Zelensky anataka kuonyesha uungwaji mkono katika mkutano mkubwa wa amani wa Ukraine

Wikendi hii, eneo la mapumziko la Uswizi lililotengwa juu ya Ziwa Lucerne litashuhudia makumi ya viongozi wa dunia na maelfu ya askari na polisi wakishuka Bürgenstock.

Muhtasari

  • Hakimu wa Kenya afariki baada ya kupigwa risasi na polisi
  • Mshambulizi wa zamani wa Arsenal na Everton Campbell afariki akiwa na umri wa miaka 54
  • Marekani iyaliwekea vikwazo kundi la Israel linalosema kushambulia misafara ya misaada ya kibinadamu inayoelekea Gaza
  • Marekani imeliwekea vikwazo kundi la Israel linalosema kushambulia misafara ya misaada ya kibinadamu inayoelekea Gaza.
  • Mchekeshaji maarufu wa Kenya Fred Omondi afariki katika ajali Nairobi
  • Bintimfalme Kate aonekana kwenye hafla ya kwanza ya umma tangu mwanzo wa matibabu ya saratani
  • Cyril Ramaphosa amechaguliwa tena kuwa rais wa Afrika Kusini
  • Zelensky anataka kuonyesha uungwaji mkono katika mkutano mkubwa wa amani wa Ukraine

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi

  1. Hakimu wa Kenya afariki baada ya kupigwa risasi na polisi

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Kando na mpiga risasi, maafisa watatu wa polisi walijeruhiwa katika shambulio hilo

    Hakimu wa Kenya aliyepigwa risasi na afisa mkuu wa polisi mapema wiki hii amefariki, kwa mujibu wa jaji mkuu wa nchi hiyo.

    Jaji Martha K Koome aliandika kwenye X, ambayo zamani ilikuwa Twitter, kwamba Hakimu Mkuu wa Makadara Monica Kivuti "ameshindwa katika vita" dhidi ya "majeraha yake makubwa".

    Bi Kivuti alipigwa risasi na polisi katika mahakama moja katika mji mkuu, Nairobi, siku ya Alhamisi baada ya kufutilia mbali dhamana ya mkewe kutokana na kutoroka kwa mwanamke huyo.

    Polisi huyo aliyetambulika kwa jina la Samson Kipchirchir Kipruto aliuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wengine kufuatia shambulizi hilo.

    Maafisa watatu kati ya hawa walijeruhiwa katika shambulio hilo lakini wanasemekana kuwa katika hali shwari.

    "Ni kwa moyo mkunjufu ninalitaarifu taifa kuwa Mhe. Monica Kivuti, Hakimu Mkuu, Mahakama ya Sheria ya Makadara ameshindwa katika mapambano dhidi ya majeraha makubwa aliyoyapata wakati wa shambulio la wazi la bunduki mahakamani," alisema Jaji Koome katika taarifa yake Jumamosi. .

    "Familia ya Mahakama inasimama kwa mshikamano wakati huu wa kiwewe kikubwa na inataka usikivu na huruma tunaposhiriki katika huzuni."

    Kulingana na gazeti la The Star, lililozungumza na chanzo katika hospitali ya Nairobi, Bi Kivuti alifariki Ijumaa usiku baada ya kupigwa risasi kifuani na mguuni.

    Mahakama za Sheria za Makadara zinapaswa kusalia kufungwa hadi Jumatatu.

    Huduma ya polisi ya kitaifa ilisema katika taarifa siku ya Alhamisi kwamba Kipruto, ambaye alikuwa msimamizi wa kituo cha polisi cha Londiani magharibi mwa Kenya, alikuwa mahakamani kwa "sababu zisizojulikana" wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya mkewe. Alishtakiwa kwa kupokea pesa "chini ya udanganyifu".

    Uchunguzi wa kilichotokea unaendelea.

    Jaji Koome alisema ni wazi kuwa Kipruto alinuia kumuua Bi Kivuti.

    Kisa hicho ndani ya chumba cha mahakama kimewashtua Wakenya.

    Polisi mara nyingi wamekuwa wakishutumiwa kuhusika na mauaji ya nje ya mahakama lakini hakuna tukio kama hilo lililoripotiwa ndani ya mahakama.

