Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Zelensky asema Urusi 'haitaki amani' akijiandaa kukutana na Trump

Jumamosi usiku, milipuko ilisikika huko Kyiv, katika kile maafisa wa Ukraine walisema ni shambulio jipya la angani la Urusi.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi & Asha Juma

  1. Idadi ya walionyongwa Iran yaongezeka mara mbili zaidi 2025 - Ripoti

    Idadi ya watu walionyongwa nchini Iran mwaka 2025 inakadiriwa kuwa zaidi ya mara mbili ikilinganishwa na idadi ya hukuma iliyotekelezwa kote nchini mwaka 2024.

    Kundi la Haki za Kibinadamu la Iran (IHR) lenye makao yake makuu nchini Norway (IHR) liliiambia BBC kuwa limethibitisha angalau watu 1,500 walionyongwa hadi mwanzoni mwa Desemba, na kuongeza kuwa wengi zaidi wametekelezwa tangu wakati huo. Mwaka jana, IHR iliweza kuthibitisha watu 975 walionyongwa - ingawa idadi kamili haiko wazi kabisa kwani mamlaka ya Irani haitoi takwimu rasmi.

    Hata hivyo, uchambuzi unaonyesha ongezeko lingine kubwa la kila mwaka, na takwimu zinalingana na zile zinazotolewa na vikundi vingine vya ufuatiliaji.

    Serikali ya Iran hapo awali ilitetea utumiaji wake wa adhabu ya kifo, ikisema kuwa inahusu tu "uhalifu mbaya zaidi".

    Takwimu za kunyongwa tayari zilikuwa zimeongezeka kabla ya maandamano makubwa yaliyozuka kote nchini humo mwaka 2022 kufuatia kifo cha Mahsa Amini. Mwanamke huyo wa Kikurdi mwenye umri wa miaka 22 alizuiliwa na polisi wa maadili mjini Tehran kwa madai ya kuvaa hijabu yake "isivyofaa".

    Soma pia:

  2. Starmer alikosolewa kwa kumkaribisha mwanaharakati wa Misri

    Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer amekosolewa kwa kukaribisha ujio wa mwanaharakati wa demokrasia wa Misri Alaa Abdel Fattah nchini humo - baada ya jumbe za zamani katika mitandao ya kijamii kuibuka zikimuonyesha mwanaharakati huyo akitaka Wazayuni wauawe.

    Abdel Fattah ambaye ana uraia pacha wa Uingreza aliondoka Misri wiki hii baada ya kuachiwa gerezani.

    Mnamo 2021 alipatikana na hatia "kueneza habari za uwongo" baada ya kuweka ujumbe kwenye mtandao wa Facebook kuhusu mateso nchini.

    Starmer alisema "amefurahi" kusikia mwanaharakati huyo ametua Uingereza kuunganishwa na familia yake.

    Lakini katibu kivuli wa haki Robert Jenrick anasema tamko la Sir Keir Starmer "halikuwa sahihi".

  3. Utambuzi wa Israel wa Somaliland unalenga 'kuwafurusa Wapalestina' - Mjumbe wa Somalia

    Mwakilishi wa kudumu wa Somalia katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Balozi Ali Abdi Awari, ameta hatua ya Israel kilitambua eneo la "Somaliland" kama taifa huru kama "kitendo cha uchokozo'', kisichokubalika kabisa, na ukiukaji wa wazi na usio na kifani wa sheria za kimataifa, maazimio ya Umoja wa Mataifa, na mikataba ya Umoja wa Kiarabu na Umoja wa Afrika."

    Katika hotuba yake katika mkutano wa dharura wa Baraza la Jumuiya hiyo katika ngazi ya wajumbe wa kudumu, uliofanyika Jumapili katika makao makuu ya yake mjini Cairo, Misri kujadili masuala yanayohusiana na tamko la Israel, Abdi alisisitiza kwamba hatua hii inaashiria "changamoto ya wazi kwa matakwa ya jumuiya ya kimataifa na kupuuza utaratibu wa kimataifa unaozingatia heshima ya mataifa."

    Mjumbe huyo wa Somalia alikichukulia hatua hiyo ya Israel kuwa "batili na ambayo haitabadilisha ukweli kwamba eneo la Kaskazini-Magharibi linalofahamika kama Somaliland ni sehemu muhimu ya Jamhuri ya Somalia."

    Aliongeza kuwa hatua ya hivi punde zaidi ya Israel inalenga "kuunga mkono taasisi inayojitenga nchini Somalia," kwa lengo la kufikia kile alichokitaja kuwa "uhamisho wa lazima wa Wapalestina kutoka katika ardhi yao," akisisitiza kwamba Jamhuri ya Somalia haitakuwa "mshirika wa jaribio lolote la kuwaondoa Wapalestina kutoka kwenye ardhi yao."

    Alidokeza kuwa Somalia haitachukulia hatua hiyo kama "shambulio lingine tu la Israel dhidi ya nchi nyingine ya Kiarabu, bali inachukulia kuwa ni shambulio la moja kwa moja na dharau kwa usalama wa taifa la Waarabu kwa ujumla, na kwa usalama wa ufikiaji katika Bahari ya Shamu."

    Somalia iimetoa wito kwa mataifa ya Kiarabu kusimama kidete dhidi ya kile ilichoeleza kuwa "mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel" dhidi ya nchi za Kiarabu, na "kuunda sera madhubuti ya kuzuia kutokea tena na kuendelea kwa hali kama hiyo."

    Soma zaidi:

  4. Zelensky asema Urusi 'haitaki amani' akijiandaa kukutana na Trump

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anatarajiwa kukutana na Rais Donald Trump wa Marekani mjini Florida leo Jumapili, kwa duru ya hivi punde ya mazungumzo yanayolenga kumaliza mzozo kati ya nchi yake na Urusi.

    Wawili hao watajadili toleo jipya la mpango wa amani unaosimamiwa na Marekani, ambao Moscow bado haijauunga mkono, pamoja na mapendekezo tofauti ya dhamana ya usalama ya Marekani.

    Mkutano wao katika makao ya rais wa Marekani Mar-a-Lago unafuatia mashambulizi makali ya Urusi dhidi ya Kyiv mwishoni mwa juma, ambayo Zelensky alisema ni ushahidi kwamba Moscow "haitaki amani".

    Siku ya Ijumaa usiku, shambulio la saa 10 la kombora na ndege zisizo na rubani zilizolenga mji mkuu wa Ukraine zilisababisha vifo vya watu wawili na wengine 32 kujeruhiwa, mamlaka zilisema.

    Trump na Zelensky watajadili mpango mpya wa amani wenye vipengele 20, toleo lililoboreshwa la mpango wa awali wenye vipengele 28 ulioandaliwa na mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff ambao uliivutia Urusi.

    Udhibiti wa eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine umekuwa nguzo kuu katika mazungumzo hadi sasa, lakini Zelensky anasisitiza kuwa "eneo huru la kiuchumi" linaweza kuwa chagua pia.

    Moscow kwa sasa inadhibiti takribani 75% ya mkoa wa Donetsk, na baadhi ya 99% ya Luhansk jirani.

    Mikoa hiyo kwa pamoja inajulikana kama Donbas. Ikulu ya Kremlin haijazungumzia pendekezo la Zelensky la kuondoa wanajeshi wake katika eneo la mashariki la Donbas, ikiwa Urusi nayo itafuata mkondo.

    Soma zaidi:

  5. Nigeria yatoa ushirikiano kuepuka hatua ya kijeshi ya Marekani

    Serikali ya Nigeria huenda imeepuka hatua ya kijeshi ya upande mmoja iliyotishiwa na Rais Donald Trump mwezi mmoja uliopita baada kwa kuamua kushirikiana na Marekani katika shambulio la anga la Siku ya Krismasi.

    Lakini wataalamu wa usalama wanasema haijulikani kama mashambulizi kama hayo yanaweza kusaidia sana kuwazuia wanamgambo wa Kijihadi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakihangaisha jamii katika maeneo tofauti ya taifa hilo la Afrika magharibi.

    Alhamisi wiki iliopita Trump alitangaza kwenye mtandao wake wa Truth Social kwamba vikosi vya Marekani vimeanzisha shambulizi dhidi ya wanamgambo wa Islamic State kaskazini magharibi mwa Nigeria kwa ombi la serikali ya Nigeria. Alisema kundi hilo limekuwa likiwalenga Wakristo katika eneo hilo.

    Trump baadaye alisema kwamba shambulio la kijeshi la Marekani lililolenga wanamgambo wa kundi la Islamic state nchini Nigeria lilitarajiwa kufanyika Jumatano, lakini aliamuru liahirishwe kwa siku moja.

    Soma zaidi:

  6. Karibu tena kwa muendelezo wa taarifa zetu za moja kwa moja leo Jumapili 28.12.2025

  7. Poland yatuma ndege haraka kulinda anga lake

    Ndege za kivita za Poland zimezingira eneo la mpaka wake na Ukraine, baada ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, kushambuliwa na makombora na ndege zisizo na rubani za Urusi usiku kucha.

    Jeshi la Poland limesema limechukua hatua ya "kulinda" anga lake, baada ya mtu mmoja kuuawa na wengine 28 kujeruhiwa huko Kyiv, Huduma ya Dharura ya Serikali ya Ukraine iliripoti.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anatarajiwa kukutana na Donald Trump huko Florida Jumapili.

    Lakini kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya Urusi, Zelensky amerudia madai yake kwamba Urusi "haitaki kukomesha vita na inajaribu kutumia kila fursa kuiumiza Ukraine zaidi".

    Pia unaweza kusoma:

  8. Urusi yashambulia Ukraine kabla ya mazungumzo ya Zelensky-Trump

    Mashambulizi makubwa ya makombora na milipuko ya Urusi yameshuhudiwa Kyiv na mapema Jumamosi asubuhi, wikendi iliyopangwa kufanyika kwa mazungumzo ya kidiplomasia ya ngazi ya juu ya kutafuta amani katika ya Zelensky na Trump.

    Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine Ihor Klymenko alisema mashambulizi hayo ya usiku kucha yameua mtu mmoja na kujeruhi wengine 28 huko Kyiv, akiongeza kuwa majengo zaidi ya 10 ya makazi katika jiji hilo yameharibiwa.

    Mashambulizi hayo yalisababisha kufungwa kwa muda kwa viwanja viwili vya ndege kusini mashariki mwa Poland baada ya jeshi la anga la Poland kutuma ndege za kivita, Shirika la Huduma za Urambazaji wa Anga la Poland lilisema kwenye mtandao wa X.

    Zelenskyy alisema Jumamosi kwamba ndege zisizo na rubani 500 za Urusi na makombora 40 yalishambulia Ukraine, kuonyesha kwamba Rais wa Urusi Vladimir Putin "hataki kukomesha vita."

    Mashambulizi ya hivi punde yametokea chini ya saa 48 baada ya Zelensky kuashiria kwamba makubaliano ya amani yalikuwa karibu, na siku moja tu kabla ya mazungumzo na Trump huko Florida Jumapili.

    Soma zaidi:

  9. IGAD yapinga vikali hatua ya Israel kutambua rasmi Somaliland

    Mamlaka ya Serikali za Kimataifa juu ya Maendeleo (IGAD) imeshutumu vikali jaribio lolote la kuitambua Somaliland, ikirejelea kwamba Jamhuri ya Shirikisho la Somalia inasalia kuwa nchi mwanachama huru wa kikanda.

    IGAD ilisema kwamba "umoja na uadilifu wa eneo la Somalia vimeainishwa katika sheria za kimataifa na utambuzi huu wa upande mmoja ni kinyume na sheria za Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na IGAD."

    Katibu Mkuu wa (IGAD) ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuzingatia sheria za kimataifa.

