Mambo 4 yaliyobadilika Venezuela tangu Maduro kuondolewa madarakani

Chanzo cha picha, Juan BARRETO / AFP via Getty Images
Mfululizo wa milipuko mikubwa unawaamsha wakazi wa mji mkuu wa Venezuela, huku milipuko mikali na kelele za ndege na helikopta zinazoruka juu ya jiji zikithibitisha kile kilichokuwa kinatarajiwa kwa miezi kadhaa: Marekani imeanzisha shambulio la kijeshi dhidi ya nchi hiyo ya Amerika Kusini.
"Marekani imefanikiwa kutekeleza shambulio kubwa dhidi ya Venezuela na kiongozi wake, Rais Nicolás Maduro, ambaye, pamoja na mkewe (Cilia Flores), wamekamatwa,"Rais Donald Trump aliandika saa kadhaa baadaye kwenye akaunti yake ya Truth Social, na hivyo kuhitimisha operesheni hiyo isiyo ya kawaida.
Rais wa Republican alitangaza kwamba wanandoa hao walikuwa "wamehamishwa nje ya nchi," na saa chache baadaye, mamlaka ya Marekani ilithibitisha usafiri wao hadi New York.
Siku mbili baadaye, makamu wa rais wa wakati huo, Delcy Rodríguez, alichukua uongozi kama kaimu rais wa Venezuela.
Maduro na Flores wanasubiri katika seli zao katika Kituo cha Magereza cha Metropolitan huko Brooklyn (MDC), Machi 17, tarehe ya kufikishwa kwao mbele ya mahakama ya shirikisho.
Wanapaswa kujibu mashtaka ya biashara haramu ya dawa za kulevya na ugaidi wa dawa za kulevya.
Mabadiliko yaliyolazimishwa na Washington yanafanyika katika nchi waliyoitawala kwa zaidi ya miaka 12, mabadiliko ambayo, hadi wiki chache zilizopita, yalionekana kuwa hayawezekani.
Tunaangazia baadhi yake.

Chanzo cha picha, LUIS ROBAYO/AFP via Getty Images
1.Kuachiliwa kutoka gerezani na msamaha
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Moja ya hatua za kwanza zilizochukuliwa na mamlaka ya Venezuela ilikuwa kuamuru kuachiliwa kwa makundi ya wapinzani, viongozi wa vyama vya wafanyakazi, watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari na waandamanaji ambao walikuwa wamefungwa kwa miezi kadhaa, wengi wao katika kesi zilizotajwa na mashirika ya kimataifa kuwa za kiholela.
Uamuzi huo uliwasilishwa kama "ishara ya upande mmoja" ya "kuimarisha amani ya Jamhuri na kuishi kwa amani," kulingana na rais wa Bunge la Taifa, Jorge Rodríguez.
Katika kipindi cha mwezi huu, mamlaka zimethibitisha kuwa zaidi ya watu 600 wameachiwa kutoka magerezani.
Hata hivyo, idadi hiyo imepingwa na makundi ya ndugu wa wafungwa na mashirika ya haki za binadamu kama Jukwaa la Adhabu la Venezuela (Venezuelan Penal Forum), ambalo kufikia Februari 1 lilikuwa limethibitisha kuachiliwa kwa watu 344 kati ya zaidi ya "wafungwa wa kisiasa" 600 wanaohesabiwa na kundi hilo.
Katika kile kinachoonekana kuwa jaribio la kuharakisha mchakato huu, mnamo Januari 30, kaimu rais Delcy Rodríguez alitangaza: "Tumeamua kuhimiza sheria ya msamaha wa jumla itakayohusisha kipindi chote cha vurugu za kisiasa kuanzia 1999 hadi sasa."
"Na iwe sheria itakayosaidia kuponya majeraha yaliyoachwa na mgogoro wa kisiasa," alisisitiza, huku akitangaza pia kufungwa kwa El Helicoide, moja ya makao ya huduma za ujasusi za Venezuela na kituo cha kizuizini ambacho Tume ya Haki za Binadamu (IACHR) na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Venezuela wamekieleza kuwa "kituo cha mateso" dhidi ya wapinzani.

Chanzo cha picha, Pedro MATTEY / AFP via Getty Images
Siku chache kabla, Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social: "Ninafuraha kuripoti kwamba Venezuela inaachilia wafungwa wake wa kisiasa kwa kasi kubwa, na kasi hii inatarajiwa kuongezeka katika wiki zijazo."
Matangazo ya Rodríguez yanapingana na msimamo ambao Maduro na maafisa wengine wa ngazi ya juu wa Chavismo walikuwa wakishikilia hadi hivi karibuni.
"Safari hii hakutakuwa na msamaha; kitakachokuwepo ni (kifungo) huko Tocorón," alionya mrithi wa marehemu Hugo Chávez kwa wale waliopinga kuchaguliwa kwake tena kwa njia tata mnamo Julai 2024.
Wiki chache baadaye, zaidi ya watu 2,000 waliishia gerezani, kulingana na takwimu za Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Venezuela.
"Hakutakuwa na sheria ya kusahau, hakuna sheria ya kutokuwajibishwa, hakuna sheria ya msamaha, hakuna maridhiano, wala upatanisho hapa," alitangaza Diosdado Cabello, sasa Waziri wa Mambo ya Ndani, mwaka 2016, wakati bunge lililodhibitiwa na upinzani lilipopendekeza sheria kama hiyo, ambayo ilizuiwa na serikali na Mahakama Kuu ya Haki (TSJ).
Na ingawa mamlaka zimeonesha uvumilivu fulani kwa maandamano ya mitaani, hasa mikesha ambayo ndugu wa wafungwa wamekuwa wakiifanya mbele ya magereza na vituo mbalimbali vya kizuizini, zinaendelea kudumisha amri ya hali ya taharuki inayoruhusu kufungwa kwa yeyote anayedharau au kubeza kukamatwa kwa Maduro.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
"Si tone lolote la mafuta lifaalo hapa kwa Marekani ikiwa wataivamia Venezuela. Hata nusu tone haliwezi kutoka chini ya mazingira yoyote."
Tishio ambalo Waziri Cabello alilitolea mnamo Desemba lilishindikana.
Saa chache tu baada ya operesheni ya kijeshi ambayo ilimalizikaa kwa kukamatwa kwa Maduro, Trump alitangaza kwamba Caracas ilikubali kumpa hadi mapipa milioni 50 ya mafuta ya kuuza kwa bei za soko. Marekani pia iliruhusu kampuni za Marekani kununua na kuuza mafuta ya Venezuela kama sehemu ya mkakati wake wa kuamsha uzalishaji wa mafuta na kuimarisha soko.
Kuhusu pesa zitakazopatikana, rais alisema: "Zitadhibitiwa na mimi kuhakikisha zinatumika kwa faida ya watu wa Venezuela na Marekani."
Badala ya kukataa hili, mamlaka za Venezuela zilithibitisha kwamba kampuni ya mafuta ya serikali Petróleos de Venezuela (PDVSA) "iko katika mazungumzo na Marekani kuhusu uuzaji wa kiasi cha mafuta," kampuni ilisema katika taarifa fupi.
Siku kadhaa baadaye, Trump aliomba kampuni za mafuta za Marekani zainvesti takribani dola bilioni 100 kuinua uzalishaji wa mafuta uliodhoofika nchini Venezuela. Hata hivyo, kampuni nyingi zimekaa nyuma kwa sababu ya kutokuwa na uhakika wa kisiasa na usalama wa kisheria.
Ili kubadilisha mtazamo huu na kuvutia uwekezaji, rais wa Bunge la Taifa alitangaza mapitio ya ghafla ya mfumo wa kisheria uliopo, ambayo tayari yamezalisha marekebisho ya Sheria ya Hidrokaboni, ambayo imefungua sekta ya mafuta kwa wawekezaji binafsi na kurekebisha baadhi ya sera za kitaifa zilizowekwa na Hugo Chávez.

Chanzo cha picha, Jesus Vargas/Getty Images
"Hizo hifadhi kubwa za mafuta (za Venezuela) lazima zichimbwe ziweze kubadilishwa kuwa shule, kuwa vituo vya afya, chini ya ardhi hazifai yeyote,"Jorge Rodríguez alieleza.
Kabla ya kukamatwa kwa Maduro, wabunge walikuwa wamepangwa kujadili marekebisho ya katiba ambayo yaliyomo hayakuripotiwa kwa umma.
Marekebisho ya Sheria ya Hidrokaboni yamekosolewa na baadhi ya makundi ya Chavismo.
"Mnamo Januari 29, 2026, Venezuela ilisimama kumiliki mafuta yake, si jinsi wewe unavyoitazama," aliandika mwanzilishi wa zamani wa Mawasiliano, Andrés Izarra.
"Tunabaki na umiliki wa kikatiba wa chini ya ardhi. Lakini tumepoteza udhibiti wa nani anachimba, kiasi wanachokichimba, kwa nani wanauza, kwa bei gani, chini ya mamlaka gani, na sehemu gani inabaki kwetu kama Jamhuri," aliongeza.
Muktadha muhimu: Marekebisho hayo ya sheria yanabadilisha sera ya miaka mingi ambayo ililinda udhibiti wa serikali juu ya sekta ya mafuta na kuruhusu kampuni binafsi na wawekezaji wa kigeni kushiriki zaidi kwenye shughuli za mafuta, sehemu ya mabadiliko ya sera yaliyojumuisha kupunguza udhibiti wa PDVSA na kuvutia uwekezaji wa nje.

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images
3.Dola inashuka, lakini bei bado ziko juu
Kutokana na kutokuwa na uhakika baada ya operesheni ya kijeshi ya Marekani, sarafu ya Venezuela (bolivar) iliathirika sana katika soko.
Mnamo Januari, bolivar ilipoteza asilimia 18 ya thamani yake dhidi ya dola ya Marekani, ikiongezeka kutoka Bs 301.37 kwa kila dola hadi Bs 367.30, kulingana na takwimu za Benki Kuu ya Venezuela (BCV).
Katika soko ambako kampuni nyingi na raia wanapata sarafu yao ya kigeni kwa shughuli zao, dola ilifikia bei ya zaidi ya Bs 800 baada ya matukio ya Januari 3, ingawa katika siku za hivi karibuni imepungua hadi juu ya Bs 400.
"Kulikuwa na kutokuwa na uhakika mwingi na watu wengi waliamini kwamba hali ingeenda kuwa ya machafuko kuliko ilivyojiri, hivyo usambazaji wa sarafu ya kigeni katika soko la giza, ambalo tayari lilikuwa adimu kwa wiki, ulipungua zaidi," alieleza mwanasayansi wa uchumi ambaye hakutaka kutajwa jina kwa BBC Mundo.
Taarifa ya mamlaka kwamba wangeingiza dola milioni 300 za Marekani kutokana na mauzo ya mafuta kwenye soko la kubadilishia sarafu, hatua ya kwanza ya uingiliaji kwa miezi mingi, inaonekana kuwa sababu kuu ya kupungua kwa pengo kati ya viwango viwili vya kubadilisha sarafu.
Hata hivyo, mtaalamu aliyepangwa alionya kwamba hatua kama hizi hazitoshi.
"Tunachojali hapa ni jinsi mtiririko utakavyokuwa, zaidi kuliko mauzo; hilo ndilo litaamua jinsi uchumi, mfumuko wa bei, na sarafu zitakavyofanya," alieleza.
Kupungua kwa pengo la viwango vya kubadilisha sarafu hakumaanishi msamaha kwa mifuko ya wananchi wa Venezuela.
"Kila kitu bado ni ghali sana, bei hazishuki, ingawa dola inashuka katika soko. Kifurushi cha mayai kilikuwa dola 2.60 wiki iliyopita na sasa ni dola 3.50. Pesa hazitoshi," alieleza Alberto Fernández, mfanyakazi huru kutoka Caracas.
Wakati soko la dola linaonekana kusimama kidogo, sarafu bado inaendelea kupoteza thamani katika soko rasmi, jambo ambalo si dogo kwa nchi ambayo kwa muda mrefu imeingiza takribani asilimia 60 ya kile inachokitumia.
Kulingana na makadirio ya hivi karibuni kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF), Venezuela ilimaliza mwaka 2025 na kiwango cha mfumuko wa bei cha takribani asilimia 549.

Chanzo cha picha, Molly Riley/The White House via Getty Images
4.Kutoka uasi hadi mazungumzo
Mwisho wa mwaka 2025, Maduro alionya kuwa shambulio lolote la Marekani dhidi ya Venezuela lisingepita bila kujibiwa.
"Hata pini moja haitasogea na mgomo, wa uasi na wa mapinduzi wa tabaka la wafanyakazi utatangazwa," alisisitiza.
Hata hivyo, utabiri wa kiongozi huyo wa zamani haukutimia, wala ule wa waliodhani kuwa kungetokea mpasuko ndani ya Chavismo.
Serikali, ambayo sasa inaongozwa na Rodríguez, aliyekuwa makamu wa rais wa Maduro, imechagua kuingia kwenye mazungumzo na Washington na inajiandaa kurejesha uhusiano wa kidiplomasia baada ya karibu miaka saba ya kusitishwa.
Wiki iliyopita tu, mwanadiplomasia wa Marekani Laura F. Dogu aliwasili Caracas kufungua tena ubalozi wa Marekani, ambao ulikuwa umefungwa tangu 2019.
Kabla ya hapo, kulifanyika ziara ya kihistoria ya mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), John Ratcliffe, mjini Caracas.
Rodríguez alitetea mkakati wake, akisema utawawezesha "kushughulikia athari za shambulio na utekaji nyara wa Rais wa Jamhuri na Mama wa Taifa."
Hata hivyo, mtazamo huo unapingwa na baadhi ya makundi ndani ya chama tawala.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












