Hospitali za siri zinazowapa wahalifu sura mpya

Na Kelly Ng,BBC News

th

Chanzo cha picha, Presidential Anti-Organised Crime Commission

Maelezo ya picha, Maafisa walipata vitanda vya wagonjwa na vifaa vingi vya matibabu katika hospitali hizi zisizo halali

Hospitali za siri nchini Ufilipino zimekuwa zikitoa huduma za upasuaji wa kubadilisha sura kwa wakimbizi na wafanyikazi wa vituo vya ulaghai ili kuwasaidia kukwepa kukamatwa, mamlaka zilisema.

Hospitali mbili kama hizo haramu zinaweza kufungwa "katika wiki zijazo" baada ya polisi kuvamia hospitali ya kwanza katika vitongoji vya kusini mwa Manila mwezi Mei, msemaji wa polisi aliambia BBC.

Vyombo vya kupandikiza nywele, vipandikizi vya meno na dripu za IV za kung'arisha ngozi zilinaswa kutoka hospitali ya Pasay City miezi miwili iliyopita.

"Unaweza kuunda mtu mpya kabisa kati ya hao," alisema Winston John Casio, msemaji wa Tume ya Rais ya Kupambana na Uhalifu uliopangwa (PAOCC).

Hospitali hizo mbili haramu zilizo chini ya uangalizi zinaaminika kuwa kubwa mara nne kuliko ile ya Pasay, mamlaka ilisema.

Wateja wao wanadaiwa kujumuisha wale kutoka kwa kasino za mtandaoni, ambao wanafanya kazi nchini Ufilipino kinyume cha sheria, Bw Casio alisema.

Kasino za mtandaoni au Pogos (Operesheni za Michezo ya Kubahatisha ya Ufilipino) huhudumia wachezaji wa Uchina Bara, ambapo kamari ni kinyume cha sheria.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini polisi wanasema Pogos zimetumika kama kifuniko cha shughuli za uhalifu kama vile ulaghai wa simu na biashara ya binadamu.

Madaktari watatu - wawili kutoka Vietnam na mmoja kutoka Uchina - mfamasia wa China, na muuguzi wa Kivietinamu walikamatwa katika uvamizi wa Pasay, ambao hakuna hata mmoja wao aliyepewa leseni ya kufanya kazi nchini Ufilipino.

Mamlaka pia ilipata mashine ya kusafisha damu, na kupendekeza kuwa kituo hicho, ambacho kilikuwa karibu kilomita mita mraba 400, kilitoa matibabu mbalimbali pamoja na upasuaji .

"Zinaonekana kama kliniki za kawaida kwa nje, lakini ukiingia, utashtushwa na aina ya teknolojia waliyo nayo," Bw Casio alisema.

"Hospitali hizi za Pogo haziulizi vitambulisho sahihi... Unaweza kuwa mtoro, au unaweza kuwa mgeni haramu nchini Ufilipino," alisema.

Mamlaka ilidokezwa kuhusu kuwepo kwa hospitali hiyo haramu katika Jiji la Pasay.

Pogos ilistawi chini ya rais wa zamani Rodrigo Duterte, ambaye alitafuta uhusiano wa kirafiki na Uchina wakati wa muhula wake wa miaka sita uliomalizika mnamo 2022.

Hata hivyo, mrithi wake Ferdinand Marcos Jr ameanzisha msako dhidi ya Pogos, akitaja uhusiano na makundi ya uhalifu.

"Rais hataki Ufilipino itambuliwe kama 'kitovu cha utapeli' na ametupa agizo la kufuata mashamba ya ulaghai kwa sababu ya jinsi yamekuwa yakilenga idadi kubwa ya watu kutoka kote ulimwenguni," Bw Casio alisema.

Mnamo Desemba 2022, maafisa wa uhamiaji walimkamata mshukiwa wa mafia wa Uchina ambaye alidaiwa kufanyiwa upasuaji ili kukwepa kutambuliwa, lakini haikufaulu. Visa kama hivyo vinaweza kuhusishwa na hospitali za chinichini, Bw Casio alisema.

Meya wa mji wa kaskazini mwa mji mkuu, Alice Guo, hivi majuzi alikumbwa na mzozo baada ya kituo cha kashfa cha Pogo kuvamiwa karibu na ofisi yake.

Pia ameshutumiwa kuwa jasusi wa Uchina baada ya mamlaka kutilia shaka rekodi zake za kuzaliwa.

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah