Vita vya Israel na Iran vyaendelea kuongezeka huku Trump akisema zinapaswa 'kufikia makubaliano'
Pande zote mbili zimeanzisha mashambulizi mchana wa leo. Israel imeendeleza mashambulizi huku Iran ikiendelea kurusha makombora dhidi ya Israel.
Muhtasari
- Tazama: Moshi ukifuka kwenye uwanja wa Tajrish Square kaskazini mwa Tehran
- Rais wa Iran aapa 'kujibu vikali' mashambulizi ya Israel
- Israel na Iran 'watafikia makubaliano' - Trump
- Iran italipa 'gharama kubwa sana', Netanyahu asema
- Makombora ya Iran yarushwa kuelekea Israel - IDF
- Uingereza kutuma ndege zaidi za kijeshi Mashariki ya Kati
- Watu saba wafariki katika ajali ya helikopta ya India
- Uingereza yashauri dhidi ya kusafiri Israel huku mashambulizi ya anga yakiendelea
- 'Siwezi tu kuondoka Tehran' - Wairani wazungumza kufuatia maagizo ya IDF ya kuwahamisha
- Lengo la Israel bado halijulikani
- Trump aonya Iran dhidi ya kushambulia Marekani kwa namna yoyote ile
- IDF yaonya Wairani kuondoka katika maeneo karibu na miundombinu ya kijeshi
- Maandamano makubwa dhidi ya Trump yafanyika kote Marekani
- Je, Israel imelenga maeneo gani ya Iran katika mashambulizi ya hivi punde?
- Tumeshambulia maeneo ya miundombinu ya nyuklia ya Iran - IDF
- Iran yaanzisha tena mashumbulizi dhidi ya Israel
Moja kwa moja
Na Asha Juma
Tazama: Moshi mkubwa ukifuka kwenye uwanja wa Tajrish Square kaskazini mwa Tehran
Contains upsetting scenes.Maelezo ya video, Moshi unafuka katika uwanja wa Tajrish wa Tehran Tahadhari: Baadhi ya picha huenda zikakuudhi
BBC imethibitisha picha zinazoonyesha athari ya shambulio la Israel siku ya Jumapili katika kitongoji cha Tehran kaskazini mwa Tajrish Square.
Baada ya shambulizi hilo, video iliyothibitishwa inaonyesha maji yakifurika eneo hilo, huku mabomba ya maji na mifumo ya maji taka ikiwa imepasuka.
Moshi mkubwa pia unaonekana katika mji mkuu wa Iran.
Rais wa Iran aapa 'kujibu vikali' mashambulizi ya Israel

Chanzo cha picha, Reuters
Kabla ya mashambulizi ya hivi punde zaidi ya Iran, rais wa nchi hiyo Massoud Pezeshkian alionya kwamba kama mashambulizi ya Israel yataendelea, Israel inapaswa kutarajia jibu "kali zaidi".
Akizungumza na waziri mkuu wa Iraq, alisema nchi nyingine katika eneo hilo pia zinaweza kuwa hatarini ikiwa mashambulizi yataendelea, na kutoa wito wa "msimamo thabiti" kutoka kwa mataifa ya Kiislamu.
Alisema Iran haikuanzisha mzozo huo lakini ilijibu kwa "ujasiri".
Soma zaidi:
Israel na Iran 'watafikia makubaliano' - Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
"Iran na Israel wanapaswa kufikia makubaliano, na watafikia makubaliano," amesema Rais wa Marekani Donald Trump, akiongeza kuwa yeye ndiye atakayefanikisha hilo.
Katika chapisho la mtandao wa kijamii, Trump anaashiria mivutano ya hivi majuzi kati ya nchi kote ulimwenguni ambayo anasema alisaidia kusitisha.
Marekani imekuwa ikisaidia katika mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya Ukraine na Urusi, pamoja na Israel na Hamas. Vita hivyo vyote bado vinaendelea.
"Vivyo hivyo, tutakuwa na AMANI, hivi karibuni, kati ya Israel na Iran!" Trump amesema.
"Wito kutoka kila upande na mikutano inafanyika kwa sasa. Ninafanya mengi, na sitambuliwi kwa lolote, lakini ni sawa tu, WATU wanajua.
"IFANYE MASHARIKI YA KATI BORA TENA!"
Soma zaidi:
Iran italipa 'gharama kubwa sana', Netanyahu asema

