Daraja muhimu la Crimea lapigwa kwa makombora, Urusi yasema
Video ambazo hazijathibitishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha moshi mwingi ukipanda karibu na daraja la Kerch.
Moja kwa moja
Mapinduzi ya Niger: Rais aliyepunduliwa atembelewa na daktari wake

Chanzo cha picha, AFP
Rais wa Niger aliyepinduliwa Mohamed Bazoum ametembelewa na daktari ambaye pia alimletea chakula, mmoja wa maafisa wake ameliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumamosi.
Hii inafuatia wasiwasi wa kimataifa juu ya afya na usalama wa rais na familia yake ambao waliripotiwa kuwekwa katika "hali ya kibinadamu".
"Ni sawa, kutokana na hali ilivyo," chanzo hicho kimeliambia shirika la habari la AFP.
Rais Bazoum, mwenye umri wa miaka 63, mkewe na mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 20 wamezuiliwa katika ikulu ya rais kwa zaidi ya wiki mbili tangu mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Abourahamane Tchiani yaliyoiangusha serikali yake.
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk amesema hali ya kukamatwa kwa Bazoum "inaweza kuwa ni sawa na kutendewa unyama na kudhalilishwa, kinyume na sheria za kimataifa za haki za binadamu".
Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani Antony Blinken amesema "amesikitishwa" na hatua ya jeshi kukataa kuiachilia familia ya Bazoum kama njia ya "kuonyesha nia njema".
Shirika la Human Rights Watch lilisema kuwa lilizungumza na Bazoum mapema wiki hii ambapo alielezea jinsi alivyotendewa binafsi, mke wake na mwanae kuwa ni "unyama na ukatili", HRW imesema.
Wakuu wa majeshi kutoka jumuiya ya kikanda, ECOWAS wanatarajiwa kukutana wiki ijayo mjini Accra, Ghana kujadili uwezekano wa kuingilia kijeshi kufuatia uamuzi wa jumuiya hiyo wa kupeleka kikosi cha ECOWAS nchini Niger.
Unaweza pia kusoma:
- Kwa nini mapinduzi ya Niger yanaigusa dunia nzima?
- Mgogoro wa mapinduzi Niger: Wahusika wakuu ni akina nani?
Vita vya Ukraine: Daraja la Crimea lapigwa kwa makombora, Urusi yasema

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Daraja la Crimea pichani mwezi Julai Makombora mawili ya Ukraine yamelenga daraja linalounganisha Urusi na rasi ya Crimea, Moscow inasema.
Video ambazo hazijathibitishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha moshi mwingi ukipanda karibu na daraja la Kerch.
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema makombora ya S-200 yametumiwa na kudunguliwa na kusababisha uharibifu wowote.
Ukraine haijazungumza lolote kuhusu shambulio hilo linalodaiwa.
Kumekuwa na angalau mashambulizi mengine mawili ya kulenga daraja katika miezi michache iliyopita.
Daraja la Kerch lilifunguliwa mnamo 2018 na kuwezesha usafiri wa barabara na reli kati ya Urusi na Crimea - eneo la Ukreni lililotwaliwa na Urusi mnamo 2014.
Ni njia muhimu ya ugavi kwa vikosi vya Urusi vinavyokalia sehemu za kusini mwa Ukraine.
Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema kuwa Ukraine ililenga muundo huo huo siku ya Jumamosi mwendo wa saa saba kamili mchana kwa saa za eneo.
Ilibaini kuwa makombora yaliyotumika ni S-200s - silaha za ardhini na angani zinazoongozwa na za enzi ya Vita Baridi ambazo awali ziliundwa kuharibu ndege za adui ambazo zimebadilishwa kwa matumizi ya ardhini.
Wakati huo huo wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ilisema kuwa "vitendo hivyo vya kinyama...havitakosa jibu".
Unaweza pia kusoma:
- Vita vya Ukraine: Changamoto za kuwafunza marubani ndege za kivita za F-16
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
Mapinduzi ya Niger: Urusi yaionya Ecowas dhidi ya kutuma wanajeshi Niger

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, rais wa Urusi Vradimir Putin Urusi imeionya Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi Ecowas kuhusu kuchukua hatua za kijeshi ambazo inasema itachukua dhidi ya wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Niger.
Inasema kuwa uamuzi huo unaweza kusababisha mgogoro ambao hautaonekana kwa muda mrefu.
Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia siku ya Ijumaa, ilizionya nchi za Afrika Magharibi kutopeleka wanajeshi Niger.
Taarifa hiyo ilisema, "Tunaamini kwamba hatua hiyo ya kijeshi haitatatua tatizo la Niger, badala yake hali hiyo itasababisha mzozo mkubwa, ambao tarehe yake haijulikani, na hali katika eneo la Sahel itakuwa ngumu tena".
Wakuu wa usalama wa Ecowas wanapanga mkutano siku ya Jumamosi kupanga jinsi ya kuandaa jeshi.
Siku ya Ijumaa, kundi la Ecowas lilikubali kuanzisha 'kikosi cha kudumu' katika maandalizi ya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya jeshi la Niger.
Tayari, rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara, alisema kuwa nchi yake itatuma takriban wanajeshi 1,000 ambao watajiunga na safu ya vikosi vingine vya kijeshi ambavyo vitakuwa kwenye mpango wa kutumwa Niger.
Marekani, Ufaransa na Umoja wa Ulaya tayari zimeunga mkono uamuzi uliochukuliwa na kundi la Ecowas kumrejesha madarakani rais mteule Mohamed Bazoum.
Unaweza pia kusoma:
- Kwa nini mapinduzi ya Niger yanaigusa dunia nzima?
- Mgogoro wa mapinduzi Niger: Wahusika wakuu ni akina nani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Siku ya Ijumaa, wafuasi wa jeshi la Niger, wakiwa wameshikilia bendera ya Urusi, walifanya maandamano katika eneo la Ubalozi wa Ufaransa mjini Yamai. Waandamanaji hao alizitaka nchi za magharibi kuondoka nchini na kuitaka Urusi kuja nchini mwao.
Urusi haikujitokeza kuunga mkono mapinduzi ya Niger.
Ufaransa na Marekani zina kambi za kijeshi nchini Niger, kwa ajili ya kupambana na wapiganaji wa jihadi katika eneo la Sahel.
Mkutano wa wakuu wa kijeshi wa Afrika Magharibi kuihusu Niger umeahirishwa

Chanzo cha picha, AFP
Mkutano uliopangwa wa wakuu wa vikosi vya ulinzi wa Afrika Magharibi kujadili mapinduzi ya Niger umeahirishwa kwa muda mfupi.
Mazungumzo hayo yaliyoitishwa na wanachama wa shirika la kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS yalitarajiwa kufanyika katika mji mkuu wa Ghana, Accra, Jumamosi hii leo.
Hakuna sababu iliyotolewa ya kuchelewa. Siku ya Alhamisi, viongozi wa Afrika Magharibi waliamuru kutumwa kwa wanajeshi kurejesha utawala wa kiraia nchini Niger.
Idadi kubwa ya wafuasi wa mapinduzi ya mwezi uliopita walikusanyika siku ya Ijumaa karibu na kambi ya jeshi la Ufaransa huko Niamey kuilaani ECOWAS na Ufaransa.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ameelezea wasiwasi wake mkubwa kwa familia ya rais aliyeondolewa madarakani wa Niger, ambaye alisema anazuiliwa katika hali mbaya zaidi.
Unaweza pia kusoma:
- Kwa nini mapinduzi ya Niger yanaigusa dunia nzima?
- Mgogoro wa mapinduzi Niger: Wahusika wakuu ni akina nani?
Boti ya wahamiaji yazama na kuua watu sita pwani ya Ufaransa

Msemaji kutoka mamlaka ya pwani ya Ufaransa Premar alisema kati ya watu watano na 10 hawajulikani walipo, AFP inaripoti.
Walinzi wa pwani wa Uingereza na Ufaransa wamewaokoa karibu watu 50 kutoka kwa meli hiyo, mamlaka ilisema.
Watu kadhaa walionekana wakitolewa kwenye boti ya kuokoa maisha, na wengine kwenye machela, katika eneo la Dover, lakini kiwango cha majeraha na idadi kamili ya watu waliokuwemo ndani ya boti hiyo bado haijulikani.
Watu kumi walipelekwa Dover na wengine kadhaa hadi Calais.
Meli iliyokuwa ikipita mara ya kwanza ilitoa tahadhari kwamba kuna mashua iliyojaa mizigo mingi ilikuwa katika matatizo katika ufuo wa Sangatte, karibu na Calais mapema Jumamosi, mamlaka ya Ufaransa ilisema.
Boti ya uokoaji ya Wafaransa ilipofika, walipata watu wengi baharini huku wengine wakipiga kelele za kuomba msaada.
Boti ya kuokoa maisha ya Dover, ambayo tayari ilikuwa kwenye Ieneo hilo ikishughulikia mashua nyingine iliyobeba wahamiaji, ilijiunga na shughuli ya uokoaji.
Waokoaji bado wanaendelea na msako ndani ya maji kwa ajili ya kuwapata manusura na miili zaidi - mara nyingi boti zinajaa kupita kiasi na ni vigumu kujua ni watu wangapi wamezipanda.
Ndege ya Jeshi la Wanamaji la Ufaransa na helikopta zimetumwa kusaidia msako huo.
Ingawa tukio hilo lilitokea katika eneo la Ufaransa, aina hizi za operesheni timu za uokoaji za hufanyika kwa ushirikiano wa Uingereza na Ufaransa ili kuokoa watu wengi iwezekanavyo.
Mfanyakazi wa kujitolea, ambaye alikuwa kwenye boti moja ya uokoaji, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa wahamiaji walikuwa wakitumia viatu kuchota maji kutoka kwa boti inayozama.
Anne Thorel alisema kumekuwa na watu "wengi" kwenye bodi.
Mwendesha mashtaka wa Ufaransa aliliambia shirika la habari la AFP kwamba wa kwanza kati ya waathiriwa wam kasa huo walikuwa ni mwanamume wa Afghanistan mwenye umri wa kati ya miaka 25 na 30.
Vikosi vya uokoaji vinasema hii ni mara ya saba wiki hii kuwaokoa watu waliozama au kukwama majini.
Msikiti wa Nigeria waporomoka: Takriban saba wafariki Zaria

Chanzo cha picha, AMMAR RAJAB
Maelezo ya picha, Makumi ya watu waliokolewa kutoka kwenye vifusi vya msikiti huo Msikiti mmoja katika mji wa Zaria nchini Nigeria umeporomoka wakati wa sala na kuua takriban watu saba, maafisa wanasema.
Mamia ya waumini walikuwa kwenye jengo hilo wakati huo sala ya Ijumaa.
Uchunguzi unaendelea ili kubaini sababu ya kuanguka. Amiri wa eneo hilo aliambia vyombo vya habari kuwa ufa uligunduliwa katika moja ya kuta siku ya Alhamisi.
Msikiti huo unadhaniwa kujengwa zaidi ya karne moja iliyopita. Nigeria ina historia ndefu ya kuporomoka kwa majengo.
"Miili minne ilipatikana awali," msemaji wa baraza hilo Abdullahi Kwarbai aliambia shirika la habari la Reuters.
“Kisha wengine watatu walipatikana baada ya timu ya uokoaji kupekua msikiti ulioporomoka,” Bw Kwarbai aliongeza.
Australia yatinga nusu-fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake baada ya kuichapa Ufaransa

Chanzo cha picha, Getty Images
Wenyeji wenza Australia wametinga nusu-fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake kwa mara ya kwanza walipoilaza Ufaransa kwa mikwaju ya penalti katika Uwanja wa Brisbane.
Kufuatia sare ya bila kufungana kwa dakika 120, Matildas walishinda 7-6 katika mikwaju ya penalti.
Cortnee Vine alifunga mkwaju wa penalti kwa Australia, baada ya Vicki Becho kufunga lango la Ufaransa.
Mlindalango wa Australia Mackenzie Arnold aliokoa jumla ya mikwaju minne ya penalti - ikiwemo mara mbili iliyopigwana Kenza Dali, baada ya kutoka nje ya mstari kwa kituo cha kwanza, na kusababisha kupigwa tena.
Arnold mwenyewe alipata fursa ya kufunga penalti ya ushindi akiwa mfungaji wa tano kwa Australia, baada ya kuokoa mpira kutoka kwa Eve Perisset, lakini akagonga nguzo huku takriban Waaustralia 50,000 ndani ya uwanja wakipitia kila hisia unayoweza kuwaziwa.
Hatahivyo wenyeji hao wa shindano wanasonga mbele, na kutinga nusu fainali ya kwanza kabisa ya Kombe la Dunia la Wanawake.
Australia itacheza na England au Colombia kwenye Uwanja wa Australia mjini Sydney mnamo 16 Agosti
Moto wa Hawaii: Idadi ya vifo vya Maui yapanda hadi 80

Watu 80 sasa wamethibitishwa kuuawa na moto katika kisiwa cha Hawaii cha Maui, maafisa wanasema.
Kuna hofu kwamba idadi hiyo itaongezeka zaidi katika kile ambacho rasmi ni janga la asili la Marekani.
Wazima moto wamekuwa wakijaribu kuzuia moto katika maeneo kadhaa, ukiwemo mji wa kihistoria wa Lahaina ambao umeharibiwa kabisa.
Mwanasheria mkuu wa Hawaii ametangaza "mmaelezo ya kina" kuhusu jinsi mamlaka inavyokabiliana na moto huo.
Hii inakuja huku maswali yakiongezeka juu ya iwapo maafisa waliwaonya wakaazi haraka vya kutosha kabla ya moto huo.
'Tutawazuia watu kutoka majumbani mwao' - Raila Odinga

Chanzo cha picha, Reuters
Kiongozi mkongwe wa upinzanina Muungano wa Azimio la Umoja nchini Kenya, Raila Odinga amesema upinzani unaweza kufanya maandamano yajayo dhidi ya serikali ili kuzuia visa vya ukatili na mauaji ya polisi.
Akizungumza mnamo Ijumaa katika, Kaunti ya Siaya, wakati wa maombi ya madhehebu mbalimbali ya kuwaombea waathiriwa wa dhuluma za polisi, Odinga alisema huenda muungano huo ukaamua kuwazuia wafuasi wake kuondoka makwao.
Akitoa mfano wa matukio ya nyuma ambapo aliishutumu serikali kwa kushambulia watu wasio na hatia na kujaribu kuzua hofu kupitia polisi, Bw Odinga alisema upinzani utawaelekeza wafuasi wake kukaa majumbani kama njia mbadala ya maandamano.
Kiongozi huyo wa upinzani alimlaumu Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua kwa mauaji yaliyoripotiwa na polisi, akizidi kuwashutumu kwa kutaja wasifu wa kikabila wa jamii ambazo hazikuwapigia kura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2022.
Odinga aliteta kuwa Rais Ruto hakuwa amejitokeza hadharani kulaani vitendo vya polisi, badala yake amekuwa akiwapongeza maafisa hao, huku naibu wake - wakati huo huo - akiendelea kukosa radhi kutokana na matamshi yake ya awali kwamba "serikali ni kampuni yenye wanahisa”
Awali rais Ruto alimlaumu Bw Odinga kwa kuitisha mandamano ya ghasia ambayo yamesababisha vifo, na kumtaka aache ghasia ili kumpatia nafasi ya kutekeleza shughuli za maendeleo alizowaahidi Wakenya.
Vita vya Ukraine: Marekani iko tayari kutoa mafunzo kwa marubani wa Ukraine kuhusu F-16 ikiwa Ulaya haina rasilimali za kutosha

