Vita vya Ukraine: Zelensky akutana na Papa Francis huko Roma

Papa Francis amewahi kusema kwamba Vatikani iko tayari kufanya kazi kama mpatanishi katika mzozo kati ya Urusi na Ukraine.

Moja kwa moja

  1. Majambazi yavamia kituo cha Redio na kupora matangazo yakiendelea

    Maafisa wa upelelezi katika Kaunti ya Nakuru nchini Kenya wanasaka taarifa kuhusu majambazi waliojihami kwa silaha waliovamia kituo cha redio, kuwatapeli wafanyakazi na kuchukua pesa taslimu na vitu vingine vya thamani.

    Katika tukio hilo lililorekodiwa moja kwa moja na kamera, majambazi hao waliokuwa na silaha za moto na mapanga walinaswa walipokuwa wakiingia kwenye studio ya Mwinjoyo FM, ambapo waliwaamuru watangazaji walale chini kabla ya kupora fedha na vitu vingine vya thamani.

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

    “Zima kitu hicho! Lala chini,” mmoja wao aliamuru huku watangazaji wawili mwanamume na mwanamke wakilala chini. Majambazi hao ambao walikuwa wameficha nyuso zao walikatiza matangazo ya moja kwa moja ya kipindi cha injili yaliyokuwa yakiendelea.

    Genge hilo la watu wanne liliondoka na simu 8, pesa taslimu zaidi ya Sh35,000 na jozi nane za viatu. Kamera tano pia ziliharibiwa na majambazi hao kabla ya kukimbia kwa kuruka uzio wa eneo hilo lililoko katika vitongoji vya kifahari vya Nakuru Milimani.

    Kwa mujibu wa taarifa Msako wa kuwasaka majambazi hao waliovalia nguo nyeusi umeanza.

  2. Mapigano Sudan: Mazungumzo ya amani kuanza tena

    sudan

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mazungumzo kati ya pande zinazozozana nchini Sudan yanatarajiwa kuanza tena mwishoni mwa juma huku jeshi la serikali na kikosi cha dharura cha Rapid Support Forces au RSF wakiendelea kupigania udhibiti wa jiji la Khartoum.

    Licha ya makubaliano ya kulinda raia na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwasilishwa mapigano yameendelea katika sehemu za mji huo.

    Bei ya dawa imepanda kwa sababu ya uhaba na viwango vya uhalifu vimeongezeka maradufu.

    Jeshi na wanamgambo wa RSF wana historia ya ukiukwaji wa haki za binadamu na sasa magenge ya wahalifu pia yanatumia fursa ya machafuko hayo.

    Licha ya makubaliano, hakuna dalili kwamba kulinda raia ni kipaumbele namba moja kwa pande zote.

  3. Zelensky yuko Roma kukutana na Papa Francis

    Volodymyr Zelensky

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky yuko Roma ambapo anakutana na viongozi wa kisiasa na amekutana na Papa Francis.

    "Ziara muhimu kwa ushindi unaokaribia wa Ukraine!" Zelensky aliandika kwenye mtandao wake wa twitter alipotua katika mji mkuu wa Italia.

    Atakutana pia na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, Rais Sergio Mattarella na kuelekea hadi Vatican baadaye Jumamosi.

    Kumekuwa na usalama mkubwa, na zaidi ya polisi 1,000 wamepelekwa kwenye eneo lisilo na ndege huko Roma.

    Papa Francis amewahi kusema kwamba Vatikani iko tayari kufanya kazi kama mpatanishi katika mzozo kati ya Urusi na Ukraine.

    Mapema mwezi huu, alisema kwamba Vatikani ilikuwa ikifanya kazi katika mpango wa amani wa kumaliza vita, akisema kwamba mpango huo "haujaonekana hadharani. Utakapowekwa hadharani, nitauzungumzia."

  4. Mapigano Sudan: 'Bibi yangu ameuawa katikati ya mapigano huko Khartoum'

    sudan

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Azhaar Sholgami anajaribu kumzika bibi yake. Bibi huyo amekufa kwa siku kadhaa sasa, hakuna anayejua ni ngapi. Alikufa akiwa peke yake, kwenye nyumba yake huko Khartoum akishindwa kutoroka vita vya kikatili kati ya majenerali wawili wanaopigana wa Sudan.

    Azhaar anashuhudia hayo akiwa New York, akijaribu sana kumuokoa bibi yake ikashindikana. Sasa, anajaribu sana kuupata mwili wake. Hayuko peke yake. Mapigano makali yanayoendelea yamefanya zoezi la kupata miili na kuzika kuwa zoezi hatari katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu wa Sudan.

    Makubaliano ya kibinadamu yaliyofikiwa na pande hizo mbili huko Jeddah siku ya Ijumaa yanaanza kusaidia wafanyakazi wa misaada kukusanya, kuwasajili na kuwazika waliouawa kwenye mapigano.

    "Tunaendelea kuona maiti mitaani, na hospitali ambazo zinahitaji huduma," anasema Patrick Youssef, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu.

    Babu na babu za Azhaar, Abdalla Sholgami na Alaweya Reshwan, walikwama kwenye joto la mapigano. Waliishi katika mtaa wa Baladiya huko Khartoum, karibu na makao makuu ya kijeshi na ubalozi wa Uingereza. Ikawa uwanja wa vita kwa pande mbili zinazopigana - jeshi la Sudan, na Jeshi la Wanajeshi wa Msaada wa Haraka (RSF).

    sudan

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bw Sholgami, raia wa Uingereza, alipigwa risasi tatu, na kumwacha mkewe mlemavu peke yake nyumbani. Kwa namna fulani alinusurika, na familia yake sasa inajaribu kumhamisha kutoka Sudan.

    Lakini hakuna taarifa yoyote kuhusu mke wake na nyanyake Azhaar, Alaweya. Wiki kadhaa za simu za Azhaar kwa ubalozi wa Uingereza hazikuweza kupata ufumbuzi.

    Sudan

    Chanzo cha picha, Getty Images

    "Nilikuwa karibu sana na bibi yangu," anasema. "Na katika mazungumzo yetu ya mwisho kabla sijaenda New York alisema, ninaogopa utaniacha peke yangu." "Nilimcheka. Nikasema, sitakuacha peke yako, hata iweje, nitakuwa nawe siku zote... ninahisi nimemwangusha."

  5. Mkulima wa Kenya: 'Nina hofu tembo wataniua'

    Kenya

    Katika mfululizo wetu wa makala kutoka kwa wanahabari wa Kiafrika, Ismail Einashe anaangazia jinsi mabadiliko ya hali ya hewa Kenya yanavyoleta wanyama na wanadamu katika migogoro mikubwa zaidi.

    Mchana mmoja katika kijiji kidogo cha Njoro Mata nchini Kenya, mkulima anakagua uharibifu uliosababishwa na tembo. Wanyama maarufu nchini Kenya wamekuwa wakivamia mashamba ya Monicah Muthike Moki, kusini mwa Kenya, karibu na mlima Kilimanjaro.

    Ni mama mwenye umri wa miaka 48 mwenye watoto watatu anayeishi bila mume na ambaye maisha yake yanategemea bidii yake ya kilimo cha mihogo, mahindi, ndizi, miwa na maembe.

    Bi Moki anasema tembo huja kila siku kutoka mbuga ya wanyama iliyo karibu ya Tsavo, mojawapo ya hifadhi kubwa zaidi za wanyama duniani, ambayo ni makazi ya takriban 15,000 ya wanyama.

    Kwa Bi Moki, uvamizi wa tembo ni "jambo linaloumiza sana" kuuona. Anasema tembo "wana ujasiri" na "hawaogopi".

    Kenya

    Kila usiku yeye hulala mbali na familia yake akiwa peke yake shambani, nakotarajia kwa woga kukutana na mlio wanyama. Cha kusikitisha ni kwamba hatua zake za uvumbuzi haziwazuii tembo, lakini angalau humuonya kuhusu uwepo wao.

    Tembo wanaweza kuwa hatari sana. "Ikiwa tembo ataniumiza, kunijeruhi au kuniua, familia yangu itateseka," Bi Moki asema.

    Kwa Bi Moki, mzozo huu unaathiri sana afya yake ya akili, ikichangiwa na kukosa usingizi. Amekuwa mtu wa wasiwasi na kukumbwa na hofu ya maisha ya baadaye ya watoto wake ikiwa tembo atamuua.

    "Ninaogopa kwa sababu ikiwa nitakufa," anasema, "ni nani atakayewatunza?"

  6. Uchaguzi Uturuki: Rais Erdogan kungo'ka madarakani baada ya miaka 20?

    Turkey

    Chanzo cha picha, APAIMAGES/SHUTTERSTOCK

    Rais Erdogan wa Uturuki anakabiliwa na upinzani mkali zaidi katika maisha yake ya siasa baada ya upinzani kuungana dhidi yake katika uchaguzi wa Jumapili.

    Mpinzani wake mkuu Kemal Kilicdaroglu alifika mbele ya umati wa wafuasi wake siku ya Ijumaa, akiwa na washirika kutoka katika vyama vingine kuonyesha kuungana pamoja.

    Huku mvua ikinyesha mjini Ankara, aliapa kurejesha "amani na demokrasia". Mtu huyo anataka wapiga kura kumuondoa madarakani Rais Recep Tayyip Erdogan aliyedumu kwa miaka 20.

    Alisema ameiingiza Uturuki katika changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na uchumi na mfumuko wa bei uliokithiri na janga la tetemeko la ardhi la Februari.

    Masuala haya yametawala kampeni hii kali ya urais na bunge. Akiwa na umri wa miaka 74, kiongozi huyo wa upinzani mara nyingi anatajwa kuwa mzungumzaji mpole, lakini alitoa hotuba yenye nguvu kwa hadhira inayoamini kuwa hili ndilo tumaini lao bora hadi sasa la kurudisha madaraka kutoka kwa rais ambaye ameyaondoa bungeni na kujiongezea kwakwe kwa kiasi kikubwa. .

  7. Papua New Guinea: Waziri ajiuzulu kwa kusafiri kifahari kuhudhuria kutawazwa kwa Mfalme Charles III

    Papua

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa mambo ya nje wa Papua New Guinea amejiuzulu baada ya kashfa ya matumizi ya fedha ya ujumbe rasmi wa nchi hiyo uliohudhuria kutawazwa kwa Mfalme Charles III.

    Justin Tkatchenko alisafiri na binti yake Savannah, ambaye alichapisha kwenye mtandao wa TikTok kuonyesha safari yake kwenye ndege ya daraja la kwanza pamoja na kuonekana akifanya manunuzi mengi nchini Singapore.

    Siku ya Jumatano, aliwataja wakosoaji wake kuwa "wanyama waliopitwa na wakati". Maoni ya Bw Tkatchenko yalizua maandamano katika mji mkuu wa Port Morseby siku ya Ijumaa nje ya Ikulu ya Bunge.

    Papua New Guinea ni taifa la Jumuiya ya Madola huko Pasifiki ambalo Mfalme Charles ni mkuu wake wa serikali.

    Bw Tkatchenko alisema katika taarifa Ijumaa kwamba "amejiweka kando" baada ya kushauriana na Waziri Mkuu James Marape.

    Aliongeza kuwa anataka kuhakikisha matukio ya hivi majuzi hayaingiliani na ziara rasmi za Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi.

    Bw Tkatchenko na bintiye walikosolewa kwa kusafiri na maafisa wasiopungua 10 kushuhudia kutawazwa kwa Mfalme Charles, kwa gharama ya karibu dola 900,000, kwa mujibu wa gazeti la Post-Courier.

    Msemaji wa serikali Bill Toraso alilithibitishia shirika la habari la Reuters kuwa wafanyakazi wake 10 walikuwa wamesafiri kwenda London, pamoja na wageni 10. Katika video hiyo ambayo imefutwa, Savannah alirekodi ziara yake katika maduka ya kifahari ya Singapore na mlo wake katika mgahawa wa daraja la kwanza alipokuwa njiani kuelekea London.

  8. Marekani yaiomba radhi Afrika Kusini kwa kudai iliiuzia silaha Urusi

    Russia

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini inasema balozi wa Marekani "ameomba radhi" kwa kudai kuwa nchi hiyo iliiuzia Urusi silaha.

    Siku ya Alhamisi Reuben Brigety alidai meli ya Urusi ilikuwa imesheheni risasi na silaha huko mjini Cape Town Disemba mwaka jana.

    Afrika Kusini inasema haina rekodi ya mauzo ya silaha na Rais Cyril Ramaphosa ameagiza uchunguzi ufanyike.

    Siku ya Ijumaa msemaji wa masuala ya usalama wa taifa wa Ikulu ya White House hakusema lolote kuhusu maelezo ya madai hayo.

    Lakini John Kirby alisema ni "suala zito" na Marekani imekuwa ikizitaka nchi mara kwa mara kutounga mkono vita vya Urusi nchini Ukraine.

    Akiandika kwenye mitandao ya kijamii baada ya kukutana na wizara ya mambo ya nje, Bw Brigety alisema "anashukuru kwa fursa ya... kurekebisha maoni yoyote potofu yaliyotokana na matamshi yangu hadharani".

    Alisema katika mazungumzo hayo "uwepo wa ushirikiano mkubwa kati ya nchi zetu mbili na ajenda muhimu ambayo marais wetu wametupa".

    Wakati huo huo waziri wa baraza la mawaziri la Afrika Kusini alikosoa "diplomasia ya aina hiyo, akisema Afrika Kusini haiwezi "kuonewa na Marekani".