Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Jeshi la Sudan lajiondoa kwenye mazungumzo, vyanzo vyaeleza

Maafisa wa Sudan wanasema kuwa jeshi limejiondoa kwenye mazungumzo ya kusitisha mapigano na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), wakilishutumu kundi hilo kwa kukiuka mara kwa mara makubaliano ya hapo awali ya kusitisha mapigano.

Moja kwa moja

  1. Wakili wa Uganda auawa kwa risasi alipokuwa akiwasili nyumbani kwake

    Wakili wa Uganda ameuawa kwa kupigwa risasi katikati mwa mkoa wa Wakiso, kaskazini-magharibi mwa mji mkuu Kampala.

    Polisi wameviambia vyombo vya habari kuwa Ronald Mukisa, 45, aliuawa Jumanne usiku alipokuwa akiwasili nyumbani.

    Naibu msemaji wa polisi wa Kampala Luke Owoyesigyire alisema majirani walisikia milio ya risasi wakati Bw Muskia, ambaye anafanya kazi katika mji mkuu, alipokuwa akiegesha gari lake mwendo wa saa saa tano.

    Mtu asiyejulikana alimpiga risasi mara kadhaa na kisha kukimbia haraka eneo la tukio, na kutoroka kwa pikipiki iliyokuwa ikisubiri, alisema.

    Polisi wameomba yeyote aliye na taarifa muhimu kuhusiana na tukio hili kusaidia maafisa katika uchunguzi.

  2. Air New Zealand yaanza kuwapima abiria kabla ya safari

    Shirika za safari za ndege la Air New Zealand linawapima abiria kabla ya kupanda ndege za kimataifa, kama sehemu ya uchunguzi wa kubainisha uzito wa wastani wa abiria.

    Uzito huo utarekodiwa bila kujulikana katika hifadhidata lakini hautaonekana kwa wafanyikazi wa ndege au abiria wengine, kampuni hiyo ilisema.

    Air New Zealand ilisema kujua uzito wa wastani wa abiria kutaboresha ufanisi wa mafuta katika siku zijazo.

    Kushiriki katika uchunguzi huo ni kwa hiari, shirika hilo la ndege liliongeza.

    "Sasa kwa kuwa safari za kimataifa zimerejea na zinaendelea, ni wakati wa mashirika ya kimataifa kupima uzani wa abiria ," shirika hilo la ndege lilisema katika taarifa kwa vyombo vya habari.

  3. Al Pacino: Nyota wa Godfather anatarajia mtoto wa nne akiwa na umri wa miaka 83

    Mwigizaji Al Pacino anatarajia mtoto wake wa nne akiwa na umri wa miaka 83, wawakilishi wake wamethibitisha.

    Nyota huyo wa 'Godfather' ametangaza kwamba mpenzi wake Noor Alfallah mwenye umri wa miaka 29 ana ujauzito wa miezi minane.

    Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Marekani Pacino na Alfallah wamekuwa pamoja tangu janga la Covid-19.

    Pacino tayari ana watoto watatu - wawili na Beverly D'Angelo na mmoja na Jan Tarrant.

    Katika kazi yake iliyochukua zaidi ya miongo mitano, Pacino ameonekana katika filamu za The Irishman, The Godfather, Scarface na Scent of a Woman, akishinda tuzo ya Oscar kwa mwigizaji bora kwa filamu ya mwisho.

    Alfallah anafanya kazi katika tasnia ya filamu na ametoa filamu kama vile Billy Knight, Little Death na Brosa Nostra.

    Hapo awali alichumbiana na mwanamuziki Mick Jagger mnamo 2017.

    Mwigizaji mwenza wa Pacino kutoka The Godfather Part II, Robert de Niro,hivi majuzi alitangaza kuwa amemkaribisha mtoto wake wa saba akiwa na umri wa miaka 79.

  4. Jaji nchini Marekani aamuru ndugu wa waathiriwa wa ajali ya ndege ya Ethiopia walipwe fidia

    Jaji wa Marekani ameamua kwamba jamaa za waliofariki wakati ndege ya Boeing 737 Max ilipoanguka Ethiopia wanaweza kuomba fidia kwa maumivu na mateso ya waathiriwa.

    Jji Jorge Alonso huko Illinois alisema mahakama inaweza kuhitimisha kuwa abiria walikuwa wanajua walikuwa wakiumia hadi kufa.

    Boeing walikuwa wamejitetea kuwa waliokuwa kwenye ndege ya Ethiopian Airlines walifariki papo hapo.

    Ndege hiyo ilianguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka Addis Ababa miaka minne iliyopita.

    Uamuzi wa hivi punde ulitolewa kabla ya kesi nchini Marekani kubainisha ni kiasi gani familia za waathiriwa zinapaswa kupokea.

    Miaka mitatu iliyopita, Boeing ilikiri kuhusika na ajali hiyo na nyingine nchini Indonesia.

  5. Mwanamke aliyemshutumu Biden kwa unyanyasaji wa kijinsia anatafuta uraia wa Urusi

    Mwanamke wa Marekani ambaye alimshutumu Rais wa Marekani Joe Biden kwa kumnyanyasa kingono amesafiri kwa ndege hadi Moscow na anatafuta uraia wa Urusi.

    Akizungumza na chombo cha habari cha serikali ya Urusi, Tara Reade, 59, alisema anajisikia salama nchini humo na alitaka kubaki huko.

    Bi Reade alidai Bw Biden alimshambulia alipokuwa akifanya kazi katika ofisi yake ya bunge mwaka wa 1993.

    Alikanusha vikali madai yake."Haijawahi kutokea, haijawahi kutokea," alisema.

    Bi Reade alifanya kazi kama msaidizi wa Bw Biden alipokuwa seneta wa Delaware.

    Aligonga vichwa vya habari mnamo 2020 wakati kampeni yake ya urais ilipokuwa ikiendelea, alipodai kwamba alimshambulia huko Capitol Hill alipokuwa na umri wa miaka 29.

    Alimshutumu kwa kumsukuma ukutani na kuweka mikono yake chini ya shati na sketi yake.

    "Niliposhuka kwenye ndege huko Moscow, kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu sana nilijihisi salama, na nilihisi kusikika na kuheshimiwa," gazeti la The Guardian linamnukuu Bi Reade akisema wakati wa mahojiano na Sputnik.

    Alisema aliondoka Marekani baada ya mwanasiasa wa chama cha Republican kumwambia kuwa maisha yake yalikuwa hatarini.

    "[Ningependa] kutuma maombi ya uraia wa Urusi, kutoka kwa rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin... Ninaahidi kuwa raia mwema," Bi Reade alisema, na kuongeza kuwa anatumai kutunza uraia wake wa Marekani. .

    Bi Reade alikuwa mmoja wa wanawake kadhaa waliojitokeza mnamo 2019 na 2020 kumshutumu Bw Biden kwa kuguswa vibaya, kukumbatiana au kupigwa busu.Alisema alikuwa amewasilisha malalamiko, ingawa hakuna rekodi yoyote iliyopatikana na haijulikani ikiwa madai yake yalichunguzwa rasmi.

    Msemaji wa Bw Biden alisema anaamini kuwa wanawake "wana haki ya kusikilizwa" lakini tukio hilo linalodaiwa "halikutokea kabisa".

  6. UN yarefusha vikwazo kwa Sudan Kusini kwa mwaka mmoja,

    Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeongeza tena vikwazo vya silaha na vikwazo vilivyoiwekea Sudan Kusini kwa mwaka mmoja zaidi, ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kwa mali na marufuku ya kusafiri kwa baadhi ya watu.

    Baraza hilo lilipiga kura siku ya Jumanne kwa kura 10 za ndio na wajumbe watano hawakupiga kura. Iliagiza nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa kuzuia usambazaji wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja, uuzaji au uhamisho wa silaha kwa Sudan Kusini.

    Vikwazo vya silaha viliongezwa hadi Mei mwaka ujao, huku baraza hilo likielezea wasiwasi wake juu ya "kuendelea kuongezeka kwa ghasia na kurefusha mzozo wa kisiasa, usalama, kiuchumi na kibinadamu katika maeneo mengi ya nchi".

    Nchi zilizosusia ni China, Urusi, Ghana, Gabon na Msumbiji. Balozi Akuei Bona Malwal kutoka Sudan Kusini alipinga kura hiyo, akisema "ilifanyika kwa nia mbaya".

    Licha ya makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka 2018, ghasia zinaendelea na hadi kufikia Aprili mwaka huu watu milioni 2.3 nchini Sudan Kusini waliwekwa kwenye orodha ya wakimbizi wa ndani.

  7. Afisa wa India atozwa faini ya dola 640 kwa kutiririsha bwawa kutafuta simu

    Afisa mmoja wa India aliyegonga vichwa vya habari kwa kutiririsha bwawa ili kuchukua simu yake ametozwa faini na serikali.

    Rajesh Vishwas ameagizwa kulipa rupia 53,092 ( sawa na dola 642) kwa kuvuta mamilioni ya lita za maji kutoka kwa bwawa hilo bila kupata kibali kutoka kwa mamlaka.

    Alikuwa amedondosha simu hilo alipokuwa akijipiga selfie na kudai kuwa ilihitaji kutolewa kwani ilikuwa na data muhimi za serikali.

    Lakini ameshutumiwa kwa kutumia nafasi yake vibaya.

    Mkaguzi huyo wa chakula alidondosha simu yake ya Samsung, yenye thamani ya rupia 100,000, kwenye Bwawa la Kherkatta lililopo jimbo la Chhattisgarh katika kati mwa India wiki iliyopita.

    Baada ya wapiga mbizi wa eneo hilo kukosa simu, alilipia pampu ya dizeli kuletwa, Bw Vishwas alisema kwenye taarifa ya video iliyonukuliwa kwenye vyombo vya habari.

    Pampu hiyo ilivuta maji ya bwawa hilo kwa kwa siku kadhaa, ikitoa maelfu ya lita za maji, lakini wakati simu ilipopatikana, ilikuwa haiwezi tena kufanya kazi.

    Wakati huo, Bw Vishwas alikuwa ameambia vyombo vya habari kwamba alikuwa na ruhusa kutoka kwa afisa kupunguza "maji kidogo kwenye mfereji wa karibu", akiongeza kwamba afisa huyo alisema "kwa kweli kungenufaisha wakulima ambao wangekuwa na maji zaidi".

  8. Jeshi la Sudan lajiondoa kwenye mazungumzo, vyanzo vyaeleza

    Maafisa wa Sudan wanasema kuwa jeshi limesitisha mazungumzo ya kusitisha mapigano na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), wakilishutumu kundi hilo kwa kukiuka mara kwa mara makubaliano ya hapo awali ya kusitisha mapigano.

    Jeshi lilichukua uamuzi huo "kwa sababu waasi hawajawahi kutekeleza hata moja ya vipengee vya usitishaji vita wa muda mfupi ambao ulihitaji kujiondoa katika hospitali na majengo ya makazi, na mara kwa mara wamekiuka makubaliano", afisa wa serikali, akizungumza kwa sharti la kutokujulikana, ameliambia shirika la habari la AFP.

    Chanzo cha kidiplomasia cha Sudan pia kililifahamisha shirika la habari la Reuters kuhusu kujiondoa kwa jeshi katika mazungumzo tete ya kusitisha mapigano, ambayo yanalenga kuwezesha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu.

    Jeshi na RSF halijatoa maoni yao hadharani kuhusu hatua hiyo ya jeshi.

    Siku ya Jumatatu, wapatanishi kutoka Marekani na Saudi Arabia walisema jeshi na RSF walikubaliana kuongeza muda wa usitishaji mapigano kwa ajili ya kutoa fursa ya msaada wa kibinadamu kwa siku tano.

    Hata hivyo, mapigano yaliendelea katika maeneo kadhaa ya Sudan, ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Khartoum, ambapo RSF ilisema ngome yake imeshambuliwa.

    Jeshi lilisema kuwa limezuia shambulio la RSF kwenye mji wa kati wa El-Obeid.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mapigano Sudan: Hakuna mazungumzo mpaka mashambulio ya mabomu yakome, Hemedti aiambia BBC
  9. Mashambulio ya Ukraine yawauwa watano, huku droni zikizua moto kwenye kiwanda cha kusafisha mafuta - maafisa wa Urusi

    Mashambulio ya makombora ya Ukraine yamewauwa watu watano katika kijiji kimoja katika jimbo la Luhansk mashariki mwa Ukraine, maafisa waliowekwa na Moscow wamenukuliwa na shirika la habari la Reuters wakisema Jumatano.

    Shambulio la ndege isiyo na rubani lilisababisha moto kwenye kiwanda cha kusafisha mafuta kusini mwa Urusi.

    Mizinga ya Ukraine pia iliupiga mji wa Urusi uliopo karibu na mpaka kwa mara ya tatu katika wiki moja, na kuharibu majengo na magari na kujeruhi watu wanne, maafisa wa Urusi walisema.

    Siku moja baada ya Kremlin kuishutumu Kyiv kwa kutuma ndege zisizo na rubani kushambulia majengo mjini Moscow, maafisa waliowekwa na Urusi katika jimbo la Luhansk wamethibitisha kuwa watu watano walmeuawa na wengine 19 kujeruhiwa

    Shambulio hilo lilitokea wakati vikosi vya Ukraine vilipotumia vifaa vya kurushia roketi zilizotengenezwa na Marekani vya HIMARS kushambulia shamba moja katika kijiji cha Karpaty usiku usiku kucha.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  10. Makubaliano ya nishati ya nyuklia kati ya Urusi na Burundi yafikia hatua ya mwisho – Lavrov

    Nchi hizo mbili zilitia saini mkataba wa ramani ya nishati ya nyuklia mwezi Novemba mwaka jana

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov anasema maandalizi ya makubaliano baina ya serikali kati ya Moscow na Burundi kuhusu nishati ya nyuklia ya kiraia yako katika hatua yake ya mwisho.

    Bw Lavrov aliyasema hayo Jumanne baada ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi Albert Shingiro mjini Bujumbura, shirika la habari la serikali la Urusi la Tass limeripoti.

    "Mwongozo wa nishati ya nyuklia tayari umetiwa saini kati ya Rosatom [Shirika la Nishati la Jimbo la Urusi] na washirika wake wa Burundi," Bw Lavrov alisema.

    Alisema pande zote mbili zimejitolea kushirikiana katika matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.

    Nchi hizo mbili zilitia saini mkataba wa rmwongozo wa nishati ya nyuklia mwezi Novemba mwaka jana, ambapo Urusi ilikubali kuisaidia Burundi kuanzisha mitambo ya atomiki.

    Kabla ya kuondoka kwake kuelekea Msumbiji, Bw Lavrov alikutana na Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye kwa mazungumzo zaidi ya pande mbili.

    Ziara hiyo ni sehemu ya ziara ya Bw Lavrov katika mataifa ya Afrika, kufuatia safari yake ya hivi karibuni nchini Kenya na kabla ya kuwasili Afrika Kusini.

    Bw Shingiro alikariri kuwa Burundi haitaunga mkono upande wowote katika vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.

  11. Vita vya Ukraine: Kanuni tano za usalama wa nyuklia zatolewa na IAEA na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

    Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mkuu wa shirika la Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Mkuu wa IAEA Rafael Grossi ameainisha kanuni hizo kuwa ni pmaoja na :

    • Kusiwe na mashambulizi ya aina yoyote kwenye Kiwanda cha Nguvu za Nyuklia cha Zaporozhye.
    • ZNPP isitumike kama hifadhi au msingi wa mizinga, silaha nzito, risasi au wafanyakazi.
    • Ugavi wa umeme wa ZNPP lazima usiwe hatarini.
    • Miundo, mifumo na vipengele vyote muhimu kwa ajili ya uendeshaji salama na wa kutegemewa wa ZNPP lazima vilindwe dhidi ya mashambulizi au vitendo vya hujuma.
    • Hakuna hatua yoyote inayopaswa kuchukuliwa ambayo inadhoofisha kanuni hizi.

    Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi alieleza kwamba aliratibu orodha hii wakati wa mikutano mingi na uongozi wa Ukraine na Urusi baada ya ziara yake ya ZNPP mwezi Septemba, 2022.

    "Ninaomba pande zote mbili zifuate kanuni hizi," Grossi aliziambia Urusi na Ukraine katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  12. Pep atwaa tuzo nyingine ya kocha bora wa mwaka wa LMA

    Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amechaguliwa kuwa kocha bora wa mwaka na Chama cha makocha wa Ligi. Hii ni mara ya tatu kwa Guardiola kutwaa Tuzo hiyo inayoitwa 'Sir Alex Ferguson Award', iinayopigiwa kura na mameneja ama makocha wa madaraja yote ya ligi nchini England.

    Mhispania huyo, 52, pia alishinda tuzo ya kocha ama meneja bora wa mwaka wa ligi kuu England baada ya timu yake kunyakua taji la tatu mfululizo na la tano katika misimu sita. Kocha wa Chelsea, Emma Hayes alishinda kwa upande wa Ligi ya Wanawake ya Super League. Ilikuwa tuzo yake ya nne mfululizo na ya sita kwa jumla.

    Guardiola amekuwa meneja wa tatu kushinda tuzo tatu au zaidi za kocha bora wa mwaka wa LMA, sawa na David Moyes, lakini bado yuko ya kocha wa zamani wa Manchester United Sir Alex Ferguson mwenye tuzo 5.

    City watamenyana na Manchester United katika fainali ya Kombe la FA Jumamosi. Ushindi katika mechi hiyo unaweza kuipa nafasi ya City kushinda makombe matatu msimu huu watakapomalizana na Inter Milan katika fainali ya Ligi ya Mabingwa mnamo Juni 10, 2023.

  13. Kasri linalouzwa kwa pauni 30,000 linalohitaji ukarabati wa pauni milioni 12

    The Brough Lodge Trust inatumai "mjasiriamali mhisani" atawezesha mipango yao kutimia.

    Kasri iliyopo Shetland huko Uskochilinauzwa kwa pauni 30,000 tu - lakini mnunuzi yeyote atahitaji pia pesa ya ziada ya £12m, kulimiliki.

    Wanaotafutya nyumba wanaweza kununua kasri la Brough Lodge lililopo kwenye kisiwa cha Fetlar kwa bei ya chini ya bei ya gorofa huko Glasgow.

    Nyumba hii ya kifahari iliyojengwa miaka 200 iliyopita imejengwa katika eneo la hekari 40 za ardhi, ikiwa na bustani na kuta

    Lakini wawekezaji wameonywa kwamba watahitaji kutumia pesa nyingi ili kufidia gharama ya ukarabati unaohitaji.

    The Brough Lodge Trust imetoa wito kwa "mjasiriamali mhisani" kuchukua mipango ya kubadilisha kasri hili kuwa makazi ya kiwango cha kimataifa.

    Mapendekezo yao ni muwekezaji alitunze vyema kasri hilo , ambalo lilianza kutumika mwaka 1820, na pia liongezewe vyumba 24 vya kulała na mgahawa.

  14. Wanaharakati wataka matumizi ya mafuta ya ndege ya wanyama yadhibitiwe

    Wanaharakati wa mazingira wanataka kudhibitiwa kwa matumizi ya mafuta ya ndege yatokanayo kwa wanayama.

    Ripoti mpya inasema mahitaji makubwa ya mafuta hayo si endelevu.

    Inatarajiwa kuwa mafuta hayo kutoka kwa wanyama yakaongezeka mara tatu katika kipindi cha miaka kumi ijayo wakati ambapo kampuni za ndege zinajaribu kupunguza viwango vya gesi ya carbon.

