Kenya: Rais Ruto aamuru uchunguzi wa miili iliyopatikana jalalani kuharakishwa

Rais wa Kenya William Ruto ameagiza mamlaka husika kuharakisha uchunguzi kuhusu maiti zilizokuwa zimefungwa kwenye mifuko ya plastiki na kutupwa jalalani katika mtaa wa Mukuru kwa Njenga, jijini Nairobi.

Muhtasari

  • Trump yuko huru kutumia mitandao ya kijamii
  • Watu wanne waokolewa Nigeria baada ya jengo lingine kuporomoka
  • Akamatwa baada ya mabaki ya binadamu kupatikana kwenye masanduku
  • Polisi wa Kenya wanachunguzwa baada ya miili ya watu kupatikana jalalani jijini Nairobi
  • Watu 71 wameuawa katika shambulio la Israel mjini Gaza - Hamas
  • Watano wafungwa kwa mauaji ya mgombea urais wa Ecuador
  • Kenya: Mbunge afukuzwa kwenye hoteli kufutia 'kauli yake dhidi yake Gen Z'
  • Mtoto wa tajiri mkubwa wa India afunga ndoa katika harusi ya kifahari

Moja kwa moja

Ambia Hirsi & Esther Namuhisa

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Rais Ruto aamuru uchunguzi wa miili iliyotupwa jalalani Nairobi kuharakishwa

    Rais wa Kenya William Ruto ameagiza mamlaka husika kuharakisha uchunguzi kuhusu maiti zilizokuwa zimefungwa kwenye mifuko ya plastiki na kutupwa jalalani katika mtaa wa Mukuru kwa Njenga, jijini Nairobi.

    Ruto amehakikishia umma kuwa waliohusika na kitendo hicho watakamatwa na kushtakiwa.

    Alisema kuwa miili iliyopatikana ni tisa, ingawa wakazi wa Mukuru kwa Njenga wanasema idadi hiyo ni kubwa zaidi kwani miili mitano zaidi ilipatikana Jumamosi asubuhi.

    “Kule Nairobi, kumepatikana mili ya Wakenya, imefika karibu tisa. Karibu wote ni wasichana na tunafanya uchunguzi. Nimeamrisha polisi na wale wote wanaohusika kwa mambo ya homicide. Nawahakikisha Wakenya, wale wote waliohusika na vifo vya Kware watachukuliwa hatua,” rais alisema.

    Ripoti ya uchunguzi wa awali inaonyesha kuwa waathiriwa - wote ni wanawake, waliuawa kwa njia sawa.

    Eneo hilo limefungwa huku polisi wakiendelea kutafuta miili zaidi.

    Haya yanajiri siku moja baada ya mkuu wa polisi nchini Kenya kujiuzulu kufuatia maandamano ya kupinga nyongeza ya kodi yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 40.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Trump yuko huru kutumia mitandao ya kijamii

    Trump

    Chanzo cha picha, Reuters

    Meta imeondoa vizuizi vilivyosalia kwenye akaunti za Facebook na Instagram za Donald Trump kabla ya uchaguzi ujao wa rais nchini Marekani mnamo mwezi Novemba.

    Akaunti za mitandao ya kijamii za Trump zilisimamishwa mwaka 2021 kutokana na maoni yake baada ya uvamizi wa bunge la Marekani, Januari 6.

    Akaunti za Trump kwa pamoja zina wafuasi milioni 60 na zilirudishwa mwaka 2023 zikiwa chini ya ufuatiliaji wa ziada ambao sasa umeondolewa.

    Meta imesema kuwa ina Wajibu wa kuruhusu maoni ya kisiasa ambayo wamarekani wanapaswa kusikia kutoka kwa wagombea wote wawili kwa usawa.

    Iliongeza kuwa wagombea urais wa Marekani "wanasalia chini ya Viwango vya Jumuiya sawa na watumiaji wote wa Facebook na Instagram, ikiwa ni pamoja na sera zilizoundwa ili kuzuia matamshi ya chuki na uchochezi wa vurugu.

    " Tangu kurudi kwenye majukwaa ya Meta, akaunti za Trump zimechapisha zaidi maelezo ya kampeni ikiwa ni pamoja na kejeli dhidi ya mpinzani wake wa kinyang'anyiro cha urais Joe Biden.

    Kabla ya marufuku yake ya 2021, machapisho ya Facebook ya Trump mara nyingi yalikuwa maarufu zaidi nchini Marekani, kulingana na data wakati huo za CrowdTangle.

    Trump ndiye rais wa kwanza wa zamani kuhukumiwa kwa uhalifu na pia alipigwa marufuku na mitandao ya Twitter na YouTube.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Watu wanne waokolewa Nigeria baada ya jengo lingine kuporomoka

    Shirika la Kitaifa la Kushughulikia hali ya Dharura nchini Nigeria (NEMA) limesema watu wanne wameokolewa baada ya jengo lingine kuporomoka katika mji mkuu Abuja mapema leo.

    Haijabainika ni nini kilisababisha jengo hilo la ghorofa mbili kuporomoka, lakini tukio hilo linakuja chini ya saa 24 baada ya watoto 22 kufariki baada ya jengo la shule kuporomoka katika Jimbo la Plateau siku ya Ijumaa.

    Kati ya watu wanne waliookolewa wakiwa hai, wawili walipelekwa hospitalini kwa matibabu, kulingana na shirika la usimamizi wa dharura.

    "Mmoja kati ya wawili ambao walipelekwa hospitalini ametibiwa majeraha madogo na kuruhusiwa," NEMA ilisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X.

    Juhudi za kutafuta watu zaidi ambao huenda wamenaswa kwenye vifusi zinaendelea, na baada ya hapo "eneo hilo litahifadhiwa na kukabidhiwa kwa mamlaka zinazofaa," NEMA iliongeza.

    Jengo hilo lililokuwa na vyumba 45 vya kujitegemea lilisemekana kuwa hoteli kabla ya kubadilishwa kwa matumizi ya makazi.

    Kuporomoka kwa majengo ni jambo la kawaida nchini Nigeria, ambapo matukio kama hayo mara nyingi hulaumiwa kutokana na matumizi ya vifaa vya chini ya kiwango, matengenezo duni, na kushindwa kutekeleza kanuni za usalama wa majengo.

  5. Akamatwa baada ya mabaki ya binadamu kupatikana kwenye masanduku

    MM

    Mtu mmoja amekamatwa kwa tuhuma za mauaji baada ya mabaki ya binadamu kukutwa kwenye masanduku karibu na Daraja la Clifton Suspension huko Bristol.

    Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 34 alikamatwa na maafisa wa Avon na Somerset katika Kituo cha Temple Meads huko Bristol alfajiri ya Jumamosi.

    Mabaki yaliyopatikana kwenye mizigo katika nyumba moja huko Shepherd's Bush, magharibi mwa London ni ya wanaume wawili, polisi wamesema.

    Naibu Kamishna Msaidizi wa Met, Andy Valentine, amesema kuwa kukamatwa kwake ni hatua kubwa.

    "Tunaelewa wasiwasi wa wakazi wa hapa Bristol na London na maafisa watabaki katika maeneo ya Clifton na Shepherd's Bush kwa siku kadhaa zijazo ili kuwahakikishia usalama wale walioathirika na tukio hili la kusikitisha," aliongeza.

    "Mtu yeyote mwenye wasiwasi wowote anahimizwa kuzungumza nao."

    Polisi wa Met walikuwa wametoa taarifa awali wakisema wanataka kuzungumza na Yostin Andres Mosquera

    Polisi hawamfuatilii mtu mwingine yeyote na mwanaume aliyekamatwa katika Kituo cha Temple Meads anapelekwa London kwa ajili ya kuhojiwa.

    Kabla tu ya saa sita usiku siku ya Jumatano, Polisi wa Avon na Somerset walipokea taarifa ya mwanaume mwenye sanduku aliyekuwa akifanya vitendo vya kutiliwa shaka kwenye Daraja la Clifton Suspension.

    Maafisa walifika ndani ya dakika 10, lakini mwanaume huyo alikuwa ameondoka, akiwa ameacha masanduku nyuma.

  6. Polisi wa Kenya wanachunguzwa baada ya miili ya watu kupatikana jalalani jijini Nairobi

    xx

    Chanzo cha picha, People Daily

    Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi nchini Kenya (IPOA) imeanzisha uchunguzi baada miili sita ya watu iliyoharibika kupatikana umbali wa mita 100 kutoka kituo cha polisi jijini Nairobi.

    Miili hiyo iliyoripotiwa kufungwa kwenye mifuko kwa kutumia kamba za nailoni ilikuwa na alama zinazoashiria mateso.

