Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Urusi yaimarisha ulinzi baada ya daraja muhimu linalounganisha nchi hiyo na Ukraine kulipuliwa

Daraja hilo ndiyo kivuko pekee kati ya rasi ya Crimea na Urusi

Moja kwa moja

  1. Tumefika tamati ya habari zetu za moja kwa moja leo, tukutane kesho majaliwa

  2. Ligi kuu EPL: Arsenal 'aikamatiki', yaichapa Liverpool na kurejea kileleni

    Mabao ya Gabriel Martinelli na Bukayo Saka aliyefunga mawili, yametosha kuipa Arsenal ushindi wa 3-2 nyumbani dhidi ya Liverpool.

    Mabao ya Liverpool yamefungwa na Darwin Nunez na Roberto Firmino.

    Kwa kiwango kikubwa, mchezo huo ulitawaliwa na Arsenal hasa dakika 20 za kwanza na sehemu kubwa ya kipindi cha pili.

    Ushindi huo umeirejesha Arsenal kileleni ikiwa na alama 24, tofauti ya alama 14 dhidi ya Liverpool inayoshika nafasi ya 10 kwenye mpaka sasa.

    Manchester City, iliyokuwa kileleni kwa masaa machache baada ya kushinda 4-0 jana dhidi ya Southampton, iko katika nafasi ya pili, kwa tofauti ya alama moja dhidi ya Arsenal.

    Liverpool anayeonekana kusuasua zaidi msimu huu, inakwenda kukutana na kibarua kingine kizito wiki ijayo, itakapocheza na City, huku vijana wa Mikel Arteta, Arsenal ikisafiri kucheza na Leeds United.

  3. Ruto 'achagiza' miaka 60 ya Uhuru Uganda, atoa wito wa ushirikiano zaidi

    Rais wa Kenya, William Ruto ni miongoni mwa viongozi kutoka mataifa mbalimbali walioungana na mamilioni ya raia wa Uganda wanaodhimisha miaka 60 ya Uhuru wa taifa hilo leo.

    Wiki iliyopita rais wa Uganda, Yoweri Museveni aliwaomba radhi wakenya kutokana na machapisho ya mtoto wake mkubwa, Jenerali Muhoozi Kainerugaba aliyeandika kupitia mtandao wa twitter kwamba jeshi lake lingeweza ‘kuiteka Nairobi baada ya wiki mbili tu’.

    Machapisho hayo yaliibua hasira miongoni mwa wakenya.

    Akizungumza leo katika sherehe za maadhimisho hayo zilizofanyika katika uwanja wa Kololo na kupambwa na gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama vya Uganda, Ruto amehimiza ushirikiano zaidi wa nchi za Afrika Mashariki, akimtaka Rais Museveni kuongoza hilo.

    'Tunaweza kutengeneza ustawi na kuunganisha fursa katika nchi zetu kwa faida ya watu milioni 300 Afrika mashariki na watu bilioni 1.2 katika bara la Afrika', alisema Ruto.

    Kabla ya kumkaribisha Ruto, Rais Museveni katika hotuba yake ya kurasa 30, na yeye alihimiza umuhimu wa kuunganisha nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, ili kujenga uchumi imara.

    Alisisitiza pia kuendelea na ujenzi wa bomba la mafuta linalounganisha Uganda na Tanzania, licha ya Umoja wa Ulaya kukosoa ujenzi wake kwa sababu za mazingira.

    Mbali na Ruto, viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo za miaka 60 ya uhuru wa Uganda ni pamoja na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit, Rais wa Somalia Hamad Sheikh Muhamud, Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi aliyemuwakilisha Rais Samia Suluhu wa Tanzania na wawakilishi wengine kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo DRC, Mali na Rwanda.

    Tangu ipate uhuru wake mwaka 1962 kutoka kwa wakoloni, Uganda imetawaliwa na viongozi kadhaa, lakini Museveni peke yake akitawala kwa miaka 36, akikosolewa zaidi kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyotajwa kukithiri nchini humo. Mara nyingi amekuwa akikanusha tuhuma hizo.

  4. Iker Casillas aomba msamaha kuhusu kujihusiaha na mapenzi ya jinsia moja

    Akaunti ya gwiji wa zamani wa Real Madrid na Hispania Iker Casillas iliandika kuhusu kwamba anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

    Hata hivyo muda mfupi uliopita, Iker amejitokeza na kuandika tena kwamba, akaunti yake ilidukuliwa, lakini sasa imerejea sawa akiomba msamaha kwa mashabiki na jamii ya wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

    'ilidukuliwa akaunti. Bahati nzuri kila kitu kiko sawa sasa. Naomba radhi kwa washabiki wangu, na pia jamii ya wapenzi wa jinsia moja', aliandika Iker kwa lugha ya kihispania.

    Kabla ya kuomba msamaha akaunti ya kipa huyo wa zamani aliyeshinda Kombe la Dunia akiwa na Hispania iliandika kwenye Twitter: "Natumai unaheshimu: mimi najihusisha na mapenzi ya jinsia moja."

    Ujumbe huo ulifuntwa ndani ya saa moja.

    Haya yanajitokeza ikiwa ni mwaka mmoja tangu atengane na mtangazaji na mwanamitindo mstaafu Sara Carbonero mnamo Machi 2021 lakini akasema wataendelea kuwa karibu ili kuendeleza "kazi nzuri" ya kulea watoto wao wawili.

    Baada ya akaunti hiyo kutangaza hivyo Casillas akaepokea ujumbe mwingi wa kumuunga mkono, akiwemo mchezaji mwenzake wa zamani wa Hispania Carles Puyol ambaye aliandika: "Ni wakati wa kusimulia hadithi yetu, Iker." Akiweka na emoji ya moyo na busu. Ujumbe ambao pia umeibua mjadala.

    Ingawa baadaye Puyol alikosolewa ikionekana kufanya mzaha.

    Mbali na Hispania, Real Madrid amewahi kuichezea Porto kwa misimu mitano mpaka mwaka 2020 alipotundika daruga kucheza soka la ushindani la kiwango cha juu.

  5. Kituo cha serikali cha runinga Iran chadukuliwa huku maandamano yakiendelea

    Kituo cha runinga cha serikali nchini Iran kilidukuliwa wakati wa taarifa ya habari siku ya Jumamosi.

    Taarifa hiyo ya habari ilikatizwa na maandamano ya kumpinga kiongozi huyo wa nchi.

    Kinyago kilionekana kwenye runinga, na kufuatiwa na picha ya Kiongozi Mkuu Ali Khamenei ikiwa na miali ya moto karibu naye.

    Kundi hilo lilijiita "Adalat Ali", au Haki ya Ali.

    Hii inakuja baada ya takriban watu watatu kuuawa kwa kupigwa risasi wakati waandamanaji walipokabiliana na vikosi vya usalama katika machafuko mapya kuhusu kifo cha Mahsa Amini.

    Bi Amini alishikiliwa mjini Tehran na polisi wa maadili kwa madai ya kutofunika nywele zake ipasavyo. Mkurd wa Irani mwenye umri wa miaka 22 alifa akiwa kizuizini mnamo Septemba 16, siku tatu baada ya kukamatwa kwake.

    Kifo chake kimezua wimbi la maandamano ambayo hayajawahi kushuhudiwa kote nchini humo.

    Taarifa ya habari ya TV ya Jumamosi saa saa tatu ilikatizwa na picha zilizojumuisha kiongozi mkuu wa Iran akiwa ameilenga shabaha kichwani kuelekea picha za Bi Amini na wanawake wengine watatu waliouawa katika maandamano ya hivi majuzi.

    Moja ya maelezo yalisomeka "jiunge nasi na uinuke", huku nyingine ikisema "damu ya vijana wetu inachuruzika kwenye makucha yako".

    Tangazo hilo la udukuzi lilidumu sekunde chache tu kabla ya kukatwa.

  6. 17 wauawa Zaporizhzhia, Urusi ikiendelea kuishambulia Ukraine

    Takriban watu 17 wameuawa katika mashambulizi ya makombora ya Urusi katika mji wa kusini-mashariki wa Zaporizhzhia, wizara ya ulinzi ya Ukraine imesema.

    Makumi wengine walijeruhiwa, na majengo kadhaa ya makazi yameharibiwa.

    Mji huo uko chini ya udhibiti wa Ukraine, lakini ni sehemu ya eneo ambalo Urusi ilidai kulitwaa mwezi uliopita.

    Zaporizhzhia imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara katika wiki za hivi karibuni, huku Urusi ikishambulia miji kadhaa baada ya kushindwa kudhibiti eneo la kusini na kaskazini-mashariki mwa Ukraine.

    Sehemu za eneo la Zaporizhzhia, kua kinu kikubwa cha nguvu za nyuklia - ambacho kiko karibu maili 30 (kilomita 52) kutoka mjini - na limekuwa chini ya udhibiti wa Urusi tangu mapema katika uvamizi huo.

    Gavana wa eneo la hilo, Oleksandr Starukh, alisema makombora 12 ya Urusi yaliharibu sehemu kubwa ya jengo la gorofa tisa, na kusambaratisha majengo mengine matano ya makazi.

  7. Rais Gambia aingilia kati vifo vya watoto 69 kutokana na dawa ya kikohozi

    Rais wa Gambia Adama Barrow ameiagiza Wizara ya Afya ya nchi hiyo kupitia upya sheria husika na kuweka miongozo ya usalama ili kudhibiti uingizaji wa dawa zisizo na viwango nchini humo.

    Katika hotuba yake kwa taifa kupitia televisheni, Bwana Barrow alielezea masikitiko yake kuhusu vifo vya watoto 66 vilivyotokana na dawa za kikohozi kutoka India zinazodaiwa kuingizwa kinyemela nchini humo. Vifo vimeongeza sasa na kufikia 69.

    Alisema kuwa nchi yake inapanga kuanzisha maabara ya kitaifa ya kudhibiti ubora wa dawa na usalama wa chakula.

    Mamlaka nchini Gambia na India zinachunguza tukio hilo.

    Shirika la afya WHO ilibaini dawa nne za kikohozi zinazotengenezwa na kampuni ya Maiden Pharmaceuticals ya India kuwa zinaweza kuhusishwa na athari na vifo vya watoto hao 66.

    Ikatoa tahadhari ya kimataifa, na kuzitaka nchi kuondoa mara moja bidhaa hiyo.

  8. Urusi yaimarisha ulinzi Crimea baada ya daraja muhimu linalounganisha nchi hiyo na Ukraine kulipuliwa

    Urusi imeimarisha usalama kwenye daraja lake pekee la kuelekea eneo la Crimea baada ya mlipuko mkubwa wa jumamosi kuharibu sehemu kadhaa za daraja hilo.

    Rais Vladimir Putin ameamuru Idara ya Usalama ya nchi hiyo (FSB) kusimamia daraja hilo muhimu kuelekea eneo la Crimea linalokaliwa kwa mabavu na Urusi.

    Daraja hilo lilikuwa sehemu ya Ukraine, pia ni ishara muhimu ya unyakuzi wa Crimea kutoka Ukraine uliofanywa na Urusi mwaka 2014.

    Taarifa zinasema mlipuko huo uliua watu watatu, wachunguzi wa Urusi walisema.

    Maafisa walisema kazi ya kurekebisha sehemu zilizoharibiwa itaanza mara moja.

    Naibu waziri mkuu wa Urusi aliamuru sehemu zilizoharibiwa za daraja hilo ziondolewe, na kuongeza wapiga mbizi wataanza kuchunguza uharibifu uliotokea chini ya mkondo wa maji kuanzia Jumapili asubuhi, mashirika ya habari ya Urusi yanaripoti.

    Inaelezwa na vyombo vya habari vya Urusi kwambadaraja hilo ni "ujenzi wa karne", na limekuwa muhimu kwa Urusi kwa usafirishaji wa zana za kijeshi, risasi na wanajeshi kuelekea kusini mwa Ukraine.

    Lakini picha mpya za satelaiti zilizotolewa Jumamosi zilionyesha moshi na moto karibu na maeneo yaliyoporomoka ya daraja hilo l;enye urefu wa kilomita 19 (maili 12), ambalo lilifunguliwa kwa sherehe kubwa miaka minne muda mfupi baada ya Urusi kulitwaa eneo la Crimea kutoka Ukraine.