    Wanaharakati wa mazingira wanasema hakuna nguruwe,ngombe na kuku wa kutosha kuweza kuzalisha nishati hiyo.

  15. Mapigano kusitishwa kwa siku 5 zaidi Sudan,

    Pande zinazozozana nchini Sudan zimekubali kuongeza muda wa usitishaji mapigano kwa siku tano zaidi, baada ya upatanishi wa Marekani na Saudi Arabia.

    Nchi hizo mbili kwa pamoja zilisema kwamba ingawa usitishaji wa mapigano haujazingatiwa kikamilifu uliruhusu kupelekwa kwa misaada katika maeneo ya Sudan.

    Ingawa jeshi la Sudan na hasimu wake, kikosi cha msaada wa maraka (RSF), wameahidi kusitisha mashambulizi ya anga, mizinga na mapigano ya mitaani, hakuna upande unaozingatia kikamilifu ahadi hiyo ya kusitisha mapigano.

    Hakuna njia za kibinadamu ambazo zimetengwa hadi sasa kusaidia kuingiza misaada na kuokoa watu, huku misaada ikifika katika maeneo machache ndani ya mji mkuu Khartoum.

    Kuongezwa kwa siku tano kwa mapatano hayo kutatoa muda wa kusaidia watu kwa misaada ya kibidamu, kurejesha huduma muhimu, na majadiliano ya uwezekano wa kusitishwa kwa mapigano kwa muda mrefu.

    Mapambano makali ya madaraka yaliyoanza katikati ya mwezi wa Aprili yameugeuza mji wa Khartoum na maeneo mengine ya mijini kuwa uwanja wa vita na hospitali kuwa vituo vya kijeshi.

    Mamia ya watu wameuawa na karibu watu milioni 1.4 wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

  16. Korea Kaskazini yathibitisha satelaiti yake ya kwanza ya kijajusi ya anga za juu imeanguka baharini

    Korea Kaskazini imethibitisha satelaiti yake ya kwanza ya anga ya juu, imeanguka baharini.

    Pyongyang ilitangaza mapema kuwa inapanga kurusha satelaiti yake ifikapo Juni 11 ili kufuatilia shughuli za kijeshi za Marekani.

    Sasa inasema itajaribu kutuma nyingine ya pili haraka iwezekanavyo.

    Hatua huiyo ilizua taharuki katika mji mkuu wa Korea Kusini Seoul, huku nchini Japan onyo lilitolewa kwa wakaazi wa Okinawa, kusini mwa nchi hiyo.

    Kulikuwa na fujo na mkanganyiko mjini Seoul wakati watu wakiamshwa kwa sauti ya king'ora na ujumbe wa dharura ukiwaambia wajiandae kuondoka – lakini dakika 20 baadae waliambiwa ujumbe huo ulitumwa kimakosa.

    Kumekuwa na mvutano baina ya nchi hizo mbili kwa miaka 70, na kilichotokea sasa kinaweza kuharibu imani ya watu katika mfumo wa tahadhari.

    Korea Kaskazini ni tishio kwa Korea Kusini, na ikiwa kuna tahadhari katika siku zijazo swali moja linaloulizwa ni kama watu watalichukulia kwa uzito, au kupuuzwa.

    Jeshi la Korea Kusini lilisema huenda roketi hiyo ilipasuka angani au kuanguka baada ya kutoweka kwenye rada mapema. Ilitoa picha za mabaki yaliyopatikana baharini.

    Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida alisema Korea Kaskazini inaonekana kurusha kombora la balistiki na kwamba serikali ilikuwa ikifuatilia maelezo hayo.

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia alilaani hatua hiyo, akisema matumizi yoyote ya teknolojia ya makombora ya balistiki ni "kinyume" na maazimio husika ya baraza la usalama.

    Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un amebainisha utengenezaji huo wa satelaiti za kijeshi kama sehemu muhimu ya ulinzi wa nchi yake.