Michezo ya Olimpiki yaahirishwa kwa hofu ya Coronavirus

Michezo ya Olimpiki ilikuwa ianze Julai

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Michezo ya Olimpiki ilikuwa iafanyike Julai

Waandalizi wa michezo ya Olimpiki Tokyo 2020, ambayo ilitarajiwa kung'oe nanga Julai 24, wamekubali kuahirisha michezo hiyo ya kimataifa kwa mwaka mmoja kutokana na janga la coronavirus.

Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, amesema kamati ya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki imeafikiana kuhusu hatua hiyo baada ya kujipatia wiki nne kufanya maamuzi.

"Napendekeza tuahirishe michezo hii kwa mwaka mmoja, Rais wa [IOC] Thomas Bach kwa 100% ," alisema akikubaliana na ombi hilo.

Mashindano hayo bado yataitwa Tokyo 2020 licha ya kuwa itafanyika mwaka 2021.

Bodi ya Utendaji ya IOC iliyokutana Jumapili jioni huku kukiwa na shinikizo kutoka kwa wanariadha na kamati za kitaifa za Olimpiki wakitaka michuano hiyo kusogezwa mbele kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Katika taarifa ya pamoja, waandalizi wa Tokyo 2020 na IOC walisema:

"Kutokana na kasi ya mlipuko wa wa coronavirus hali kuwa mbaya duniani kote...bodi ya utendaji leo imeanzisha mchakato mpya wa mpango wa mazingira maalum," taarifa ilisema.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe amekiri kwa mara ya kwanza kuwa kuwa kuahirisha michuano ya Olimpiki ni jambo linalowezekana endapo hakutakuwa na uwezekano wa kuiandaa kwa "ukamilifu wake".

Woman wearing a mask at a bus stop with Tokyo 2020 advertising

Chanzo cha picha, AFP

Abe ameliambia bunge la Japani kuwa nchi hiyo inaweza isiwe na "chaguo lengine zaidi ya kuahirisha michuano," huku akisisitiza kuwa kuifuta kabisa michuano hiyo ni jambo lisilowezekana.

Kauli hiyo ya Abe inakuja baada ya mara kadhaa kusema kuwa nchi yake itaweza kuandaa michuano hiyo kwa ufanisi na kwa muda uliopangwa bila tatizo lolote licha ya mlipuko wa virusi vya corona.

Michuano mbali mbali ya michezo ulimwenguni imesimamishwa kutokana na janga linaloendelea kwa sasa ambapo zaidi ya watu 290,000 wapeta maambukizi ya virusi hivyo huku zaidi ya 12,000 wakipoteza maisha.

Ligi ya Primia (EPL) imeahirishwa mpaka Aprili 4, huku kukiwa na hofu ya muda wa kuahirishwa kuongezwa. Michuano ya Euro 2020 imeahirishwa mpaka 2021.

Canada, Australia kutopeleka wanariadha Tokyo

Team Canada

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Canada yatangaza kutoshiriki Olimpiki 2020

Wakati IOC na serikali ya Japani wakitazama nini cha kufanya, tayari kamati ya Olimpiki ya Canada imefanya maamuzi ya kutoshiriki michuano hiyo kwa ratiba iliyopo sasa.

Canada inaitaka OIC kuahirisha michuano hiyo kwa mwaka mmoja.

"... kwa sasa dunia ipo katika janga kubwa ambalo ni muhimu kulishughulikia kuliko michezo," imeeleza taarifa ya kamati ya Olimpiki ya Canada.

Kwa upande wa Australia, runinga ya ABC inaripoti kuwa nchi hiyo imewataka wanariadha wake kujiandaa kwa michuano ya Olimpiki kwa mwaka 2021 na si mwaka huu.