Yoweri Museveni: Mwanamapinduzi aliyegeuka mfumo usiorithika Uganda

Chanzo cha picha, Getty Images
Mei 12, 2026, Yoweri Museveni anaapishwa rasmi kuanza muhula wake wa saba kama rais wa Uganda hatua inayohitimisha miaka 40 kamili madarakani, na ikimpa nafasi ya kuiongoza nchi hiyo kwa miaka mingine mitano hadi mwaka 2031. Akimaliza muhula huu, atakuwa ametawala Uganda kwa miaka 45 mfululizo akiwa na umri wa miaka 87.
Ni safari ndefu ya kisiasa kwa mwanamapinduzi aliyeingia madarakani mwaka 1986 kupitia vita ya msituni, katika taifa lililokuwa limechoka kwa mapinduzi, mauaji ya kisiasa na kuporomoka kwa uchumi. Wakati huo anaingia madarakani, baadhi ya mawaziri wake wa leo walikuwa bado hawajazaliwa. Namibia ilikuwa bado haijapata uhuru, Eritrea ilikuwa bado chini ya Ethiopia, na Sudan Kusini ilikuwa haijazaliwa kuwa taifa huru na kamili.
Uganda yenyewe ilikuwa na watu takribani milioni 13 pekee. Leo ina zaidi ya watu milioni 52 maana yake karibu robo tatu ya Waganda wa sasa hawakuwa wamezaliwa Museveni alipoingia madarakani. Kwa wengi wao, hajawahi kuwa na 'rais mwingine' yeye ndiye sura ya Uganda yenyewe.
Lakini miaka 40 baadaye, Museveni amebeba sura mbili zinazopingana. Kwa upande mmoja, anatajwa kama mtu aliyerejesha usalama, akaufufua uchumi na kuipa Uganda heshima ya kimataifa. Kwa upande mwingine, anakosolewa kwa kung'ang'ania madaraka, kubana demokrasia na kutumia dola kudhibiti wapinzani wake.
Na pengine hapo ndipo simulizi yake ilipo ama inapoanzia kama mwanamapinduzi aliyepigana kuondoa mfumo wa mabavu, baadaye naye akageuka kuwa mfumo wenyewe.
Alivyoijenga Uganda akitoka msituni

Chanzo cha picha, Getty Images
Yoweri Museveni hakuingia madarakani kupitia sanduku la kura, bali kupitia vita ya msituni iliyoitwa Bush War. Baada ya uchaguzi wa mwaka 1980 uliopingwa vikali na upinzani, Museveni alianzisha mapambano ya silaha dhidi ya serikali ya Milton Obote akiongoza kundi la National Resistance Army (NRA).
Vita hivyo vilidumu kwa takribani miaka mitano katika maeneo ya katikati mwa Uganda, hasa Luwero, ambako maelfu ya watu waliuawa katika mapigano kati ya waasi na jeshi la serikali. Wakati huo Uganda ilikuwa ikiendelea kuzama katika mzunguko wa mapinduzi, mapigano na tawala za muda mfupi baada ya miaka ya utawala wa Idi Amin na migogoro ya kisiasa iliyofuata kuondolewa kwake.
Mnamo mwaka 1985, Obote alipinduliwa na wanajeshi walioongozwa na Tito Okello Lutwa, lakini hata serikali hiyo haikudumu. Januari 26, 1986, vikosi vya Museveni viliingia Kampala na kuutwaa rasmi utawala hatua iliyofungua ukurasa mpya katika historia ya Uganda.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Museveni aliikuta Uganda ikiwa karibu kusambaratika. Uchumi ulikuwa umeanguka, miundombinu imeharibika na taifa limechoka kwa vita na mapinduzi ya mara kwa mara. Katika miaka yake ya mwanzo madarakani, alijijenga kama kiongozi imara aliyeahidi kurejesha usalama na kuifufua nchi.
Serikali yake ilisaidia kuimarisha usalama wa ndani, kuvutia wawekezaji wa kigeni na kukuza uchumi uliokuwa umeanguka vibaya. Kipato cha mwananchi wa kawaida kiliongezeka kwa zaidi ya mara kumi ukilinganisha na miaka ya 1980, huku Uganda ikianza kuonekana kama moja ya uchumi unaokua kwa kasi katika Afrika Mashariki.
Katika upande wa afya, Uganda ilitajwa duniani kama moja ya nchi zilizofanikiwa zaidi kupambana na UKIMWI katika miaka ya 1990. Wakati mataifa mengi ya Afrika yakisita kulizungumzia tatizo hilo, serikali ya Museveni ilianzisha kampeni za wazi zilizosaidia kupunguza maambukizi kwa kiasi kikubwa.
Kwa sehemu kubwa ya Waganda walioishi kabla ya 1986, haya ndiyo mafanikio yanayompa Museveni uhalali wa kuendelea kubaki madarakani. Kwao, Uganda ya leo ni tofauti kabisa na taifa la hofu, mapinduzi na vurugu walilolifahamu zamani. Na wanamuona Museveni kama 'lulu.
Kizazi kipya kinataka sura mpya

Chanzo cha picha, Getty Images
Museveni aliyeshinda uchaguzi mkuu wa Januari, 2026 kwa kupata asilimia ia 71.65% ya kura zote, anaapishwa na kuanza muhula wake wa 7 kama Rais wa Uganda akiingia katika orodha ya marais wachache wa Afrika waliotawala kwa zaidi ya miaka 40, akiwemo Denis Sassou Nguesso wa Congo brazaville, Teodoro Obiang, Rais wa Guinea ya Ikweta na Paul Biya wa Cameroon.
Lakini changamoto kubwa ya Museveni leo ni kwamba Uganda imebadilika kuliko simulizi iliyomuingiza madarakani.
Kizazi cha sasa ambacho hakijawahi kushuhudia enzi za vita, mapinduzi na machafuko ya kabla ya 1986. Kimezaliwa katika nchi ya Uganda yenye amani kiasi, yenye teknolojia, mitandao ya kijamii na matarajio mapya ya kisiasa.
Kwa vijana wengi, hoja ya "nilileta amani" haitoshi tena kuwa sababu ya kutawala milele. Wanataka ajira, uhuru mkubwa wa kisiasa, taasisi imara na mabadiliko ya uongozi. Ndiyo maana sura za upinzani kama Robert Kyagulanyi zimepata mvuto mkubwa kwa kizazi kipya.
Wakosoaji wake wanamshutumu kwa kutumia vyombo vya dola kuzuia upinzani, kuwakamata wakosoaji wake na kuminya demokrasia. Kizza Besigye na Bobi Wine wamewahi kukamatwa mara kadhaa katika vipindi vya uchaguzi jambo ambalo limeifanya Uganda kushutumiwa kimataifa kuhusu hali ya haki za kisiasa. Besigye anashikiliwa mpaka sasa, Bobi amekimbilia ughaibuni.
Hata hivyo, ndani ya chama chake cha National Resistance Movement (NRM), Museveni bado ana nguvu kubwa kisiasa. Chama hicho kinaendelea kushinda kwa wingi katika uchaguzi huku taasisi kuu za dola zikionekana kubaki karibu naye.
Mfumo uliomzunguka Museveni

Chanzo cha picha, Getty Images
Kadri miaka ilivyopita, Museveni hakuendelea kuwa rais pekee bali aligeuka kuwa kitovu cha mfumo mzima wa dola ya Uganda.
Mkewe, Janet Museveni, ni mmoja wa mawaziri wenye ushawishi mkubwa serikalini, huku mtoto wake Muhoozi Kainerugaba akiwa mkuu wa majeshi ya Uganda. Muundo huo umeongeza mjadala kuhusu namna familia ya Museveni ilivyozidi kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya siasa na usalama wa taifa hilo.
Mchambuzi wa siasa za Afrika Mashariki, Ezekiel Kamwaga, anaamini hapo ndipo ilipo siri kubwa ya maisha marefu ya kisiasa ya Museveni.
"Mara zote, hatabiriki, mwangalifu na hamwamini yeyote" anaandika Kamwaga kwenye moja makala zake kuhusu Museveni na hiyo pengine hii ndiyo siri yake kubwa zaidi ya kukaa madarakani kwa takribani miongo minne sasa.
Kwa miaka mingi, Museveni ameonekana kuwa mwanasiasa anayewatangulia wapinzani wake, anayebadilika kulingana na mazingira ya kisiasa na anayehakikisha mihimili muhimu ya dola inaendelea kuwa karibu naye.
Miaka mitano mengine na swali la urithi

Chanzo cha picha, Getty Images
Museveni sasa anaingia katika muhula ambao unaweza kuwa wa mwisho katika maisha yake ya kisiasa lakini pia muhula ambao utaamua namna historia itakavyomhukumu.
Kwa baadhi ya Waganda, matarajio yao kwake bado ni kuona uchumi ukiendelea kukua, ajira zikiongezeka, huduma za afya na elimu zikiboreshwa, na Uganda ikiendelea kuwa taifa lenye utulivu katika ukanda wa Afrika Mashariki unaokabiliwa na migogoro ya mara kwa mara.
Lakini kwa wengine, matarajio makubwa zaidi ni kuona nafasi ya mabadiliko ya kisiasa ikifunguliwa zaidi, taasisi zikijengwa nje ya kivuli cha mtu mmoja, na Uganda kuanza kufikiria maisha baada ya Museveni.
Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa Rais Museveni, anatajwa kuwa miongoni mwa warithi wake, licha ya kukosolewa mara kadhaa kwa namna anavyotumia mitandao ya kijamii kutishia wapinzani wa baba yake. Awe yeye ama mwingine, wengi wanaona hakuna kipya kinachoweza kuonekana.
Mmoja wa waandishi wa habari na siasa za Uganda anasema miaka mitano ijayo huenda isiwe ya mageuzi makubwa.
"Miaka yake mitano ijayo hayatazamiwi kuwa na mabadiliko makubwa. Yumkini hali itaendelea kubaki kama ilivyo."
Na hivyo, miaka 40 baada ya kuingia madarakani akiwa mwanamapinduzi mwenye asili ya mtutu wa bunduki kutoka msituni, Museveni anaendelea kuiongoza Uganda akiwa si tu rais wake wa muda mrefu zaidi bali mtu ambaye kwa kiasi kikubwa ameigeuza historia ya Uganda kuwa historia yake mwenyewe.