    IGAD ilihimiza jumuiya ya kimataifa na washikadau wengine kuheshimu sheria za kimataifa na kuunga mkono mazungumzo na michakato ya amani inayoimarisha utulivu wa kikanda, ushirikiano, na amani.

    IGAD pia ilithibitisha tena uungaji mkono wake kwa serikali ya Somalia na watu wake, ikisisitiza kujitolea kwake kwa michakato ya kisiasa inayojumuisha kila mmoja na ushirikiano wa kikanda unaolenga kufikia amani ya kudumu, utulivu, na ustawi wa pamoja kwa Somalia na nchi zote wanachama wa IGAD.

    Taarifa hiyo ya shirika la kikanda la IGAD inakuja baada ya Israeli kutangaza kwamba inaitambua rasmi Somaliland kama taifa huru.

    Soma zaidi:

  10. Mwanajeshi wa akiba Israel amgonga Mpalestina akisali kando ya barabara

    Mwanajeshi wa akiba wa Israeli amemgonga mwanamume Mpalestina kwa gari lake wakati anasali kando ya barabara katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa siku ya Alhamisi, baada ya kufyatua risasi mapema katika eneo hilo, jeshi la Israeli lilisema.

    "Video iliyoonekana inaonyesha mtu mwenye silaha akimgonga kimaksudi Mpalestina," ilisema katika taarifa, ikiongeza kuwa mtu huyo alikuwa mwanajeshi wa akiba na utumishi wake wa kijeshi umefutwa.

    Jeshi lilisema kwamba mwanajeshi huyo wa akiba "alikiuka pakubwa mamlaka yake" na silaha yake imechukuliwa.

    Vyombo vya habari vya Israeli viliripoti kwamba alikuwa chini ya kuzuizi cha nyumbani.

    Hata hivyo, polisi wa Israeli hawakujibu mara moja ombi la Reuters la kutoa maoni.

    Video iliyoonyeshwa kwenye televisheni ya Palestina na kuthibitishwa na Reuters inaonyesha mwanamume aliyevaa mavazi ya kiraia akiwa na bunduki begani mwake huku akiendesha gari nje ya barabara na kumgonga mwanamume aliyekuwa akisali kando ya barabara.

    Soma zaidi:

  11. Trump apinga uwezekano wa Marekani kuitambua rasmi Somaliland

    Rais Donald Trump amesema anapinga uwezekano wa Marekani kuitambua Somaliland katika mahojiano na New York Post yaliyochapishwa Ijumaa.

    Hii inafuata baada ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu ambaye pia ni mshirika mkubwa wa Trump kuwa nchi ya kwanza kuitambua rasmi Somaliand kama taifa huru.

    "Hapana," rais Trump aliambia New York Post alipoulizwa kuhusu Marekani kuitambua Somaliland.

    "Ninajifunza mambo mengi na huwa nafanya maamuzi mazuri. Aliongeza: "Je, kuna mtu yeyote anayejua Somaliland ni nini, kweli?".

    Siku ya Ijumaa, Israeli ilikuwa nchi ya kwanza kuitambua rasmi Somaliland kama taifa huru.

    Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, ambaye alifanya mazungumzo ya video na Rais wa Somaliland Abdirahman Mohamed Abdullahi, alisema atamjulisha Trump kuhusu hatua hiyo na kuhusu nia iliyoonyeshwa ya Somaliland ya kujiunga na Makubaliano ya Abraham wakati wa mkutano wao Jumatatu.

    Somalia inashutumu utambuzi huo, ikiungwa mkono na Misri, Uturuki na Baraza la Ushirikiano la Ghuba, wote wakionya kwamba kuhalalisha Somaliland kunahatarisha kuyumbisha Pembe ya Afrika ambayo tayari inayumba.

    Soma zaidi:

  12. Thailand na Cambodia zakubaliana kusitisha mapigano

    Mawaziri wa ulinzi wa nchi za Thailand na Cambodia wamesema katika taarifa ya pamoja siku ya Jumamosi kwamba nchi hizo mbili zimekubaliana kusitisha mapigano mara moja.