Chanzo cha picha, Avi Ohayon/LPO
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Iran italipa "gharama kubwa sana" kwa vifo vya raia wa Israel.
Akizungumza katika eneo kulikotokea shambulizi la kombora kwenye jengo la makazi huko Bat Yam, Netanyahu anayaita "mauaji ya kukusudia ya raia, wanawake na watoto", na anasema Iran ni "tishio" kwa Israel.
Aliongeza kuwa "nina huzunika" kwa waliouawa, na kwamba "mioyo yetu iko pamoja na familia", huku akiwataka watu kufuata maagizo ya usalama kutoka kwa maafisa.
Habari za hivi punde, Makombora ya Iran yarushwa kuelekea Israel - IDF
Jeshi la Ulinzi la Israel linasema ving'ora vimelia katika maeneo kadhaa kote Israel baada ya kutambua makombora yaliyorushwa kuelekea nchini humo kutoka Iran.
Jeshi la Wanahewa la nchi hiyo "linafanya kazi ya kuzuia na kushambulia pale inapobidi ili kuondoa tishio," linasema.
Inaongeza kuwa watu wanapaswa kuendelea kufuata maagizo kutoka kwa Kamandi ya Masuala ya Ndani ya Nchi.
Wakati huo huo, Televisheni inayomilikiwa na serikali ya Iran imesema 'makombora ya kulipiza kisasi' yamerushwa dhidi ya Israel.
soma zaidi:
Uingereza kutuma ndege zaidi za kijeshi Mashariki ya Kati

Chanzo cha picha, Getty Images
Ndege zaidi za RAF zinatumwa Mashariki ya Kati huku kukiwa na mapigano makali kati ya Israel na Iran, waziri mkuu amesema.
Sir Keir Starmer alisema ndege za kijeshi, ikiwa ni pamoja na ndege za kivita za Typhoons na za kuhamisha mafuta kwa ndege zingine angani, zilikuwa zikitumwa "kwa ajili ya usaidizi wa dharura katika eneo lote".
Alisema hali inaendelea kuwa mbaya kwa haraka na kulikuwa na majadiliano yanayoendelea na washirika, na kuongeza: "Ujumbe wa mara kwa mara unaongezeka."
Uingereza ilitangaza mara ya mwisho kuwa ilipeleka ndege katika eneo hilo mwaka jana, wakati serikali ilisema ndege za Uingereza zimekuwa zikichukua jukumu la kuzuia kutokea kwa mzozo.
Soma zaidi:
Watu saba wafariki katika ajali ya helikopta ya India

Chanzo cha picha, Reuters
Watu saba wamefariki katika ajali ya helikopta katika jimbo la Uttarakhand kaskazini mwa India, maafisa wamesema.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani, ndege hiyo ilikuwa ikitoka Kedarnath kwenye njia maarufu ya Hija ya Wahindu katika milima ya Himalaya.
Inafahamika kuwa timu za uokoaji zilitumwa mara moja na operesheni ya kutafuta miili hiyo imefanywa na polisi wa eneo hilo.
Rubani na mtoto wa miaka miwili ni miongoni mwa waliouawa, Kurugenzi Mkuu wa Usafiri wa Anga ilisema, na kuongeza kuwa Ofisi ya Uchunguzi wa Ajali za Ndege (AAIB) itachunguza ajali hiyo.
Pia unaweza kusoma':
Uingereza yashauri dhidi ya kusafiri Israel huku mashambulizi ya anga yakiendelea

Chanzo cha picha, EPA-EFE/Shutterstock
Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza (FCDO) imeshauri dhidi ya safari zote za kwenda Israel huku kukiwa na ongezeko la shughuli za kijeshi kati yake na Iran.
Ushauri huo unaohusu Israel na maeneo yanayokaliwa ya Palestina, unamaanisha kuwa bima ya usafiri inaweza kubatilishwa ikiwa watu binafsi hawataifuata.
Hili linawadia huku makombora yakirushwa na nchi zote mbili katika siku za hivi karibuni huku anga ya Israel ikisalia kufungwa.
"Hali ina uwezekano wa kuzorota zaidi, kwa haraka na bila ya onyo," FCDO ilisema.
Soma zaidi:
'Siwezi tu kuondoka Tehran' - Wairani wazungumza kufuatia maagizo ya IDF ya kuwahamisha

