Buriani Raila Odinga: Shughuli ya kumuaga 'Baba' uwanjani Nyayo yakamilika

Wakenya wanaoishi jijini Nairobi wamepata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho kwa Raila Odinga kwa siku ya pili mfululizo baada ya ibada ya mazishi.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma, Ambia Hirsi & Lizzy Masinga

  1. Mwili wa Raila kulazwa katika makafani ya Lee

    Kamati ya Kitaifa ya Mazishi imebadili ratiba ya mazishi ya marehemu Raila Odinga, ikisema mwili wake hautapelekwa katika makazi yake ya Karen kama ilivyopangwa awali.

    Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), katika taarifa yake Ijumaa jioni, kilisema uamuzi huo ulifanywa kutokana na "sababu ambazo hazingeepukika."

    ODM ilibaini kuwa baada ya kuagwa katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo, mwili wa raila utarejeshwa katika makafani ya Lee ili kuhifadhiwa.

    Mazishi hayo yatafanyika Jumapili katika eneo la Bondo, Kaunti ya Siaya, kuongozwa na Kanisa la Kianglikana la Kenya ambalo Odinga alikuwa akiambuda wakati wa uhai wake.

  2. Shirika la ndege la Kenya Airways laongeza safari za Kisumu kabla ya mazishi ya Raila

    Ndege

    Chanzo cha picha, Kenya Airways

    Shirika la ndege la Kenya Airways limeongeza safari za kuelekea Kisumu mwishoni mwa juma kabla ya hafla ya maziko ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.

    Shirika la ndege la kitaifa lilihusisha hatua hii ili kukidhi mahitaji makubwa ya usafiri kufuatia kuweka maombi ya safari.

    KQ iliahidi kuhakikisha safari kwa urahisi wakati wa wikendi. "Tumeongeza muda wa safari zetu za ndege hadi Kisumu mwishoni mwa juma ili kukidhi mahitaji makubwa ya usafiri," Kenya Airways ilichapisha kwenye X.

  3. Maelfu wajitokeza kwa ajili ya mazishi ya kitaifa ya Raila Odinga

    Maelfu ya waombolezaji walikusanyika katika uwanja wa kitaifa wa Nairobi kwa mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.

    Kifo cha wanasiasa hao wenye umri wa miaka 80 kimeshuhudia idadi kubwa ya waombolezaji wakikusanyika katika miji mbalimbali nchini kote.

    Kutoka mji mkuu wa Nairobi Akisa Wandera anaripoti. Walikuja kwa wingi kuomboleza mtu anayeitwa Baba.

    Huku matawi yakiwa juu kama ishara ya huzuni, utamaduni wa kabila la Waluo ambalo Bw. Odinga alitoka.

    Gari la kijeshi lililobeba jeneza la Odinga lilizunguka uwanja kwa he huku wale waliokusanyika wakilia na kupunga mkono.

    Waziri Mkuu huyo wa zamani alionekana kama mmoja wa watu mashuhuri wa kisiasa nchini Kenya.

    Aligombea kiti cha juu mara 5 lakini hakuwahi kushinda kiti cha urais.

    Badala yake, aliongoza upinzani kwa miongo kadhaa.

    Raila alijulikana kwa juhudi zake za kukuza mazungumzo na upatanishi wa amani katika eneo hilo na kote barani Afrika kama mjumbe wa Umoja wa Afrika.

    Na viongozi wa kigeni, wakiwemo wakuu wa mikoa na wajumbe walikuwa miongoni mwa waliohudhuria mazishi yake.

    Usalama uliimarishwa vikali zaidi leo baada ya umati wa watu kuzidiwa na viongozi siku ya Alhamisi wakati wa hafla ya kutazama miili hiyo.

    Polisi walijibu kwa kufyatua mabomu ya machozi na risasi na kuua takribani watu watatu.

