Malkia anatarajiwa kuzikwa kitaifa kesho, lakini leo baadhi ya viongozi hao wakuu watatoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo aliyetawala kwa miaka 70
Moja kwa moja
Arsenal yarejea kileleni ikimchezesha mtoto wa miaka 15, na kuvunja rekodi ya EPL
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Ethan Nwaneri (kulia) akipiga makofi, wakati akiimbiwa na mashabiki wa timu yake "leo mpira, asubuhi kesho darasani,". Yuko na Gabriel Martinell ambaye alitoka katika dakika za mwisho za kipindi cha pili.
Arsenal imerejea kileleni mwa ligi kuu England baada ya ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Brentford.
Mabao ya William Saliba, Gabriel Jesus na Fabio Vieira yalitosha kuipa alama 3 Arsenal na kufikisha 18, moja zaidi ya Manchester City walio katika nafasi ya pili.
Katika mchezo huo, kijana mdogo Ethan Nwaneri, mwenye umri wa miaka 15 aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kucheza ligi kuu England(EPL)
Mwanafunzi huo aliingia dakika za majeruhi kuchukua nafasi ya Fabio Vieira na angalau aligusa mpira mara moja.
Kinda huyo aliitwa tu kwa mazoezi ya kikosi cha kwanza kwa mara ya kwanza siku ya jana, hasa baada ya kukosekana kwa nahodha Martin Odergaard aliye majeruhi.
Kocha Mikel Arteta akavutiwa naye na leo kampa nafasi. Ethan alizaliwa mwaka 2007, ambapo uwanja wa Emirates unaotumiwa na Arsenal ulifunguliwa kabla hajazaliwa!
Jaribio la bunge Uganda kulizima tamasha la 'Nyege Nyege' lapandisha mauzo ya tiketi
Chanzo cha picha, Getty Images
Waandaaji wa tamasha la muziki nchini Uganda la 'Nyege Nyege' wanasema jaribio la bunge la kupiga marufuku tamasha hilo kwa sababu ya wasiwasi kwamba linapotosha maadili limeongeza mauzo ya tiketi.
Tamasha hilo karibu na kingo za Mto Nile limevutia takriban watu elfu kumi na mbili, wengi wao kutoka nje ya nchi.
Tangazo la bunge kutaka tamasha hilo kusitishwa ni kama limesaidia kulitangaza zaidi. Waandaaji wanasema limeongeza mauzo ingawa hawajasema ni kwa kiasi gani.
Baadhi ya wale ambao wameelekea nchini Uganda kufurahia muziki wanasema walikuwa hawajasikia kuhusu tamasha hilo hadi wanasiasa walipoliweka kwenye vichwa vya habari kwa kutishia kulipiga marufuku.
Wabunge walisema litaendeleza vitendo viovu. Baadhi ya watoa maoni nchini Uganda walisema watunga sheria nchini humo labda hawakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kujadili mada ya maadili.
Malkia Elizabeth II: Mti alioupanda akiwa ziarani Kenya unaashiria utawala mrefu wa kiongozi huyo
Katika kanisa la Anglikana la Mtakatifu Philip huko Naro Moru, katikati mwa Kenya, Malkia alikumbukwa kwenye ibada maalum ya shukrani siku ya Jumamosi.
Ilikuwa hapa, maili 12 kusini mwa Ikweta, ambapo Binti mflame Elizabeth wa wakati huo alishiriki ibada mnamo Februari 1952 - siku chache baadaye kifo cha baba yake kilisababisha kutawazwa kwake kwa Malkia na kuanza safari ya utawala wake.
Washiriki wa ibada hiyo wakati wanaenda kukaa kwenye viti vyao walitembea juu ya zulia la bluu lililokuwa Westminster Abbey wakati wa Kutawazwa kwa Malkia mnamo 1953 na baadaye zulia hilo walipewa Kanisa kama zawadi.