    Pande zote mbili zimekubaliana kusimamisha harakati zote za wanajeshi na kuwaruhusu raia wanaoishi katika maeneo ya mpakani kurudi nyumbani, na kusitisha mapigano makali ya mpakani ya wiki kadhaa ambayo yameua watu wasiopungua 41 na kuwafukuza karibu watu milioni moja.

    Usitishaji mapigano ulianza saa sita mchana saa za eneo (05:00 GMT). Yatakapodumu kwa saa 72, wanajeshi 18 wa Cambodia walioshikiliwa na Thailand pia wataachiliwa, taarifa hiyo ilisema.

    Mafanikio hayo yalikuja baada ya maafisa wa Thailand na Cambodia kufanya mazungumzo ya siku kadhaa yenye lengo la kukomesha mapigano mapya kati ya nchi hizo mbili.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Penalti ya Salah yaingiza Misri kwenye mwondoano AFCON 2025

    Mohamed Salah ameihakikishia Misri tiketi ya kushiriki katika hatua ya mtoano ya AFCON 2025 baada ya kufunga bao la ushindi la Mafarao dhidi ya Afrika Kusini.

    Penalti ya Mohamed Salah iliipa Misri ushindi huku mabingwa hao mara saba wakicheza kipindi cha pili wakiwa wachezaji 10 na kujikatia nafasi katika hatua ya mtoano ya Kombe la Mataifa ya Afrika la 2025 wakiwa wamesalia na mchezo mmoja.

    Baada ya kuongoza kupitia mpira wa adhabu uliopigwa na Salah dakika ya 45, Mafarao walijikuta katika hali ngumu ya kihesabu wakati beki wa kulia Mohamed Hany alipopewa kadi ya pili ya njano wakati wa mapumziko mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

    Bafana Bafana walifanya mabadiliko ya mashambulizi wakati wa mapumziko, wakimtoa Thalente Mbatha na kumtia Sipho Mbule, lakini walitumia muda mwingi wa kipindi cha pili wakijitahidi kupata njia ya kumpita kipa Mohamed El Shenawy, ambaye timu yake ilifanikiwa kudumisha mashambulizi ya kukabiliana.

    Afrika Kusini ilinyimwa penalti yenye uwezo wa kutolewa kwa mpira ulioshikwa kwa mikono baada ya saa kupita dakika 90, huku mwamuzi wa Burundi Pacifique Ndabihawenimana akiangalia tukio hilo kwenye skrini ya pembeni mwa uwanja.

    Misri wana pointi sita kutoka michezo yao miwili ya ufunguzi.

    Afrika Kusini wana pointi tatu kutoka michezo yao miwili, huku Zimbabwe na Angola zikiwa na pointi moja kila moja baada ya kutoka sare ya 1-1 mapema siku hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Zelensky kukutana na Trump Jumapili kwa mazungumzo ya kukomesha vita

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema atakutana na mwenzake wa Marekani Donald Trump huko Florida siku ya Jumapili, huku mazungumzo yakiendelea kuhusu kukomesha vita vya Urusi.

    Zelensky alisema alitarajia mkutano huo uzingatie mpango wa amani unaosimamiwa na Marekani, na mapendekezo tofauti ya dhamana za usalama za Marekani. Lakini afisa mmoja mwandamizi wa Urusi alisema mpango huo ulikuwa "tofauti kabisa" na ule uliokuwa ukijadiliana na Marekani.

    Urusi imezungumzia "maendeleo ya polepole lakini thabiti" katika mazungumzo ila haijatoa maoni yoyote kuhusu ofa ya Zelensky ya kuondoa wanajeshi kutoka eneo la mashariki mwa Donbas la Ukraine, ikiwa Urusi pia itajiondoa.

    Jumamosi usiku, milipuko ilisikika huko Kyiv, katika kile maafisa wa Ukraine walisema ni shambulio jipya la angani la Urusi.

    Soma zaidi:

  15. Hujambo msomaji wetu. Karibu katika matangazo yetu mubashara kipindi hiki cha sikukuu. Tarehe ni 27/12/2025.