Marekani na Iran zarejea kushambuliana baada ya shambulio la Larak
Iran yasema imedungua droni na kushambulia wanajeshi wa Marekani nchini Jordan
Muhtasari
- Iran imeshindwa katika vita vinavyoendelea - Trump
- Denise Dusauchoy, mkosoaji wa serikali ya DRC, akamatwa Tanzania
- China yakataa tuhuma za kuficha taarifa kuhusu mafuriko Nepal
- Dolly Parton azikwa Nashville, karibu na mumewe
- Bei ya mafuta yapanda zaidi ya asilimia 2 baada ya shambulio la Marekani Larak
- Shirika la ndege la Kenya Airways latangaza ucheleweshaji wa safari kwa zaidi ya saa sita
- Iran yasema imeshambulia vituo vya Marekani vilivyoko Jordan na UAE baada ya shambulio la Larak
- IRGC: Meli kubwa ya mafuta yashika moto katika Mlango-Bahari wa Hormuz baada ya kushambuliwa
- Abiria walala JKIA huku mgomo wa wafanyakazi wa sekta ya anga ukiendelea
- Trump atoa video ya shambulio dhidi ya kisiwa cha Kharg iliyotengenezwa kwa akili mnemba (AI)
- Familia 32 za Kenya zitagawana fidia ya Ethiopian Airlines
- Watu wanane wafariki na wengine 18 hawajulikani walipo baada ya kivuko kupinduka karibu na pwani ya Cyprus
- Mamia ya raia wa kigeni bado hawajulikani walipo katika eneo la mpaka Nepal
- Nepal yaimarisha juhudi za kuwanusuru mamia ya watu waliokwama mahandaki ya umeme
- Marekani yashambulia mitambo ya kurushia makombora vya Iran kwenye Kisiwa cha Larak
Moja kwa moja
Abdalla Seif Dzungu & Mariam Mjahid
Barcola ajiunga na Liverpool kwa dau la hadi pauni milioni 123

Chanzo cha picha, Getty Images
Liverpool imekamilisha usajili wa mshambuliaji wa Ufaransa, Bradley Barcola, kutoka Paris Saint Germain kwa dau linaloweza kufikia pauni milioni 123.
Liverpool italipa pauni milioni 106 mwanzoni, huku pauni milioni 17 zikilipwa kama bonasi kulingana na masharti ya mkataba.
Barcola, mwenye umri wa miaka 23, amesaini mkataba wa miaka mitano na kuwa mchezaji wa tano kusajiliwa na Liverpool katika dirisha hili la usajili.
Mshambuliaji huyo ambaye atavaa jezi namba 29, hupendelea kucheza upande wa kushoto wa safu ya ushambuliaji, lakini anaweza pia kucheza katika nafasi nyingine za ushambuliaji.
Msimu uliopita, Barcola alifunga mabao 13 na kutoa pasi saba za mabao katika mechi 49 kwa PSG katika mashindano yote.
Pia alicheza mechi zote nane za Ufaransa katika Kombe la Dunia la 2026, akifunga mabao matatu huku Les Bleus wakifika mechi ya kuwania nafasi ya tatu.
Barcola alijiunga na PSG akitokea Lyon mwaka 2023 kwa ada ya takriban pauni milioni 38.5, na amesaidia klabu hiyo kushinda mataji matatu ya Ligue 1 na Ligi ya Mabingwa mara mbili, miongoni mwa mataji mengine.
Iran imeshindwa katika vita vinavyoendelea - Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump amesema Iran imeshindwa katika vita vinavyoendelea, akidai nchi hiyo sasa iko katika hali ya udhaifu mkubwa na migogoro inayozuia kuwa na ushawishi mkubwa duniani.
Katika ujumbe kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump ameita Iran nchi iliyofeli, akidai haina jeshi la anga na jeshi la wanamaji lenye uwezo, sarafu yake imedhoofika na serikali imeshindwa kulipa vikosi vyake vya usalama.
Trump pia amesema mfumuko wa bei nchini humo umepanda kwa kasi, huku akiwatuhumu viongozi wa Iran kwa kushindwa kuiwakilisha nchi ipasavyo.
Aidha, ameituhumu serikali ya Iran kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji na kuwataka viongozi wake wawajibishwe kwa madai ya uhalifu wa kivita na ukiukaji wa haki za binadamu.
Kauli hiyo inakuja wakati Marekani na Iran zikirejea kushambuliana, baada ya Marekani kufanya mashambulizi dhidi ya vituo vya makombora vya Iran katika Kisiwa cha Larak, kwenye Mlango wa Hormuz. Iran ilijibu kwa kulenga vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Jordan.
Denise Dusauchoy, mkosoaji wa serikali ya DRC, akamatwa Tanzania

Chanzo cha picha, SOCIALS
Denise Mukendi Dusauchoy, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ubelgiji, ameripotiwa kukamatwa nchini Tanzania.
Dusauchoy anajulikana nchini DRC kama mwanasiasa na mtu mashuhuri kwenye mitandao ya kijamii na amewahi kuhusishwa na shughuli za kisiasa za Alliance Fleuve Congo, AFC, pamoja na kundi la waasi la M23.
Vyanzo kadhaa vya habari nchini DRC vinasema amekamatwa nchini Tanzania na baadaye kuhamishiwa Dar es Salaam, huku mamlaka za Congo zikitarajiwa kuomba arejeshwe nchini humo ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
Hata hivyo, mazingira kamili ya kukamatwa kwake, mashtaka rasmi yanayomkabili na iwapo ombi rasmi la kurejeshwa kwake limewasilishwa bado hayajawekwa wazi na mamlaka za Tanzania au DRC.
Dusauchoy amekuwa akijulikana kwa kauli kali dhidi ya viongozi na mamlaka za Congo, huku katika kipindi cha hivi karibuni akihusishwa hadharani na AFC na M23.
China yakataa tuhuma za kuficha taarifa kuhusu mafuriko Nepal

Chanzo cha picha, Getty Images
China imekanusha tuhuma za kuficha taarifa kuhusu mafuriko yaliyosababisha vifo na uharibifu mkubwa katika mpaka wake na Nepal.
Beijing imesema taarifa kuhusu hali ya maafa zimetolewa kwa njia iliyo wazi, ya uwazi na kwa wakati.
Kauli hiyo imekuja baada ya BBC kuripoti madai kwamba video zinazoonyesha uharibifu mkubwa katika eneo la Gyirong Port, mojawapo ya vivuko muhimu vya mpaka kati ya Tibet na Nepal, zilikuwa zikidhibitiwa nchini China.
Kufikia sasa, ni picha moja pekee ya tukio hilo iliyoonyeshwa katika taarifa kuu ya televisheni ya serikali ya China.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Guo Jiaqun, amesema juhudi za uokoaji na kukabiliana na maafa zinaendelea kwa dharura lakini kwa utaratibu.
Amesema pia jaribio lolote la kutumia maafa hayo kuichafua China au kutia chumvi hali hiyo halitapata uungwaji mkono.
Hata hivyo, ripoti ya Reuters imeonyesha kuwa maafisa wa Nepal walikuwa wameomba taarifa zaidi kutoka China kuhusu hatari za barafu na viwango vya maji, lakini hawakupokea taarifa zote walizohitaji.
Taarifa hiyo inazidisha maswali kuhusu kiwango cha ushirikiano wa nchi hizo katika kutoa tahadhari za mapema wakati wa majanga ya asili.
Dolly Parton azikwa Nashville, karibu na mumewe

Chanzo cha picha, Getty Images
Gwiji wa muziki wa Marekani, Dolly Parton, amezikwa katika mazishi ya kifamilia yaliyofanyika kwa faragha mjini Nashville, siku chache baada ya kifo chake akiwa na umri wa miaka 80.
Parton amezikwa kando ya kaburi la mumewe, Carl Dean, katika eneo la Woodlawn Memorial Park and Mausoleum, Nashville, Tennessee.
Mpwa wake mkubwa, Lainey Parton, ametoa heshima zake kwa mwimbaji huyo, akisema ''bado ni vigumu kuamini kwamba ameondoka na kwamba atakumbuka sauti yake, kicheko chake na kumbatio lake''.

Chanzo cha picha, Reuters
Bei ya mafuta yapanda zaidi ya asilimia 2 baada ya shambulio la Marekani Larak

Chanzo cha picha, Getty Images
Bei ya mafuta duniani imepanda kwa zaidi ya asilimia 2 baada ya Marekani kushambulia vituo viwili vya kurushia makombora katika Kisiwa cha Larak, kwenye Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Bei ya mafuta aina ya Brent imepanda kwa dola 2.22, sawa na asilimia 2.52, hadi dola 90.32 kwa pipa. Mafuta ya Marekani aina ya West Texas Intermediate, WTI, yamepanda kwa dola 2.10, sawa na asilimia 2.41, hadi dola 85.41 kwa pipa.
Kupanda kwa bei kunachangiwa na hofu kwamba kuongezeka kwa mapigano kati ya Marekani na Iran kunaweza kuvuruga usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa nishati duniani.
Shambulio la Jumapili lilikuwa hatua ya kwanza ya wazi inayojulikana ya Marekani kuishambulia Iran tangu mwishoni mwa Julai.
Pia unaweza kusoma:
Shirika la ndege la Kenya Airways latangaza ucheleweshaji wa safari kwa zaidi ya saa sita

Shirika la ndege la Kenya Airways limesema mgomo unaoendelea wa wafanyakazi wa sekta ya anga nchini Kenya umesababisha usumbufu wa safari katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA, huku baadhi ya safari zikichelewa kwa zaidi ya saa sita.
Katika taarifa yake Jumatatu, Kenya Airways imesema baadhi ya safari zimelazimika kupangwa upya kutokana na mrundikano wa safari uliosababishwa na mgomo huo.
Abiria wanaosafiri na shirika hilo wameelekezwa kwenda uwanja wa ndege baada ya kuthibitisha safari zao pamoja na hali ya ndege zao.
Wale wanaotaka kubadili muda wa safari wameelezwa kuwa wanaweza kufanya hivyo bila kutozwa ada ya ziada.
Kenya Airways imesema timu zake zinaendelea kushughulikia mrundikano wa safari ili kupunguza athari za mgomo huo kwa abiria.
Hatua hiyo ya wafanyakazi wa anga ilianza Jumapili, baada ya wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Anga Kenya, KAWU, kuanza mgomo wa kupunguza kasi ya kazi katika viwanja vya ndege nchini.
Wafanyakazi hao wanadai kuboreshwa kwa maslahi yao, mazingira bora ya kazi na kutekelezwa kwa makubaliano ya awali kuhusu mafao ya ajira.
Soma Zaidi Hapa:
Iran yasema imeshambulia vituo vya Marekani vilivyoko Jordan na UAE baada ya shambulio la Larak

Chanzo cha picha, Getty Images
Iran imesema imeshambulia vituo vya Marekani nchini Jordan pamoja na maeneo ya kijeshi ya Marekani katika kambi ya anga ya Al Minhad nchini Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE, baada ya vikosi vya Marekani kushambulia kurunzi mbili za roketi katika Kisiwa cha Larak nchini Iran.
Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC, wamesema shambulio hilo la Marekani dhidi ya Kisiwa cha Larak liliwaua na kuwajeruhi wanajeshi kadhaa wa Iran pamoja na raia, kwa mujibu wa shirika la utangazaji la serikali, IRIB.
Hata hivyo, Wizara ya Ulinzi ya UAE imekanusha madai ya Iran kwamba Kambi ya Anga ya Al Minhad ililengwa.
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema Tehran haitafuti vita, lakini haiwezi kukaa kimya inaposhambuliwa.
Wakati huo huo, vikosi vya Israel vimefanya operesheni kubwa katika mji wa Nablus, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, ambapo Wapalestina wawili wameripotiwa kuuawa.
Soma Zaidi Hapa:
Abiria walala katika uwanja wa ndege wa JKIA nchini Kenya huku mgomo wa wafanyakazi wa sekta ya anga ukiendelea
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Laillah Mohammed
- Nafasi, BBC Swahili

Chanzo cha picha, Getty Images
Shughuli za usafiri zimeendelea kutatizika katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jommo Kenyatta nchini Kenya kwa siku ya pili Jumatatu hii, maelfu ya wasafiri wakilalamikia kuahirishwa kwa safari zao au nyingine kukwama wasijuwe watasafiri lini.
Uwanja huu ndio wenye shughuli nyingi kabisa katika ukanda wa Afrika Mashariki na maziwa makuu, ukiwa na wasafiri 13,000 kila siku, huku watu milioni 8.6 wakisafiri kupitia uwanja huo kila mwaka huku ndege 200 zikitua uwanjani humo na nyingine 195 zikiondoka.
Baadhi ya wasafiri wameelezea mahangaiko ya kusubiri hadi saa 10 katika uwanja wa ndege ili kusafiri.
Hapo jana mamlaka ya kusimamia viwanja vye ndege KAA ilitoa taarifa kusema kuwa inashughulikia suala hilo kupunguza mahangaiko ya wasafiri katika viwanja vya ndege lakini hali hiyo imeendelea kukumba viwanja vyote vya ndege vya umma nchini Kenya kutokana na mgomo wa wafanyakazi wa viwanja vye ndege.
Akizungumza na BBC mapema Jumatatu, Bwana Moss Ndiema amesema kwamba wana mengi ya kulalamikia ila masuala makuu matatu yamewalzaimu kurejelea mgomo miezi michache tu baada ya KAWU kuafikiana na serikali ya Kenya kusitisha mgomo mwingine.
Kulingana na KAWU, Mamlaka ya kudhibiti mishahara ya watumishi wa umma nchini Kenya SRC iliiamrisha Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya KCAA kutumia moja kati ya mikataba mitatu ya makubaliano yaliyotiwa Saini kati ya 2015 na 2025.
Mpango huu ungeangazia suala la nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi wa viwanja wa ndege ambao wamelalamikia kutopata nyongeza hiyo tangu 2015.
Hatua ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya kusimamia viwanja vya ndege KAA Moses Wekesa kuwatumia maafisa wa huduma ya vijana NYS kutekeleza majukumu ya Ulinzi wa viwanja ambao KAWU imesema ni jukumu la maafisa wa KAA limewakera mno wakimtaka kuondolewa kazini kwa ajili ya kile wamekitaja kama kiburi na dharau kwao.
Suala la tatu ambalo wamesema ni muhimu kwao ni wafanyakazi wa kampuni ya ndege ya Jambo Jet ambayo inamilikiwa na shirika la ndege nchini Kenya – Kenya Airways. Jambo Jet imedaiwa kutowaruhusu wafanyakazi wake kujiunga na vyama vya wafanyakazi kama vile KAWU , hali ambayo wamedai inawanyimanafasi ya kutetea haki zao ambazo KAWU inasema inadhulumiwa kazini.
Na japo Katibu Mkuu Ndiema amesema wasafiri wanaendelea kuhangaika uwanjani kwa kuwa safari zao zimeahirishwa au kukwama, inawabidi kufanya hivyo kwa ajili ya kupata haki yao ya kikatiba.
‘Ni masikitiko makubwa lakini hatuna budi ila kuilazimu serikali kuketi nasi chini mezani na kutatua mzozo huu ambao sasa tunahisi umekuwa mbaya zaidi kwetu,’ alisema Bwana Ndiema kwenye mahojiano ya simu n BBC.
Katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, wasafiri waliendelea kulalmikia kukwama kwa siku ya pili Jumatatu.
Siku ya Jumapili wengi waliwaeleza wanahabari kuhusu hali ya kukata tamaa. Kulingana na badhi ya wasafiri, hali hiyo iliwapata kwa mshtuko mkubwa.
Nicole Jepkorir, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 24 anayesoma katika chuo kikuu nje ya Kenya amesema; "Tulitakiwa kuondoka saa kumi jioni leo, lakini kutokana na usumbufu na maandamano yaliyokuwepo hapa asubuhi ya leo, tutaondoka saa sita usiku. Hali hii inaleta usumbufu mkubwa kwa sababu tulifika hapa mapema sana asubuhi.
Tulitakiwa kuwa tumekamilisha taratibu za kuingia kwenye ndege (check-in) kufikia sasa, lakini hatuwezi kufanya hivyo. Hatuna la kufanya kwa sababu KAA [Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya] inapaswa kupokea ndege ili ziweze kuja kutuchukua na kuondoka; kwa hivyo hakuna kinachoendelea. Tunapata taarifa kwa kuchelewa; kama tungeambiwa mapema, tusingekuja hapa. Labda tungekuja wakati ambao tulitakiwa kuondoka."
Naye William Obino, ambaye ni mwanafunzi pia amesema,"Tulitakiwa kukamilisha taratibu za kuingia kwenye ndege (check-in) majira ya saa sita mchana na kuondoka saa kumi jioni, lakini safari yetu ya ndege sasa imecheleweshwa hadi saa sita usiku. Kuna watu wengi waliokwama hapa, ikiwemo sisi wenyewe, kwa hivyo ni jambo la kusikitisha sana."
William Obino, mwenye umri wa miaka 22 amesema kwamba ;"Imetuathiri sana kwa sababu inavuruga ratiba yetu; tulikuwa na ratiba iliyopangwa kwa ajili ya siku zote za safari yetu, na sasa kutokana na kuchelewa huku, huenda tukalazimika kuondoa baadhi ya mambo kwenye ratiba hiyo."
Hazikizimana Lolewi Spoil, mfanyabiashara kutoka Rwanda amesema ; "Nilipaswa kusafiri saa 11 jioni, lakini nilipofika hapa, nilipokea barua pepe ikisema kuwa kuna ucheleweshaji na kwamba safari yangu ya ndege imeahirishwa hadi saa 5 usiku. Nilipomuuliza mmoja wa wafanyakazi, aliniambia ni kweli, na kwamba tunapaswa kuwa na subira na kusubiri hadi wakati huo."
KAWU imesema inatarajiwa kukutana na Waziri wa uchukuzi wa umma nchini Kenya davis Chirchir, Katibu wake Teresiah Mbaika, Maafisa kutoka wizara ya Leba, Maafisa wa Mamlaka za KCAA na KAA na Katibu Mkuu wa vyama vya wafanyakazi nchini kenye, COTU Francis Atwoli kujaribu kutatua mzozo uliopo..

Trump atoa video ya shambulio dhidi ya kisiwa cha Kharg iliyotengenezwa kwa akili mnemba (AI)

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Kisiwa cha Iran cha Kharg Rais wa Marekani Donald Trump amechapisha video iliyotengenezwa kwa teknolojia ya akili mnemba (AI) kwenye mtandao wa Truth Social, ikionyesha kituo kikubwa cha mafuta kikilipuka na kuungua.
Bw. Trump aliandika katika maelezo ya video hiyo: "Kisiwa cha Kharg kinaharibiwa kabisa na kusawazishwa na ardhi!!!"
Video hiyo imetoka wakati ambapo mivutano ya kijeshi kati ya Iran na Marekani imepamba moto kwa wakati mwengine.
Hapo awali, vikosi vya Marekani vililenga mifumo miwili ya kurushia makombora ya Iran kwenye Kisiwa cha Larak, na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi lilitangaza kuwa lilijibu mashambulizi hayo kwa kulenga kambi mbili za Marekani nchini Jordan kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani (drones).
Kisiwa cha Kharg ni mojawapo ya vituo muhimu zaidi vya Iran vya kusafirisha mafuta nje ya nchi katika Ghuba ya Uajemi, na sehemu kubwa ya mauzo ya nje ya mafuta ghafi ya nchi hiyo hufanyika kupitia vituo vilivyoko kisiwani humo.
Familia 32 za Kenya kugawanya fidia ya ndege ya Ethiopian Airlines iliopata ajali
Karibu miaka saba baada ya ndege ya Ethiopian Airlines Nambari 302 kuanguka ikiwa safarini kuelekea Nairobi, familia 32 za Kenya zinatarajiwa kupokea malipo mapya ya fidia kufuatia kesi ndefu dhidi ya kampuni ya kutengeneza ndege ya Boeing katika mahakama za Marekani.
Kila familia itapokea dola milioni 2.73, sawa na takriban Shilingi milioni 353, chini ya mpango wa hivi karibuni wa fidia kutokana na ajali hiyo ya Machi 2019. Malipo hayo mapya yanafikia jumla ya dola milioni 87.36, au takriban Shilingi bilioni 11.3, kwa kaya hizo 32 za Kenya zilizoathirika.
Ikijumuishwa na fidia iliyolipwa katika hatua za awali za mchakato wa kisheria, jumla ya fedha ambazo familia hizo zitapokea inakadiriwa kuwa Shilingi bilioni 17.3.
Ndege hiyo nambari 302 ilianguka tarehe 10 Machi 2019, dakika sita baada ya kupaa kutoka Addis Ababa, Ethiopia, ikiwa safarini kuelekea Nairobi.
Abiria na wahudumu wote 157 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walipoteza maisha katika ajali hiyo. Kenya ilirekodi idadi kubwa zaidi ya vifo miongoni mwa raia wa mataifa zaidi ya 30 waliokuwemo kwenye ndege hiyo.
Makubaliano hayo ya hivi karibuni ya fidia yanakuja kufuatia kesi zilizofunguliwa nchini Marekani, ambapo familia hizo zilidai fidia kutoka kwa Boeing kuhusiana na ajali hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, familia hizo zilipata hadhi ya kisheria kama waathiriwa wa uhalifu ndani ya mfumo wa haki ya jinai wa Marekani baada ya Boeing kushutumiwa kwa kuwapotosha wadhibiti wa sekta hiyo.
IRGC: Meli kubwa ya mafuta yashika moto katika Mlango-Bahari wa Hormuz baada ya kushambuliwa

Chanzo cha picha, Dutch Coastguard
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (IRGC) linasema kuwa "meli ya mafuta iliyokuwa ikijaribu kupita katika njia isiyo halali kusini mwa Mlango-Bahari wa Hormuz ilishika moto na kusimama baada ya kushambuliwa na makombora miwili ya baharini"
Katika taarifa iliyochapishwa na vyombo vya habari vya Iran, IRGC ilionya: "Hatima ya meli zinazokiuka kanuni za usalama za Mlango-Bahari wa Hormuz haitakuwa tofauti na hii."
Haijulikani wazi jina la meli hiyo au nchi inayomiliki meli hiyo.
IRGC imezitaka meli zinazopita katika Mlango-Bahari wa Hormuz "kuzingatia kikamilifu kanuni zilizotolewa na Jeshi la Wanamaji la IRGC kuhusu upitaji na usafiri wa baharini," na kuzishauri zisiruhusu "kudanganywa" na Marekani kupita njia nyingine, wala kuziweka mali na maisha ya wafanyakazi wa meli hizo katika hatari ya uharibifu usio wa lazima.
Mamia ya raia wa kigeni bado hawajulikani walipo katika eneo la mpaka Nepal

Chanzo cha picha, RSS
Watalii kutoka kote duniani huja Nepal kwa ajili ya milima na maeneo yake matakatifu.
Taarifa kuhusu watu hao waliopotea ni kama ifuatavyo:
- India - Takriban raia 320 wa India hawajulikani walipo, kulingana na wizara ya mambo ya nje mjini Delhi
- China - Wizara ya mambo ya nje ya China inasema karibu raia 100 wa China hawajulikani walipo nchini Nepal
- Marekani - Wamarekani 90 bado hawajulikani walipo, kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani
- Ukraine - Raia 62 wa Ukraine hawajulikani walipo, polisi wa Nepal wanasema
- Malaysia - Raia 51 wa Malaysia waliokuwa wakisafiri na kampuni ya Fishtail Tours and Travels hawajulikani walipo kufuatia mafuriko, maafisa wanasema
- Australia - Hakuna taarifa kuhusu walipo raia 41 wa Australia, kulingana na naibu waziri wa uhamiaji wa nchi hiyo
- Uingereza - Polisi wa Nepal wanasema raia 33 wa Uingereza hawajulikani walipo; shirika la utangazaji la serikali ya China, CCTV, pia linaripoti kuwa raia 15 wa Uingereza ni miongoni mwa waliopotea huko Tibet - haijulikani ni wangapi kati yao ambao tayari wamejumuishwa katika takwimu zilizotolewa na Nepal
- Canada - raia 30 wa Canada hawajulikani walipo, wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo inasema
- Idadi ndogo ya wasafiri kutoka Korea Kusini, Afrika Kusini, Ureno, Uholanzi na New Zealand pia ni miongoni mwa waliopotea.
Nepal yaimarisha juhudi za kuwanusuru mamia ya watu waliokwama katika mahandaki ya umeme

Chanzo cha picha, Reuters
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Nepal imesema kuwa juhudi za uokoaji katika handaki kwenye mradi wa umeme wa maji wa Trishuli-3A zimeongezewa nguvu, zikijumuisha shughuli za ulipuaji.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, ofisi hiyo imesema kuwa timu ya pamoja ya watu 90 imetumwa eneo la tukio, ikijumuisha vikosi vya usalama, polisi, na waokoaji wanaoambatana na mbwa waliofunzwa.
Awali, shimo lenye ukubwa wa futi 2 kwa 3 (mita 0.6 kwa 0.9) lilitengenezwa kwenye sehemu ya juu ya handaki, na waokoaji wakashuka chini kwa kutumia kamba. Hawakupata majibu yoyote kutoka ndani walipopiga kelele kuita.
Shughuli za uokoaji zinaendelea, huku timu hiyo ikifanya kazi bila kuchoka usiku na mchana licha ya kuwepo kwa mazingira magumu na hatari, ofisi ya Waziri Mkuu imesema.
Miongoni mwa watu zaidi ya 2,500 waliopotea, mamia wanadhaniwa kuwa ni wafanyakazi katika miradi ya umeme wa maji nchini Nepal.
Marekani yashambulia mitambo ya kurushia makombora ya Iran kwenye Kisiwa cha Larak

Chanzo cha picha, Reuters
Vikosi vya Marekani vimeshambulia mitambo miwili ya kurusha makombora ya Iran, afisa mmoja wa Marekani amesema, akiashiria mashambulizi ya kwanza yanayojulikana ya Marekani dhidi ya Iran tangu mwishoni mwa Julai.
"Vikosi vya Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) vilionekana vikijiandaa kurusha makombora yenye mabomu ya baharini kwenye Mlango wa Hormuz," mshirika wa BBC wa Marekani CBS News alimnukuu msemaji wa Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) Cdr Tim Hawkins akisema.
IRGC ilisema shambulio la Jumapili liliua na kujeruhi watu kadhaa, na kuapa "kulipiza kisasi".
Baadaye ilisema ilizindua shambulio dhidi ya malengo ya kijeshi ya Marekani huko Jordan, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya Iran.
BBC imewasiliana na Centcom kwa maoni.
Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja



