Mishumaa ilimulika madirishani, huku nje jua la mchana likipiga mti wa 'rosewood' wa Brazili uliopandwa kuashiria ziara yake. Sasa ukiwa na umri wa miaka 70 na kuongezeka urefu zaidi, ni ishara ya utawala wa muda mrefu wa Malkia, unaokumbukwa kwa furaha na jumuiya hii.
India kuona mnyama duma kwa mara ya kwanza baada ya miaka 70
Chanzo cha picha, Getty Images
Duma mnyama jamii ya chui wanatarajiwa kuanza kuzurura nchini India kwa
mara ya kwanza tangu walipotangazwa kutoweka rasmi mwaka wa 1952.
Kundi la duma wanane waliwasili kutoka Namibia
kwenye sherehe ya siku ya kuzaliwa ya Waziri Mkuu Narendra Modi Jumamosi.
Watawekwa karantini kwa mwezi mmoja kabla ya
kuachiliwa na kuanza kuzurura katika mbuga ya kitaifa katikati mwa India.
Duma walikuwa wakipatikana kwenye misitu kama
ilivyo kwa wanyama wengine wakubwa wa aina yake kama simba na simbamarara
lakini walitoweka miaka 70 iliyopita.
Ni wanyama wa nchi kavu wenye kasi zaidi
duniani, wenye uwezo wa kufikia kasi ya maili 70 (113km) kwa saa.
Hii ni mara ya kwanza kwa wanyama wakubwa
wanaokula nyama kuhamishwa kutoka bara moja hadi jingine na kurudishwa porini.
Angalau duma 20 wanasafirishwa kwenda India
kutoka Afrika Kusini na Namibia, nyumbani kwa zaidi ya theluthi moja ya duma
7,000 duniani.
Kundi la kwanza la duma wanane - majike watano na madume watatu, wenye umri kati ya miaka miwili na sita - waliwasili
kutoka Windhoek nchini Namibia hadi mji wa Gwalior nchini India siku ya
Jumamosi.
Uchunguzi unaonyesha kwamba angalau duma 200
waliuawa nchini India, hasa na wachungaji wa kondoo na mbuzi, wakati wa
ukoloni.
DR Congo: Ukraine yaondoa wanajeshi wake katika kikosi cha MONUSCO
Chanzo cha picha, MONUSCO
Ukraine imeondoa wanajeshi wake katika vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini DR Congo kwa ombi maalumu la serikali ya Kyiv, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DR Congo umesema.
Wanajeshi hao walipanda ndege kurejea nyumbani siku ya Ijumaa kutoka uwanja wa ndege wa Goma mashariki mwa DRC katika hali ya inayotokea kwa nadra ya kujitoa kwa askari kwenye vikosi vya Umoja wa Mataifa.
Kamanda wa kikosi cha ujumbe wa Brazil Luteni Jenerali Marcos Da Costa ameshukuru "miaka yao 10 ya mchango mkubwa" kwa watu wa DRC.
Mwezi Machi, Rais Volodymyr Zelensky alitia saini amri ya kuwataka walinda amani wote wa Ukraine kuunga mkono jeshi kufuatia uvamizi wa Urusi.
Wataalam walikuwa wameelezea wasiwasi wao ikiwa wanajeshi wa Ukraine watajiondoa kwenye misheni hiyo nchini DR Congo.
Jeshi la Ukraine linaendesha operesheni za kukabiliana na mashambulio ya Urusi hasa katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo ambapo maafisa wanasema kuwa wanajeshi wamefanikiwa kurejesha baadhi ya miji iliyokuwa inakaliwa na jeshi la Urusi.
Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya wanajeshi mia mbili na hamsini wa Ukraine walikuwa wakihudumu nchini DR Congo kwa ujumla katika kitengo cha anga ambapo nchi hiyo ina helikopta nane katika misheni hiyo.
Helikopta za Ukraine ni karibu theluthi moja ya zile zinazotumika katika misheni huko Kongo, taarifa za misheni hiyo zinaonyesha.
MONUSCO, inayodorora polepole baada ya miaka 22 nchini DR Congo, imekosolewa vikali kwa kushindwa kurejesha amani katika eneo la mashariki linalokumbwa na mzozo.
