Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Rais Ruto awaongoza Wakenya kumuaga Raila Odinga baada ya ghasia

Awali polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waombolezaji waliokusanyika katika uwanja wa Kasarani, baada ya hali ya msongamano na mvutano kuibuka.

Moja kwa moja

Na Asha Juma, Mariam Mjahid & Ambia Hirsi

  1. Tunakomea hapo kwa sasa. Kwaheri.

  2. Watatu waripotiwa kufariki katika mkanyagano wakimuaga Raila Odinga

    Watu watatu wamefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa katika machafuko yaliyozuka katika uwanja wa Kimataifa cha Michezo wa Moi, Kasarani, ambapo maelfu ya Wakenya walikuwa wamekusanyika kuto aheshima zao za mwisho kwa aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Raila Odinga.

    Mkanyagano ulitokea baada ya umati wa watu kufurika kuelekea lango la kuingilia jukwa la Rais, na kuwalazimu maafisa wa usalama kufyatua risasi hewani ili kudhibiti umati mkubwa wa waombolezaji waliokuwa na hamu ya kutoa heshima zao za mwisho.

  3. Wakenya waruhusiwa kuuaga mwili wa Raila Odinga

    Baada ya viongozi wakuu serikalini wakiongozwa na Rais Ruto wakenya wameruhusiwa kuuaga mwili wa kinara wa cha chama cha ODM katika uwanja wa Kasarani.

    Japokuwa umati umejaa, maafisa wa polisi wa Kenya wanaongoza shughuli hiyo ili kurahisisha mchakato mzima wa kuruhusu wakenya na wafuasi wa Raila Odinga kumuenzi na kumuombolez.

    Raia wametakiwa kupanga foleni ili kuutazama mwili wa Odinga na kitengo cha kusimamia shughuli hiyo kuwaomba wawe watulivu.

    Ikiwa ni saa kumi na mbili na dakika kumi na tano jioni saa za Afrika mashariki huenda shughuli hiyo ikaendelea hadi usiku kufuatia wingi wa watu.

    Katika hali hii, tangazo limetolewa kuwa ibada ya wafu ya taifa itafanyika katika uwanja wa Kasarani na sio Uwanja wa Nyayo kama ilivyoratibiwa.

    Awali vurugu zilishuhudiwa uwanjani Kasarani na maafisa wa polisi wa Kenya wakalazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya waombolezaji.

  4. Rais Ruto aongoza shughuli ya kuuaga mwili wa Raila Odinga Kasarani

    Na tukirejea Jijini Nairobi Rais Ruto akiwa ameandamana na familia ya kigogo wa siasa Raila Odinga wanamuomboleza kwa maombi.

    Kigogo huyo ambaye anaonekana akiwa kwa jeneza lililofunguliwa amevalishwa kitambaa kifuoni cha rangi ya machungwa kikiashiria chama alichokiasisi na kukiongoza kwa takariban miaka 20 chama cha Oranga Democratic Party.

    Aliyekuwa rais wa nne wa Kenya Uhuru Kenyatta pia amehudhuria shughuli hiyo inayofanyika katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi.

    Shughuli imeanza kwa maomba kutoka kwa viongozi wa kidini. Haya yanajiri baada ya purukushani kutokea katika uwanja huo kufuatia wafuasi wa Raila kujaa pomoni uwanjani.

    Polisi wa Kenya waliwatawanya waombolezaji na kwasasa hali imekuwa tulivu wakibaki waombolezaji wachache uwanjani.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Tamaduni zaanza baada ya kakake Raila Odinga kuwasili Bondo

    Maandalizi yanaendelea kwa ajili ya shughuli ya kuuaga mwili wa Raila Odinga siku ya Ijumaa katika uwanja wa Jomo Kenyatta, Mamboleo.

    Awali, shughuli hiyo ilikuwa imepangwa kufanyika mjini Kisumu.

    Eneo hilo litakuwa na maeneo maalum ya kuingilia na kutoka ili kudhibiti msongamano.

    Dkt. Oburu Odinga, kaka yake Raila na Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Mazishi, amewasili nyumbani kwa Raila huko Bondo, Kaunti ya Siaya.

    Kwa mujibu wa utaratibu wa jamii ya Wajaluo, ujio wake unaashiria kuwa boma limefunguliwa rasmi kwa waombolezaji na kwamba familia imetangaza rasmi kifo cha ndugu yao.