Chanzo cha picha, Reuters
Raia wa Iran wanasema nini kuhusiana na maagizo yaIDF ya kuhama maeneo yao.
"…Kwa bahati mbaya nimeshaona ujumbe huo" ilikuwa jibu la kwanza kutoka kwa mtu aliyezungumza na BBC, nilipowatumia onyo la IDF linalowataka Wairani wote kuondoka maeneo karibu na maeneo ya kijeshi.
"Tunastahili kujua vipi wapi ni eneo la jeshi na wapi sio?" Miongoni mwa watu waliozungumza na BBC, raia wa Tehran walikuwa na wasiwasi.
"Siwezi tu kuondoka Tehran. Siwezi kuwaacha wazazi wangu wazee ambao hawawezi kusafiri mbali na kwa muda mrefu na kuondoka mjini. Mbali na hilo, lazima niende kazini. Sasa nifanye nini?" raia mwingine wa Tehran alisema.
Iran haijafunga rasmi shughuli zake, ingawa maafisa wa nchi hiyo wamekuwa wakisema mara kwa mara kuwa nchi hiyo iko vitani.
Watumiaji wa mtandao waliita onyo la Israel kuwa "lisilo na uwazi". Baadhi yao wamekuwa wakishirikisha onyo lisilo rasmi lenye kufanana na maagizo ya IDF. Imeandikwa kwa Kiebrania, na inawaambia watu kuondoka "Maeneo Yanayochukuliwa" ili "kuokoa maisha yao".
Soma zaidi:
Lengo la Israel bado halijulikani

Chanzo cha picha, Reuters
Watu wengi nchini Israel wamekubwa na mshtuko asubuhi ya leo baada ya mashambulizi mawili ya makombora ya Iran yaliyoua takriban watu 10, wakiwemo wanawake wanne wa familia moja katika mji wa Tamra, na mvulana wa miaka 10 na msichana wa miaka minane katika mji wa Bat Yam.
Maafisa wa Israel walikuwa wameonya kuwa nchi hiyo itakabiliwa na siku ngumu, huku wakifanya mashambulio yasiyo na kifani dhidi ya Iran.
Israel imedokeza kuwa hii itakuwa tukio la muda mrefu - ambalo linaweza kuchukua wiki, sio siku - lakini lengo lake la mwisho bado haliko wazi.
Jana usiku, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema mashambulizi ambayo tayari yametekelezwa si kitu ikilinganishwa na yale ambayo Iran itashuhudia katika siku zijazo.
Mamlaka za Israel zinasema kuwa ni haki kwa hatua kama hiyo kuchukuliwa kwa sababu Iran ilikuwa inafikia kiwango kibaya cha utengenezaji wa silaha za nyuklia.
Wengi wanahoji hilo, na Iran imekuwa ikisema mara kwa mara kwamba mpango wake wa nyuklia ni kwa madhumuni ya amani, jambo ambalo Israel inaendelea kukataa.
Wakosoaji wa waziri mkuu wanasema hivi ni vita vya kujichagulia, na kwamba diplomasia inasalia kuwa njia pekee ya kutatua suala linalozunguka mpango wa nyuklia wa Iran.
'Asubuhi ya huzuni na ngumu sana' - rais wa Israel
Wakati huo huo, Rais wa Israel Isaac Herzog ameandika kwenye X, "Asubuhi ya huzuni na ngumu sana," alisema wakati nchi hiyo inaamka ikiwa imeshambuliwa na Iran katika maeneo yake ya kati na kaskazini.
"Mashambulizi ya uhalifu ya Iran" yaliwaua na kujeruhi "Wayahudi na Waarabu, raia wa Israel na wahamiaji wapya, wakiwemo watoto na wazee, wanawake na wanaume," Herzog anasema.
Aliongeza: "Niko pamoja na familia wakati huu wa maombolezo mazito na msiba huo mbaya. Ninawaombea majeruhi wapone na kupatikana kwa waliopotea. Tutaomboleza pamoja. Tutashinda pamoja."
Soma zaidi:
Trump aonya Iran dhidi ya kushambulia Marekani kwa namna yoyote ile

