Rwanda yapiga marufuku simu za Galaxy Note 7

Note 7

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Baadhi ya wadadisi wa bidhaa walikuwa awali wamesema Note 7 ilikuwa simu bora zaidi ya Android kuwahi kuundwa

Serikali ya Rwanda imepiga marufuku uagizaji na usambazaji wa simu za kampuni ya Samsung aina ya Galaxy Note 7.

Hatua hiyo imechukuliwa siku chache baada ya kampuni hiyo ya Korea Kusini kutangaza kwamba ingesitisha uundaji na uuzaji wa simu hizo kutokana na kuongezeka kwa visa vya simu hizo kushika moto au kulipuka.

Mamlaka inayosimamia bidhaa na matumizi nchini Rwanda imesema hatua ya kupiga marufuku simu hizo imechukuliwa kwa sababu za kiusalama.

"Kwa sababu za kiusalama, wateja ambao huenda walinunua simu hizi binafsi nje ya nchi wanatakiwa kuzizima na kuzirejesha eneo walizozinunua," imesema taarifa ya kaimu mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo Meja Jenerali Patrick Nyirishema.

Baadhi ya simu za Note 7 zimekuwa zikishika moto

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baadhi ya simu za Note 7 zimekuwa zikishika moto

Samsung pia imewashauri walio na simu hizo kuzizima na kutozitumia tena.