Mafuriko: Watu robo milioni waachwa bila makao Kenya

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limesema watu 100 wamefariki kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini humo.

Idadi ya watu ambao wameachwa bila makao imekaribia robo milioni huku shirika hilo likitoa tahadhari kwamba huenda kukazuka magonjwa yanayoenezwa na maji machafu.

Maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni Tana River na Garissa.

"Idadi ya walioathirika inaendelea kupanda. Sidhani kama kuna mtu aliyetarajia kwamba mambo yatakuwa mabaya hivi, na tunasema kwamba hatua lazima zichukuliwe kwa haraka," Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Abbas Gullet alisema wakati wa mahojiano na runinga ya kibinafsi ya NTV.

Bw Gullet ametoa wito kwa mafuriko kutangazwa kuwa janga la taifa.

Amesema maeneo ya pwani na kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ndiyo yaliyoathiriwa zaidi ambapo kaya takriban 42,180 zimeachwa bila makao.

"Tunazungumzia Wakenya takriban 242,000 ambao wameachwa bila makao kote nchini. Wengi wa walioathiriwa wanapatikana katika majimbo ya Tana River na Garissa. Kuna pia Kilifi, Wajir, Isiolo, Nyeri, na kuna Kajiado sasa, na sasa tumesikia Kilifi idadi inaongezeka," Gullet alisema.

Katibu mkuu huyo alisema kuna wasiwasi kwamba huenda kukazuka mlipuko wa magonjwa yanayotokana na maji machafu, ikiwemo kipindupindu.

Wengi wa waliopoteza makao wanaishi katika kambi za muda kwenye mahema ambapo hali ya usafi ni duni.

"Afya ni suala kuu kwa sasa pamoja na makazi. Lakini tunaziomba serikali za majimbo na serikali kuu ya taifa kujitokeza na kusaidia," alisema Bw Gullet.

Mwishoni mwa wiki, wanajeshi wakisaidiana na polisi walishiriki juhudi za uokoaji za kuwahamisha watu waliokuwa wameathiriwa na mafuriko na kuwasafirisha hadi maeneo salama.

Mataifa jirani ya Tanzania na Somalia pia yameathiriwa na mafuriko.