Rais Museveni atoa rambirambi kwa familia ya Jenerali aliyeshambuliwa na watu wasiojulikana

Rais Yoweri Museveni ametoa rambirambi kwa familia ya Jenerali Katumba Wamala, na kuongeza kuwa amezungumza naye kwa njia ya simu

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo haya ya moja kwa moja kwa leo, tukutane tena kesho majaaliwa.

  2. DJ mwenye umri wa miaka sita anayetaka kuwa daktari

    DJ

    Mtoto wa Nigeria mwenye umri wa miaka sita King Chikamso anayefahamika zaidi kama DJ Irish anasema anataka kusomea udaktari na kuendelea kufanya kazi ya DJ.

    Aliiambia Idhaa ya BBC Igbo kwamba anataka kufanya kazi hizo mbili kwa pamoja.

    “Ninataka kuwa daktari, kuwafanya watu wahisi vyema wanapokuwa wanaumwa.Haitakuwa rahisi lakini nitakuwa daktari na pia nitafanya vyema kama DJ ," alisema.

    DJ

    DJ Irish kwanza alihisi kuingia katika taaluma ya kupiga miziki alipokuwa na umri wa miaka mitano na kumuomba baba yake amnunulie zana za muziki.

    Alimlipa mtu ambaye alimfundisha kazi ya DJ na sasa anaweza kuifanya kwa urahisi.

    “Marafiki zangu shuleni wananiambia kuwa mimi ni DJ mzuri, kwamba ninawaburudisha watu vyema na kuwafurahisha ,” alisema.

    Mama yake DJ Irish Adaobi King anasema kazi yake kama DJ haiathiri elimu yake, na ndio maana anaiunga mkono.

  3. Rais Museveni atoa rambirambi kwa familia ya Jenerali aliyeshambuliwa na Watu wasiojulikana.

    Museveni amesema mlinzi wa Jenerali angefyatua risasi kuwauwa washambuliaji badala ya kufyatua hewani kuwatisha

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Museveni amesema mlinzi wa Jenerali angefyatua risasi kuwauwa washambuliaji badala ya kufyatua hewani kuwatisha

    Rais Yoweri Museveni ametoa rambirambi kwa familia ya Jenerali Katumba Wamala, na kuongeza kuwa amezungumza naye kwa njia ya simu.

    Rais Museveni amesema kwamba upelelezi mpya wa mfumo wa kidigitali utazuia matumizi ya uhalifu unaoptekelezwa kwa kutumia pikipiki.

    Amesema kwamba mlinzi wa Jenerali asingepaswa kufyatua risasi hewani kuwatisha washambuliaji, bali angefyatua kuwauwa.

    General Wamala amepata majeraha ambayo hayahatarishi maisha yake kwenye mikonona bado yuko hospitalini.

    Chanzo cha picha, UGANDA PRESIDENCY

    Maelezo ya picha, General Wamala amepata majeraha ambayo hayahatarishi maisha yake kwenye mikono na bado yuko hospitalini.

    General Wamala amepata majeraha ambayo hayahatarishi maisha yake kwenye mikonona bado yuko hospitalini.

    Alishambuliwa na watu waliokuwa kwenye pikipiki Jumanne asubuhi. Dereva wake pamoja na binti yake pia waliuawa katika shambulio hilo la risasi.

    Msemaji wa jeshi alisema kuwa jeshi linachunguza simu kadhaa ambazo zinaonekana kuhusiana na mpango wa jaribio la kuua.

    Maafisa kadhaa wa ngazi ya juu, akiwemo mbunge, msemaji wa polisi na hakimu, waliuawa katika mauaji ya aina hiyo kwa kipindi cha miaka michache iliyopita. Hakuna kisa chochote kilichofanikiwa kuchunguzwa.

  4. Wanandoa wakamatwa kwa madai ya kumzika hai mtoto wao

    Kaburi

    Chanzo cha picha, KOFI ADJEI/ BBC PIDGIN

    Polisi nchini Ghana wamemkamata mwanaume mmoja na mke wake ambao walidaiwa kumzika mtoto wao wa kiume wa miaka miwili akiwa bado hai, katika jimbo la kati.

    Walioshuhudia tukio hilo wanasema wanandoa hao pamoja na kasisi mmoja walikutana majira ya alfajiri na kumzimtoto wao aliyejulikana kwa jina Yaw Adobaw.

    Abubakari Mohammed, ambaye alishuhudia uhalifu huo unaodaiwa akiwa ndani ya chumba cha nyumba yake alifichua kuwa aliwaona watatu hao wakiwa na mienendo ya ajabu.

    "Nilipokuwa chumbani, niliona mtoto akiwa amebebwa kwenye bega la mmoja wa watu hao watatu…nikagundua baadaye kama wanamzika mtoto" aliwaambia waandishi wa habari na kuongeza kuwa:"Kwahiyo niliripoti jambo hilo kwa polisi na baada ua kuchimba kaburi, tuligundua kutoka kwao kwamba kweli walimzika mvulana huyo " Bw Abubakar aliyeshuhudia tukio hilo aliongeza.

    Polisi wa kanda Kati nchini Ghana PRO, DSP Irene Oppong alisema "Abubakari Mohammed aliripoti tukio hilo takriban saa tisa usiku.

    Polisi wa Ghana wanamsaka Kasisi wa kike ambaye ametoroka

    Chanzo cha picha, KOFI ADJEI

    Maelezo ya picha, Polisi wa Ghana wanamsaka Kasisi wa kike ambaye ametoroka

    ‘’Alimuona Paul Adobaw al maarufu Kojo Okor, ambaye ni mwenye nyumba pamoja na wanawake wawili, lakini aliona ni kama wanamdhuru mtoto ."

    Kufuatia ripoti hiyo polisi walimkamata Paul Adobaw na kumpeleka kwenye eneo la tukio, na kumuamuru mshukiwa kufukua kaburi fupi ambako waliupata mwili wa marehemu mtoto , Yaw Adobaw.

    Walipokua wakiondoa mwili waliupeleka kuufanyia uchunguzi na baadaye kugundua kuwa damu ilikuwa ikitiririka kutoka mdomoni na puani kabla ya kuupeleka kwenye hifadhi ya maiti

    Mshukiwa, Paul Adobaw yuko katika mahabusu ya polsi kusaidia uchunguzi wa mauaji hayo, huku polisi wakimtafuta kasisi wa kike ambaye ametoroka.

    Idhaa ya BBC Pidgin imepata taarifa zinazosema kuwa Mchifu na wazee a eneo hilo hutumia damu ya binadamu kumwaga kwenye ardhi kwa kile wanachoamini ni kuitakasa kwa kuwazika watoto wakiwa hai.

  5. Maafisa Saudia watetea uamuzi wa kuwataka wapunguze idadi ya adhana misikitini

    Saudia

    Chanzo cha picha, AFP

    Maafisa nchini Saudi Arabia wametetea uamuzi wao wa kupunguza idadi adhana katika misikiti.

    Waziri wa masuala ya kidini alitangaza kwamba adhana katika misikiti zitapunguzwa kwa theluthi moja.

    Waziri wa masuala ya kigeni wa Saudia, Abdullatif al-Sheikh alisema kuwa amechukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa umma kwamba misikiti haijibu maswala yanayohusu umma.

    Hatahivyo, hatua ya kupunguza idadi ya adhana imekosolewa vikali na umma kwenye mitandao ya kijamii.

    Suala hilo pia limesababisha kubuniwa kwa ukumbi wa mitandao unaotoa wito wa kupigwa marufuku kwa matumizi ya miziki inayopigwa kwa sauti ya juu katika migahawa na chai nchini humo. .

    Al-Sheikh amesema kuwa watu waliolalamika kuhusu adhana ni pamoja na wazazi ambao walisema sauti yake inawazuia watoto wao kulala.

    Akizungumza katika matangazo ya Televisheni, Al-Sheikh alisema kuwa watu wanaotaka kusali hawahitaji kusubiri adhana kwa ajili ya kusali.

  6. Waziri wa Uganda ajeruhiwa na mwanae kufa baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana

    Kuna takriban mashimo saba ya risasi kwenye dirisha la gari la Jenerali Katumba Wamala

    Chanzo cha picha, Daily Monitor

    Maelezo ya picha, Kuna takriban mashimo saba ya risasi kwenye dirisha la gari la Jenerali Katumba Wamala

    Watu wenye silaha wamemshambulia na kumjeruhi Waziri na Kamanda wa zamani wa jeshi la Uganda, na kumuua binti yake na dereva.

    Walioshuhudia tukio hilo wanasema washambuliaji ambao hawajafahamika walliokuwa kwenye pikipiki walifyatua risasi kadhaa kwenye gari alimokuwa Jenerali Katumba Wamala.

    Shambulio hilo limeonekana kama jaribio la kumuua kamanda huyo wa zamani wa jeshi na Mkuu wa zamani wa polisi ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ujenzi na Uchuku na limemewashtua wengi nchini Uganda.

    Kuna takriban mashimo saba ya risasi kwenye dirisha la gari la Jenerali Katumba Wamala. Binti yake na dereva wote wameuawa.

    Wanajeshi wamepelekwa kulinda hospitali ambapo Jenerali Wamala Katumba anatibiwa

    Chanzo cha picha, PATIENCE ATUHAIRE/BBC

    Maelezo ya picha, Wanajeshi wamepelekwa kulinda hospitali ambapo Jenerali Wamala Katumba anatibiwa
    Askari

    Washambuliaji walitoroka kwa pikipiki zao baada ya kutekeleza shambulio hilo.

    Picha ya video kutoka kwenye eneo la tukio inamuonesha Jenerali Wamala huku nguo zake zikiwa zimejaa damu –akibebwa kwenye pikipiki na kukimbizwa hospitalini.

    Shambulio hili dhidi ya mmoja wa wanasiasa na wanajeshi wanaoheshimika zaidi nchini Uganda pia linawakumbusha wengi mauaji ya watu maarufu waliouawa miaka ya nyuma kwa risasi.

    Katika miaka ya hivi karibuni mashambulio sawa na shambulio hili ni pamoja na hakimu, viongozi wa Kiislamu , mshirika maarufu wa kisasa wa Rais Yoweri Museveni na Mkuu wa ngazi ya juu wa polisi.

    Wahusika wa mauaji hayo hawajawahi kushitakiwa.

    n

  7. Spika wa Tanzania amfukuza bungeni mbunge aliyevaa suruali ya kubana

    Bunge

    Chanzo cha picha, Bunge

    Maelezo ya picha, Spika alisimama na kumtaka mbunge aliyevaa mavazi hayo asimame na aondoke ndani ya ukumbi ili akavae mavazi yenye staha

    Spika wa Bunge la Tanzania , Job Ndugai amemtimua bungeni mbunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuvaa suruali inayombana.

    Mbunge huyo wa Momba Condester Sichwale alitimuliwa bungeni na Spika, kulingana na kanuni za Bunge, ambazo zinawataka wabunge wanawake kutovaa suruali za kubana.

    Hatua ya kufukuzwa bungeni kwa Mbunge Sichwale imekuja baada ya mbunge wa CCM wa Nyang'wale Hussein Amar kusimama na kuomba mwongozo wa Spika, huku akisema kuwa kuna wanawake waliokiuka kuvaa mavazi ya staha.

    Spika Ndugai alimpa nafasi mbunge huyo kumtaja mwenzake aliyevaa mavazi ambayo hayakuwa na staha ili iwe mfano na ndipo alipoashiria alipokaa mbunge huyo bila kumtaja jina.

    Hatahivyo Spika alisimama na kumtaka mbunge aliyevaa mavazi hayo asimame na aondoke ndani ya ukumbi ili akavae mavazi yenye staha ndipo atarejea tena bungeni.

  8. Waziri wa Uganda apigwa risasi na watu wasiojulikana karibu na nyumba yake

    Jenerali Katumba Wamala ni Kamanda wa zamani wa jeshi

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Jenerali Katumba Wamala ni Kamanda wa zamani wa jeshi

    Jenerali Katumba Wamala, Mkuu wa zamani wa Jeshi la Uganda na Waziri wa sasa wa Ujenzi na Uchukuzi amepigwa risasi na kujeruhiwa na watu wasiojulikana karibu na nyumba yake katika mji mkuu Kampala.

    Walioshuhudia wanasema watu hao wenye silaha walikuwa kwenye pikipiki.

    Kwa miaka michache iliyopita, nchi hiyo imekuwa ikikumbwa na mashambulizi kama hayo ya watu wenye silaha wanaoendesha pikipiki.

    Mnamo Juni 2018, Ibrahim Abiriga, mwanasiasa shupavu na aliyekuwa mfuasi wa Rais Museveni alipigwa risasi na kuuawa karibu na nyumba yake. Andrew Felix Kaweesi wakati huo akiwa Mkuu wa Operesheni wa Polisi aliuawa kwa njia kama hiyo mnamo Aprili 2017. Hakimu na maulama kadhaa wa Kiislamu waliuawa vivyo hivyo.

    Hakuna mauaji yoyote ambayo yamewahi kuchunguzwa kwa mafanikio au washukiwa kushtakiwa.

    Jerali Wamala alikuwa mkuu wa jeshi la UPDF mwaka 2013 hadi 2017baadaye akapewa cheo cha waziri wa ujenzi na uchukuzi i na kwa wakati huu ni mmoja wa wabunge 10 wanaowakirisha jeshi la UPDF katika bunge la 11. Mwaka 2001 hadi 2005 alikuwa mkuu wa jeshi la polisi IGP.

  9. Kenya yaonya kuwa huenda ikapiga marufuku kabisa safari za misaada ya kibinadamu Somalia

    Uhuru Farmaajo
    Maelezo ya picha, Rais wa Somalia Mohammed Farmaajo ( kushoto) na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wamekuwa wakikutana mara kwa mara kutanzua mizozo ambayo imekuwa ikiibuka baina ya nchi zao

    Kenya imeonya kuwa inaweza kuweka marufuku kabisa kwa ndege kutoka Somalia pamoja na zile za misaada ya kibinadamu.

    Wizara ya maswala ya kigeni ilisema katika barua kwa ujumbe wa kidiplomasia kwamba safari za misaada ya kibinadamu zinatumiwa vibaya kwa "mambo ya nchi hizo mbili na kisiasa" hata baada ya Kenya kusitisha safari zake.

    Hivi majuzi Kenya ilisitisha safari za ndege kutoka nchi hiyo jirani lakini ilisamehe safari za dharura za matibabu na zile zilizo kwenye shughuli za misaada ya kibinadamu za UN.

    Lakini sasa inaonya kuwa "safari za kibinadamu lazima zitumike kabisa kwa madhumuni ya kibinadamu ili kuepuka tangazo linalowezekana na serikali ya Kenya la kuzuiliwa kabisa kwa ndege zote".

    Wizara pia imehitaji ndege zote za misaada ya kibinadamu kutafuta kibali kwanza - na kutoa orodha ya abiria pamoja na bidhaa zinazosafirishwa.

    Kenya na Somalia zimekuwa katika mzozo wa kidiplomasia kwa muda mrefu, pamoja na mzozo wa mpaka wa baharini ambao umeendelea tangu 2014, wakati Mogadishu ilipoleta kesi dhidi ya Kenya katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

    Awali Somalia ilikata uhusiano wa kidiplomasia na Kenya mnamo Desemba, ikiishtumu kwa kuingilia masuala yake ya kisiasa ya ndani - kwa kuunga mkono utawala wa eneo lenye uhuru la Jubaland

    Mnamo Mei 6, ilisema kwamba uhusiano wa kidiplomasia umerejeshwa baada ya upatanishi wa Qatar lakini Kenya ilisitisha safari za ndege wiki kadhaa baadaye. Kenya inasema kwamba anga yake na Somalia bado imefungwa kwa sababu ya kukatika kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

  10. Wabunge wa AU watakiwa kuwa watulivu baada ya kukabiliana bungeni

    Kamishina Mkuu wa AU anasema ghasia zinachafua picha ya taasisi

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Kamishina Mkuu wa AU anasema ghasia zinachafua picha ya taasisi

    Mwenyekiti wa tume ya Muungano Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amewaomba wabunge wa bunge la Afrika "kurejesha utulivu wao" baada ya makabiliano kuripotiwa katika kikao cha bunge la AU Jumatatu.

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

    Ghasia ziliibuka katika vikao vilivyokuwa vimepangwa kwa ajili ya kumchagua kiongozi wa Muungano wa Afrika.

    Vyombo vya habari vya Afrika Kusini ambako vikao hivyo vilifanyika viliripoti kuwa wabunge walivutana mashati na makoti na kupigana makonde wakati wa ghasia hizo.

    SABC

    Chanzo cha picha, SABC

    Bunge hilo la Afrika, ni taasisi ya sheria ya Muungano wa Afrika.

    Limekuwa likipigia debe "mpango wa kuifanya Afrika kuwa Muungano wa mataifa ya Afrika".

  11. Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu mubashara leo tarehe Mosi Juni, 2021