Watu 36 wakiwemo walinda amani wanne wa Umoja wa Mataifa wamefariki dunia mwezi Julai wakati waandamanaji walipoharibu majengo ya Umoja wa Mataifa katika baadhi ya miji mashariki mwa DRC.
Kimbunga Nanmadol kupiga kisiwa cha Kyushu Japani leo, watu milioni 13 hatarini
Chanzo cha picha, Reuters
Maelfu ya watu nchini Japani wamehimizwa kuhama makazi yao huku kukiwa na onyo la hatari "isiyo na kifani" kutokana na dhoruba inayokaribia kutokea.
Kimbunga Nanmadol kinatarajiwa kutua katika kisiwa cha Kyushu leo Jumapili. Kitavuma kwa upepo unaweza kufikia 270km/h (168mph) na baadhi ya maeneo yanaweza kupata mvua ya 500mm kwa saa 24 tu.
"Tahadhari maalum" inachukuliwa huko Kyushu, na maonyo ya maporomoko ya ardhi na mafuriko.
Huduma za treni na safari za ndege zimesitishwa kwa muda.Kyushu ndicho kisiwa kilicho kusini zaidi kati ya visiwa vinne vinavyounda sehemu kuu ya Japani na kina wakazi zaidi ya milioni 13.
Kaka wa Paul Pogba, Mathias ashtakiwa kwa 'unyanganyi' wa fedha za nduguye
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Mathias (kulia) akiwa na ndugu yake Pogba kumuunga mkono kwenye sherehe za ubingwa wa kombe la dunia walioupata timu ya taifa ya Ufaransa mwaka 2018
Mathias Pogba amefunguliwa mashtaka na kuwekwa kizuizini kwa madai ya kula njama ya unyang'anyi ama kutaka 'kumuibia' pesa kwa mabavu, kaka yake Paul, ambaye ni kiungo wa kati wa Ufaransa na Juventus.
Watu wengine wanne pia wanachunguzwa rasmi kwa ulaghai na uhalifu huo, vyanzo vya mahakama viliambia mashirika ya habari ya Reuters na Agence France-Presse.
Wakili wa Mathias Pogba, Yassine Bouzrou, alisema mteja wake hana hatia. Aliliambia shirika la utangazaji la Ufaransa BFMTV: "Tutapinga uamuzi huu."
Mathias Pogba, 32, amekiri kuwa anahusika na video ambayo ilionekana mtandaoni mwezi uliopita ikiahidi "kufichua" mambo kadhaa yanayomuhusu kiungo huyo wa kati wa Juventus mwenye umri wa miaka 29.
Waendesha mashtaka wa Ufaransa walifungua jalada la uchunguzi wa kimahakama mapema mwezi huu baada ya mchezaji wa zamani wa Manchester United Paul kusema alikuwa analengwa na unyang'anyi na vitisho kutoka kwa genge moja la uhalifu linalomuhusisha ndugu yake.
Aliwasilisha malalamiko yake kwa waendesha mashitaka wa Turin mnamo tarehe 16 Julai akidai alikuwa mlengwa wa njama ya ulaghai ya euro 13m (£11.29m).
Mshindi huyo wa Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa mwaka 2018, Pogba alihamia Juventus kwa uhamisho wa huru msimu huu baada ya kuondoka Manchester United.
Mathias Pogba pia ni mwanasoka wa kulipwa ambaye amewahi kuichezea Guinea na amevichezea vilabu mbalimbali barani Ulaya vikiwemo vya Crewe, Wrexham, Crawley na Partick Thistle.
Aliyekwepa kupanga foleni ya kuaga mwili wa Malkia kufikishwa Mahakamani kesho
Chanzo cha picha, WPA ROTA
Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 28 ameshtakiwa kwa kukwepa kupanga mstari wa foleni ya waombolezaji na kujaribu kulifikia kwa karibu jeneza la Malkia siku ya Ijumaa.
Muhammad Khan, kutoka Tower Hamlets mashariki mwa London, aliyekamatwa siku hiyo hiyo, sasa atafikishwa katika Mahakama ya Westminster Jumatatu.
Urushaji wa matangazo ya moja kwa moja ya maombolezo kutoka katika Ukumbi wa Westminster yalikatwa wakati tukio lilipotokea.
Taarifa kutoka kwa Polisi ilisema: "Muhammad Khan, 28, wa Barleycorn Way, Tower Hamlets, alishitakiwa Jumamosi, Septemba 17, chini ya Kifungu cha 4A cha Sheria ya Utaratibu wa Umma; kwa kitendo kinachokusudia kusababisha hofu na unyanyasaji."Atafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Westminster siku ya Jumatatu, Septemba 19."
Ni mtu wa pili kushtakiwa kwa kutenda kosa akiwa kwenye foleni ya kuuaga mwili wa Malkia. Mwanaume mwingine mwenye umri wa miaka 19 alishtakiwa baada ya kudaiwa kuvua nguo na kujaribu kuwanyanyasa kingono waombolezaji wa kike walipokuwa wakisubiri kwenye foleni katika bustani ya Victoria Tower siku ya Jumatano.
Kijana huyo aliyefahamika kama Adio Adeshine alishtakiwa kwa makosa mawili ya unyanyasaji wa kijinsia na makosa mawili ya kukiuka amri ya kuzuia madhara ya kingono.
Atafikishwa katika Mahakama ya Southwark Crown tarehe 14 Oktoba. Marehemu Malkia Elizabeth II atasalia katika Ukumbi wa Westminster hadi siku ya mazishi yake Jumatatu.
Maelfu wapiga kambi kuzunguka Kasri tayari kumzika Malkia hapo kesho
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelfu ya watu wameendelea kupiga kambi katika kasri la, maombolezo yakiingia katika siku ya mwisho kabla ya maziko ya Malkia hapo kesho.
Tayari mamlaka zimetangazwa kufungwa kwa foleni ya watu kuenda kutoa salamu za mwisho kwa kiongozi huyo.
zaidi ya watu 1000 wamelazimika kuhudumia na magari ya dharura kutokana na hali ya baridi iliyopo.
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Joe Biden, na Samia Suluhu wa Tanzania ni miongoni mwa viongozi waliowasili jijini London tayari
kuhudhuria mazishi ya kitaifa ya Malkia Elizabeth II siku ya Jumatatu.
Rais wa Kenya, William Ruto nae ameelekea huko kuungana na viongozi wengine wakuu na wa kigeni karibu 500 wanaokuja London kwa tukio linalowakutanisha viongozi wa ulimwengu
wengi zaidi kuonekana kwa pamoja kwa miongo kadhaa.
Mawaziri wakuu wa Canada, Australia na New Zealand tayari
wako Uingereza.
Mzozo unazingira baadhi ya wageni waalikwa, kama vile
Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed Bin Salman.
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Kwa siku 4 sasa kumekuwa na msusuru wa watu wakikesha licha ya baridi kali lililopo
Kwa mujibu wa taarifa zaidi ya wanajeshi 10,000 wanatarajiwa kutumika kwenye mazikoya Malkia.
Viongozi wa Afrika waliohudhuria mbali na Rais Samia na Ruto, yupo rais wa Ghana Nana Akufo-Addona Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje
Mwisho wa X ujumbe
Mbali na hao na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese na Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinta Ardern, viongozi wengine wa Jumuiya ya Madola wanaotarajiwa kuhudhuria ni pamoja na Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina na Rais wa Sri Lanka Ranil Wickremesinghe.
India itawakilishwa na Rais Droupadi Murmu.
Viongozi walioalikwa leo wamepata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho huko Westminster na kutia saini kitabu cha maombolezo.
Mazishi ya kitaifa ya Malkia Elizabethi II yatafanyika kesho Jumatatu Westminster Abbey, London, kabla ya mwili wake kulazwa kwenye kasri la Windsor.