Mkenya Sawe aweka rekodi ya dunia kwa kukimbia chini ya saa mbili London

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanariadha wa Kenya, Sabastian Sawe, ameandika historia katika mashindano ya riadha ya London Marathon baada ya kuwa mwanariadha wa kwanza kukimbia mbio za ndefu (marathon) chini ya saa mbili katika mashindano rasmi.
Sawe mwenye umri wa miaka 30 alimaliza mbio kwa kutumia muda wa saa 1:59:30, akivunja rekodi ya awali ya marehemu Kelvin Kiptum ya saa 2:00:35 iliyowekwa mwaka 2023.
Awali, Eliud Kipchoge aliwahi kuwa mtu wa kwanza duniani kukimbia chini ya saa mbili mwaka 2019, lakini mafanikio hayo hayakutambuliwa rasmi kwa kuwa hayakufanyika katika mashindano ya kawaida.
Sawe alikuwa kwenye kasi ya rekodi alipofika nusu ya mbio kwa saa 1:00:29, kabla ya kuongeza mwendo katika nusu ya pili na kuweka muda wa kihistoria.
Katika kilomita 10 za mwisho, aliongeza kasi zaidi huku Yomif Kejelcha (Ethiopia) akimfuata kwa karibu. Kejelcha naye aliandika historia kwa kuwa mwanariadha wa pili kukimbia chini ya saa mbili katika mashindano rasmi, akimaliza wa pili kwa saa 1:59:41.
Anayeshikilia rekodi ya dunia ya nusu marathon, Mganda Jacob Kiplimo, alimaliza katika nafasi ya tatu kwa saa 2:00:28, pia akivunja rekodi ya awali ya Kiptum.
Akizungumza na BBC, Sawe alisema: “Ninajisikia vizuri sana. Nina furaha kubwa. Hii ni siku ya kukumbukwa kwangu. Tulianza mbio vizuri, na nilipokaribia kumaliza nilikuwa najisikia imara. Nilipoona muda nilipofika mwisho, nilifurahi sana.”



















