Hali ilivyokuwa: Mugabe ahutubia taifa kupitia runinga

Mugabe amelihutubia taifa moja kwa moja na kuashiria kwamba ataendelea kuongoza taifa hilo, ingawa amesema kwamba lazima kuwe na mabadiliko katika uongozi wa taifa hilo.

Moja kwa moja

  1. Tsvangirai ashangazwa na hatua ya Mugabe

    Wiki iliyopita, Tsvangirai alikuwa amemhimiza Mugabe ajiuzulu

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Wiki iliyopita, Tsvangirai alikuwa amemhimiza Mugabe ajiuzulu

    Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai ambaye wakati mmoja alihudumu kama waziri mkuu katika serikali ya umoja wa taifa na Rais Robert Mugabe ameambia shirika la habari la Reuters kwamba ameshangazwa sana na hotuba ya Mugabe.

    Sawa na baadhi ya raia wengine Zimbabwe, kiongozi huyo wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC) amesema alikuwa anamtarajia Mugabe, 93, ajiuzulu baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa serikali wiki iliyopita.

  2. Raia wa Zimbabwe washangazwa na hotuba ya Mugabe

    Raia wengi nchini Zimbabwe wameonekana kushangazwa na hotuba ya Bw Mugabe ambaye alitarajiwa na baadhi yao kujiuzulu.

    Hivi ndivyo hali ilivyokuwa baadhi ya maeneo nchini humo, wengi wakifuatilia hotuba hiyo moja kwa moja runingani:

    Mugabe

    Chanzo cha picha, AFP/Getty

    Mugabe

    Chanzo cha picha, AFP/Getty

    Zimbabwe

    Chanzo cha picha, EPA

    Zimbabwe

    Chanzo cha picha, AFP/Getty

    Zimbabwe

    Chanzo cha picha, AFP/Getty

    Zimbabwe

    Chanzo cha picha, AFP

  3. Maveterani wanataka Mugabe aondolewe

    Chris Mutsvangwa (kati) alikuwa amesherehekea hatua ya Mugabe kuvuliwa uongozi wa Zanu-PF mapema leo

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Chris Mutsvangwa (kati) alikuwa amesherehekea hatua ya Mugabe kuvuliwa uongozi wa Zanu-PF mapema leo

    Kiongozi wa chama chenye ushawishi cha maveterani wa vita vya ukombozi wa Zimbabwe Chris Mutsvangwa, ameambia shirika la habari la AFP kwamba sasa Robert Mugabe huenda akaondolewa madarakani baada yake kukosa kujiuzulu leo.

    Amesema hotuba ya kiongozi huyo haijazingatia uhalisia.

    "Tutafuata njia ya kumuondoa madarakani na tunawataka watu warejee tena barabarani kuandamana."

    Maveterani walikuwa wakati mmoja wafuasi sufu wa Bw Mugabe.

    Waliongoza uvamizi wa mashamba yaliyomilikiwa na Wazungu mwaka 2000 na wametuhumiwa kwa kutumia ghasia na fujo uchaguzini kumsaidia Mugabe kusalia madarakani.

    Lakini mwaka jana, waliacha kumuunga mkono.

  4. Mugabe 'atakuwa mgumu' kumtoa madarakani

    Dkt Sue Onslow kutoka Taasisi ya Masomo ya Jumuiya ya Madola jijini London ameambia BBC kwamba amefuatilia hotuba ya Rais Mugabe "kwa mshangao".

    Anasema Mugabe alikuwa akitoa ishara za kutojali kwenye hotuba yake na "kusisitiza kuheshimiwa kwa katiba".

  5. Mugabe amaliza hotuba bila kujiuzulu

    Wengi walitarajia kwamba Rais Robert Mugabe angetumia hotuba yake ya moja kwa moja kwenye runinga kujiuzulu, hasa baada ya kuvuliwa uongozi wa chama cha Zanu-PF.

    Lakini hilo halijafanyika.

    Badala yake amesema ni yeye atakayeongoza mkutano mkuu wa chama hicho wiki chache zijazo.

    Amewahimiza raia wa Zimbabwe kuvumiliana na kusameheana.

  6. Mugabe: Asante Sana

    Mugabe amemalizia hotuba yake kwa shukrani kwa lugha kadha, miongoni mwake amesema 'Asante sana'.

    Msikilize hapa:

  7. Hatuwezi kuongoza na machungu na kulipiza kisasi

    Bw Mugabe amesema: "Hatuwezi kuongozwa na machungu au ulipizaji kisasi, hayawezi kutufanya wanachama wema au raia wema.

    "Sera yetu ya maridhiano tuliyotangaza miaka ya 1980 ambayo tulitumia hata kwa waliotudhalilisha kwa miaka mingi na tuliopigana haiwezi kosa kutumiwa kwa wenzetu - ndani ya chama na hata nje.

    "Lazima tujifunze kusameheana na kutatua mizozo yetu, halisi na ya kudhaniwa. Kwa urafiki.

    "Tusonge mbele, tukijikumbusha kuhusu kauli mbiu yetu ya wakati wa vita."

  8. Uongozi wa 'kiimla' lazima ukome

    Enzi ya kuwalaumu baadhi ya watu na maamuzi ya kiimla sharti ikome.

    "Lazima tutambue kwamba Zanu-PF ni chama cha utamaduni na kimeongoza na utamaduni wa muda mrefu wa maadili ambao lazima uendelee," amesema.

    "Masuala ya mizozo ya marika ni lazima itatuliwe kwa kuoanisha kwa njia nzuri wale wazee na wale wa vizazi vipya kwa kufuata mfumo unaoeleweka wa kutoa amri na urithi."

    Amesema hayo yatajadiliwa katika mkutano mkuu ujao wa chama kuondoa shaka na mambo ambayo yameathiri chama hicho.

    "Mkutano utafanyika wiki chache zijazo. Nitaongoza shughuli zake," amesema.

  9. Waliopigania uhuru watatekeleza mchango muhimu

    Mugabe amesema kunao waliopigania uhuru ambao bado wapo na kwamba ni lazima waendelee kutekeleza mchango muhimu katika uongozi wa taifa.

    Amesema ni muhimu kuwalipa.

  10. 'Mizozo sasa itakoma, na raia watafaidi'

    Amesema mizozo na mivutano ambayo ilikuwa imekwamisha shughuli nyingi nchini humo sasa itakoma.

    Serikali itajizatiti kuimarisha hali ya wananchi kiuchumi na kimaendeleo.

    Amesema serikali itazindua mpango mkubwa wa ujasiamali wa kuwafaa hata raia maeneo ya mashinani.

  11. Nguzo za serikali zilisalia kuwa imara

    Mugabe amesema hata wakati wa mzozo wa sasa, mfumo wa mamlaka uliendelea kuheshimiwa. Amesema hilo lilidhihirika pia hata katika mkutano wa leo.

  12. Mugabe: Yaliyotokea yamedhihirisha msingi wa amani

    Amesema yaliyotokea wiki iliyopiya yamedhihirisha msingi wa amani na demokrasia nchini Zimbabwe.

    Aidha, kujitolea kwa watu wa Zimbabwe kutatua mizozo kwa amani - jambo ambalo ni nadra sana katika nchi nyingine.

    "Ni rasilimali muhimu sisi hutumia nyakati za dhiki," amesema.

  13. Habari za hivi punde, Mugabe aanza kuhutubia taifa

    Mugabe ameanza kuhutubia taifa moja kwa moja kupitia runinga ya taifa ZBC.

  14. Mugabe kuhutubia taifa

    Karibu kwa taarifa za moja kwa moja. Kituo cha matangazo cha serikali kinasema kuwa Rais Robert Mugabe atahutubia taifa muda mfupi unaokuja.

    Mugabe akimsalimia mkuu wa jeshi la wanahewa Perence Shiri

    Chanzo cha picha, AFP/Getty

    Maelezo ya picha, Mugabe alikutana na wakuu wa jeshi ambao wamechukua udhibiti wa serikali mapema leo