jeshi la Uganda limemkamata kamanda wa kundi la waasi linaloshirikiana na Islamic State ambaye ni mtaalamu wa kutengeneza vilipuzi, au mabomu, ambayo kundi hilo limetumia kufanya mashambulizi mabaya siku za nyuma, jeshi lilisema Jumapili.

    Mpiganaji huyo, Anywari Al Iraq, raia wa Uganda, alikamatwa katika misitu ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako kundi la waasi la Allied Democratic Forces lina makao yake, jeshi la Uganda People's Defense Forces, lilisema katika taarifa yake.

    Wakati wa operesheni hiyo, watu tisa wakiwemo watoto pia waliokolewa kutoka eneo la jimbo la Ituri mashariki mwa Kongo, jeshi lilisema."Aina ya vifaa vya kutengenezea vilipuzi vilivyoboreshwa (IED) vilipatikana," ilisema.

    Waasi wa ADF walianza uasi nchini Uganda lakini wamejikita nchini Kongo tangu mwishoni mwa miaka ya 1990.

    ADF iliahidi utiifu kwa Islamic State katikati ya 2019 na inashutumiwa kuwaua mamia ya wanakijiji katika uvamizi wa mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni.

  14. Habari za hivi punde, Jeshi la DRC latangaza kuzuia jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais Felix Tshisekedi

    Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza kuwa limezuia jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais Felix Tshikedi huko Kinshasa.

    Msemaji wa jeshi la DR Congo Brig Jenerali Sylavin Ekenge amesema kwenye kituo cha runinga cha taifa RTNC TV kwamba washukiwa kadhaa wanazuiliwa na "hali sasa imedhibitiwa".

    Tangazo hili liinajiri saa chache baada ya watu wenye silaha kushambulia nyumba ya Vital Kamerhe, mkuu wa zamani wa majeshi na mshirika wa karibu wa Rais Felix Tshisekedi Jumapili asubuhi.

    Walioshuhudia wanasema kundi la takriban washambuliaji 20 wakiwa wamevalia sare za jeshi walishambulia makazi hayo na ufyatulianaji wa risasi ukafuatia.

    Ripoti za vyombo vya habari vya ndani zilisema washambuliaji hao walikuwa wanachama wa Vuguvugu la New Zaire linalohusishwa na aliyekuwa mwanasiasa aliyeko uhamishoni Christian Malanga.

    Walinzi wawili na mshambuliaji waliuawa katika shambulio la nyumba ya Bw Kamerhe, msemaji wake na ubalozi wa Japan umeandika kwenye machapisho ya mtandao wa kijamii wa X.

    BBC imeona video ya Bw Malanga akisema kwa Kilingala, lugha ya wenyeji: "Sisi wanajeshi tumechoka, hatuwezi kuandamana pamoja na Vital Kamerhe na Rais Félix Tshisekedi."

    Rais Tshisekedi alichaguliwa tena kwa muhula wa pili katika uchaguzi uliozozaniwa mwaka jana mwezi Disemba.

    Alishinda takriban 78% ya kura. Takriban watu 20 waliuawa katika ghasia zinazohusiana na uchaguzi wakati wa maandalizi ya upigaji kura.

    Kongo ni nchi yenye utajiri mkubwa wa madini na idadi kubwa ya watu, lakini licha ya hali hii maisha hayajaboreka kwa watu wengi, huku migogoro, ufisadi na utawala mbovu vikiendelea.

    Sehemu kubwa ya maliasili za nchi hiyo ziko mashariki ambako ghasia bado zinaendelea licha ya jitihada za Bw Tshisekedi za kukabiliana na hali hiyo na kuleta wanajeshi wa kikanda.

    Rais Tshisekedi hajatoa tamko lolote kuhusu tukio hili kufikia muda wa machapisho.

    Balozi wa Japani katika mji mkuu wa Kongo amewaonya wajapani walioko DRC kutotoka nje.

    Tutakujuza habari zaidi kadri zitakapotufikia...

  15. Waziri wa baraza la vita la Israel kujiuzulu ikiwa hakuna mpango wa baada ya vita kwa Gaza

    Waziri wa baraza la vita nchini Israel Benny Gantz ametishia kujiuzulu iwapo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu hatoweka mpango wa baada ya vita kwa Ukanda wa Gaza.

    Bw Gantz aliweka makataa ya Juni 8 kwa mpango wa kuafikia "malengo 6 ya kimkakati", ikiwa ni pamoja na mwisho wa utawala wa Hamas huko Gaza na kuanzishwa kwa utawala wa kiraia katika eneo hilo.

    "Ukiweka taifa juu ya ubinafsi, utapata washirika katika mapambano," alisema. "Lakini ukichagua njia ya ushabiki na kuliongoza taifa zima kwenye shimo, tutalazimika kuondoka katika serikali."

    Bw Netanyahu alipuuzilia mbali maoni hayo na kusema "ni maneno " ambayo yangemaanisha "kushindwa kwa Israeli".

  16. Natumai hujambo