    IPOA inachunguza kuhusika kwa polisi katika vifo hivyo na imetaka uchunguzi wa haraka ufanyike ili kuwabaini waliofariki.

    Siku ya Ijumaa polisi walisema wamepata miili sita kwenye eneo la kutupia taka lakini mashirika ya haki za binadamu yanasema miili hiyo ni zaidi ya tisa.

    Ripoti ya uchunguzi wa awali inaonyesha kuwa waathiriwa - wote ni wanawake, waliuawa kwa njia sawa.

    Eneo hilo limefungwa huku polisi wakiendelea kutafuta miili zaidi.

    Haya yanajiri siku moja baada ya mkuu wa polisi nchini Kenya kujiuzulu kufuatia maandamano ya kupinga nyongeza ya kodi yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 40.

  7. Watu 71 wauawa katika shambulio la anga mjini Gaza - Hamas

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takribani Wapalestina 71 wameuawa katika shambulizi la angani la Israel, lililolenga eneo lenye watu wengi waliokimbia makazi yao Khan Younis mjini Gaza, wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas imesema.

    Jeshi la Israel lilikuwa limeteua eneo hilo kuwa eneo salama, na kuwataka Wapalestina kutafuta hifadhi huko.

    Zaidi ya watu 90 walijeruhiwa katika shambulizi hilo, kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya afya.

    Jeshi la Israel limesema linachunguza tukio hilo, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

    Kituo cha redio cha jeshi la Israel kilisema vyanzo vimeelezea lengo la shambulio hilo kama "muhimu sana".

    Mtu aliyeshuhudia shambulio hilo aliaimbia BBC kwamba eneo la tukio lilionekana kana kwamba limekumbwa na "tetemeko la ardhi", na video kutoka eneo hilo zinaonyesha moshi ukifuka na majeruhi waliolowa damu wakibebwa kwenye machela.

    Watu pia wanaonekana wakipekua vifusi kwenye shimo kubwa kwa kutumia mikono yao.

    Soma pia:

  8. Watano wafungwa kwa mauaji ya mgombea urais wa Ecuador

    Mwanaharakati wa kupinga ufisadi na mwandishi wa habari, Fernando Villavicencio aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 2023.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mwanaharakati wa kupinga ufisadi na mwandishi wa habari, Fernando Villavicencio aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 2023.

    Watu watano wanaohusishwa na genge la wahalifu nchini Ecuador wamefungwa kwa mauaji ya mgombea urais Fernando Villavicencio mwaka jana.

    Bw Villavicencio, mjumbe wa bunge la taifa la nchi hiyo na mwanahabari wa zamani, aliuawa kwa kupigwa risasi alipokuwa akitoka kwenye mkutano wa kampeni katika mji mkuu, Quito, Agosti mwaka jana.

    Carlos Angulo, anayedaiwa kuwa kiongozi wa genge la Los Lobos, na Laura Castilla walihukumiwa kifungo cha miaka 34 na miezi minane jela kwa kuongoza mauaji hayo.

    Wanaume wawili na mwanamke mmoja walihukumiwa kifungo cha miaka 12 na mahakama ya Quito kwa kusaidia genge lililofanya shambulizi hilo.

    Waendesha mashtaka walidai kuwa Angulo - anayejulikana sana kama The Invisible - aliongoza shambulizi hilo kutoka katika gereza la Quito ambako anazuiliwa.

    Alikanusha mashtaka hayo, akidai alikuwa akifanywa "mbuzi wa kafara" kwa kuhusishwa na mauaji hayo.

    Castilla Inadaiwa kusambaza silaha, pesa na pikipiki kwa watu waliotekeleza shambulizi hilo.

    Wengine - Erick Ramirez, Victor Flores na Alexandra Chimbo - walishtakiwa kwa kusaidia kikosi hicho kufuatilia mienendo ya Bw Villavicencio.

    Zaidi ya watu 70 walitoa ushahidi wakati wa kesi hiyo, akiwemo shahidi mkuu ambaye alisema genge hilo lilikuwa limepewa zaidi ya dola 200,000 za Kimarekani ili kumuua Bw Villavicencio.

    Mwanaharakati wa kupinga ufisadi, Bw Villavicencio alikuwa mmoja wa wagombea wachache wanaodai uhusiano kati ya uhalifu uliopangwa na maafisa wa serikali nchini Ecuador.

  9. Kenya: Mbunge afukuzwa kwenye hoteli kufuatia 'kauli yake dhidi ya vijana waandamanaji'

    Fara Maalim

    Chanzo cha picha, Kenyan parliament/YouTube

    Mbunge wa Dadaab Farah Maalim amefukuzwa katika hoteli ya Sarovah Whitesands mjini Mombasa pwani ya Kenya kufuatia kauli yenye utata aliyotoa hivi karibuni dhidi ya waandamanaji vijana wa Gen Z.

    Katika video iliyosambaa kwa kasi mitandaoni mbunge huyo anaonekana akisema ‘’waandamanaji walifanya uhaini na laiti angelikuwa rais angeliwangamiza’’

    Vyombo vya Habari vya ndani vinaripoti kuwaMbunge huyo alifika katika hoteli hiyo siku ya Ijumaa.

    Mkurugenzi Mkuu wa Sarovah Hotels and Resorts Kenya Jimi Kariuki alitoa tangazo la kufukuzwa kwa mbunge huyo katika mtandao wa X zamani Twitter baada ya baadhi ya watumiaji wake kuishtuma kwa kumruhusu kukaa hapo.

    Bw. Kariuki asisitiza kuwa hoteli hiyo haikubaliani kwa vyovyote na kauli ya Maalim.

    Katika video hiyo ambayo haijulikani ilirekodiwa lini, Maalim, akizungumza kwa lugha ya Kisomali anaonekana, akisema kuwa kama angekuwa Rais wa Kenya angewaua waandamanaji 5,000 kila siku.

    Tafsiri ya video iliyothibitishwa ilifichua kuwa mbunge huyo alikuwa akiwashutumu Vijana wa Kenya kwa jaribio lao la kuandamana hadi Ikulu wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa fedha wa 2024.

    Mbunge huyo hata hivyo amekanusha madai hayo akisema video hiyo ilifanyiwa ukarabati.

    Soma zaidi:

  10. Mtoto wa tajiri mkubwa wa India afunga ndoa katika harusi ya kifahari

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Sherehe za kifahari za harusi ya mwana wa tajiri mkubwa barani Asia zilianza tena Jumamosi, wageni mashuhuri wakiwemo waigizaji mashuhuri wa Hollywood, viongozi wa biashara duniani na mawaziri wakuu wawili wa zamani wa Uingereza wakihudhuria.

    Anant Ambani, mtoto wa mwenyekiti wa Reliance Industries Mukesh Ambani, alifunga ndoa na Radhika Merchant, binti wa mfanyabiashara wa maduka ya dawa Viren na Shaila Merchant.

    Jumamosi kutakuwa na sherehe maalum ambapo matajiri na maarufu duniani watatoa heshima zao kwa wanandoa hao katika ukumbi wa mkutano ulio na uwezo wa kuchukuwa watu 16,000 unaomilikiwa na muungano wa familia ya Ambani.

    Baadaye kutakuwa na tafrija kubwa na ripoti ambazo hazijathibitishwa zinasema wasanii nyota wa pop Drake, Lana Del Rey na Adele huenda wakatumbuiza.

    Sherehe ya Ijumaa ilikuwa kilele ya cha msururu wa tafrija zilizoandaliwa na familia tangu Machi, ikishirikisha wasanii wa pop wakiwemo Rihanna na Justin Bieber.

    Wengine ni mwanamieleka na mwigizaji wa Marekani John Cena, ambaye alionekana kukumbatiana na kuwapongeza jamaa wa mwenyeji huyo.

    Barabara kuu mjini Mumbai zinafungwa kwa saa kadhaa kwa siku hadi sherehe hizo ziishe Jumatatu.

    Mitandao ya kijamii imesheheni maelezo harusi hiyo, huku watu wakishiriki maelezo ya moja kwa moja kuhusu nyota wa Bollywood na watu mashuhuri wanaowasili

    Lakini utajiri wa ajabu pia umesababisha kuzorota - wakaazi wa jiji wamelalamika kufungwa kwa barabara kumesababisha matatizo ya trafiki yaliyosababishwa na mafuriko ya monsuni, huku wengine wakihoji juu ya maonyesho ya kifahari ya utajiri katika sherehe zinazoonekana kutokuwa na mwisho.

    Maelezo zaidi:

  11. Hujambo na karibu.