    Mahakama imesema itaimarisha hatua za usalama na imewahakikishia wafanyakazi wa mahakama na watumiaji wengine wa mahakama usalama na usalama wao.

    Chama cha Wanasheria nchini Kenya kilisema katika taarifa kwamba tukio hilo "halikuwa tukio la pekee bali ni sehemu ya mwelekeo wa kutatiza wa ongezeko la vitisho na mashambulizi dhidi ya maafisa wa mahakama na mawakili".

    "Migogoro ya kisheria inaweza kuwa na hisia nyingi, na hatari kwa maafisa wa mahakama na mawakili haziwezi kupunguzwa."

    Jumuiya hiyo iliongeza kuwa itafanya kazi na Jaji Koome "kutayarisha mikakati ya kina inayolenga kulinda mfumo wetu wa haki na watendaji wake".

  2. Mshambulizi wa zamani wa Arsenal na Everton Campbell afariki akiwa na umri wa miaka 54

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mshambulizi wa zamani wa Arsenal na Everton Kevin Campbell amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 54 baada ya kuugua kwa muda mfupi.

    Campbell alifunga mabao 148 katika mechi 542 akiwa na klabu nane katika maisha yake ya soka.

    Alishinda mataji manne makubwa akiwa na Arsenal na pia alichezea Leyton Orient, Leicester, Nottingham Forest, Trabzonspor, Everton, West Brom na Cardiff.

    Campbell alijitokeza mara ya mwisho kama mchezaji mnamo Februari 2007 kabla ya kuhamia kwenye utangazaji.

    Everton ilisema mapema mwezi huu aliugua mwezi Mei na "alikuwa mgonjwa sana" hospitalini.

    "Tumesikitika sana kujua kwamba mshambuliaji wetu wa zamani Kevin Campbell amefariki baada ya kuugua kwa muda mfupi," Arsenal ilisema.

    "Kevin alisifiwa na kila mtu kwenye klabu. Sote tunawafikiria marafiki na familia yake katika wakati huu mgumu. Pumzika kwa amani, Kevin."

    Everton alisema: "Kila mtu katika Everton amehuzunishwa sana na kifo cha mshambuliaji wetu wa zamani Kevin Campbell akiwa na umri wa miaka 54 tu.

    "Sio tu shujaa wa kweli wa Goodison Park na kielelezo cha mchezo wa Kiingereza, lakini mtu wa ajabu pia - mtu yeyote aliyewahi kukutana naye atajua. RIP, Super Kev."

  3. Marekani iyaliwekea vikwazo kundi la Israel linalosema kushambulia misafara ya misaada ya kibinadamu inayoelekea Gaza

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wizara ya Mambo ya Nje ilisema kuwa mali ya Marekani ya Tsav 9, shirika lenye uhusiano na askari wa akiba wa Israel na walowezi wa Ukingo wa Magharibi, itasitishwa, na Wamarekani watapigwa marufuku kufanya biashara nayo.

    Kwa miezi kadhaa, wanaharakati wa Israel wamekuwa wakizuia kuvuka kwa misafara ya misaada inayoelekea kwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

    Mnamo Mei 13, waandamanaji walirekodiwa wakishambulia lori mbili katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, kurarua na kuharibu magunia ya nafaka, na kuchoma lori. Ikulu ya White House ilielezea "uporaji" wa misafara ya misaada kama "ghasia kamili."

    Wakati huo, Tsav 9 ilisema baadhi ya vitendo vya waandamanaji "haviendani na maadili ya harakati zetu.''

    Wizara ya Mambo ya Nje ilisema Ijumaa kwamba vikwazo hivi vya Marekani kwa shirika la Israel viliwekwa kwa mujibu wa amri ya utendaji inayohusiana na ghasia katika Ukingo wa Magharibi ambayo ilitiwa saini na Rais Joe Biden.

  4. Mchekeshaji maarufu wa Kenya Fred Omondi afariki katika ajali Nairobi

    h

    Chanzo cha picha, Fred Omondi

    Mchekeshaji maarufu nchini Kenya Fred Omondi amefariki katika ajali ya barabarani.

    Omondi ambaye ni kakake Mchekeshaji maarufu na mwigizaji Eric Omondi, aliripotiwa kuhusika katika ajali ya barabarani iliyotokea kwenye barabara kuu ya Outering jijini Nairobi.

    Kufuatia kifo chake, waigizaji na waandaaji wa maudhui mbalimbali wameomboleza kifo cha Fred wakimtaja kuwa mmoja wa watu mahiri katika tasnia hiyo.

    Katika mtandao mitandao yake ya kijamii kaka yake Eric Omondi pia alimuomboleza marehemu kaka yake akisema, "Ndugu yangu, si sawa. Mungu akupokee, hadi wakati mwingine."

    Siku ya Ijumaa usiku, Fred aliandaa hafla ya Girl's Night Out katika mgahawa wa Captains Lounge and Grill uliopo Athi River- viungani mwa jiji la Nairobi.

    Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha mcheshi huyo akiwa na furaha pamoja na marafiki zake kwenye chumba cha mapumziko.

    Mchekeshaji huyo pia alitarajiwa kuandaa hafla nyingine siku ya Jumamosi katika Ukumbi wa BVB Lounge huko Meru.

    Fred alifuata nyayo za kaka yake na kuibuka kuwa mmoja wa wachekeshaji mahiri nchini. Alikuja kujulikana wakati wa sehemu kwenye Maonyesho ya Churchill na baadaye akaanzisha hafla kama mshiriki.

  5. Bintimfalme Kate aonekana kwenye hafla ya kwanza ya umma tangu mwanzo wa matibabu ya saratani

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Bintimfalme Kate akiwa kwenye gari kwenye Gwaride laa Kuinua Bendera ya Kifalme

    Bintimfalme wa Wales, ambaye anaendelea na matibabu ya saratani, alionekana kwenye gwaride kuashiria kupandishwa kwa bendera ya kifalme. Hili ni tukio la kwanza la umma kuhudhuria tangu utambuzi wake kutangazwa.

    Duchess of Cambridge alionekana kwenye gari la hali ya kioo la wafalme wa Uingereza. Baadaye, ataonekana pia kwenye Veranda la Jumba la Buckingham.

    Katika taarifa iliyotolewa siku moja kabla, Kate alisema matibabu yake yalikuwa yanampa "maendeleo mazuri" na akatangaza kwamba atashiriki gwaride kwa heshima ya Mfalme.

    Lakini pia aliongeza kuwa tiba hiyo haijakamilika na itaendelea kwa miezi kadhaa zaidi.

    "Bado kuna njia ndefu mbele," aliandika katika ujumbe wake uliowekwa kwenye mitandao yake ya kijamii.

    Tangu Bintimfalme huyo anayefahamika kama Princess wa Wales afichue utambuzi wake wa maradhi ya saratani katika video ya kibinafsi kwenye mitandao ya kijamii mnamo Machi, hakujawa na habari mpya kuhusu afya yake kutoka kwa ufalme.

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ujumbe mpya wa binti mfalme unaambatana na picha mpya iliyopigwa na mpiga picha Matt Porteous nje ya nyumba yake huko Windsor.

    Bintimfalme, hata hivyo, anaonya kwamba habari yoyote njema kuhusu ugonjwa wake inapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari.

    "Mtu yeyote ambaye amepitia [tiba ya mionzi] chemotherapy anajua kwamba kuna siku nzuri na mbaya," alielezea.

    "Siku moja unahisi dhaifu, umechoka, na unapaswa kuuruhusu mwili wako kupumzika. Lakini siku inayofuata, unahisi kuwa na nguvu na unataka kutumia zaidi afya yako nzuri," Kate aliendelea.

    "Ninajifunza subira, hasa katika hali ya kutokuwa na uhakika. Ninaichukua kila siku inavyokuja; ninasikiliza mwili wangu na kujipa muda unaohitajika sana wa kupona," aliongeza.

  6. Cyril Ramaphosa amechaguliwa tena kuwa rais wa Afrika Kusini

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Cyril Ramaphosa akijibu bungeni baada ya kuchaguliwa tena kuwa rais

    Bunge la Afrika Kusini limemchagua tena Cyril Ramaphosa kuwa rais wa nchi hiyo kufuatia makubaliano ya kihistoria ya muungano kati ya chama tawala cha African National Congress (ANC) na vyama vya upinzani.

    Serikali mpya ya umoja wa kitaifa inachanganya ANC ya Bw Ramaphosa, Muungano wa mrengo wa kati wa Democratic Alliance (DA) na vyama vidogo.

    Katika hotuba yake ya ushindi, Bw Ramaphosa alipongeza muungano huo mpya, na kusema wapiga kura wanatarajia viongozi "kuchukua hatua na kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya kila mtu katika nchi yetu".

    Makubaliano hayo yaliharakishwa katika siku moja katika siku ya hali ya juu ya kisiasa, ambayo ilisababisha Bunge kukaa hadi jioni kwa kura kuthibitisha ni nani angeshika madaraka katika utawala mpya.

    Hapo awali, makubaliano yaliafikiwa kufuatia wiki kadhaa za uvumi kuhusu nani ANC ingeshirikiana naye baada ya kupoteza wingi wake wa wabunge kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30 katika uchaguzi wa mwezi uliopita.

    Ilipata 40% ya kura, huku DA ikishika nafasi ya pili kwa 22%.

    Katibu mkuu wa ANC Fikile Mbalula aliutaja mpango wa muungano kuwa "hatua ya ajabu".

    Ilimaanisha kuwa Bw Ramaphosa - ambaye alichukua nafasi ya Jacob Zuma kama rais na kiongozi wa ANC kufuatia mzozo mkali wa madaraka mnamo 2018 - aliweza kushikilia mamlaka.

    Hatua inayofuata ni kwa Bw Ramaphosa kutenga nyadhifa za baraza la mawaziri, ambazo zitajumuisha wanachama wa DA.

    Mkataba wa vyama vingi hauhusishi vyama viwili vilivyojitenga na ANC, na huenda vitanufaika iwapo vitashindwa kuleta uboreshaji wa kiuchumi unaodaiwa na wapiga kura.

    Lakini kura za maoni zinaonyesha Waafrika Kusini wengi wanataka muungano huu mkuu ambao haujawahi kushuhudiwa ufaulu.

  7. Zelensky anataka kuonyesha uungwaji mkono katika mkutano mkubwa wa amani wa Ukraine

    g

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Bw Zelensky aliwasilisha mpango wake wa pointi 10 wa amani mwishoni mwa 2022

    Wikendi hii, eneo la mapumziko la Uswizi lililotengwa juu ya Ziwa Lucerne litashuhudia makumi ya viongozi wa dunia na maelfu ya askari na polisi wakishuka Bürgenstock.

    Zaidi ya nchi 90 na taasisi za kimataifa zinahudhuria hafla hiyo, ambayo inalenga kujadili kanuni za msingi za kumaliza mzozo nchini Ukraine.

    Uswisi wanatumai kwamba mkutano wa kilele wa Ukraine unaweza kutoa alama za kwanza za majaribio za mchakato wa amani, takriban miezi 28 baada ya Urusi kuivamia jirani yake.

    Ni mkusanyiko mkubwa zaidi wa viongozi wa dunia unaokutana kwa ajili ya Ukraine tangu uvamizi kamili wa Urusi uanze.

    Mkutano huu unafanyika wahusika wakuu kama vile Uchina kukaa pembeni, na Rais wa Urusi Vladimir Putin akitoa uamuzi mpya - akitaka Ukraine itolewe madaraka na kudai kuwa pendekezo la amani - matarajio ya maendeleo makubwa ni madogo.

    Urusi haijaalikwa.

    Kwa Ukraine, ukweli kwamba mkutano huu unafanyika ni jambo zuri.

    Wanasiasa mjini Kyiv wamekuwa wakimsifu kila mshiriki aliyethibitishwa kama ishara ya kumuunga mkono.

    Kwao, mkutano huo mkubwa unapaswa kuionyesha Moscow kwamba ulimwengu unasimama upande wa Ukraine - na sheria za kimataifa.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  8. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya mubashara leo ikiwa ni tarehe 15.06.2024