Kimbunga jobo: Serikali ya Zanzibar yasitisha shughuli zote za baharini kama tahadhari

Kimbunga

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesitisha shughuli zote za baharini kuanzia Jumamosi ikiwa ni sehemu ya tahadhari ya kutokea kwa kimbunga kilichopewa jina ''jobo''

Shughuli za baharini zilizofungwa ni pamoja na uvuvi, safari za meli na vyombo vyengine vya usafiri baharini, kuanzia na kulingana na tangazo la tahadhari shughuli hizo zimefungwa '' kuanzia Aprili 24, 2021 saa tatu (3:00) asubuhi, mpaka itakapotolewa taarifa nyengine na mamlaka zinazohusika, ikiwa ni sehemu ya tahadhari ya kutokea kimbunga kilichopewa jina la 'Jobo'.

Uvuvi ni mojawapo ya shughuli za baharini zilizositishwa Zanzibar kufuatia tahadhari ya kimbunga ''jobo'
Maelezo ya picha, Uvuvi ni mojawapo ya shughuli za baharini zilizositishwa Zanzibar kufuatia tahadhari ya kimbunga ''jobo''

Wakati huo huo taarifa ya Mamlaka ya Hali ya hewa nchini Tanzania kuhusu mwenendo wa kimbunga jobo katika Ppwani ya Tanzania imewashauri kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Kulingana na Mamlaka hiyo mwenendo wa kimbunga "Jobo" kilichopo bahari ya Hindi kwa sasa kipo umbali wa kilomita 200 mashariki mwa kisiwa cha Mafia.

Imesema kimbunga hicho kimepungua nguvu kwa haraka baada ya kuingia katika mazingira yenye mzunguko wa upepo kinzani. ''Hivyo, "Jobo" kwa sasa ni kimbunga hafifu'', imesema Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania katika taarifa yake.

Uwepo wa kimbunga hafifu baharini, unatarajiwa kusababisha mawimbi makubwa.

Chanzo cha picha, TOMMY TRENCHARD

Maelezo ya picha, Uwepo wa kimbunga hafifu baharini, unatarajiwa kusababisha mawimbi makubwa

Kimbunga jobo kinachosafiri kwa kasi ya kilometa 18 kwa saa baharini, kinatarajiwa kusababisha vipindi vya mvuakubwa katika maeneo machache hususan ya ukanda wa Pwani kadri kinavyosogea nchi kavu kwa siku ya leo tarehe 24 na kesho 25 mwezi Aprili, 2021

Uwepo wa kimbunga hafifu baharini, unatarajiwa kusababisha mawimbi makubwa.

Maeneo yanayotarajiwa kupata athari za moja kwa moja ni pamoja na mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikiwemo kisiwa cha Mafia), Dar es Salaam pamoja na kisiwa cha Unguja.