    Kutakuwa na nafasi kwa wale waliokusanyika kutazama mwili wa Bw Odinga kabla ya kuzikwa nyumbani kwake Magharibi mwa Kenya Jumapili.

    Unaweza kusoma;

  4. Mama Ida akumbuka miaka 52 ya ndoa yake na Raila Odinga kwa kihisia

    Mjane wa Raila Odinga Mama Ida Odinga

    Chanzo cha picha, Peter Njoroge/BBC

    Maelezo ya picha, Mjane wa Raila Odinga Mama Ida Odinga

    Mjane wa marehemu Raila Odinga, Mama Ida Odinga, amezungumza kwa mara ya kwanza tangu mume wake alipfariki dunia nchini India.

    Akizungumza katika ibada ya rasmi ya mazishi, Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya, Mama Ida alikumbuka kwa masikitiko miaka 52 ya ndoa yake na Raila akielezea jinsi walivyokutana naye mwanzoni mwa miaka ya 1970 na kumpenda na hatimaye kufunga pingu za maisha mwaka wa 1973.

    Aliongeza kuwa ndoa yao ilistahimili mtihani wa hasa wakati Raila alipozuiliwa kama mfungwa wa kisiasa kwa uasi dhidi ya serikali za wakati huo.

    "Safari yetu ya ndoa haikuwa rahisi. Tulikumbana na pandashuka nyingi, lakini kadiri tulivyoendelea kuishi pamoja, tulijifunza jinsi ya kukabiliana na changaoto zilizojitokeza kwa sababu hakuna mja asiye na udhaifu. Tulijifunza kuzungumza kwa uwazi, kusema ukweli, kusamehe na kusonga mbele."

    Mama Ida pia alielezea jinsi Raila ilivyoipenda nchi yake kwa dhati na kutoa wito kwa Wakenya kudumisha amani kwa heshima ya mume wake.

    ''Raia alichukizwa sana na watu waliofuja mali ya auma na wale wanaojipatia mali kwa nji za kifisadi'', aliongeza kusema.

    Kiongozi huyo wa muda mrefu wa siasa za upinzani atazikwa nyumbani kwake Bondo, magharibi mwa Kenya siku ya Jumapili,

    Unaweza kusoma;

  5. ‘Mfalme amekufa, lakini taji lake liishi milele’: Winnie Odinga amuaga Raila

    .

    Chanzo cha picha, NMG

    Winnie Odinga, bintiye aliyekuwa Waziri Mkuu Marehemu Raila Odinga, amtoa pongezi kwa babake na kumueleza kuwa "Baba na shujaa" ambaye upendo, akili na ujasiri vilibadilisha maisha yake.

    "Sijui nitamkosa nani zaidi - Baba yangu au shujaa wangu," alianza, huku waombolezaji wakisikiliza kwa makini.

    "Mimi ndiye msichana mwenye bahati zaidi duniani kwa sababu ulikuwa Baba yangu.

    Ni binadamu wengine watatu tu walikuwa na bahati kama mimi Fidel, Rozzy na Junior.

    "Winnie alimuelezea baba yake kama mwanga mwepesi “usiobadilika na binadamu wa kina” ambaye uwepo wake uliamsha usikivu popote alipoenda.

    "Kwa ulimwengu, ulijulikana kwa majina mengi," alisema. "Hata ulimpa karibu kila mtu uliyekutana naye jina la utani pia.

    Lakini kwangu, ulikuwa tu Baba

    "Alikumbuka kwa moyo mkunjufu maisha yao ya nyumbani, ambayo aliyataja kuwa “mahali pa kufanyia majaribio vitendawili,” ambapo Raila angewapa watoto wake changamoto na mafumbo na yaliwafungua akili .

    “Nyumba yetu ilijaa maswali ambayo yalitujaribu kwa njia nzuri… wakati mwingine,” alisema huku akitabasamu kidogo. Winnie alisema alicheka aliposikia kuhusu nia ya mwisho ya babake kutaka kuzikwa ndani ya saa 72 baada ya kifo chake.