    Oburu amekutana na wazee wa mtaa, jamaa wa familia, marafiki wa karibu wa Raila, pamoja na viongozi wa kidini ili kuweka misingi ya maandalizi ya mazishi.

    Mazishi yanatarajiwa kufanyika kwa mujibu wa taratibu za Kanisa la Kianglikana.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Polisi wawatawanya waombolezaji kwa vitoa machozi uwanjani Kasarani

    Polisi wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waombolezaji waliokusanyika katika uwanja wa Kasarani, baada ya hali ya msongamano na mvutano kuibuka.

    Hii ni baada ya mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kufikishwa katika Uwanja huo ili umma wampatie heshima ya mwisho.

    Ni idadi hiyo ya waombolezaji ambayo ilijaza uwanja huo wa Kasarani unao uwezo wa kuhimili zaidi ya mashabiki elfu hamsini .

    Kwasasa shughuli nzima ya kuuona mwili wa kigogo huyo wa siasa Raila Oding imesitishwa ghafla hii ni baada ya shughuli hiyo kusitishwa awali katika bunge la kitaifa la Kenya.

    Kwa mujibu wa ripoti kutoka vyombo vya habari nchini humo, baadhi ya waombolezaji walionekana wakirusha mawe eneo la wageni maalum wakitaka kushinikiza kuuona mwili wa Raila uliokuwa umehifadhiwa hapo.

    Ripoti kutoka eneo hilo zinaonesha kuwa kumetokea mkanyagano na watu kadhaa wamejeruhiwa vibaya.

    Katika hali ya kutuliza rabsha maafisa wa polisi walitumia mabomu ya machozi kutawanya waombolezaji ambayo walikuwa wamejaa mlangoni na kupelekea kukimbia kujikinga na hilo.

    Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari nchini humo watu kadhaa wameripotiwa kujeruhiwa katika vurumai hiyo.

  7. Maelfu wafurika uwanja wa Kasarani kumuaga Raila Odinga

    Maelfu ya waombolezaji wanaendelea kumiminika katika uwanja wa kitaifa wa Kasarani kutoa heshima zao za mwisho kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Raila Odinga.

    Viongozi wa matabaka mbali mabi pia wamefika katika uwanja huo kusubiri mwili wa kiongozi huyo wa wa muda mrefu wa upinzani nchini Kenya kufikishwa katika uwanja huo.

    Baadhi ya waombolezaji walioenda kuulaki mwili huo katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta wanatembea kuelekea uwanjani hapo.

    Kwasasa msafafara huo uko kwenye barabara kuu ya Thika kuelekea uwanja wa Kasarani.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Kwanini ratiba ya kuuaga mwili wa Raila Odinga Bungeni ilibadilishwa?

    Machafuko yalizuka nje ya majengo ya Bunge jijini Nairobi wakati waombolezaji walipojaribu kuingia kwa nguvu katika jengo hilo ili kusubiri kuwasili kwa mwili wa Waziri Mkuu wa zamani wa Kenye Raila Odinga.

    Hali iligeuka kuwa ya vurugu wakati maelfu ya wafuasi, waliokuwa wamekusanyika kando ya Barabara ya Bunge, walipovunja vizuizi vya vilivyowekwa kando ya barabara ya City Hall.

    Walipanda juu ya lango, wakiimba nyimbo za ukombozi na kulia kwa majonzi.

    Maafisa wa usalama walijitahidi kuzuia umati uliokuwa ukiendelea kufurika, huku waombolezaji wakijitahidi kufikia lango la kuingia majengo ya bunge.

    Baadhi walionekana wakisukuma lango hilo kwa nia ya kulivunja huku baadhi ya waombolezaji wakipanda kwenye milango na ua wa Bunge wakipeperusha matawi na bendera hewani wakiomba waruhusiwe kuingia.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Oburu Oginga ateuliwa kaimu kiongozi wa chama cha ODM

    Seneta wa Siaya Oburu Oginga ameteuliwa kuwa kaimu kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kufuatia kifo cha mdogo wake Raila Odinga.

    Odinga, kiongozi wa muda mrefu wa chama hicho, alifariki siku ya Jumatano nchini India, ambako alikuwa akipokea matibabu ya ugonjwa ambao haukutajwa.

    Wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Alhamisi asubuhi, chama kilikubaliana kwa kauli moja kwamba Oginga achukue uongozi wa chama hadi kamati hiyo itakapokutana tena kupanga mustakabali wake.

    Rais William Ruto ametangaza siku saba ya maombolezo ya kitaifa, ambapo bendera ya Kenya itapeperushwa nusu mlingoti kwa heshima ya Waziri Mkuu huyo wa zamani.

    Odinga atazikwa siku ya Jumapili huko Bondo, Kaunti ya Siaya magharibi mwa Kenya.

  10. Habari za hivi punde, Shughuli ya kutazama mwili wa Raila Odinga imehamishwa hadi uwanja wa Kasarani

    Shughuli ya kutazama mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Amollo Odinga imehamishwa kutoka maeneo ya Bunge hadi uwanja wa Michezo wa Kimataifa wa Moi, Kasarani, baada ya umati mkubwa wa watu waliokusanyika nje ya majengo ya bunge kufanya iwe vigumu shughuli hiyo kuendelea kama ulivyopangwa.

    Mipango ya awali ya kupeleka mwili wa Raila Odinga kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) hadi makafani ya Lee kwa ajili ya matayarisho ya mwisho kabla ya kupelekwa kutazamwa na umma ilifutiliwa mbali huku kukiwa na ongezeko la machafuko ya umati.

    Maafisa wa kijeshi na waandalizi wa maiti waliokuwa wametumwa katika kituo cha makafani cha Lee kupokea na kuandaa mwili huo badala yake wameagizwa kuelekea Kasarani, ambako shughuli hiyo sasa itafanyika.

    "Umati wa watu haukuweza kudhibitiwa. Waandalizi wa maiti na timu yake wameondoka kwa gari la kijeshi," afisa mkuu wa Hifadhi ya Maiti ya Lee aliwaambia waandishi wa habari.

  11. Tazama: Waombolezaji wakiandamana na mwili wa Raila Odinga

  12. JKIA yafungwa kwa muda baada ya waombolezaji kuvunja ulinzi

    Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini Kenya (KCAA) imesitisha kwa muda shughuli zote katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), kufuatia hali ya taharuki ya kiusalama iliyoibuka baada ya kuwasili kwa mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amolo Odinga.

    Katika taarifa kwa vyombo vya habari, KCAA imesema kundi kubwa la waombolezaji lilivamia maeneo ya uwanja yaliyokuwa yamewekewa vizuizi vya kiusalama, hatua iliyolazimu uwanja kufungwa kwa tahadhari ili kutoa nafasi kwa vikosi vya usalama kurejesha utulivu na kuhakikisha usalama wa wasafiri na wafanyakazi wa uwanja huo.

    Wananchi na wasafiri wametakiwa kuepuka eneo la JKIA kwa sasa, hadi itakapotolewa taarifa mpya.

    KCAA imesema shughuli za kawaida zinatarajiwa kurejelewa pindi tu uwanja utakapothibitishwa kuwa salama, ndani ya takriban saa mbili zijazo.

    Aidha, taarifa rasmi kwa mashirika ya ndege (NOTAM) tayari imetolewa, ikieleza kuhusu usitishaji huo wa muda wa safari za anga.

    KCAA imeomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza na imelitaka taifa la Kenya kuwa na subira wakati huu wa maombolezo ya kitaifa.

  13. Maandalizi ya kuuaga mwili wa Raila bungeni yaendelea

    Maandalizi ya kuuonesha umma mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, yanaendelea katika majengo ya Bunge la taifa nchini Kenya.

    Ulinzi umeimarishwa vikali nje ya Bunge huku waombolezaji wakisubiri kuwasili kwa mwili wa Raila Odinga.

    Hata hivyo, waombolezaji wameonekana kutokuwa na subira huku wakiomba wasiwekewe zuio wapatiwa muda wa kumuomboleza kinara wao.

    Wanakwaya wa bunge la taifa wanatumbuiza ndani ya bunge kwa nyimbo za maombolezi.

    Siku ya Ijumaa ibada ya wafu itafanyika katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi.

