Kwanini vita vya Iran vinaweza kumponza Trump kisiasa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump Pamoja na utawala wake wamekuwa wakitoa taarifa za kukanganya kuhusu oparasheni ya Pamoja kati ya taifa lake na Israel dhidi ya Iran.
Jumatatu iliyopita siku ya kumi ya vita hivyo, bei ya mafuta ilikuwa imepanda, rais huyo wa Marekani alifanya kikao na waandishi wa habari kujaribu kutuliza hali, ila juhudi zake hazikufua dafu.
Aliiambia shirika la habari la CBS "nimepanga kila kitu na watafurahia, vita hivi nikama vimekwisha"
Trump alipoulizwa iwapo oparesheni hiyo itamalizika hivi karibuni alisema "sijui, itategemea. Kumalizika kwa vita hivyo uamuzi ni wangu wala sio mtu mwingine"
Baada ya kikao na waandishi wa habari, bei ya mafuta ilishuka kutoka dola $120 kwa pipa moja had idola $90.
Siku chache zilizopita Trump alisema hatasitisha vita hivyo hadi Iran itakapojisalimisha.
Vita hivyo vilidhaniwa kumalizika ila Trump alibadilisha mawazo yake na kusema "tunaweza kusema tumefanikiwa, na tunaweza kuendelea, na tutaendelea"
Trump aliongezea kuwa "tuko karibu kumaliza vita hivi" ila akaonya kuwa ataongezea mashambulizi dhidi ya Iran, iwapo Iran itashambulia meli za mafuta zinazopitia ghuba ya uajemi.
"Tutawashambulia na nguvu kubwa zaidi, wao au yeyote atakayewasaidia katika vita hivi"
Alielezea kuwa lengo lake la vita hivi ni kuhahakisha Iran haina uwezo wa kutengeneza silaha wanazoweza kutumia kuishambulia Marekani, Israel au washirika wao.
Hiyo inahitaji mabadiliko katika utawala wa Iran ambao Trump ameshindwa kufanikiwa baada ya mwanawe Ayatollah Ali Khamenei kumrithi baada ya kifo chake.
Mkanganyiko
Siku zinavyokwenda ujumbe wa rais wa Marekani unazidi kufifia, na hakuna dalili ya ni lini vita hivi vitakamilika
Katika mahojiano na televisheni la CBS, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth alisema kuwa awamu ya pili ya oparesheni ya Marekani na Israel itakuwa yenye nguvu zaidi. "Tutalenga vituo vya kijeshi kupitia mashambulio ya angani na mabomu yenye nguvu zaidi, hatujaanza kampeni hiyo bado," alisema.
Trump alipoulizwa kuhusu mkanganyiko wa semi zake na Waziri wa ulinzi alisema kuwa " huu ndiyo mwanzo wa kujenga taifa jipya"
Kutokana na semi za Trump masoko za kimataifa yalianza kuwa dhabiti isipokuwa bei ya gesi ambayo bado haijashuka.
Bei ya galoni moja ya gesi nchini Marekani ni dola $3.48, huku hali ya uchumi ikiendelea kuzua wasiwasi.

Chanzo cha picha, Bloomberg vía Getty Images
Gharama ya Maisha ni jambo ambalo huwatia wasiwasi raia wengi wa Marekani, huku kura za maoni zikionyesha wengi wanapinga hatua ya Trump kuivamia kijeshi Iran.
Hii inahatarisha uongozi wa Trump, kwani imesalia miezi chache tu kabla taifa hilo kupiga kura za katikati ya muhula, ambazo zitatoa mwongozo wa jinsi bunge la Congress litafanya kazi.
Trump amesema kupanda kwa bei ya bidhaa ni kwa muda tu, na hali itakuwa imerejea kuwa kawaida kabla ya uchaguzi mdogo wa mwezi Novemba.
Athari ya kura.
Kaskazini mwa jimbo la Georgia, wakazi wa eneo hilo wanapiga kura siku ya Jumanne kuhusu viti maalum.
Vita vya Iran vimeanza kuzua wasiwasi huku wapiga kura wakielezea wasiwasi wao kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta.
Angie mkazi wa jimbo la Georgia, ambaye hivi karibuni amestaafu baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu kama muuguzi, alieleza wasiwasi kwamba kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli kunaweza kuathiri bajeti yake wakati ambapo tayari Maisha yamekuwa magumu
Alipoulizwa maoni yake kuhusu vita dhidi ya Iran na athari zake kwa bei ya petroli, alisema kuwa anajali zaidi watu wa Iran na kwamba Marekani haikupaswa kuhusika.
"Ukweli ni kwamba sipendi jambo hili kabisa," alisema. "Naelewa kwamba walihitaji msaada, lakini je, hatukuweza kupata njia nyingine ya kufanya hivyo?"alihoji.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Trump ameahidi mara kwa mara kupunguza gharama ya maisha, na yeye pamoja na timu yake wameonyesha kuwa wanafahamu umuhimu wa suala hili.
Mwisho wa mwaka uliopita, alianzisha kile alichokiita "ziara ya uwezo wa kumudu gharama" huko Pennsylvania, lakini haijapata mafanikio makubwa.
Operesheni za kijeshi nchini Venezuela na Iran zimekuwa zikitawala vichwa vya habari katika miezi kadhaa, kuna hatari kwamba Trump sasa anaonekana kama rais anayejikita zaidi katika uingiliaji wa mambo ya nje, badala ya kushughulikia bei za chakula nchini mwake.
Kupanda kwa bei ya mafuta kunakosababishwa na oparesheni ya kijeshi ya Iran huku kura za maoni zikionyesha kuwa Wamarekani wachache wanaunga mkono hatua ya Trump, hii inahatarisha uongozi wa kisiasa wa Trump.
Hata hivyo, vita si tu kurusha makombora au kudondosha mabomu.
Gharama ya vita hivi inapimwa na uharibifu kwa uchumi wa dunia na wa Marekani, pamoja na gharama za kisiasa kwa Trump na wenzake wa chama cha Republican ambazo bado hazijaonekana wazi.