  6. Buriani Raila Odinga: Raila Junior amuomboleza baba yake

    .

    Chanzo cha picha, Mitandao ya Kijamii

    'Baba nataka kukuhakikishia kuwa nitatunza familia yetu…. Asante kwa kunipa jina lako…'

    "Nafahamu kwa hakika kwamba kaka yangu Fidel hayupo tena, mimi ndio mwanamume wa familia. Baba, nataka kukuhakikishia kwamba nitatunza familia yetu - Mama, Rosie, Winnie - na familia kubwa ya kisiasa ambayo umeiacha ... asante kwa kunipa jina lako na kamwe hukuwahi kunipa uzito wa jina hilo." - Raila Odinga Jr.

  7. Ruto: Nitakuwa mwaminifu kwa kile tulichokubaliana na Raila

    .

    Chanzo cha picha, Ikulu ya Rias

    Maelezo ya picha, Rais William Ruto

    Rais William Ruto ametoa salamu za kibinafsi na za kihisia kwa marehemu Raila Amolo Odinga, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya na kiongozi wa upinzani, na kuthibitisha kwamba atakuwa mwaminifu kwa kile walichokubaliana kuhusu mustakabali wa Kenya.

    Katika salamu zake za rambirambi Ruto ameomboleza kifo cha Raila kwa maneno ya moyoni ambayo yalikubali safari yao tata ya kisiasa, nyakati za umoja, na maono ya pamoja ya mustakabali wa Kenya.

    Katika ujumbe wake ulioandikwa katika kitabu cha rambirambi akiwa Bungeni, alimtaja kama "ari ya demokrasia yetu" na mzalendo ambaye kujitolea kwake kutatengeneza hatima ya taifa milele.

    "Baba Agwambo, umekuwa ari ya demokrasia yetu kupitia dhoruba na usaliti wa jela, lakini ulikuwa mwaminifu kwa wito wa juu zaidi wa kuwa mzalendo wa Kenya," Ruto aliandika.

    Raila Odinga alifariki Oktoba 15, 2025 akiwa na umri wa miaka 80 alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Ayurvedic huko Kerala, India.

    Kifo chake kimesababisha kipindi cha siku saba za maombolezo ya kitaifa, huku bendera zikipepea nusu mlingoti na mazishi ya serikali yakiandaliwa.

    Unaweza kusoma;

  8. Buriani Raila Odinga: Mlinzi wa aliyekuwa Waziri Mkuu ashindwa kujizuia

    .

    Chanzo cha picha, Screen Grab

    Maelezo ya picha, Maurice

    Hali ya hisia kali ilijitokeza Bungeni mapema leo wakati Maurice Ogeta, mlinzi wa muda mrefu wa marehemu Raila Odinga, alipobubujikwa na machozi wakati wa kutazamwa kwa mwili wa Waziri Mkuu huyo wa zamani.

    Kulingana na gazeti la The Star Daily, akiwa amevalia suti ya buluu na miwani ya jua, Ogeta alionekana kutetemeka wakatoi alipokuwa akiingia ukumbini kuuaga mwili wa marehemu.

    Akiwa ameshikiliwa na Seneta wa Narok Ledama Olekina, alimkumbatia Rais William Ruto katika muda uliovuka mipaka ya kisiasa.

    Midomo yake ilikuwa ikitetemeka na hatua zake hazikuwa thabiti alipokuwa akielekea kwenye kiti chake.

    Mara baada ya kuketi, Ogeta alionekana akilia, akifuta machozi yake, huzuni yake ikirejelea huzuni iliyokumba taifa zima.

  9. Buriani Odinga: Wakenya wazidiwa na hisia katika ibada ya kumuaga Raila

    .

    Wakenya wazidiwa na hisia baada ya kuwasili kwa mwili wa Raila Odinga katika uwanja wa Nyayo kwa ajili ya kuagwa.

