Saratani aina 11 zinaongezeka kwa vijana, wanasayansi wagundua

Caroline Mousdale na mwanawe Bradley Coombes, aliyefariki kwa saratani ya utumbo mpana akiwa na umri wa miaka 23.

Chanzo cha picha, Caroline Mousdale

Maelezo ya picha, Caroline Mousdale na mwanawe Bradley Coombes, aliyefariki kwa saratani ya utumbo mpana akiwa na umri wa miaka 23.
Muda wa kusoma: Dakika 5

Saratani aina kumi na moja zinaongezeka kwa vijana nchini Uingereza, utafiti mkubwa umeonesha.

Maelezo kamili kuhusu kwa nini viwango vya saratani vinaongezeka bado hayajajulikana kikamilifu. Hata hivyo, utafiti unaonesha kuwa mwenendo wa miongo kadhaa wa watu kuongezeka uzito kupita kiasi huenda unachangia kwa kiasi fulani, ingawa si sababu pekee.

Wanasayansi katika Taasisi ya utafiti wa Saratani na Chuo cha Imperial London walisisitiza kuwa saratani kwa vijana bado ni nadra, na kwamba kila mtu anaweza kupunguza hatari kwa kuishi maisha yenye afya.

Sababu za ongezeko la saratani kwa vijana miaka ya 20, 30 na 40 zimekuwa zikiwashangaza wanasayansi kwa miaka mingi.

Bradley Coombes, kutoka Portsmouth, alikuwa na umri wa miaka 23 tu alipofariki kutokana na saratani ya utumbo mpana. Mama yake, Caroline Mousdale, alisema kwamba licha ya kuwa na dalili nyingi za "hatari" za saratani hiyo, mara nyingi mwanae alipuuzwa kwa sababu alionekana kuwa mdogo sana kuwa na ugonjwa huo.

Alisema alikuwa "kijana mwenye afya njema na mwenye nguvu," aliyekuwa karibu kusaini mkataba wa kucheza mpira wa miguu alikuwa akifurahia maisha. Hakukuwa na kitu chochote kilichoonekana wazi kumuweka kwenye hatari, anasema.

Lakini baada ya mwaka wake wa kwanza chuoni, alianza kupungua uzito kwa kiasi kikubwa na kupata maumivu tumboni. Kisha kuharisha na kuwa na damu kwenye kinyesi chake.

 n

Chanzo cha picha, Caroline Mousdale

Maelezo ya picha,

Ilichukua miezi 18 ya kuwa na dalili ndipo akagundulika kuwa na ugonjwa. Kufikia wakati alipofanyiwa uchunguzi wa video wa utumbo wake, unaoitwa colonoscopy , saratani ilikuwa imekua sana kiasi kwamba ilizuia kamera kuingia.

Upasuaji na tiba ya mionzi, hazikuweza kuzuia uvimbe wake, na Bradley Coombes alifariki akiwa na mbwa wake Buster kando yake.

"Nilihisi sana, kama mzazi yeyote angehisi, kwamba angefanikisha ndoto zake za mpira wa miguu, angekuwa na maisha mazuri sana, na hilo limeondolewa kwake, kwa sababu saratani ya utumbo mpana inayotokea mapema haikutambuliwa," anasema Caroline Mousdale.

 Caroline Mousdale anataka kujua kwa nini mwanae pamoja na vijana wengine wanakufa kutokana na saratani

Chanzo cha picha, John Angerson

Maelezo ya picha, Caroline Mousdale anataka kujua kwa nini mwanae pamoja na vijana wengine wanakufa kutokana na saratani
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ni nadra sana kujua sababu hasa ya mtu kupata saratani. Hata hivyo, timu ya wanasayansi ilichambua mwenendo wa kitaifa wa saratani pamoja na mitindo ya maisha ya watu ili kuona kama wangeweza kubaini muundo fulani.

Walionesha kwamba mbali na saratani ya utumbo mpana, pia saratani za tezi (thyroid), myeloma , ini, figo, kibofu cha nyongo, kongosho, utando wa mfuko wa uzazi , mdomo, matiti na ovari zilikuwa zinaongezeka.