  14. Mwili wa Raila unasafirishwa kuelekea makafani ya Lee

    Kufuatia wafuasi wa Raila Odinga kuvuruga shughuli ya mapokezi ya mwili Jkia, muunganisho wa intaneti katika uwanja wa ndege wa JKIA umekatizwa.

    Kwa sasa, jeshi limechukua usukani na hafla iliyokuwa imepangwa kufanyika uwanjani humo imefutwa. Kinachojiri sasa, msafara uliojaa wafuasi wa wa Raila Odinga unafuata mwili huo.

    Rais Ruto pamoja na viongozi walioenda kuchukua mwili wa Odinga India wamekwama katika uwanja wa ndege wa JKIA kutokana na umati kufurika barabarani.

    Soma pia:

  15. Kifo cha Raila: Polisi wazidiwa nguvu uwanja wa ndege wa JKIA

  16. Ulinzi mkali waimarishwa katika makafani ya Lee Jijini Nairobi, wakisubiri mwili wa Odinga

    Taharuki Ikitanda JKIA, serikali imeimarisha ulinzi katika Hifadhi ya Maiti ya Lee jijini Nairobi huku maandalizi yakiendelea kupokea mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amolo Odinga.

    Vikosi vya usalama vikiwemo vya polisi wa kawaida, GSU, na maafisa wa ujasusi vimeonekana wakilinda maeneo ya kuingia na kutoka kwenye hifadhi hiyo, wakijiandaa kwa mapokezi rasmi ya mwili wa kiongozi huyo mashuhuri.

    Mwili wa Raila Odinga utasafirishwa kutoka JKIA hadi makafani ya Lee kabla ya kupelekwa bungeni.

  17. Wafuasi wa Raila wavamia uwanja wa JKIA, polisi wazidiwa nguvu

    Wafuasi wa Raila Odinga wamevamia lango kuu la uwanja wa ndege wa JKIA baada ya kuwazidi nguvu polisi waliokuwa wakilinda eneo hilo.

    Hali ya taharuki imetanda, huku kukiwa na wasiwasi mkubwa juu ya kitakachotokea endapo watapenya na kuingia ndani ya uwanja huo.

    Serikali imeongeza kikosi cha jeshi kwa dharura ili kudhibiti hali kabla haijazidi kuwa mbaya.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Habari za hivi punde, Mwili wa Raila wawasili nchini Kenya kutoka India

    Mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga umewasili katika uwanja wa ndege wa JKIA.

    Mwili huo unapokelewa na Rais William Ruto, aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, familia ya Raila Odinga na maafisa wengine wakuu serikalini.

    Ujumbe kutoka Kenya ulitumwa jana kwenda kuuchukua mwili huo nchini India ambako Raila Odinga alikuwa anapata matibabu.

  19. Ndege iliyobeba mwili wa Raila Odinga ndiyo inayofuatiliwa zaidi duniani

    Ndege iliyobeba wajumbe wa Kenya yenye mwili wa Raila Odinga kutoka India imekuwa ikifuatiliwa zaidi duniani kwenye Flightradar24.

    Mara tu baada ya kupaa saa 6:30 jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi, ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la Kenya KQA202 hadi Mumbai ilikuwa ya pili kwa kufuatiliwa duniani kote kwenye huduma maarufu ya kufuatilia trafiki ya moja kwa moja.

    Kufikia saa sita usiku, ilikuwa imefuatiliwa zaidi duniani kote, ikiwa na zaidi ya watu 7,000 wakiifuatilia.

    Ndege ilifika Mumbai mwendo wa saa 1 asubuhi Alhamisi, Saa za Afrika Mashariki (EAT), na kupaa kuelekea Nairobi saa tis ana nusu Alfajiri saa za Afrika Mashariki. Inatarajiwa kutua uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mwendo wa saa 9:30 asubuhi

    Saa 7 asubuhi, data ya Flightradar24 ilionyesha kuwa ndege ya kurudi KQA203 ilikuwa ikifuatiliwa na zaidi ya watu 5,000.

    KQ imesema kuwa ndege hiyo itabadilishwa jina kuwa RAO001, rejeleo la herufi za jina la Odinga, mara tu itakapofika kwenye anga ya Kenya "kumheshimu na kumheshimu kiongozi wetu aliyeondoka."

    Soma zaidi:

  20. Kifo cha Raila: Wafuasi wakisubiri kuwasili kwa mwili wa Odinga