    Uwanja ulijaa vilio na huzuni huku wengine wakiwa tayari kuufuata mwili wakati unazungushwa kwenye uwanja. Hata hivyo, ulizinzi umeimarishwa

    Kwa Picha, tazama Wakenya wakimuomboleza Raila Odinga.

    .

    Chanzo cha picha, BB

    .
    .
  10. Habari za hivi punde, Buriani Raila Odinga: Mwili wa 'Baba' wawasili uwanjani Nyayo kwa ibada ya wafu na kuagwa

    .

    Chanzo cha picha, State House

    Mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga umewasili Nyayo kwa Mazishi ya Kitaifa.

    Msafara wake ulivuka barabara kuu ya Uhuru hadi uwanjani mwendo wa 9:46m.

    Gari la maiti lilipoingia polepole, waombolezaji waliangua vilio, kabla ya kuzunguka katka uwanja huo.

    Mwili huo ulikuwa umeondoka kwenye Majengo ya Bunge kuelekea Uwanja wa Taifa wa Nyayo, kuashiria awamu inayofuata katika mazishi ya serikali.

    Msafara huo ulianza muda mfupi baada ya saa 9:20 asubuhi, huku wanajeshi wakiwa wamebeba jeneza lililokuwa na bendera nje ya lango kuu la Bunge.

    Mlinzi wa sherehe za heshima alisimama makini huku gari la kubebea maiti, lililozungukwa na maafisa waliovalia sare na wanafamilia, likipitia barabara za Nairobi.

    Umati wa watu ulijipanga njiani, wengi wakipeperusha bendera, vijiti, na kushikilia picha za marehemu.

    Wengine walilia hadharani, wengine waliimba nyimbo ambazo zilirejelea mapambano ya miongo kadhaa ya Raila ya demokrasia na mageuzi.

    Baadhi ya waombolezaji walipeperusha bendera na vijiti, alama za maombolezo, huku wengine wakiwa na mabango na picha za kiongozi huyo aliyepewa jina Baba kwa upendo.

  11. Habari za hivi punde, Mke wa Raila Odinga, Ida Odinga awasili uwanjani Nyayo

    Mke wa Raila Odinga Ida Odinga amewasili katika uwanja wa Kimataifa wa Nyayo.

    Tayari msafara wa kijeshi ulibeba mwili wa Raila Odinga uko njiani kuelekea uwanjani Nyayo.

    Ibada ya kumuaga Raila kuanza muda mfupi ujao.

  12. Habari za hivi punde, Rais Ruto na Viongozi wakuu Serikalini wawasili uwanjani Nyayo

    Rais William Ruto anaongoza maelfu ya Wakenya katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi katika ibada ya wafu ya marehemu Raila Odinga.

    Aidha aliyekuwa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta , naibu rais Kithure Kindiki , jaji Mkuu Martha Koome ni miongoni mwa viongozi mbalimbali ikiwemo wale wa kimataifa wanaohudhuria hafla hiyo.

    Baada ya ibada hiyo Wakenya waliohudhuria hafla hiyo watapata fursa ya kuuaga mwili wa marehemu

  13. Mwili wa Raila Odinga wapelekwa katika uwanja wa michezo wa Nyayo

    Mwili wa Raila Odinga sasa umetoka kwenye maeneo ya Bunge kuelekea kwenye uwanja wa michezo wa Nyayo kwa ibada ya kitaifa.

    Mwili huo umebebwa na gari la kijeshi na unalindwa na wanajeshi.

    Wabunge wameshawasili katika uwanja huo.

    Muda mfupi ujao ibada ya kitaifa ya kumuaga inatarajiwa kuanza.

  14. Habari za hivi punde, Buriani Raila Odinga: Aliyekuwa waziri Mkuu aagwa Bungeni

    .

    Chanzo cha picha, Bunge

    Mwili wa Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, umeagwa bungeni.

    Wabunge na viongozi wengine serikalini wamepata fursa ya kumuaga.

    Na sasa jicho limeelekezwa kwa ibada ya kitaifa inayofanyika uwanja wa Nyayo.

  15. Habari za hivi punde, Rais William Ruto awasili bungeni

    Rais William Ruto amewasili katika majengo ya bunge kuungana na viongozi wengine kumuaga Raila Odinga.

    Ratiba ya kumuaga Raila inaendelea.

    Mwili wa Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, ulipelekwa bungeni kabla ya ibada ya kitaifinayofanyika leo kwenye uwanja wa Nyayo.

  16. Buriani Baba: Tazama Wakenya wakimsubiri Raila uwanjani Nyayo

    Maelezo ya video, Buriani Baba: Wakenya waendelea kuwasili uwanjani Nyayo

    Wakenya wameshawasili katika uwanja wa michezo wa Nyanyo kwa ajili ya ibada ya kitaifa ya kumuaga aliyekuwa Waziri Mkuu nchini Kenya Raila Odinga.

    Usalama umeimarishwa nje na ndani ya uwanja wa Nyayo na kwa sasa wafuasi wa Raila wanaimba na kucheza.

    Kulingana na ratiba, wananchi wanatakiwa kuwa wameketi kufikia saa mbili asubuhi.

    Mwili wa Raila Odinga tayari umeshatolewa katika Makafani la Lee na umefikishwa kwenye majengo ya bunge kwa ajili ya wabunge na viongozi wengine kumuaga.

    Inatarajiwa kuwa baada ya bunge, moja kwa moja utapelekwa katika uwanja wa nyayo kwa ibada ya kitaifa ya kumuaga.

    Raila Odinga aliaga dunia alipokuwa anapata matibabu nchini India.

    Maelezo ya video, Buriani Baba: Wakenya wawasili uwanjani Nyayo
  17. Habari za hivi punde, Buriani Baba: Wabunge kumuaga Raila Odinga katika majengo ya Bunge

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ratiba ya mazishi ya Raila Odinga imebadilika kwa mara nyengine hii leo baada ya mwili wake kupelekwa hadi bunge ili kuagwa na viongozi hao.

    Mwili huo uliotarajiwa kusafirishwa moja kwa moja hadi katika uwanja wa Nyayo, ulipelekwa bungeni ili kuwapa fursa wabunge kuuaga kabla ya kupelekwa katika uwanja wa Nyayo.

    Hapo Jana ratiba hiyo ilibadilika kwa mara ya kwanza baada ya waombolezaji kuupokea mwili wake katika uwanja wa ndege wa JKIA na kutembea nao moja kwa moja hadi Kasarani ili kuagwa.

    Hii ilikuwa kinyume na ratiba hiyo ambapo ulitarajiwa kuchukuliwa kutoka JKIA , kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee kabla ya kupelekwa bungeni ili kuagwa.

    Mwili huo sasa utaagwa bungeni ambapo rais atawaongoza viongozi tofauti kuuaga mwili huo.

    Inasemekana kuwa wabunge waliombwa kuwa maeneo ya bunge mapema leo kwa ajili ya kumuaga.

    Baadaye mwili huo utapelekwa katika uwanja wa Nyayo ambapo ibada ya mazishi itafanyika kuanzia saa 9 asubuhi kabla ya Wakenya kupewa fursa nyengine kuuaga

    Soma zaidi:

  18. Mahakama yakataa ombi la kupinga mazishi ya Raila ndani ya saa 72

    .

    Chanzo cha picha, The Judiciary

    Mahakama kuu imekataa kusitisha agizo la kuzikwa kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Amolo Odinga ndani ya saa 72.

    Jaji Chacha Mwita, hapo jana Alhamisi, Oktoba 16, 2025, alitoa uamuzi kuwa mlalamishi hakuonyesha uhitaji wa haraka kuhalalisha uingiliaji kati mazishi hayo haraka.