Saratani za utumbo mpana na matiti ndizo zinazopatikana zaidi kwa vijana, zikiwa na jumla ya takriban kesi 11,500 kila mwaka, wakati saratani za kongosho na kibofu cha nyongo ni nadra zaidi. Ni saratani za utumbo mpana na ovari pekee zilizoonekana kuongezeka kwa vijana pekee, huku zile nyingine tisa zikiongezeka pia kwa watu wazima.

Utafiti huo uliofanywa na taasisi ya utafiti wa saratani na Chuo cha Imperial London pia ulichambua mienendo ya tabia zinazojulikana tayari kuongeza hatari ya saratani.

Lakini ulionesha kuwa viwango vya uvutaji sigara, matumizi ya pombe, kiwango cha mazoezi ya mwili, ulaji wa nyama nyekundu na iliyosindikwa, pamoja na lishe yenye nyuzinyuzi chache, vyote vilikuwa vinaimarika au kubaki vilevile.

Tabia hizi zote zina mchango katika kusababisha saratani, lakini haziwezi kueleza kikamilifu kwa nini saratani imekuwa ikiongezeka.

Ripoti hiyo ilisema kwamba data pekee iliyolingana na ongezeko la saratani ni viwango vya uzito kupita kiasi, ambavyo vimekuwa vikiongezeka tangu miaka ya 1990.

Inadhaniwa kuwa mafuta ya ziada mwilini hubadilisha homoni kama vile insulini, jambo ambalo linaweza kuongeza hatari ya kupata saratani.

Hata hivyo, hata maelezo haya si kamili.

Kwa mfano, katika saratani ya utumbo mpana, watafiti wanakadiria kwamba kati ya kila kesi 100 za ziada, takriban 20 zinaweza kusababishwa na uzito kupita kiasi, huku 80 nyingine zikiwa bado hazijafafanuliwa.

Watafiti wanasema ni muhimu kuzuia aina zote za saratani, si zile "za ziada" pekee. Inakadiriwa kuwa karibu asilimia 40 ya saratani duniani zinaweza kuzuilika kupitia uchaguzi wa mtindo wa maisha, kama vile kuto kuvuta sigara.

"Ni jambo la kutia wasiwasi sana kusikia habari kwamba saratani zinaongezeka kwa vijana," Profesa Montserrat García Closas kutoka taasisi ya utafiti ya saratani, aliiambia BBC.

"Hata hivyo, kuna mambo yanayoweza kufanywa kupunguza hatari ya saratani kwa kuishi maisha yenye afya, kwa mfano, kuwa na mazoezi ya mwili na kudumisha uzito unaofaa."

Watafiti pia walisema kuwa ingawa saratani kwa vijana zinaongezeka, ni muhimu kukumbuka kuwa bado ni chache sana ikilinganishwa na saratani kwa wazee.

Walisema kuwa mtu mmoja kati ya 1,000 vijana (wenye umri wa miaka ya 20, 30 na 40) hutambuliwa kuwa na saratani kila mwaka, ikilinganishwa na takriban mtu mmoja kati ya 100 kwa makundi ya umri mkubwa (miaka ya 50, 60 na 70).

Utafiti wa kutafuta sababu nyingine za hatari bado unaendelea. Profesa Marc Gunter kutoka Imperial College London alisema kuna mjadala kuhusu vyakula vilivyosindikwa kupita kiasi, kemikali sugu zinazoitwa PFAS na matumizi ya antibiotiki, lakini akaongeza kuwa "bado kuna mengi hatujayajua."

Vinywaji vyenye sukari, uvimbe wa muda mrefu mwilini , uchafuzi wa hewa, bakteria wa utumbo na dawa za kuulia magugu pia vimeelezwa kama sababu zinazoweza kuchangia.

Pia kuna uchunguzi unaoendelea kubaini kama kuboreshwa kwa njia za kugundua saratani kunasababisha kugunduliwa kwa kesi nyingi zaidi katika umri mdogo.