Tanzania haitapeleka majeshi yake Msumbiji
Serikali ya Tanzania, imesisitiza kuhusu haja ya mazungumzo kama njia ya kuleta amani na utulivu nchini Msumbiji.
Moja kwa moja
Ambia Hirsi
Tanzania haitapeleka majeshi yake Msumbiji

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Watu wamelazimika kuhama makazi yao ambayo wengi yameharibiwa. (picha kutoka hifadhi) Tanzania imesema haitawapeleka wanajeshi wake nchini Msumbiji kukabiliana na wanamgambo katika eneo lenye utajiri wa mafuta la Cabo Del Gado ambalo liko karibu na mpaka wa na nchi hizo mbili, Gazeti la The Citizen linaripoti.
Badala yake serikali, imesisitiza kuhusu haja ya mazungumzo kama njia ya kuleta amani na utulivu nchini Msumbiji, na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia nchi hiyo na msaada wa maendeleo.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya nje wa Tanzania Liberata Mulamula, wakati wa ufunguzi wa mashauriano ya wiki mbili ya kujadili jinsi ya kudhibiti wanamgambo huko Cabo Delgado, yaliyoratibiwa na Kituo cha Sera ya Kimataifa (CIP), mjini Dar es Salaam.
Kamati ya kiufundi imependekeza Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kukipeleka kikosi cha wanajeshi 3 000 kitakachojumuisha wanajeshi wa ardhini, hewani na majini kusaidia katika juhudi za kukabiliana na wanamgambo.
Hatua ya kuingilia kati mzozo huo kijeshi ni ishara wazi kwamba uvamizi wa wanamgambo hao, ambao ulianza mwezi Oktoba 2017, umepita kiwango ambacho sio suala linaloweza kutatuliwa na Msumbiji kama taifa huru.
Soma zaidi:
- Kwanini ni vigumu kukabiliana na kundi la IS Msumbiji?
Maelfu ya wakazi wa Goma nchi DRC wakimbilia Rwanda

Maelfu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wamevuka mpaka na kuingia mji wa Gisenyi nchini Rwanda baada ya mamlaka ya jiji la Goma kutangaza kuondolewa kwa karibu thuluthi tatu ya wakazi wa mji huo, kwa kuhofia uwezekano wa mlima Nyiragongo kulipuka tena.
Wakazi wa Goma na wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa walionekana Alhamisi wakiondoka mji huo kuelekea Gisenyi nchini Rwanda.


Mamlaka nchini Rwanda wanawaelekea za watu hawa katika shule ya sekondari na kituo cha Nkamira ambacho kilikuwa kambi ya zamani ya wakimbizi vilayani Rubavu.
Wale ambao wanaazimia kueleka miji wa mashariki ya Musanze na mji mkuu wa Kigali wanaombwa kuwasilisha cheti cha kuonesha hawana ugonjwa wa Covid-19.
- Mlipuko wa Volkano Goma: ' Mume wangu alikuwa mgonjwa,sikuweza kumuokoa akaochomwa na lava'
Kiongozi wa mapinduzi ya Mali ajitangaza rais

Chanzo cha picha, AFP
Kiongozi wa zamani wa Baraza la jeshi nchini Mali, Kanali Assimi Goïta, amejitangaza kuwa rais wa mpito wa nchi hiyo baada ya kuwavua madaraka rais wa mpito na waziri mkuu wa zamani.
Rais Bah Ndaw na Waziri Mkuu Moctar Ouane sasa wameachiwa huru na jeshi.
Walipelekwa katika kambi ya kijeshi usiku wa Jumatatu katika hatua ambayo iliifanya Mali kukabiliwa na mapinduzi ya pili ya kijeshi ndani ya miezi tisa.
Hatua hiyo ilichochewa na mageuzi katika baraza la mawaziri ambapo maafisa wawili wa jeshi waliohusika na mapinduzi ya awali walipoteza kazi zao.
Kanali Goïta alilalamika kwamba rais aliyeondolewa madarakani hakushauriana naye kuhusu baraza jipya la mawaziri .
Hali ya taharuki imetanda nchini Mali hivi leo lakini kuna utulivu.
- Assimi Goïta afanya Mapinduzi ya pili ya kijeshi chini ya mwaka mmoja
Kagame: Maneno ya Macron 'yana thamani kuliko kuomba msamaha'

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema maneno ya Rais Macron yalikuwa ‘kitu chenye thamani kuliko msamaha’’baada ya Rais wa Ufaransa kutoomba msamaha rasmi kwa Rwanda kuhusu jukumu la nchi hiyo katika mauaji ya kimbari.
Katika hotuba aliyoitoa katika eneo la makumbusho ya mauaji ya kimbari mjini Kigali, Bw Macron aliomba msamaha kutoka kwa manusura, lakini hakuomba rasmi msamaha wa wazi kama ilivyotarajiwa.
"Maneno yake yalikuwa kitu ambacho ni zaidi ya msamaha. Yalikuwa ukweli," Kagame alisema katika mkutano wa pamoja baadae.
Egide Nkuranga, rais wa manusura wakuu' shirika la Ibuka, aliambia AFP amesikitika kwamba Macron "hakuomba msamaha kwa niaba ya nchi ya Ufaransa".
Hatahivyo Bw. Nkuranga alisema Macron "alijaribu sana kuelezea mauaji ya kimbari najukumu la Ufaransa.Ni muhimu sana. Inaonesha kwamba anatuelewa.", AFP inaripoti.
- Kwa nini Rwanda inasubiri kuombwa radhi na rais wa Ufaransa?
Nigeria: Watu kadhaa waliotoweka wahofiwa kufariki baada ya boti kuzama Nigeria

Makumi ya watu wanahofiwa kufariki kaskazini mwa Nigeria baada ya boti iliyokuwa na abiria 200 kuvunjika mara mbili na kuzama mtoni, maafisa wanasema.
Abiria wengi walikuwa wanawake na watoto waliokuwa wakisafiri kutoka jimbo la Niger kuelekea jimbo jirani la Kebbi.
Watu 20 wameripotiwa kuokolewa, huku mamlaka ikilaumu ajali hiyo ya Jumatano ilisababishwa na uzito kupita kiasi.
Wapiga mbizi na wafanyakazi wa dharura wamekuwa wakisaidia kuwaokoa wengine katika mto Niger, maafisa wa eneo hili waliiambia BBC.
Rais Muhammadu Buhari ameelezea kusikitishwa na ajali hiyo ''mbaya", na kutuma rambirambi zake kwa jamaa za waathiriwa.
Chuo Kikuu Uganda chasitisha masomo ya ana kwa ana kufuatia ongezeko la corona
Chuo Kikuu cha Kyambogo nchini Uganda kimesitisha masomo ya ana kwa ana baada ya visa vinane vya maambukizi ya corona kuthibitishwa katika chuo hicho.
Naibu Chansela Prof Elly Katunguka anasema baadhi ya wanafunzi wanaonesha dalili ya Covid-19 lakini wamekataa kufanyiwa vipimo.
Mamlaka nchi Uganda imeripoti kuongezeka kwa viwango vya maambuukizi katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
Jopokazi la serikali la kushughulikia janga la corona linatarajiwa kukutana leo kutathmini idadi ya walioambukizwa na huenda likatoa tahadhari zaidi.
Wizara ya afya imetangaza mwanzo wa wimbi la pili la maabukizi, huku idadi ya walioambukizwa ikifika 44,281 na zaidi ya watu 500,000 wakipewa chanjo.
Mbowe: Siwezi kujipendekeza kwa rais Samia,

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwenyekiti wa chama upinzani cha (Chadema) nchini Tanzania, Freeman Mbowe amesema Tanzania isitarajie mabadiliko kutoka kwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu kwani anatoka Chama Cha Mapinduzi ambacho kimeshika dola toka uhuru.
Katika mahojiano ya mtandaoni Mbowe amesema anataka kuona haki na si vinginevyo kwani anachokitaka ni haki na uhuru wa watu kwani viko kwa mujibu wa sheria.
''Demokrasia haitakiwi kutolewa kama zawadi Demokrasia inapiganiwa Pamoja na maumivu tunayo yapata tuna amini hiyo ndio safari halisi ya kuitafuta demokrasia” , alisema.
Mbowe anasema ni mapema sana kusema iwapo Tanzania ni salama sana kwa viongozi wa upinzani walioko ndani na nje ya nchi kwani bado viongozi wengi wa upinzani wanasota magerezani kwa kesi za kusingiziwa na wengine wamekimbia wakihofia usalama wao na serikali haijatoa tamko lolote kuhusiana na hali hiyo.
Pia anasema uhuru ambao umetolewa kama haki kwenye katiba bado umebinywa , akitoa mfano wa uhuru wa mikutano ya kisiasa, uhuru wa maandamano na hata vyombo habari kwani serikali inatumia sheria kuwanyima wananchi haki yao.
Licha ya kauli za Rais Samia kuleta faraja na matuamaini, Bwana Mbowe anasema kuna haja ya mabadiliko ya kisheria ili haki itendeke kwa mujibu wa sheria na sio huruma ya rais.
Mbowe anasema binafsi anatambua kauli njema za matumaini ambazo amezitoa Mama Samia na wanamheshimu kama mlezi na hata wanavyofanya siasa wana mipaka kwani wanamuheshimu kama mama.
Habari za hivi punde, Baraza la kijeshi nchini Mali lawaachia huru Rais na Waziri Mkuu
Viongozi wa kijeshi nchini Mali walioipindua serikali wamewaachilia huru Rais wa mpito Bah Ndaw na Waziri Mkuu Moctar Ouane.
Waliachiwa huru saa saba usiku wa Alhamisi, Mwandishi wa BBC Noel Ebrin Brou anaripoti.
Viongozi hao wawili wamekuwa wakizuiliwa katika kambi ya kijeshi tangu Jumatatu.
Walilazimishwa kujiuzulu baada ya kuvuliwa madaraka na jeshi - mapinduzi ya pili katika taifa hilo la Afrika Magharibi katika miezi tisa.
Maelezo zaidi:
- Mali :Assimi Goïta afanya Mapinduzi ya pili ya kijeshi chini ya mwaka mmoja
Rais Macron awasili Rwanda

Chanzo cha picha, Wizara ya Mambo ya nje Rwanda
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amewasili katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali, katika juhudi za kufufua uhusiano kati ya nchi hizo mbili ambao ulisambaratika kwa zaidi ya miongo miwili.
Wiki iliyopita katika mkutano wa kilele wa Paris kuhusu Afrika, Bwana Macron aliwaambia waandishi wa habari kwamba amekubaliana na Rais wa Rwanda Paul Kagame "kuanzisha ukurasa mpya wa mahusiano…"
Wizara ya maswala ya kigeni ya Rwanda imetoa picha za kuwasili kwa Bwana Macron.

Chanzo cha picha, Wizara ya Mambo ya nje Rwanda

Chanzo cha picha, Wizara ya Mambo ya nje Rwanda
Macron azuru Rwanda kurekebisha uhusiano wa kidiplomasia

Chanzo cha picha, AFP
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anazuru Rwanda katika jaribio la kufufua uhusiano ambao ulisambaratika kufuatia tuhuma juu ya jukumu la Paris katika mauaji ya kimbari ya 1994.
Ziara hiyo inafuatia hatua ya Ufaransa kutoa ripoti rasmi mwezi Machi inayokiri kuwa serikali ya wakati huo ya Francois Mitterrand "ilizembea" kwa kutotabiri mauaji hayo.
Ripoti hiyo, ambayo imekaribishwa Kigali, imeiondolea Ufaransa jukumu la moja kwa moja katika mauaji ya zaidi ya Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani.
Rais wa Rwanda Paul Kagame, Hivi karibuni alisema Wanyarwanda hawatasahau lakini wanaweza kuisamehe Ufaransa kwa jukumu lake na kuashiria kwamba Paris na Kigali zinaelekea kufungua ukurasa mpya wa historia ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Bwana Macron anatarajiwa kutembelea na kutoa hotuba kwenye kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya Kigali. Anatarajiwa pia kumteua balozi Ufaransa mjini Kigali - ambaye atakuwa wa kwanza katika kipindi cha miaka sita.
- Kwa nini Rwanda inasubiri kuombwa radhi na rais wa Ufaransa?
Maelfu ya watu wakimbia Goma kuhofia mlipuko mpya wa volkano

Chanzo cha picha, Reuters
Mamlaka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimeamuru wakaazi wa mji wa Goma ulio na watu milioni mbili kuondoka katika maeneo yao kwa hofu ya mlipuko wa pili wa volcano.
Siku ya Jumamosi, Mlima Nyiragongo ulilipuka na kusababisha maafa kwa maisha na mali za watu.
Amri ya watu kuondoka inakuja baada ya onyo kutolewa kuhusu uwezekano wa kutokea kwa milipuko mingine ya volcano katika mlima huo na chini ya Ziwa Kivu lililo karibu.
Tayari makumi ya maelfu ya wakaazi wa mji huo wameshayakimbia makaazi yao ili kunusuru maisha.
Kwa mujibu wa mamlaka ni wakazi wa wilaya 10 ambao wanahamishwa.
"Hii inaweza kutokea hata bila onyo lolote" na inaweza kuwaweka wakazi katika hatari inayohusishw ana mtiririko wa lava, alisema Jenerali Costant Ndima, Gavana wa kijeshi wa eneo la Kivu- Kaskazini .

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Uharibifu uliosababishwa na mlipuko wa Jumamosi "Shughuli ya uokoaji lazima ifanyike kwa umakini chini ya uratibu wa wafanyakazi wa kibinadamu.
"Watu watarejea nyumbani baada ya mapendekezo ya mamlaka ya," aliongeza.
Gavana wa jimbo hilo pia ametoa wito kwa wakazikukaa mbali na mtiririko wa lava.
Tunapendekeza watu wakae mbali na lava ambayo ni hatari na inaweza kuua mtu kukosa hewa au kuchoma.
Hatari zingine ni mchanganyiko wa maji na lava ni aina tofauti: mchanganyiko wa uji uji wa na maji ya ziwa, unapunguza kiwango cha gesi kinachoyeyushwa chini ya maji ya Ziwa Kivu, hali ambayo huenda ikasababisha kuenea kwa gesi hatari kwa watu walio karibu.
Wakazi wameshauriwa kuzingatia maelekezo wanayopewa na kuwa waangalifu
Pia wameombwa "kubeba vitu kidogo ili kila mmoja apate nafasi" katika magari ambayo yatatolewa na mamlaka ya mkoa katika kila wilaya.
Mlima Nyiragongo mara ya mwisho ulilipuka mwka 2002, kuua watu 250 na kuwaacha wengine 120,000 bila makao. Mlipuko hatari zaidi wa volkano ulifatokea mwaka 1977, ambapo zaidi ya watu 600 people walifariki.
- Mlipuko wa Volkano Goma: ' Mume wangu alikuwa mgonjwa,sikuweza kumuokoa akaochomwa na lava'
Karibu katika matangazo Mubashara leo Alhamisi 27.05.2021
