Rais mpya wa Venezuela ataweza kustahimili shinikizo kutoka Marekani?

Mchoro wa picha ya Nicolas Maduro na mkewe Cilia Flores, ulitanda katika anga za mji wa Caracas mwezi Januari.
Mchoro huo ulikuwa umetumia mwanga za droni, na iliwekwa na serikali ya Venezuela.
Picha hizo zilisalia kwenye mabango kwa muda kabla ya kubadilishwa na kuandikwa neno "El pueblo los reclama," kumaanisha ''Watu wanawataka warudishwe nyumbani"
Baada ya oparesheni ya Januari 3, iliyofanywa na Marekani na kumkamata rais wa taifa hilo na mkewe, Venezuela imejipata katika njia panda.
Licha ya Delcy Rodríguez, makamu wa rais ambaye anakaimu sasa kama rais wa Venezuela, amekuwa akitoa wito wa kutaka Maduro na Flores kuachiliwa huru, ila hakuna dalili la hilo kutokea.
Maduro na Mkewe wanazuiliwa mjini Newyork, wakisuburia kufikishwa mahakamani kwa mashtaka ya ulanguzi wa dawa za Kulevya,madai ambayo wanakanusha.

Chanzo cha picha, Government of Caracas
Rodríguez, ambaye ni mshirika wa karibu wa Maduro anajaribu kudumisha hali ya usawa, akijaribu kuwavutia wafuasi wake wakisosholisti akiendelea kumuunga mkono Maduro kwa kutumia kauli za kupinga ubeberu, huku akibadilisha sera za taifa hilo chini ya shinikizo kutoka kwa rais wa Marekani Donald Trump, ambaye amemtishia kuwa asipofuata wanachotaka, atakamatwa kama walivyomfanya Maduro.
"Trump amedokeza kuwa Venezuela iko chini ya ulinzi wa Marekani, na kwa hivyo anahudumu kwa huruma ya Marekani" anasema Christopher Sabatini, mtafiti wa Chatham House Amerika ya kusini. "Pia amechunguzwa na DEA, ila hakupatikana na hatia, ila vitisho bado vipo."
Idara ya Marekani ya kudhibiti dawa za kulevya (DEA) hawakutupa jibu tulipowauliza kuhusu uchunguzi walioufanya.
Rodríguez sasa anatembea kwenye mstari mwembamba wa kidiplomasia. "Rais Maduro alikuwa tayari ameonya kuhusu shambulio la aina hii kutokana na tamaa ya Marekani ya nishati," Rodríguez alisema katika taarifa yake ya kwanza baada ya operesheni hiyo. Hata hivyo, muda mfupi baadaye, Trump alitangaza kwamba Caracas ilikuwa imekubali kuwapa mapipa milioni 50 ya mafuta na kwamba yeye angesimamia fedha hizo za mafuta.