    Katika uamuzi wake, Jaji huyo alibainisha kuwa mshitaki hakuonyesha kuwa taratibu za maziko zilikuwa zikifanywa kinyume na matakwa ya marehemu.

    "Baada ya kuzingatia maombi hayo, sijaridhishwa na uhitaji wa suala hili. Mshitaki hajaonyesha kuwa mchakato unafanyika kinyume na matakwa ya marehemu ili kuwezesha mahakama hii kuchukua hatua za kutoa amri za usitishaji shughuli za maziko," alisema.

    Haya yanajiri kufuatia ombi lililowasilishwa na Michael Onyango Otieno, ambaye alitaka kutangazwa kuwa kuzikwa kwa Raila Odinga ndani ya saa 72 kunakiuka Katiba.

    Mlalamishi alisema kuwa mazishi yaliyoharakishwa yanakiuka Kifungu cha 44 cha Katiba, ambacho kinamhakikishia kila mtu haki ya kushiriki katika maisha ya kitamaduni ya jumuiya yao.

  19. Uchimbaji wa kaburi la Raila Odinga unaendelea

    .

    Chanzo cha picha, The Star

    Uchimbaji wa kaburi la Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga katika makazi ya kijijini ya Bondo unaendelea.

    Waziri mkuu wa zamani atazikwa Jumapili nyumbani kwake mjini Bondo.

    Kupitia vyombo vya habari vya ndani, trekta ilionekana ikichimba kaburi pale ambapo Raila Odinga atazikwa.

    Shughuli hii ilianza baada ya Seneta wa Siaya Oburu Odinga ambaye ni kaka mkubwa wa Raila Odinga kufunguwa rasmi nyumba ya Bondo ya Raila kwa waombolezaji, kuwajulisha rasmi wanakijiji kuwa wamepatwa na msiba na kuonyesha sehemu ambayo kaka yake atazikwa katika eneo la makaburi ya kwao kama sehemu ya desturi ya jamii la luo.

    Awali, kulikuwa na tetesi kuwa Raila Odinga alitaka kuzikwa karibu na mama yake Mary Juma lakini ndugu yake Oburu Odinga, ameonyesha sehemu ambayo ndugu yake atazikwa ambako ni kando ya baba yake, Jaramogi Oginga Odinga, kwenye eneo la makuburi ya kwao la Ang’oka Jaramogi.

    Soma zaidi:

  20. Buriani Baba: Mwili wa Raila kuagwa kwa siku ya pili Nairobi baada ya ibada ya mazishi

    .

    Wakenya hususan wale wanaoishi Mjini Nairobi hii leo siku ya Ijumaa watapata fursa ya kuuaga mwili wa Raila Odinga kwa siku ya pili mfululizo katika uwanja wa Nyanyo Jijini Nairobi.

    Hatua hii inajiri baada ya Serikali Kutangaza siku kuu ya Raila siku ya ijumaa ili kutoa fursa ya kuuaga mwili wa marehemu.

    Kulingana na ratiba ya mazishi iliotolewa na serikali, Kutakuwa na na ibada ya mazishi mapema leo kabla ya mwili wake kuagwa.

    Naibu rais Kithure Kindiki anayeongoza ratiba ya mazishi ya kiongozi huyo maarufu nchini Kenya amesema kwamba Wageni ikiwemo viongozi wa mataifa jirani Afrika na wale wa kimataifa wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo.

    Amewasihi Wakenya kuwasili katika uwanja huo mapema zaidi kuanzia saa tatu asubuhi ili kuzuia ghasia kama zile zilizoshuhudiwa katika uwanja wa kasarani.

    Siku ya Alhamisi watu watatu wlifariki na wengine kadhaa kujeruhiwa katika machafuko yaliyozuka katika uwanja wa Kimataifa,

    Kasarani, ambapo maelfu ya Wakenya walikuwa wamekusanyika kutoa heshima zao za mwisho

    Soma zaidi:

    Pia unaweza kusoma: