Watanzania waombwa kujitolea viungo vya maiti kusaidia katika upandikizaji kwa wagonjwa

organ

Chanzo cha picha, BSIP

Maelezo ya picha, Kuna uhaba wa viungo vinvayoweza kuokoa maisha kama figo, ini au kioo cha jicho vinavyoweza kuokoa maisha ya wagonjwa baada ya kupandikizwa

Je umewahi kusikia kwamba baadhi ya viungo vya maiti vinaweza kuwa msaada katika matibabu ya wagonjwa wengine walio hai?

Kampeni mpya imeanzishwa nchini Tanzania kuhamasisha na kutoa wito kwa wananchi kuruhusu baadhi ya viungo vya ndugu zao waliofariki kuchukuliwa ili visaidie wengine walio na uhitaji wa viungo hivyo.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Mawezi mkoani Kilimanjaro, kaskazini mwa Tanzania, Dr.Japhet Joseph ameielezea BBC kwamba jitihada zimeidhinishwa kujaribu kuwaeleimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujitolea kuridhia kutumiwa viungo hivyo kuwasaidia wagonjwa nchini.

Anafafanua kuwa kuna madaktari waliobobea katika fani mbalimbali ambao wanaweza kufanya upandikizaji wa viungo vinvayoweza kuokoa maisha. Lakini tatizo linakuja wakati viungo vyenyewe kama figo, au ini au kioo cha jicho havipatikani.

Ni kutokana na uhaba huu ndio kampeni imeidhinishwa kuelimisha wananchi kusudi angalau waweze kusaidia kuibadili hali na kuwasaidia wengine.

Dkt Joseph anafananisha mchakato huo na utoaji damu ambao kampeni na uhamasishaji mkubwa umefanyika na kuwafanya watu kuchangia damu 'kwa ajili ya kuweza kuwasaidia ndugu ambao watakuwa na matatizo'.

Kwa namna hiyo anaeleza kuwa wananchi watapokuwa wamepata elimu hiyo, ina maana kwamba na kwa mfano wa mataifa mengine kama Ulaya, mtu atatakiwa kusaini fomu ya kuridhia na kusema 'iwapo mtu anafariki kiungo changu kitumike kumsaidia mwingine.'

organ

Chanzo cha picha, BSIP

Maelezo ya picha, Daktari anasema kuna muda ambao viungo bado viko hai baada ya mtu roho kutoka na vinaweza kutolewa na kuhifadhiwa

Lakini utoaji wa viungo unafanyika kwa muongozo upi?

Baada ya mtu kufariki kuna muda ambao viungo bado viko hai baada ya mtu roho kutoka.

na ni katika muda huo ambapo vikiwahi kutolewa na vinaweza kusaidia watu wengine walio hai katika upasuaji wa upandikizaji wa viungo kama inavyofanyika katika matiafa ya Ulaya na hata India.

Anasema ni wachache mno katika bara la Afrika walio na uelewa wa kuridhia namna hiyo na kujitolea viungo kama inavyokuwa kwa utoaji damu.

hali ilivyo kwa sasa ni kwamba hakuna malipo yanayotolewa kwa utoaji huo wa viungo. Anaeleza tena ni kama uchangiaji damu ambao hufanyika kwa uhisani tu wa mtu binfasi.

daktari anafafanua kuwa kuna viungo maalum vinavyolengwa.

Mfano Moyo , figo au kioo cha jicho ndio viunge vyenye uhitaji mkubwana hutumika katika upandikizaji kuwasaidia wagonjwa.

Maelezo ya video, Upandikizaji wa visikizi kwa watoto waliozaliwa na tatizo la usikivu.

Je wananchi wanaridhia utoaji viungo vyao?

Katika eneo la makumbusho mjini Dar Es salaam, BBC imezungumza na baadhi ya vijana akiwemo mmoja aliyeelezea wasiwasi wa uaminifu wa utaratibu huu.

'Shida kubwa ni uaminifu, kwamba je nikitoa kwa ajili ya kumsaidia mtu mwingine, je wale watu wanapokea vile viungo vitawanufaisha? Mimi naweza kusema nimetoa msaada wao wanafanya 'business''.

Mwingine ametilia shaka ufanisi wa mchakato huo kutokana na sababu za kidini:

'Kwanza imani za watu za dini, kuna mwingine anaweza kukubaliana na hilo suala, kuna mwingine imani yake haimruhusu kufanya hivyo vitu. Maana ataona... ninatoa viungo vya ndugu yangu kuwapa watu wakafaidike, tayari nimeshamkosea Mungu. Kwanini nauza viungo?'

Kijana mmoja amegusia pia suala la heshima kwa marehemu :

'Kwangu haiwezekani, ni kama kudhalilisha utu wa mtu. Ijapokuwa keshakufa, lakini marehemu bado ana heshima zake'.