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Ndege ya mapigano ya F-16 ya Marekani wakati wa onyesho la anga Mratibu wa Baraza la Usalama la Kitaifa la Ikulu ya Marekani - White House nchini Marekani John Kirby amesema Marekani iko tayari kuanza kutoa mafunzo kwa marubani wa Ukraine ya kurusha ndege za F-16 katika ardhi yake ikiwa washirika wa Ulaya hawana rasilimali za kutosha kwa hili.
"Ikiwa Ulaya haitaweza kutoa mafunzo, bila shaka, tuko tayari kuanza kutoa mafunzo kwa marubani wa Kiukreni hapa Marekani," Kirby alinukuliwa na CNN.
Wakati huo huo, Kirby alionya kwamba wakati ambapo Ukraine inapokea wapiganaji wa Magharibi na inaweza kuwaunganisha katika jeshi lake la anga, bado kuna safari ndefu. "Sababu ya sisi kufanya hivi ni mapambano yetu ya muda mrefu na ya kuboresha uwezo wa kijeshi wa Ukraine kujilinda," alisema.
Kirby aliongeza kuwa pamoja na kuhamisha ndege na marubani wa mafunzo, washirika wa Ukraine pia wanapaswa kutengeneza vifaa vyote muhimu kwa ajili ya matengenezo na uendeshaji wa ndege za Magharibi.
Alibainisha kuwa "yote haya huchukua muda", na alithibitisha kuwa mafunzo hayo yanajumuisha pia mafunzo ya lugha kwa marubani.
CNN inasema kuwa Marekani bado inasubiri washirika wa Ulaya kutoa mpango wa kuwafunza marubani wa Ukraine kuhusu F-16. Kabla ya mafunzo kuanza, Washington lazima iidhinishe rasmi mpango huu.
Hapo awali, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na maafisa wa Ulaya walisema marubani wa Ukraine wangepewa mafunzo mapema mwezi Agosti, lakini mpango huu hauonekani kuwa wa kweli.
Siku ya Ijumaa, gazeti la Washington Post, likiwanukuu maafisa wakuu wa serikali na jeshi la Ukraine, wakisema kwamba kundi la kwanza la marubani sita wa Ukraine - karibu nusu ya kikosi - hawataweza kukamilisha mafunzo yao ya F-16 hadi majira ya kiangazi yajayo.
Gazeti hilo likinukuu maafisa kadhaa wa Ukraine, marubani watalazimika kuchukua kozi za Kiingereza za miezi minne nchini Uingereza ili kujifunza istilahi zinazohusiana na wapiganaji wa ndege.
Wakati huo huo, wawakilishi wa serikali ya Ukraine wanasema kwamba marubani hawa wa Ukraine tayari wanajua Kiingereza vizuri.
Mamlaka ya Ukraine inasisitiza kwamba Kyiv inapaswa kupokea ndege za kivita za mtindo wa Magharibi haraka iwezekanavyo. Lakini maafisa wa Marekani hawaamini kwamba ndege kama hizo zinaweza kusaidia katika mashambulizi ya sasa ya Ukraine, gazeti la Washington Post lilisema.
Unaweza pia kusoma:
- Vita vya Ukraine: Changamoto za kuwafunza marubani ndege za kivita za F-16
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja ya leo Jumamosi tarehe 12.08.2023