Chanzo cha picha, Reuters
Rais Donald Trump amesema Marekani haihusiki katika vita vinavyoendelea kati ya Israel na Iran.
"Marekani haikuwa na uhusiano wowote na shambulio dhidi ya Iran, usiku wa leo," Trump amesema katika chapisho kwenye jukwaa lake la Truth Social platform.
Iran imeionya Marekani na washirika wake kutoisaidia Israel kuzuia mashambulizi yake ya kulipiza kisasi.
"Ikiwa tutashambuliwa kwa namna yoyote na Iran, mutakabiliana na nguvu kamili na nguvu ya wanajeshi wa Marekani katika viwango ambavyo havijawahi kuonekana," Trump ameongeza."Hata hivyo, tunaweza kufikia makubaliano kwa urahisi kati ya Iran na Israel, na kumaliza mzozo huu wa umwagaji damu!!!"
Soma zaidi:
IDF yaonya Wairani kuondoka katika maeneo karibu na miundombinu ya kijeshi

Chanzo cha picha, Getty Images
Vikosi vya Ulinzi vya Israel vimetoa onyo la dharura kwa Wairani, na kuwaambia wakaazi kuondoka katika eneo lililo karibu na vituo vya kijeshi.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, akaunti ya IDF ya lugha ya Kifarsi inasema: "Watu wote ... waliopo ndani au karibu na viwanda vya utengenezaji silaha za kijeshi na taasisi zao zinazowasaidia wanapaswa kuondoka mara moja katika maeneo haya na wasirudi hadi watakapopewa taarifa zaidi.
"Uwepo wako karibu na miundombinu hii unaweka maisha yako hatarini."
Picha zaonyesha matokeo ya mashambulizi ya Iran nchini Israel
Ni saa sita asubuhi nchini Israel na sasa tunaona baadhi ya picha za matokeo ya mashambulio ya Iran.
Maeneo ya makazi yameshambuliwa kaskazini na kati mwa Israel baada ya Iran kurusha makombora ya balestiki kuelekea Israel usiku kucha ili kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya anga ya Israel kwenye maeneo lengwa ya Iran.
Huduma za dharura za kitaifa za Israel zimeripoti kuwa takriban watu 10 wameuawa, huku zaidi ya watu 100 wakijeruhiwa.

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Vikosi vya uokoaji vya Israel kwenye eneo la jengo lililoharibiwa huko Rehovot, katikati mwa Israel 
Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Katikati mwa Israel asubuhi ya leo, kuna marundo ya vifusi baada ya mashambulizi ya Iran kupiga eneo la makazi 
Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Wafanyakazi wa uokoaji wa Israel katika jengo hili ambalo liliachwa wazi kufuatia uharibifu wa mashambulio ya Iran Soma zaidi:
Maandamano makubwa dhidi ya Trump yafanyika kote Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Maandamano dhidi ya Rais Donald Trump yamefanyika katika miji na majiji kote Marekani, yaliyoandaliwa na kundi liitwalo "No Kings".
Maandamano hayo yalifanyika kupinga gwaride la nadra la kijeshi lililoandaliwa na Trump huko Washington DC, na yalitokea baada ya siku kadhaa za maandamano huko Los Angeles na kwingineko juu ya sera zake za uhamiaji.
Wabunge, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wanaharakati walitoa hotuba katika miji ikiwa ni pamoja na New York, Philadelphia na Houston kwa umati wa watu waliokuwa wakipeperusha bendera za Marekani na mabango ya kumkosoa Trump.
Gwaride la kijeshi Jumamosi jioni, ambayo pia ilikuwa siku ya kuzaliwa kwa Trump, liliwekwa wakati wa kusherehekea kumbukumbu ya miaka 250 ya Jeshi la Marekani. Alionya kuwa maandamano yoyote katika gwaride hilo yatakabiliwa na "nguvu kubwa".
Soma zaidi:
Je, Israel imelenga maeneo gani ya Iran katika mashambulizi ya hivi punde?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati Israel na Iran zikianzisha mawimbi mapya ya mashambulizi dhidi ya kila mmoja Jumamosi usiku, haya ndio maeneo ambayo Israel imeshambulia nchini Iran:
Wizara ya mafuta ya Iran imesema kuwa mashambulizi ya Israel yalilenga bohari ya mafuta ya Shahran na tanki la mafuta mjini Tehran. Maeneo yote mawili yalikuwa yanadhibiti, wizara ilisema.
Wizara ya mafuta pia ilisema kuwa maeneo mawili makubwa ya gesi katika jimbo la Bushehr kusini yalishambuliwa na Israel.
Mashambulizi ya Israel pia yalilenga wizara ya ulinzi ya nchi hiyo mjini Tehran, na kuharibu kidogo moja ya majengo ya ofisi, pamoja na Shirika la Ubunifu na Utafiti, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran na IDF.
Maeneo haya yalilengwa kwa sababu ya uhusiano wao na mradi wa silaha za nyuklia wa Iran, IDF ilisema.
Siku ya Jumamosi usiku, IDF ilisema Israel pia ililenga eneo la chinichini magharibi mwa Iran "lililotumika kuhifadhi na kurusha makombora ya kutoka ardhini hadi juu na makombora ya cruise", na kwamba "vigogo waandamizi waliohusika na mradi huo pia wameuawa".
Soma zaidi:
Tumeshambulia maeneo ya miundombinu ya nyuklia ya Iran - IDF

