Nilitoa mayai yangu kumsaidia abiria mwenzangu

k

Chanzo cha picha, Gini Bhogal

Maelezo ya picha, Gini (kushoto) alikutana na Anita kwenye treni mwanzoni mwa miaka ya 1990 na akaamua kumsaidia kupata mtoto.
Muda wa kusoma: Dakika 4

Gini Bhogal anatabasamu anapokumbuka safari ya chini ya ardhi ya London iliyobadilisha maisha yake.

Ilikuwa mwanzoni mwa miaka ya 90 na alikuwa na marafiki, wakipanda treni ya Piccadilly.

Kulikuwa na mtoto aliyekuwa akimfurahisha kila mtu, jambo lililosababisha mazungumzo ya kati ya Gini na mwanamke aliyesimama karibu naye - Anita.

Muda si mrefu walianza kuzungumzia kuhusu watoto na kujadili kuhusu mtoto wa Gini ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka miwili. Anita alieleza kwamba hangeweza kupata watoto kwa sababu ya tatizo la mayai yake. Alisema alikuwa akitafuta mfadhili, na Gini mara moja akahisi hamu ya kumsaidia.

Wanawake hao wawili walishuka kwenye treni kwenye kituo kilichofuata na kubadilishana namba.

Gini anamkumbuka Anita akimtazama na kumuuliza: "Je, utanisaidia kweli?"

Ilikuwa vigumu sana kwake kuamini ofa aliyopewa. Na mume wa Gini mwanzoni alikuwa na shaka.

"Alidhani nilikuwa nimechanganyikiwa," Gini anakumbuka. "Aliniuliza: 'Vipi ikiwa mtoto huyu atakuja nyumbani kwetu miaka 13 baadaye? Utafanya nini? Na watoto wako watasema nini?'"

Licha ya wasiwasi wake, Gini alisema "hakukuwa na shaka yoyote akilini mwangu."

Kuchangia mayai

o

Chanzo cha picha, Christopher Wedick

Maelezo ya picha, Anita alihakikisha kila mara Christopher anamjua "Shangazi yake Gini", hata walipokuwa wakiishi nje ya nchi.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Gini alianza kufanya taratibu na hatimaye aliweza kutoa mayai 17. Kumi yakawa viinitete, lakini majaribio tisa ya kwanza hayakwenda vyema baada ya kuhamishiwa kwenye tumbo la uzazi la Anita. Hatimaye, kiinitete cha 10 na cha mwisho kilifanya kazi, na Anita akapata mimba.

Miezi tisa baadaye, Anita na mumewe walimkaribisha mtoto Christopher.

"Hatukuwa na makubaliano yoyote," Gini anaelezea.

Hata hivyo, wanawake hao waliendelea kuwasiliana, na Gini akawa "Shangazi Gini"

"Walinitumia barua pepe kila mara," Gini anasema, "nami nilimtumia zawadi kwa ajili ya siku yake ya kuzaliwa ya kwanza."

"Na, kuanzia hapo na kuendelea, [Anita] alikuwa akinitumia barua pepe au kunitumia barua zenye picha."

Gini alisema kila Anita na familia yake walipokuja London, "tungeonana, hata kama wangekuwa wakisimama uwanja wa ndege kwa usiku mmoja njiani kuelekea mahali pengine".

Lakini, Christopher hakujua Gini alikuwa nani hasa.

Kisha, miaka mitatu iliyopita, simu ya Gini iliita. Ilikuwa Anita, ambaye alimweleza kwamba anataka kumwambia Christopher ukweli.

'Mtoto wa miujiza'

l

Chanzo cha picha, GINI

Maelezo ya picha, Gini (kushoto), Christopher na Anita, miaka 30 baadaye

Christopher anatabasamu anapokumbuka wakati alipogundua. Jua linamulika usoni mwake kupitia dirishani katika ofisi yake ya Miami ambapo anafanya kazi kwa sasa. Lakini sasa ni nyumbani kwake El Salvador.

"Nilipokuwa nikikua, sikujua chochote," anasema Christopher.

Alipojua halikuwa jambo gumu kwani wanawake wote wawili wana asili ya Kihindi. "Anita ana asili ya Goa, ilhali Gini ana asili ya Kipunjabi, na hivyo wana rangi sawa ya ngozi."

Alisema siku ambayo wazazi wake walimwambia ukweli, ilikuwa kwenye simu ya video huku Shangazi Gini akiwapo.

"Wananiona kama mtoto wa miujiza, kwa sababu mchakato wenyewe ni mgumu sana - hasa miaka ya 90."

"Na kwa hivyo ilikuwa aina ya mchakato wa muujiza, na ilichukua watu watatu kuzaa mtoto mmoja, unajua?

o

Chanzo cha picha, Christopher Wedick

Maelezo ya picha, Christopher alikulia bila kujua ukweli, lakini anasema imekuwa "jambo zuri" kugundua asili yake

Baadaye Christopher alisafiri kwa ndege hadi Uingereza ili kutumia muda na familia yake mpya, na hata akajiunga nao likizoni.

Kwa Gini, changamoto kubwa ilikuwa kuwaambia wazazi wake, ambao wote ni "Sikh ambao ni wahafidhina sana", alielezea.

Mwanzoni alimtambulisha Christopher kama mwana wa rafiki, lakini kisha, kwa msaada wa ndugu zake sita, Gini aliketi chini na kuwaelezea wazazi wake hadithi nzima.

"Baba yangu alisikia hadithi yangu, akamtazama Christopher na kusema kwa sauti kubwa, Mimi ni babu yako, na mama yangu akamkumbatia Christopher na kusema, 'Mwanangu'".

Walimkaribisha Christopher katika familia.

p

Chanzo cha picha, Christopher Wedick

Maelezo ya picha, Gini na Christopher sasa wanawasiliana mara kwa mara, bila kujali umbali kati yao

Gini na Christopher wanaendelea kukuza uhusiano wao - "familia ya ziada", kama Christopher anavyoiita.

Na, wameamua sasa ni wakati wa kuizungumza hadithi yao, kwa baraka ya Anita na familia zao.

Tangu alipoeleza hadithi yake, Gina anasema alikuwa na "watu wengi, haswa wanawake wa Asia Kusini, walionifikia wakisema kwamba nimewapa ruhusa ya kuzungumzia safari zao wenyewe."

"Hakuna anayejadili kuhusu utasa, hakuna anayejadili kuhusu mchango wa mayai kwa sababu si ukoo."

Christopher amekuwa mstari wa mbele tangu wakati huo, na bado hawezi kuamini jinsi mazungumzo ya bahati nasibu kwenye treni ya chini ya ardhi huko London yalivyosaidia kumleta duniani.

"Inavutia sana kufikiria wakati huo ndio uliosababisha maisha yangu," anasema Christopher.

"Tangu wakati huo, nimeweza kuwasaidia watu wengine wengi katika maisha yao."

"Na nadhani, kila mmoja wetu yuko hapa duniani kufanya mema, kusaidiana, kueneza upendo na muunganisho, na kuleta mabadiliko makubwa duniani."

"Na nahisi hilo ni moja ya jambo ambalo niko hapa kulifanya."