Chanzo cha picha, Reuters
Katika hotuba yake ya kwanza katika bunge la kitaifa la Venezuela, Rodríguez alikashifu vikali ubeberu wa Marekani. Siku hiyo hiyo, Rodríguez alikutana na mkurugenzi wa idara ya uchunguzi ya CIA John Ratcliffe mjini Caracas.
"Uhalali wa Rodríguez unategemea uwezo wa jeshi la Marekani. Atadumu iwapo Trump atataka kwa hivyo hawezi kumpinga." Alisema Carmen Beatriz Fernández mchambuzi wa masuala ya kisiasa.
Swali linaloibuka ni kuwa kwa muda gani Rodríguez, ataendelea na mchezo wa upande mmoja anataka kuwaridhisha mrengo wa kushoto wa Venezuela kwa upande mwingine utawala wa Marekani. Na iwapo atalazimika kuchagua upande mmoja, itakua maamuzi magumu kwani upande mmoja una nguvu zaidi.
'Arejeshwe nyumbani'
Caracas, mji mkuu wa Venezuela ina idadi ya watu millioni tatu, na imejaa mabango ya kumtaka Maduro arejeshwe nyumbani na kukataa uingiliwaji wa Marekani.
"Anajaribu kudumisha mawasiliano bora na pia kuanzisha sera na sheria mpya zakuliongoza taifa hili" Leonardo arca aliiambia BBC mwezi uliopita katika maandamano yaliyofanyika mjini Caracas.
Hafla za kutoa wito wa kumrejesha maduro Marekani huandaliwa na serikali.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Maduro na Flores wanazuiliwa kipindi ambacho Venezuela inapitia mabadiliko kwa kasi sana.
Nguvu kuu ya Chavismo, ni itikadi ya kisiasa ya mrengo wa kushoto iliyodumisha uongozi wa Hugo Chávez na baadaye Maduro, na inaweza kubadilisha mwelekeo kwa haraka ili kumweka rais yeyote yule madarakani.
Baada ya kuchukua urais, Delcy Rodríguez mfuasi wa Chavista kwa muda mrefu aliteua zaidi wataalamu wa kiufundi badala ya wanasiasa wenye itikadi, na kuonesha busara wakati Venezuela inaingia katika enzi mpya.
Pamoja na kupitisha sheria iliyoruhusu kampuni za mafuta za Marekani kuhudumu nchini Venezuela, pia aliruhusu kuachiliwa kwa wanasiasa na wanaharakati wengi wa haki za binadamu ambao walikuwa wamefungwa kwa miezi au miaka kadhaa. Upinzani unadai kuwa hili limefanyika tu kwa sababu Marekani iliweka shinikizo, na wanaeleza kuwa bado wafungwa wengi wa kisiasa wamesalia gerezani.
Trump amemtaja Rodríguez kuwa "mtu mzuri" ambaye amefanya naye kazi. Rodríguez,kwa upande wake amesema wamekuwa na mawasiliano na Trump kwa njia ya "heshima" na "uangalifu"
Shinikizo yaongezeka
Rodríguez amejizuia kutoa semi za kumkashifu Trump. Ila alitumia msemo maarufu inayotumika Marekani ya kusini kuwa Marekani "ina nguvu za nyuklia" "ni wavamizi" na "mabeberu"
Phil Gunson, mchambuzi katika shirika la International Crisis Group,anasema, "Washington inapaswa kuelewa kwamba lazima aendelee na hotuba hii. Ni njia ya kudumisha mshikamano ndani ya mrengo wa Chavista, ingawa inajulikana kwamba si ya kweli."
Hii inaonyesha kwamba Rodríguez anatumia kauli kali dhidi ya Marekani zaidi kama mbinu ya kisiasa ya kuendeleza umoja wa chama chake badala ya kuweka ukweli wa uhusiano wake na Washington wazi. Wataalamu wote tuliowazungumza wanakubaliana kwamba shinikizo na tishio kutoka Marekani dhidi ya Venezuela na dhidi ya Rodríguez ni ya kweli.
Ingawa Rodríguez anajaribu kuhakikisha mrengo wa kushoto unafurahia, kundi hili ni 20% ya raia wa Venezuela, na kuna raia wengi wa taifa hilo ambao hawajahi kumuunga mkono Maduro.
Katika muda wa miaka 13 akiwa madarakani, umaarufu wake ulikuwa umedidimia. Katika uchaguzi wa mwaka 2024 ambapo alishinda kura hizo, uchaguzi huo umetiliwa shaka na kusheheni madai ya wizi wa kura.
Katika kura zilizohesabiwa na upinzani, kiongozi wao wa upinzani alishinda kura kwa 67% ya kura zilizopigwa na Maduro alipata 30% za kura. Ila Maduro aliapishwa kuwa rais kwa kusema alishinda kura hizo kwa 53%.
Zaidi ya raia millioni 7.9 wa Venezuela wamehama taifa hilo tangu mwaka wa 2014, huku millioni 6.5 wakiwa wakiishi kama wakimbizi kulingana na ripoti ya shirika la wakimbizi la umoja wa mataifa UNHCR.
"Hii sio serikali iliyokuwa na ushawishi," alisema Sabatini. "Raia wengi wa Venezuela wameanza kupata matumaini baada ya kuondolewa kwake"
Kuna kigezo kimoja kikuu ambacho kinaweza kumsaidia Rodríguez, ahadi ya kukuza uchumi wa Venezuela uliokumbwa na changamoto kwa muda mrefu. Mfumuko wa bei nchini humo uko juu zaidi duniani, na 86% ya raia wa Venezuela wanaishi kwa umaskini kulingana na ripoti ya mwaka wa 2024 ya Chuo cha Fedha cha Venezuela.
Bei ya chakula nchini Venezuela ni ghali mno. Utafiti uliofanywa mwaka wa 2025 ulipata kuwa bidhaa za matumizi ya kawaida zinazonunuliwa dukani kila siku zinagharimu hadi dolla 526.83.
Taifa hilo limekumbwa na mfumuko wa bei kwa miaka kadhaa na wanatumai ujio wa Marekani na kununua mafuta yao itawanufaisha wananchi wa kawaida.
Kundi la colectivos
Delcy Rodríguez pia amejipata katika njia panda na jeshi la taifa hilo, ambão uaminifu wao bado uko kwa Maduro.
Waziri wa usalama wa ndani Diosdado Cabello ana ushawishi mkubwa na Rodríguez anashirikiana naye kwa tahadhari. "Anaongoza si tu jeshi lililoghubikwa na ufisadi bali pia kundi la wanamgambo la kiraia la colectivos. Askari hao wametumiwa kuwatishia waandamanji" Anasema Christopher Sabatini. Colectivos pia ni kundi ambalo lilikuwa likitumiwa kuwatishia viongozi wa upinzani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Licha ya kujaribu kuhakikisha kila kitu kinakaa sawa, huenda Rodríguez si mnyonge mbele ya Trump kama inavyodhaniwa.

Chanzo cha picha, Reuters
Kulingana na Sabatini, Trump anataka dunia ione kuwa alifanikiwa katika kumkamata Maduro
Taifa lililogawanyika
Mvutano ndani ya serikali ya Marekani huenda imempa nguvu Rodríguez. Marco Rubio Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani amekuwa na ajenda ya kikomunisti na Venenzuela na amekuwa akitaka serikali ya taifa hilo kupinduliwa
"Rubio… mara nyingi amekuwa akizungumza kuhusu upinzani aambao hawajafurahia. Rubio na wengine wamekuwa wakishinikiza uchaguzi wa mapema kufanyika, ila ni Rodriugez atafanya uamuzi huo" anasema Sabatini
Iwapo hali itakuwa sawa na uchumi kuimarika huenda uchaguzi ukafanyika, anaongezea Sabatini.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula












