Idadi ya watu waliopoteza maisha katika tetemeko la ardhi la Uturuki na Syria yafika 2300

Tetemeko la pili la ardhi limetokea kusini-mashariki mwa Uturuki ,wilaya ya Elbistan karibu na mji wa Kahramanmaras, kwa mujibu wa ripoti.

Moja kwa moja

  1. Mpaka hapa tumefika mwisho wa matangazo ya moja kwa moja ya ukurasa wa BBCSwahili, Shukrani

  2. Mwanasoka wa Ghana ahofiwa kupotea baada ya tetemeko la ardhi Uturuki

    m

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wafanyakazi wa uokoaji wanamtafuta mchezaji mpita wa miguu wa Ghana Christian Atsu, ambaye huenda amenasa chini ya vifusi baada ya tetemeko la ardhi kuikumba Uturuki.

    Vyombo vya habari vya ndani vinasema mchezaji huyo wa Hataysport bado hajajulikani alipo.

    Tetemeko la ardhi lilipiga sehemu za Uturuki na Syria mwendo wa saa 04:00 saa za huko (01:00 GMT) siku ya Jumatatu na lingine lilifuata baada ya muda mfupi.

    Atsu alikuwa amefunga bao la ushindi kwa Hayatspor katika mechi yao ya Jumapili muda mfupi tu kabla ya tetemeko la ardhi kutokea nchini humo.

    Zaidi ya watu 2,000 wamepoteza maisha nchini Uturuki na Syria baada ya matetemeko hayo.

  3. Tazama video inayoonesha tetemeko la ardhi la Uturuki na Syria

    Maelezo ya video, Idadi ya watu waliopoteza maisha katika tetemeko la ardhi la Uturuki na Syria yafika 2300
  4. Milio ya risasi yasikika katika mji unaozozaniwa wa Somalia

    "Shambulio la kigaidi" dhidi ya jeshi limewaacha wanajeshi wawili wakiwa wamejeruhiwa, inasema Jamhuri iliyojitangaza kuwa ya Somaliland.

    Mapema Jumatatu Hoteli ya Hamdi katika mji wa Las Anod ulioshambuliwa na kundi la wanamgambo ambao walirushiana risasi na wanajeshi wa serikali, kwa mujibu wa ripoti za ndani.

    Mtu aliyeshuhudia aliiambia BBC kuwa kumekuwa na "mapigano ya risasi" kwa "saa sita bila kukoma".

    "Familia yangu imekimbia leo asubuhi, watoto sita na mke wangu, na wako umbali wa kilomita 80," anaongeza mkazi ambaye tunaficha utambulisho wake kwa sababu ya usalama wake.

    Ni wimbi la hivi karibuni la ghasia, kufuatia kuongezeka mwishoni mwa mwaka jana na kusababisha vifo vya takriban watu 10 na wengine kadhaa kujeruhiwa.

    Taarifa za Jumatatu za milio ya risasi zinakuja wakati viongozi wa kimila na mawaziri wa Somaliland wakikutana Las Anod.

    Hata hivyo wana matumaini ya kutatua mvutano unaoendelea kati ya serikali na jamii za Sool, Sanaag na Cayn.

    Ingawa maafisa wa Somaliland hawajajibu maombi ya BBC ya kutaka watoe maoni yao.

    Somali land
  5. Puto la pili juu ya Amerika ya Kusini ni yetu - China

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Serikali ya Uchina imekiri puto iliyoonekana Amerika Kusini siku ya Ijumaa inatoka China - lakini ilidai kuwa inakusudiwa kutumiwa na raia.

    Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Mao Ning alisema puto hiyo ilikuwa imebadlisha njia yake, baada ya kulipuliwa.

    Puto kama hilo lilidunguliwa katika anga ya Marekani na ndege za kijeshi siku ya Jumamosi huku kukiwa na madai kuwa lilikuwa linatumika kwa uchunguzi.

    China imekanusha madai ya kufanya ujasusi, ikisema kuwa inafuatilia hali ya hewa.

    Tukio hilo limesababisha mzozo wa kidiplomasia kati ya Washington na Beijing.

    Siku ya Ijumaa - kabla ya ndege za kivita kuangusha puto mwishoni mwa juma - maafisa wa kijeshi wa Marekani walisema puto ya pili ya Uchina ilikuwa imeonekana Amerika Kusini.

    Siku ya Jumatatu, China ilikiri kuwa kifaa "kiliingia kwa bahati mbaya katika anga ya Amerika Kusini na Caribbean".

    Bi Mao aliwaambia waandishi wa habari kwamba puto ya pili "imepotoka sana" kutoka kwa njia iliyokusudiwa, akitaja "uwezo mdogo" wa ndege na hali ya hewa.

    "Ndege isiyo na rubani inayozungumziwa ambayo ilitoka China ni ya kiraia na inatumika kwa majaribio ya ndege," aliongeza.

    "China ni nchi inayowajibika na inatii sheria za kimataifa kila wakati ili kufahamisha na kushughulikia ipasavyo pande zote zinazohusika, bila kuwa na tishio lolote kwa nchi yoyote."

    Mwishoni mwa wiki, jeshi la anga la Colombia lilisema kitu chenye "tabia zinazofanana na puto" kiligunduliwa tarehe 3 Februari katika anga ya nchi hiyo kwa urefu wa futi 55,000.

    Colombia ilisema imefuata kitu hicho hadi ilipoondoka kwenye anga, na kuongeza kuwa sio tishio kwa usalama wa taifa.

    th

    Chanzo cha picha, bbc

    Unaweza pia kusoma

    • Puto la China: Ndege ya Marekani yalidungua juu ya bahari ya Atlantic
    • Marekani inatafuta mabaki ya puto linaloshukiwa kuwa la kijasusi kutoka China
  6. Waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wanaochochea mgawanyiko - HRW

    m

    Chanzo cha picha, AFP

    Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limeonya juu ya kuongezeka kwa hatari ya mvutano kati ya jamii za Watutsi na Wahutu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kutokana na mapigano yanayohusisha wanamgambo ambao Rwanda inashutumiwa kuwaunga mkono.

    Shirika hilo linasema kundi la wapiganaji la M23 limefanya mauaji na kulazimisha raia katika kikosi hicho.

    Shirika hilo linasema wanamgambo hao wanaongeza hatari ya uhalifu wa kivita.

    Aidha inataka msaada wowote wa kijeshi kwa Rwanda usitishwe.

    Serikali ya Rwanda imekanusha kuunga mkono kundi la M23.

    Human Rights Watch pia inasema jeshi la DRC limekuwa likifanya kazi na makundi mbalimbali yenye silaha, wakiwemo wanamgambo wa Kihutu, ambao wamekuwa na rekodi ya kufanya unyanyasaji.

    Soma zaidi:

    • Fahamu baadhi ya makundi ya waasi yanayoyumbisha amani ya DR Congo
    • DR Congo: Je taifa hili limelaaniwa na utajiri wake?
  7. Tetemeko la ardhi la Uturuki na Syria: Picha za angani zaonyesha uharibifu huko Syria

    Maelezo ya video, Tetemeko la ardhi la Uturuki na Syria: Picha za angani zaonyesha uharibifu huko Syria

    Picha za ndege zisizo na rubani zinaonyesha athari za tetemeko la ardhi katika mji wa Sarmada katika kijiji cha kaskazini magharibi mwa mkoa wa Idlib nchini Syria.

    Wanachama wa ulinzi wa raia wa Syria, wanaojulikana kama White Helmets wanatafuta majeruhi chini ya vifusi.

    Tetemeko hilo kubwa la ardhi limesababisha uharibifu katika maeneo ya kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria. Zaidi ya watu 1,700 wamefariki , lakini idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.

    th
  8. Vifo vyaongezeka mpaka 1,900 wakati tetemeko la pili likipiga Uturuki

    m

    Chanzo cha picha, reuters

    Takriban watu 1,900 wanaaminika kufariki baada ya matetemeko mawili ya ardhi kupiga Uturuki na Syria.

    Idadi ya waliothibitishwa kufariki kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea asubuhi ya leo nchini Uturuki sasa imefikia 1,121, mkuu wa Mamlaka ya kudhibiti Maafa na Dharura nchini humo amesema.

    Idadi ya waliouawa nchini Syria sasa imefikia 783, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, ambalo limekuwa likijumuisha takwimu kutoka kwenye mamlaka katika maeneo yanayoshikiliwa na serikali na wale wa kundi la uokoaji la The White Helmets katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi.

    Takwimu zinaleta jumla ya pamoja kuwa takribabi 1,797.

    Taarifa bado zinaibuka kuhusu athari za tetemeko la pili lililokumba mkoa wa Kahramanmaras nchini Uturuki saa chache baada ya lile la kwanza kutokea karibu na mji wa Gaziantep, karibu maili 80 kusini.

    Watu wapatao 70 walikuwa tayari wamethibitishwa kuuawa huko Kahramanmaras kabla ya tetemeko la pili kupiga.

    Idadi ya waliofariki sasa inatarajiwa kuongezeka huku juhudi za kuwaokoa zikiendelea.

    ,
  9. Manchester City washtakiwa kwa kuvunja sheria za kifedha na Ligi ya Premia

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ligi ya Premia imeishtaki Manchester City kwa ukiukaji zaidi ya 100 wa sheria zake za kifedha kufuatia uchunguzi wa miaka minne.

    Imeipeleka klabu hiyo kwa tume huru kwa madai ya kukiuka kanuni kati ya 2009 na 2018.

    Pia ilishutumu City kwa kutoshirikiana tangu uchunguzi uanze mnamo Desemba 2018.

    City walisema "walishangazwa" na mashtaka hayo na wanaungwa mkono na "ushahidi usiopingika".

    Tume inaweza kutoa adhabu kuanzia faini, kukatwa pointi na kufukuzwa Ligi Kuu.

    "Manchester City imeshangazwa na kutolewa kwa madai haya ya ukiukaji wa Kanuni za Ligi Kuu, haswa ikizingatiwa ushiriki mkubwa na vifaa vingi vya kina ambavyo EPL imepewa," klabu hiyo ilisema katika taarifa.

    "Klabu inakaribisha mapitio ya suala hili na tume huru, kwa kuzingatia bila upendeleo mwili wa kina wa ushahidi usio na shaka ambao upo kuunga mkono msimamo wake.

    "Kwa hivyo tunatazamia jambo hili lisitishwe mara moja na kwa wote."

    Msimu uliopita City ilishinda taji lao la sita la Ligi Kuu tangu ilipotwaa 2008 na Kundi la Abu Dhabi United.

  10. Raia wa Sudan Kusini wataka viongozi wao kufanyia kazi ujumbe wa Papa

    mm

    Chanzo cha picha, Reuters

    Viongozi wa Sudan Kusini wamesisitizwa kufanyia kazi ombi la Papa Francis la kuleta amani katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita vya muda mrefu.

    Papa alifanya "hija ya amani" nchini humo mwishoni mwa juma akiwa na wakuu wa makanisa wa nchini Uingereza na Scotland.

    Katika mahubiri yake ya Jumapili wakati wa misa katika mji mkuu wa Juba, Papa aliitaka nchi hiyo kukataa "sumu ya chuki".

    Raia wa Sudan Kusini wana matumaini kuwa viongozi wao watazingatia ushauri huo.

    "Natarajia viongozi wetu kubadilisha mioyo yao na kutekeleza ujumbe wa amani ulioletwa na Papa Francis ili watu wa Sudan Kusini wawe na amani ya kudumu," Imma Lasu aliiambia BBC baada ya misa.

    Rose Adao, muumini wa Kanisa la Pentekoste, alisema anawataka viongozi wa Sudan Kusini watubu na kutekeleza ujumbe wa amani ulioletwa na Papa Francis.

    Elisabeth Mayak Thomas mwenye umri wa miaka 20, alikuwa miongoni mwa waliojitolea katika maandalizi ya kuwa mwenyeji wa Papa. Alisema anatarajia viongozi "kutekeleza makubaliano ya amani na kupatanisha watu wetu".

    Soma zaidi:

    • Papa, Askofu Mkuu katika ziara ya kihistoria ya amani nchini Sudan Kusini
    • Papa Francis nchini DR Congo: Mamilioni ya watu wahudhuria katika ibada ya Kinshasa
  11. Tetemeko la pili lapiga kusini mashariki mwa Uturuki

    Tetemeko la pili la ardhi limetokea kusini-mashariki mwa Uturuki ,wilaya ya Elbistan karibu na mji wa Kahramanmaras, kwa mujibu wa ripoti.

    Utafiti wa Jiolojia la Marekani limesema limepima nguvu ya tetemeko hilo kuwa na kipimo cha ukubwa wa 7.5.

    Elbistan iko karibu maili 80 moja kwa moja kaskazini mwa Gaziantep, ambapo kitovu cha tetemeko la leo asubuhi lilikuwa.

    Tetemeko la pili lilitokea majira ya saa 13:24 saa za nchini humo (10:24 GMT).

    Afisa kutoka Mamlaka ya kudhibiti Maafa na Dharura ya Uturuki alisema limetokea lenyewe tu na halihusiani na tetemeko la asubuhi.

    Takribani watu 70 wamepoteza maisha katika eneo la Kahramanmaras kufuatia tetemeko la kwanza.

    Bado haijabainika ni athari gani tetemeko hili la pili limekuwa nalo baada ya tetemeko la asubuhi ya leo ambalo liliua zaidi ya watu 1,200.

    Hata hivyo tetemeko la kwanza ,Utafiti wa Jiolojia wa Marekani ulisema tetemeko hilo la kipimo cha 7.8 lilitokea saa 04:17 saa za ndani (01:17 GMT) katika kina cha kilomita 17.9 (maili 11) karibu na mji wa Gaziantep.

    th
  12. Tetemeko la ardhi la Syria-Uturuki: Mtoto mchanga aokolewa kutoka kwa jengo lililoporomoka

    Maelezo ya video, Tetemeko la ardhi la Syria-Uturuki: Mtoto mchanga aokolewa kutoka kwa jengo lililoporomoka

    Mtoto mdogo alitolewa kutoka kwenye vifusi huko Azaz, baada ya tetemeko kubwa la ardhi kutikisa Syria na Uturuki, na kusababisha mamia ya watu kupoteza maisha.

    Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Richter lilitokea alfajiri ya Jumatatu wakati watu walipokuwa wamelala na makumi ya mitetemeko ya ardhi imesikika saa chache tangu wakati huo .

    th

    Unaweza pia kusoma

  13. Maandamano huku kanisa la Orthodox la Ethiopia likigawanyika

    .Mikutano ya hadhara ilifanyika katika jiji la Dessie, kaskazini mwa nchi, na nje ya nchi huko Washington DC

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mikutano ya hadhara ilifanyika katika jiji la Dessie, kaskazini mwa nchi, na nje ya nchi huko Washington DC

    Wafuasi wa Kanisa la Othodoksi la Ethiopia wanaanza maandamano ya siku tatu siku ya Jumatatu huku mvutano na viongozi ukiendelea kuongezeka.

    Takriban watu watatu waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa mwishoni mwa juma katika mji wa Shashemene, eneo la Oromia, baada ya vikosi vya usalama kufyatua risasi kanisani, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vinavyohusishwa na kanisa hilo.

    Mapigano yaliripotiwa katika maeneo mengine huko Oromia huku kanisa hilo likidai kukamatwa kwa wafuasi wake katika baadhi ya maeneo mkoani humo.

    Wiki iliyopita, baraza kuu la kanisa hilo, sinodi, liliamuru waumini wake kuvaa nguo nyeusi kama ishara ya kuandamana wakati wa hafla ya Mfungo wa Ninawi ya kanisa kuanzia Jumatatu.

    Ilijiri baada ya kanisa kushutumu serikali kwa kusaidia makasisi waliojitenga kutoka eneo la Oromia - ambao waliteua maaskofu bila sinodi kujua.

    Makasisi waliojitenga walisema walikuwa na uungwaji mkono "mkubwa" huko Oromia.

    Taarifa iliyotolewa na ofisi ya mawasiliano ya serikali ya shirikisho haikusema lolote kuhusu shutuma za kanisa hilo na matukio ya ghasia.

    Lakini ilionya dhidi ya vikosi ambavyo havikutajwa jina ambavyo ilisema vimejaribu kusambaratisha nchi hiyo bila mafanikio na sasa vinafanya kazi ya kuzidisha tatizo hilo.

    Mikutano ya hadhara ilifanyika katika jiji la Dessie, kaskazini mwa nchi, na nje ya nchi huko Washington DC.

    Watu mashuhuri wengi wametoa taarifa zinazoonyesha mshikamano na kanisa huku wengine wakichapisha picha - kwenye mitandao ya kijamii - wakiwa wamevalia nguo nyeusi.

  14. Serikali ya Mali yamfukuza mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa kitengo cha haki za binadamu

    w

    Chanzo cha picha, AFP

    Serikali ya kijeshi ya Mali imempa mkuu wa kitengo cha haki za binadamu cha tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa masaa 48 kuondoka nchini humo.

    Katika taarifa yake iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa, msemaji wa serikali alisema Guillaume Ngefa-Atondoko Andali amefanya "vitendo vya kupindua" katika uteuzi wake wa mashahidi kutoa ushahidi kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Mali.

    ''Andali alikuwa amejitwika jukumu la kuamua nani walikuwa wawakilishi wa mashirika ya kiraia, akipuuza mamlaka na taasisi za kitaifa, taarifa hiyo iliongeza.

    "Upendeleo wa Andali ulidhihirika zaidi wakati wa mapitio ya mwisho ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Mali", iliongeza taarifa hiyo.

    Mwezi uliopita, mwanaharakati wa mashirika ya kiraia wa Mali ambaye alitoa ushahidi katika mkutano wa Umoja wa Mataifa aliwashutumu washirika wa kijeshi wa serikali ya Urusi kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov anawasili nchini Mali siku ya Jumatatu kwa ziara inayolenga kuimarisha uhusiano wa kiulinzi na usalama.

    Itakuwa ni ziara ya kwanza rasmi katika taifa hilo la Afrika Magharibi kwa waziri wa mambo ya nje wa Urusi.

  15. Familia ya kitajiri Uingereza kuomba msamaha kwa mababu zao kumiliki watumwa zaidi ya 1000 hapo zamani

    Granada

    Familia moja ya Uingereza itaomba msamaha hadharani kwa watu wa kisiwa cha Caribbean cha Grenada, ambapo mababu wa familia hiyo walilkuwa wanamiliki watumwa zaidi ya 1,000 katika Karne ya 19.

    Familia ya kifahari ya Trevelyan, iliyomiliki mashamba sita ya sukari huko Grenada, pia italipa fidia.

    Mwandishi wa BBC Laura Trevelyan, ambaye ni mwanafamilia hiyo, alitembelea Grenada mnamo mwaka 2022. Alishtuka kubaini kwamba mababu zake walikuwa wamelipwa fidia na serikali ya Uingereza wakati utumwa ulipokomeshwa mnamo 1833 - lakini watumwa wa Kiafrika walioachiliwa hawakupata chochote.

    Akizungumza na BBC Bi Trevelyan alikumbuka ziara yake katika kisiwa hicho kwa ajili ya filamu. "Ilikuwa ya kutisha sana... nilijionea mwenyewe mashamba ambayo watumwa waliadhibiwa, nilipoona vifaa vya mateso vilivyotumika kuwazuia." "Niliona aibu, na pia nilihisi kwamba ilikuwa ni wajibu wangu.

    Huwezi kurekebisha yaliyopita - lakini unaweza kukiri maumivu." Bi Trevelyan alisema watu saba wa familia yake watasafiri hadi Grenada baadaye mwezi wa Februari ili kuomba msamaha kwa umma.

    Familia hiyo itatoa £100,000 sawa na dola $120,000 kuanzisha mfuko wa jamii kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi katika kisiwa hicho maskini na mashariki mwa Caribean.

    Bi Trevelyan alisema kuwa mwaka wa 1834, Familia yake walipokea takriban £34,000 kwa kupoteza "mali" zao huko Grenada - sawa na £ 3m kwa thamani ya pesa za sasa.

    "Kwa mimi kutoa £100,000 karibu miaka 200 baadaye ... labda hiyo inaonekana kama haitoshi," alisema. "Lakini ninatumai kuwa tunaweka mfano kwa kuomba msamaha kwa yale ambayo mababu zetu walifanya."

    Tume ya Kitaifa ya Malipo ya Grenada ilielezea ishara hiyo kuwa ya kupongezwa.

  16. Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa auawa katika shambulio la ndege mashariki ya Congo

    UN

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Afrika Kusini ameuawa na mwingine kujeruhiwa katika shambulio la helikopta yao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya Jumapili.

    Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO, umesema helikopta hiyo iliungua moto mchana wakati ikielekea Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, ambako ilifanikiwa kutua.

    Imesema mlinda amani mwingine alijeruhiwa katika shambulio hilo. "Monusco inalaani vikali shambulio hili la woga dhidi ya ndege yenye nembo ya Umoja wa Mataifa," ilisema katika taarifa.

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

    Jeshi la Ulinzi la Kitaifa la Afrika Kusini (SANDF) pia limethibitisha shambulio hilo. "Helikopta ya Oryx iliungua huko Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumapili Februari 5, 2023," ilisema katika taarifa yake.

    "SANDF iko katika harakati ya kuwafahamisha wanafamilia kuhusu wanajeshi waliohusika."

  17. Tems ashinda tuzo ya Grammy - ya kwanza kwa msanii wa kike wa Nigeria

    Mwimbaji wa Nigeria Tems alishinda tuzo ya Grammy siku ya Jumapili - na kuwa msanii wa kwanza wa kike kutoka nchini humo kushinda tuzo hiyo ya kifahari.

    Mwenzake Burna Boy alishindwa katika kategoria mbili alizoteuliwa. Tems, ambaye jina lake halisi ni Temilade Openiyi, alishinda tuzo katika kitengo cha Best Melodic Rap Performance kutokana na mchango wake katika wimbo wa Wait for U - alioshirikiana na wanamuziki Future na Drake.

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

  18. Idadi ya waliofariki katika tetemeko kubwa la ardhi nchini Uturuki yafikia watu 1200

    e

    Chanzo cha picha, EPA

    Idadi ya waliokufa katika tetemeko kubwa la ardhi kusini-mashariki mwa Uturuki, karibu na mpaka wa Syria yafika watu 912 kwa upande wa Uturuki pekee, na 5,383 wamejeruhiwa kutokana na tetemeko hilo.

    Rais Recep Erdogan amesema kuwa hawezi kutabiri kama idadi ya vifo itaongezeka huku juhudi za uokoaji zikiendelea.

    Utafiti wa Jiolojia wa Marekani ulisema tetemeko hilo la kipimo cha 7.8 lilitokea saa 04:17 saa za ndani (01:17 GMT) katika kina cha kilomita 17.9 (maili 11) karibu na mji wa Gaziantep. Huko Uturuki, maafisa walithibitisha vifo vya zaidi ya 76 hadi sasa na miji 10 iligonga, pamoja na Diyarbakir.

    Huku nchini Syria, zaidi ya watu 320 waliuawa, Kituo cha Kuchunguza Haki za Kibinadamu cha Syria chenye makao yake nchini Uingereza kimeripoti.

    Hii ina maana kuwa jumla ya makadirio ya vifo kutokana na tetemeko hilo mpaka sasa inazidi 1,200.

    Majengo mengi yameporomoka na timu za uokoaji zimetumwa kutafuta manusura chini ya lundo kubwa la vifusi.

    w

    Chanzo cha picha, Getty Images

    w

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Suleymon Soylu alisema miji 10 iliathirika: Gaziantep, Kahramanmaras, Hatay, Osmaniye, Adiyaman, Malatya, Sanliurfa, Adana, Diyarbakir na Kilis.

    Mwandishi wa BBC Kituruki mjini Diyarbakir, aliripoti kuwa duka moja la maduka mjini humo liliporomoka. Nchini Syria, vyombo vya habari vya serikali viliripoti vifo vingi katika maeneo ya Aleppo, Hama na Latakia.

    w

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Hili ni janga kubwa zaidi kutokea nchini humo tangu mwaka 1939, Erdogan amewaambia waandishi wa habari, akiongeza kuwa majengo 2,818 yaliporomoka kutokana na tukio hilo.

  19. Tuzo za Grammy 2023: Beyoncé avunja rekodi ya kushinda tuzo nyingi zaidi katika historia

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Beyoncé amevunja rekodi ya mshindi wa tuzo nyingi zaidi za Grammy, baada ya kukusanya taji lake la 32 katika sherehe za mwaka huu. Mwimbaji aliweka historia aliposhinda albamu bora ya densi/kielektroniki, kwa ngoma yake ya euphoric opus Renaissance. Kwa kufanya hivyo, alimpita gwiji wa Hungary-Muingereza George Solti, ambaye rekodi yake ya tuzo 31 ilikuwa imesimama kwa zaidi ya miaka 20. "Ninajaribu kutokuwa na hisia sana," nyota huyo alisema, akipokea tuzo.

    "Najaribu kupokea tu usiku huu." Aliendelea kuishukuru familia yake, akiwemo mjomba wake marehemu Jonny, ambaye alimsaidia kutengeneza mavazi ya jukwaani kabla ya kuwa maarufu. Beyoncé alisema hapo awali vita vyake na VVU viliathiri hamu yake katika muziki wa dansi, na uhusiano wake wa kihistoria na jumuiya ya LGBTQ, kwenye Renaissance.

    Wasanii wa Uingereza walikuwa na usiku mzuri pia, huku Styles akishinda albamu bora ya pop ya Harry's House na Sam Smith akipokea onyesho bora zaidi la duo/kundi la Unholy.

  20. Tetemeko kubwa la ardhi lakumba Uturuki, kusini-mashariki karibu na mpaka wa Syria

    w

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Tetemeko kubwa la ardhi limekumba Gaziantep kusini-mashariki mwa Uturuki, karibu na mpaka na Syria na kuua takriban watu watano.

    Utafiti wa Jiolojia wa Marekani ulisema tetemeko hilo la kipimo cha 7.8 lilitokea saa 04:17 saa za ndani (01:17 GMT) katika kina cha kilomita 17.9 (maili 11) karibu na mji wa Gaziantep.

    Tetemeko hilo lilisikika katika mji mkuu Ankara na miji mingine ya Uturuki, na pia katika eneo zima.

    Idadi ya majengo yameporomoka, na baadhi ya watu huenda wamenaswa.

    Mwandishi wa BBC Kituruki aliyeko Diyarbakir anaripoti kuwa jengo moja la maduka mjini humo liliporomoka. Rushdi Abualouf, mtayarishaji wa BBC katika Ukanda wa Gaza, alisema kulikuwa na takriban sekunde 45 za kutikisika katika nyumba aliyokuwa akiishi.

    Wataalamu wa tetemeko la ardhi wa Uturuki walikadiria nguvu ya tetemeko hilo kuwa ya kipimo cha 7.4. Walisema kuwa tetemeko la pili lilipiga eneo hilo dakika chache baadaye.

    Uturuki iko katika mojawapo ya ukanda wa maeneo yenye tetemeko la ardhi duniani. Mnamo 1999, zaidi ya watu 17,000 waliuawa baada ya tetemeko kubwa lililotikisa kaskazini-magharibi mwa nchi.

    th