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Eneo la nyuklia ya Isfahan mnamo Aprili 16 Vikosi vya Ulinzi vya Israel vilisema kuwa vimefanya mfululizo wa mashambulizi katika maeneo ya miundombinu mjini Tehran yanayohusiana na mpango wa nyuklia wa Iran.
Jeshi linasema maeneo lengwa ni pamoja na makao makuu ya wizara ya ulinzi ya Iran na Shirika la Ubunifu na Utafiti.
Iliongeza kuwa pia ilishambulia "maeneo zaidi yaliyolengwa" ambayo "yaliendeleza juhudi za serikali ya Iran kupata silaha za nyuklia na ambapo serikali ya Iran ilificha hazina yake ya nyuklia".
Awali, Shirika la Udhibiti wa Nishati ya Atomiki la Iran lilifahamisha Shirika la Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuwa viwango vya mionzi nje ya eneo la nyuklia la Isfahan havijabadilika.
Haya yanajiri baada ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki kuthibitisha kuwa "majengo manne muhimu" yameharibiwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel
Soma zaidi:
Iran yaanzisha tena mashumbulizi dhidi ya Israel

Chanzo cha picha, EPA
Iran imefanya mashumbulizi mengine dhidi ya Israel, huku Televisheni ya taifa ya nchi hiyo ikisema kuwa imeanzisha "mashambulizi makubwa ya ndege zisizo na rubani".
Milipuko mikubwa imesikika katikati mwa Israel.
Video iliyothibitishwa na BBC pia inaonyesha moto ukiwaka karibu na kiwanda cha kusafisha mafuta cha Haifa nchini Israel kufuatia makombora yaliyorushwa kutoka Iran usiku wa kuamkia leo.
Mapema siku hiyo, runinga ya taifa ya Iran ilisema "zaidi ya makombora 100" yalirushwa Israel, yakilenga Haifa na Tel Aviv huku watu watatu wakifariki baada ya Iran kushambulia eneo la Bat Yam, pwani ya Israel, kulingana na huduma za dharura za Israel.
Waliofariki ni mwanamke mwenye umri wa miaka 69, mwanamke mwenye umri wa miaka 80 na mtoto wa miaka 10 wameuawa huko Bat Yam.
BBC haijaweza kuthibitisha hili kwa kujitegemea.
Kitongoji kimoja katika mji wa kaskazini wa Tamra pia kimeshambuliwa, na kuua takriban watu watano, vyombo vya habari vya Israel viliripoti huku hali ikisemekana kuwa bado ni tete.
Zifuatazo ni picha za hivi punde zinazotoka katika jiji la Tamra, katika Wilaya ya Kaskazini ya Israel.

Chanzo cha picha, Sinai Koren

Chanzo cha picha, Sinai Koren

Chanzo cha picha, Sinai Koren
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 15/6/2025. Siku nyingine tena ambayo tutaendelea kukufahamisha kuhusu vita vinavyoendelea kati ya Israel na Iran.

